Monday, August 31, 2015

SOMO: KUMJUA MUNGU


JUMAPILI:  30 AUGUST 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
 
 
Na:     BRYSON LEMA (RP)        &
Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)
 
Utangulizi: Imeandikwakatika 2KORINTHO 2:14….[Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu.]…Unaweza kumfahamu mtu lakini papo hapo usimjue huyo mtu. Kuna tofauti kubwa sana kati ya kumjua mtu na kumfahamu mtu. Kumjua mtu ni zaidi ya kumfahamu mtu husika.
 
Paulo aliwahi kuwauliza watu katika MATENDO  17:23, kama ilivyoandikwa ..[Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. ]… Pengine hata wewe umewahi kujiuliza kwa nini hawa watu walifanya hivyo kwa kuyaandika maneno hayo?. Musa na wana wa Israeli walitofautiana katika kumjua na kumfahamu Mungu. Wakati wana wa Israeli walimfahamu  Mungu kuwa ndiye aliyewavusha Bahari ya Shamu, Musa alimjua zaidi kwa namna alivyokuwaanawasiliana naye ana kwa ana.
 
Ukijua jinsi Mungu wako anavyofanya kazi hata tatizo lako litaisha, kwa sababu unamjua Mungu  unayemtumika. Mtumishi wa Elisha alipotoka nje na kuona majeshi yaliyomzunguka, alirudi  ndani na kumwambia Elisha,  Bwana wangu na  Mungu wangu.” Ndiposa Elisha akamuuliza kwani kuna nini ulichokiona? Yule mtumishi akamwelezea vikosi  vya jeshi alivyoviona nje. 
 
Ukimjua unayemtumikia wala hatatishika.  Ungejua wapi tumaini lako lilipo utaishi  maisha mazuri sana. Ni kama vile Tanzania leo hii itangaze vita kupigana na Marekani leo hii, je unadhani Marekani itatishika hata kidogo? Hapana, kwa sababu Marekani inajua ilicho nacho cha kuiteketeza Tanzania. Tatizo la wakristo wengi hawamjui Mungu ila wanajua maandiko ya Mungu‼! Ukimuuliza mkristo andiko  fulanii lipo  wapi, atakutajia,lakini hajui Mungu aliyeyasema hayo maneno.
 
MITHALI 2:5…[Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.]…Kumbe kufunga,siyo kumjua Mungu. Kumbe kuomba siyo kumjua Mungu. Kumbe kuja kanisani siyo kumjua Mungu. Yamkini mtu anakuja kanisani kwa sababu zake binafsi, lakini kumjua Mungu anayemuamini hakupo. Wakristo wengi ni bingwa wa kubeba Biblia lakini siyo wa  kumjua Mungu. Kumjua Mungu huanza kwa “kusikia”, kwani  ndicho chanzo cha kumjua Mungu. Kabla ya kumjua Mungu unaanza kumfahamu Mungu  kwa njia ya kuzisikia habari zake.
 
Ndiyo maana katika Biblia kuna watu wanatajwa majina na wengine hawatajwi kabisa. Mfano ni "Tajiri mmoja" na "maskini mmoja jina lake Lazaro". Tajiri hajatajwa kwa sababu mbele za Mungu hakuwa na mahusiano yoyote. Lazaro ametajwa kwa sababu alimjua Mungu na kuwa na mahusiano na Mungu. Maisha ya  wokovu ni kukua  kutoka hapo ulipo na kwenda hatua nyingine. Maisha ya kila siku kama hayajabadilika ndiyo maana hata wewe hujabadilika‼
 
Mungu huangalia kile unachokihitaji wewe. Ndiyo maana Mungu maeiweka siku  ya hukumu,  kwa ajili ya kutuhukumu kwa matendo yetu.
 
WAFILIPI 3:8..[Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;]… Paulo aliyaacha yote ya kumfanya asiwe na uhusiano na Mungu ,  na kuyahesabu kama hasara /  mavi kwake. Paulo ndani yake alikuwa na shauku  ya kutengeneza uhsiano na Mungu wake. Wapo watu wanatengenza mahusiano na kanisa au mchungaji kiongozi, na kuacha kuweka mahusiano na Mungu ambaye mwishowe kwake watatolea hesabu mbele zao zake. Shida ya watu ni kusahau kuwa, tunawajibika kwa Mungu mbinguni.  Je, Mungu anakuona wewe kama nani?  
 
Uhusiano wako na Mungu kama una kasoro, amka usingizini na kuweka mahsuaino mazuri na Mungu‼ Hivi mimi na Mungu tunashauriana? Kanisa haliwezi kukua na watu wanafiki, bali na wale walioamua ndani kuwa na Yesu Kristo. Siyo muda wa kufumbia  macho dhambi.  Kanisa linaanzia nyumbani, na maisha ya kila siku yapaswa yakuelezee jinsi ulivyo.  Ili uweze kuwa wa thamani kwa Mungu, tengeneza uhusiano wako na Mungu. Fanya mazoezi ya kuwa na Mungu ndanimwako. Yesu Kristo akae ndani yako.Wokovu wako uwe  wa kila saa na kila dakika. 
 
Unajua kuna vitu  vingine vinatupata kwa sababu ya kutotengeneza mahusiano yetu naMungu? Ukristo unakoelekea kwa sasa ni kubaya. Wokovu unakoelekea kwa sasa ni kwenye kuwa “DINI”.  Hii ni  kwa sababu hakuna mabadiliko ya ndani. Mtu alikuwa mwizi anaacha kuiba. Mtu alikuwa kahaba anaacha ukahaba. Leo hii wote hawa na tabia zao wanakuja kanisani nakutoa sadaka zao wakiwa na tabia zile zile. Hii ni kwa sababu watu wanapenda kumfurahisha mchungaji kiongozi badala ya kumpendezesha Mungu.
 
Biblia inasema “Usimpe ibilisi nafasi.” Lakni  je, hii nafasi tunampa je shetani? Ni kwa sababu hatutaki kutengeneza mahusiano na Mungu. Kwani Mungu wako ni  wa wakati wa kuumwa tu? Mungu wako ni  wa ndani kwa ndani tu?  Hapana. Ifike mahali watu wakikuona wamuone Mungu  unayemtumikia.  Inafaa kila mahali  tunapotembea Mungu wetu adhihirishwe. Ndiyo maana Biblia ikasema,  mtoto Yesu akakua katika kummjua Mungu  na kuwapendezesha wanadamu.
 
2 PETRO 1:2-3…[Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. 3 Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.]… Nikianza mimi kumjua Mungu  ananikirimia ili  kupata vyote. Kuna vitu unavishikilia ambavyo kwa Mungu ni dhambi, na hivyo huwezi kusaidiwa na Mungu kwa kujichanganya changanya. Kumbuka aliyewaokoa wana wa Israeli,  ni huyo huyo aliyewaangamiza Wamisri.
 
Shetani ana uwezo wa kukujengea ukuta kiasi kwamba kuomba kwako kukashindikana. Mtu wa aina hii, ni mzuri sana katika kusoma magazeti ya udaku au 'kucheza games' katika simu lakini kuomba Mungu hayupo tayari. Mchana wa leo, tunaenda kuvunja kila  uzio ambao adui amekuwekea ili kusababisha kukosekana kwa kiu ya maombi. Leo tutamuomba Bwana atupe kiu ya kujifunza neno la Mungu,  na kiu ya kusikiliza neno  la Mungu.
 
Kila kitu ukifanyapo huanzia ndani. Endapo  ndani  kukitaa, huwezi kufanya lolote. Shetani hupenda kuleta mawazo ya kukataa kufanya maombi. Hii  ni kufanya mahusiano yako na Mungu yasiwepo. Tumejifunza kuwa, ukimjua Bwana unapata vyote. Maisha yako yatabadilika  pindi tu  mtu akijenga mahusiano haya na Mungu.
 
 Kama  mtu uliyepo hapa hujaokoka, na kumwamini  Yesu Kristo kuwa  Bwana na Mwokozi wako, leo ndiyo  fursa ua kufanya hivyo. Na hata kama uliwahi kuokoka na baadae kuacha wokovyi, leo pia ni vizuri kufanya maamuzi upya na kugeuka ili  kuanza upya na Bwana Yesu.
 
UKIRI
Leo ninasambaratisha kila mashetani  walionizuia, kila mashetani mliokaa ili kunifunga,  kila  waliotumwa ili kunifunga ili  nisitengeneze mahusiano ya kudumu na Mungu leo nawasambaratisha Kwa Jina la Yesu Kristo. Amen
 
 
=== © Information Ministry ===
(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
 /or
Contact our Church Leadreship:
 Bishop Dr. Godson Issa Zacharia
 (Glory of Christ (Tanzania) Church in Morogoro)
Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545
Share:

Monday, August 24, 2015

SOMO: HATARI ZA MAISHA


JUMAPILI:  23 AUGUST 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 
Na:     BRYSON LEMA (RP)        &

Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)

 

Utangulizi: Paulo alikuwa anamwamini Bwana Yesu kama na wewe unavyomuamini. Paulo alikuwa mwanadamu kama wewe ulivyo. Hata hivyo iliifika wakati ambapo alijiuliza swali, kama ambavyo imeandikwa katika  1KORINTHO 15:30…[Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa?]…Ndani ya maisha kuna hatari. Kama wewe hadi leo hujaweza kujua kwa nini unakuwa hatarini, hutaweza kufanikiwa. Hayupo aliyeyaongea mambo ya  maisha kama Paulo (Mfano aliongelea jela, njaa, dhiki n.k.). Paulo  anapoongelea hatari ni kwa sababu yeye pia ni mtu wa hatari. Hauwezi kushinda kama haupo tayari kupitia shida, hatari na magumu ya maisha.

 

Kwa macho tu ni mbaya sana kuangalia hatari za maisha.Lakini baada ya hatari ujue yapo mafanikio. Yeremia naye aliliona hili. Imeandikwa katika MAOMBOLEZO 5:9…[Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.]…. Hatari zipo kila siku kwa sababu hakuna aliye tayari kukuona wewe unafanikiwa na kusonga mbele. Mafanikio ya mwanadamu wa leo ni ya yule aliye tayari kuingia katika hatari. Hii ni kwa sababu kile ninachotaka kukipata, ni lazima nijihatarishe.

 

Shetani anakuona wewe ni hatari pale unapoanza kudai afya yako, watoto wako, uponyaji wako, mali zako n.k.  Ni rahisi sana kumtia moyo "mtu anayetoa uhshuhuda wake" kwa kumwambia hongera, lakini unasahau kumuuliza siri ya mafanikio yake.  Ndiyo maana Biblia inasema kuwa Eliya alisema “mvua haitanyesha ila kwa neno langu” na ikawa hivyo. Ukisoma katika Agano Jipya, Biblia inasema “Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi akaomba kwa bidiii na mvua haikunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu”. Daudi hakuvumilia kumuona Goliath akilitukana Jina la Bwana. Kwa siku moja tu, Daudi alimsikia Goliath akitukana na kuchukua hatua kwenye ile hatari, wakati wale Israeli walimsikia Goliath akitukana kwa siku zote 40 mfululizo bila wao kuchukua hatua yoyote, kwa kuogopa hatari.

 

Hatari zipo, lakini kuna baraka katika hizo hatari. Kuna kujiingiza katika hatari ili uweze kutoka hapo ulipo. Kumbuka Samsoni alimuua simba, Na baada ya siku ile Samsoni alijipatia asali ndani ya mzoga wa simba yule yule.

 

KUTOKA 13:18-21…[ lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. 19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi. 20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa. 21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ]…. Hapo ulipo unatakiwa  kutoka na kuufuata ushindi wako pale ulipo. Nyakati zingine watu hawajui njia za kulibeba andiko na kulifanya liwe  lao. Wana wa Israeli hawakupigana wakiwa Kanaani. Wana wa Israeli walipokuwa Kanaani, hawakupigana na badala yake waliuzunguka ukuta wa Yeriko.Walipokuwa nyikani, Wana wa Israeli walipambana na Mfalme Ogu, na baada ya kumuua waliweza kusonga mbele.  Wakiwa nyikani walipambana na nyoka wa jangwani na ili kupona, iliwabidi waingalie sanamu ya nyoka wa shaba‼‼

 

Unapojiona wewe ni mgonjwa, ujue una tatizo. Kila ugonjwa una chanzo chake. Kila tatizo pia kwenye maisha yako lina mwanzilishi aliyelileta hilo tatizo.

 

1 SAMWELI 14:1-10…[Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye. 2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita; 3 na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. 4 Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene. 5 Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba. 6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache. 7 Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. 8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao. 9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie. 10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana Bwana amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu.]… Yonathani anatukumbusha kuwa hakuna cha kumzuia Bwana kutenda;  Iwe ni  kwa wengi au  kwa wachache. Yonathani alikuwa anaijua ishara na sauti ya watu waoga.

 

Kila anayeingia katika safari yangu lazima apigwe nyundo. Haijalishi huyu mzuiaji ni  nani!!!. Yesu Kristo alikuwa na uhakika wa kufika ng’ambo ya Bahari,  na ndiyo maana alilala usingizi wakati ule merikebu inapigwa na mawimbi kona zote.  Leo hii tunamsoma Goliath kwa sababu ya Daudi. Mwisho wa Kitabu cha Samweli, Biblia inawataja mashujaa 320 wa Daudi ambao ni wale watu waliokuwa na madeni, wenye dhiki na kila aina ya adha.

 

UKIRI
Baba Mungu, leo nakataa kurudi nyuma, nakataa vitisho vya adui zangu, kila mamlaka za giza zinazokaa ili kunitisha, leo nazisambaratisha kwa Jina la Yesu. Ewe adui uliyesababisha vita hii, nakufuata, wewe na wajumbe wako na kila  mtu aliyekaa na wewe. Leo nafanya vita na kila vuruugu, kila adui na ninaanza kuwapiga kwa Jina la Yesu, mliokaa ili kuniletea vita leo nawasha moto  kwa Jina la Yesu. Amen.

 

Usioogope aliyekupiga vita au kusimama mbele yako. Kama upo na hujaokoka kwa kumpokea Yesu Kristo maishani mwako,leo ni fursa muhimu  ya kumwamini Yesu Kristo ili  aweze kukushindia yote.

 

=== © Information Ministry ===

(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Church Leadreship:

 Bishop Dr. Godson Issa Zacharia

 (Glory of Christ (Tanzania) Church in Morogoro)

Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545.

 
Share:

Monday, August 17, 2015

SOMO: ROHO YA DHULUMA

JUMAPILI:  16 AUGUST 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 
Na:     BRYSON LEMA (RP)        &

Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)
 

Utangulizi: Imeandikwa katika MITHALI 13:23…[Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini;  Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.].. Biblia inasema chakula kipo kingi kwa mkulima lakini vipo viharibuvyo. Leo unafanya kazi zako kwa nguvu kubwa lakini matokeo ya kile ulichofanya hayaji kama ulivyotegemea kwa sababu wapo wanaokudhulumu. Adui zako kila kukicha wanaangalia ni jinsi gani wanaweza kukudhulumu, na ndio maana maisha yako hayawezi kwenda vizuri na kile unachokitegema huwezi kukipata kwa sababu adui ambaye ni “roho ya dhuluma” anataka uharibiwe.

 

MWANZO 6:11…[Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.]…Biblia inasema kuwa “Dunia ikaharibika, na dunia ikajaa dhuluma” na kila mwenye mwili amejiharibia njia yake. Hapa Mungu aliona dunia imeharibika maana binadamu wamejaa dhuluma na hawawazi kujitafutia vya kwao bali wamekaa ili wakuharibie na kukudhulumu, lakini leo tutawapiga kwa Jina la Yesu.

 

Maisha tunayoishi leo si kama tunavyofanya kazi, kwa sababu hiyo maisha yetu yanakuwa magumu kila siku.Tumefanya mambo mengi kwa bidii lakini tumepokea tofauti maana matokeo yamekuwa madogo maana yupo adui anayefanana na mchwa maana anasubiri uwekeze yeye aharibu.



Inawezekana umeomba Mungu uongezewe mshahara, lakini baada ya kipato kuongezeka ndipo unaona matatizo mapya yanakuja maana yupo adui wa kukudhulumu ambaye anaamka maskini na jioni anakuwa tajiri. Hii dunia imejazwa na dhuluma maana msingi wa Shetani katika dunia amejenga katika kudhulumu, maana yeye Shetani yupo kwa ajili ya kuharibu, kuchinja na kuiba.

 

ZABURI 55:1-8…[Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.2 Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua.3 Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi.4 Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia.5 Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.6 Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.7 Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.8 Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.]… Tunaona Daudi anamwendea Mungu kwa kuomba maana aliiona dunia kwa wakati wake imejaa dhuluma. Kwa sababu ya dhuluma hii Daudi akasema hofu ya mauti imemzunguka maana yake wako tayari kumwua. Daudi kutokana na kudhulumiwa akaona kama angekuwa na mabawa angeruka kama tai aende mbali ili asikae karibu na wale wanaotaka kumdhulumu.

 

Tunaona tatizo la Daudi lilianza pale alipopakwa mafuta. Na matatizo hayo yalianza kwa kasi, na yalianza mara alipomwua Goliathi na hapo ndipo mfalme akataka kumwua Daudi, badala ya kumsifia Daudi kwa kitendo chake cha kumsaidia mfalme kumwua Goliathi. Inawezekana hata wewe kwenye maisha yako kutokana na bidii yako kazini, bosi wako badala ya kukusifu kwa uchapakazi wako lakini badala yake atainua vita juu yako maana anakuwa anahisi labda utachukua nafasi yake. Unapoonekana una bidii tayari wanaanza kukufuatilia na vita inaanza maana wameona kitu ndani yako. Lakini mtu aliye mvivu hutaona akifuatiliwa wala kuinuliwa vita. Huu ni mwaka wa kumiliki, kutiisha na kutawala, hivyo ni lazima kuwapiga wanaokudhulumu na lazima warudishe vitu  vyote walivyo viiba. Inawezekana umeibiwa afya, kazi, ndoa n.k, vitu hivi unaweza kudhulumiwa kwa sababu wanaweza kukuwekea afya, kazi au ndoa bandia.

 

Kwa kadiri dunia inavyoongeza maarifa na Shetani naye anaongeza maarifa. Na hivyo dunia hii inahitaji wapambanaji wanaosema hapana sikubali. Saa imefika ukakatae hayo magonjwa na matatizo ya kwamba hapana mimi sikuumbwa hivyo. Wapo walioibiwa akili na watoto wamekuwa wa kifeli mitihani.

 

ZABURI 55:9-14…[Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.10 Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake;11 Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.12 Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione.13 Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.14 Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.]…  Daudi hakuachia pale akasema anayeniletea dhuluma ni rafiki yangu sana ambaye tulipeana ushauri na tuliingia nyumbani mwa Mungu pamoja. Ina maana kwamba hadi kanisani wapo wanaodhulumu. Kanisani pamefika mahala kuwa si mahali pa watu kujengwa bali watu kulalamika.

 

Saa ndio hii kanisa la kweli lionekane nalo litaonekana kama wewe utasimama na kumpiga adhulumuye. Kanisani hatuji kwa ajili ya kuombewa bali ili Mungu atusaidie. Unapoenda kanisani ni lazima kanisa likufanye ubadilike. Kanisa linaanza na wewe mwenyewe na si mtu mwingine hivyo ni lazima umpige yule akudhulumuye. Wapo watu waliodhulumiwa kwenye akili, unaweza ukamwona kama mtu lakini ndani amewekewa akili ya mnyama. Ni afadhali ukutane na Simba usiku unaweza ukamkwepa, lakini si kukutana na binadamu wakati wa usiku.  Ndio maana tuona watu wameweka mbwa katika nyumba zao ili kujilinda na wanadamu. Utaona wapo watu wanaoweza kujilipua wenyewe ili kuwadhuru wengine, uwe na uhakika watu hao ndani yao si watu bali ni kitu kingine.

 

Jambo lolote unaloliona limetokea ujue ipo nguvu ya rohoni iliyosababisha jambo hilo kutokea. Dunia inapoelekea ni kwenye hatari na hivyo ni lazima uamke usingizini maana Shetani anataka kuleta madhara makubwa katika kudhulumu. Mfano tunaona ipo ndege ambayo ilianguka na hata unywele mmoja haukoonekana,” HII HAIWEZEKANI”. Shetani hapa alipofika hatuwezi kumwondoa kwa ibada ya siku moja bali inatupasa kuingia ndani sana na kuweza kumpiga. Ni muhimu uwe mtu wa kufanya ibada si kanisani tu bali hadi nyumbani. Na hii ni Saa ya Ufufuo na Uzima duniani ni saa ya kupeleka msingi mwingine katika dunia hii, ni saa ya kuvunja vunja nguvu za Shetani. Saa imefika na saa ndio hii kanisa limeinuka na misingi imeiunuka, ni saa yako ya kuinuka na ni saa ya waganga wa kienyiji kuondoka Tanzania. Ni saa ya kila kilichoibiwa kurudishwa. Acha kupewa moyo na amani tuliyonayo, amani hii ni utumwa na hivyo ni lazima tupigane safari hii. Ni saa ya kuangusha misingi ya uovu.  Hatuikubali hiyo amani maana wanakula wengine. Je! Amani hiyo ipo wapi?

 

Unapookoka ndiyo kazi inaanza maana ndipo watu wanainuka kukupinga. Lakini ukiokoka na kustarehe hutaona ukipingwa.Unapoona nyumba imejengwa ujue umechimbwa msingi na nyumba ndio ikasimama. Ukitaka usimame hapo ulipo ni lazima uchimbe umpige Shetani na baada ya hapo hakuna atakaye kupinga nawe utasimama juu. Unapochimba dhahabu kuna jiwe ambalo lazima ulipasue kwa baruti vingenevyo huwezi kupata dhahabu. Hivyo nawe ni lazima umpige Shetani, na usikubali kufarijiwa kwa kuambiwa Bwana atatenda, bali utake Bwana atende.

 

ZABURI 55:21…[Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.]…Mdhulumaji haji kwa ghafla bali anakuotea. Ni saa ya kupambana sikubaliani na vitu vinavyoendelea katika maisha yangu,  nataka mabadiliko, na mabadiliko hayo si ya Taifa nataka mabadiliko yangu.

 

ZABURI 10:15…[Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.]…Anasema aneyekudhulumu mkono wake uvunjwe. Kila mkono ulionyooshwa mahali popote uvunjwe kwa jina la Yesu. Wakuvunja mkono huo ulionyooshwa si mwingine bali ni wewe.

 

ZABURI 55:15…[Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.]..Daudi anasema  wanaokudhulumu mauti iwapate, maana biblia inasema usimwache mwanamke mchawi aishi.

 

Ni lazima uokoke ili uweze kupata kibali cha kuvunja mkono ulionyooshwa juu yako na vitu vyako.

 

=== © Information Ministry ===

(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Church Leadreship:

 Bishop Dr. Godson Issa Zacharia

 (Glory of Christ (Tanzania) Church in Morogoro)

Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545.
Share:

Monday, August 10, 2015

SOMO: WALIOTAKA UAIBIKE WANAAIBIKA WAO


JUMAPILI:  09 AUGUST 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 

Na:   BRYSON LEMA (RP) &
         Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)

 

Utangulizi: Imeandikwa katika YEREMIA 17.18…[Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.] ..Katika maisha ya  kila siku kuna vitu huwa vinaibuka maana kuna watu wanataka wewe uaibike. Kuna watu wamekaa vikao na wanataka wewe uangamie na uende kuzimu, lakini leo hayo maangamizi na hiyo aibu inarudi kwao. Bwana anasema hiyo aibu itapiga kona na kurudi kwao walioituma, maana unaye dereva Yesu Kristo anayeendesha maisha yako. Jehova anasema yeye ndiye dereva anayeendesha maisha yako haijalishi aibu waliyokuwekea maana yeye alikujua toka tumboni mwa mama yako na akakutakasa. Usihofu maana dereva uliyenaye yupo macho halali anazunguka kuangalia adui zako naye anafanya njia mahali pasipo na njia katika maisha yako. Haijalishi  tatizo lako limekaa muda gani na nani aliyelitengeneza maana ninachojua sitaaibika maana imeandikwa “achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe na ategaye mtego utamnasa mwenyewe”. Tunaona Goliathi alipoyatukana majeshi ya BWANA, Daudi alipoenda hakuangalia ni nani, ndipo akasema ni “nani anayeyatukna majeshi ya Bwana”. Ndivyo Bwana anavyosema kwako pia ni nani anayekutukana, ni nani anayekuletea aibu‼.

 

Mungu tunayemtumikia hawezi kukuacha uangamie, lakini mwanadamu anataka uangamie maana anachora michoro ili uangamie na uaibike, lakini tunaye dereva Yesu ambaye atakuongoza. Umefika mahali unaona kila mtu anakupinga na kukuambia kwa nini unaenda kusali mbali, wasichokijua ulikuwa na dereva Yesu aliyekuongoza kuja katika Bonde la Maono, Ufufuo na Uzima. Adui amekaa ili uaibike lakini Bwana anasema hiyo aibu haitakupata. Pamoja nao wamekesha usiku kucha  lakini kila wanachokifanya hakitakupata bali kitawarudia wao na uzao wao, maana maandiko yanasema “Bwana asipolinda mji waulindao waulinda bure”. Umesahau yupo wapi Yule Siseri aliyekuwa na magari ya chuma na yupo wapi mfalme  Ogu ambaye alikuwa ni mtu hodari kuliko wafalme wote lakini wana Waisraeli walimshinda kwa kuwa Ogu alitumainia nguvu zake mwenyewe , wakati wana Waisraeli walimtumainia Mungu, na hivyo wote walishindwa kusimama mbele ya wana Waisraeli. Hivyo usimwogope yule aendaye kwa waganga bali mwogope Mungu (ZABURI 35:1-4).

 

Wakati Daudi hana kitu hakuna aliyemwinukia hata mmoja, lakini baada ya kupakwa mafuta ndipo watu waliinuka juu yake ili kumpinga. Kumbe adui wanainuka juu yako baada ya kuona kitu ndani yako cha thamani kama vile Daudi. Vita ni vingi duniani kwa sababu hakuna mwanadamu anayetaka mwenzake afanikiwe, na ni furaha kwao wanapokuona unaangamia. Wote waliomwita Bwana , Bwana aliwaponya wote, hivyo unapomtumainia Bwana ndipo anapokuponya na aibu walizokuandalia adui zako. Kama vile Modekai alivyowekewa aibu na Naamani lakini Bwana alimtetea na hakuipata aibu hiyo bali ilimrudia Naamani mwenyewe.

 

Ipo vita iliyotengenezwa mbele yako, lakini wakati wao wanasherekea  kwa ajili ya aibu yako ndipo aibu itawarudia wenyewe. Leo  kila aliyeinua aibu juu yako tunamwambia Bwana geuza hiyo aibu iwarudie wenyewe na tunaomba Bwana aigawe vipande vipande kwa kiwango walichokutendea.

 

Unatakiwa ujue yale unayokutana nayo yupo aliyoyaandaa, maana kabla ya kuzaliwaBwana alishakuandalia baraka zako. Lakini adui wameinuka na kukuondelea yale ambayo ulikusudiwa uyapate. Sara alichelewa kupata mtoto hadi  katika umri wa miaka 90 maana huo ndio ulikuwa wakati wake ingawa alishakata tamaa. Hivyo nawe inawezekana sasa ndio wakati wako ingawa umeona umechelewa kupata.

 

Ili aibu isikupate unatakiwa kufanya yafuatayo:-
 
1.      Cha kwanza ni kubadilisha mtazamo wako kwanza.

Kila mtu ana mtazamo wake kwa sababu ya ile imani au jinsi unavyo muona Mungu, jinsi unavyo muona Mungu ndivyo unaweza kupata matokeo. Kama tunavyo muona Shedrack, Meshack na Abgenego walipokaa kwenye moto maana walikuwa wanamjua Mungu wanayemtumikia na kwamba atawaokoa na ni kweli akawaokoa.

 

Uwezo wako wa kumfahamu Mungu ndiyo uwezo wako wa kushinda. Lakini wewe unaliangalia tatizo na unalipima na uwezo wako na kujiona kama sisimizi mbele ya hilo tatizo. Maana unaliona hilo tatizo kama ni kubwa na limezidi na ndio maana miaka yote uko hapo hapo na tatizo halitoki, hivyo ni lazima ubadili mtazamo wako na umwangalie Mungu unayemtumikia. Tunamwona Gideon anapokutana na malaika, malaika anamwambia wewe ni shujaa wakati Gideon alikuwa akijificha kwenye ngano akiwaogopa Wamidiani. Ndivyo ilivyo kwako umekuwa ukijificha kwa ajili ya adui zako na kujiona udhaifu wakati ni shujaa. Gideon hakuombewa bali alibadili mtazamo wake na kujua yeye ni shujaa.

 

Utakapobadilisha mtazamo wako ndipo utaona uwezo wako na kuweza kushinda na pia utaona muujiza wako. Ibrahim hakuamini Mungu alipomwambia atapata mtoto Isaka katika uzee wake, ndipo Mungu akamtoa nje na kumwonesha nyota na kumwabia azihesabu ila akasema ni nyingi mno, ndipoMungu akamwambia huo ndio uzao wako. Kila alipokuwa akiangalia nyota za angani alimwona Isaka na ndio maana hata alipoambiwa amtoe Isaka hakuogopa.

 

Historia ni historia, hivyo usiangalie historia ya nyuma kama kuna makosa uliyafanya, bali iangalie kesho yako kwa kufuta makosa ya nyuma na kusonga mbele ili kuitengeneza kesho ya maisha yako. Ukifanikiwa kugeuza mtazamo ulionao juu ya tatizo ulilo nalo, muelekee Mungu aliye jibu la maisha yako.  Usiogope watu kukuongelea vibaya, bali wanapofanya hivyo na wewe jisifu kwa sababu una nguvu. Ukiona watu wanakusemasema ujue wameisha kuchungulia ndani, wanaona hapo ulipo sio pako wanataka uende sehemu nyingine, lakini hiyo aibu haitakupata maana ni lazima uivuke ng’ambo.

 

Saa imefika yakufanya ile aibu iwarudie wenyewe na saa yenyewe ndio sasa.Unatakiwa usiweke macho yako kumwangalia adui bali mwangalie Mungu maana amesema hata kuacha hadi mwisho wa dahari.  Haijalishi ni nani anaye kushambulia maana wamekaa katika njia yako ili kukuzuia na kukupinga lakini sisi tunaye Mungu mkuu kuliko miungu yote ambaye atawavua mavazi yao ili waaibike maana wanajifanya kama kondoo lakini ndani mwao ni mbwa mwitu.

 

2.      Baada ya kugeuza mtazamo, cha pili usikate tamaa.

Usikate tamaa maana Shetani huwa anacheza na macho yako akipima ukubwa wa tatizo na ukaliona ni kubwa kwa mapana yake. Biblia inasema Shetani ni kama Simba angurumaye, kumbe ni kama Simba lakini siyo Simba, hivyo hutakiwi kumuogopa. Lazima ifike mahali upambane kama kuku wa kienyeji maana kuku wa kienyeji huwa anakufa kishujaa. Inatakiwa uamke usikubali kutishwa, ile aibu waliyokutengezea kwa ajli yako ikawarudie wao wenyewe.

 

=== © Information Ministry ===

(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Church Leadreship:

 Bishop Dr. Godson Issa Zacharia

 (Glory of Christ (Tanzania) Church inMorogoro)

Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545

 
Share:

Monday, August 3, 2015

KADIRI WALIVYONITENDA, NDIVYO NITAWATENDA


JUMAPILI:  02 AUGUST 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 
Na:   BRYSON LEMA (RP) &
         Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)
 

Utangulizi: Wapo Wafilisti waliomuonea Samsoni, kwa kuwa tu walishazoea sana kuwaonea wana wa Israeli, wakiwaona ni wanyonge na wa kawaida, na hivyo wakawafanya wanavyotaka. Kwa kipindi kirefu  hali hii iliendelea, na wana wa Israeli wakaizoea. Hatimaye Mungu  alimweka shujaa mmoja wa familia ya Manoa,  ili aje kuwaokoa watu wake Israeli. Imeandikwa katika WAAMUZI 15:9-11 kwamba...[Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. 10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. 11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.]… Wafilisti wanaonekana kuijua kanuni hii muhimu: “ Ukitendewa  na wewe lazima uwatende”. Ndiyo maana watu wa Yuda walimfuata Samsoni kumuuliza kwa nini amefanya vile alivyofanya, kwa sababu wanajua kuwa na wao watafanyiwa vivyo hivyo‼.  Hata wewe hapo ulipo siyo mpango wa Mungu kupitia kile unachopitia katika maisha yako. Siyo kwamba Mungu alitaka uishi jinsi unavyoishi. Hata vile ulivyo  navyo usiridhike ukadhani ndivyo alivyokusudia Mungu uwe navyo, la hasha‼!  Shetani  ndiye aliyekuja na kukunyang’anya ile hati miliki yako, ili upitie yale unayopitia leo hii au umiliki vile uvimilikivyo  leo hii.

 

Kwa siku ya Leo hatujaja kanisani kwa ajili ya kusali, kama yupo mtu mwenye fikra hizo amekosea‼!. Leo tumekuja kanisani ili kuwatenda wale waliotutenda maishani kwetu. Unapoiona ndoa yako haiko sawa, siyo  kwamba mumeo au mkeo ndiye mbaya. Kuna kitu‼! Unapomuona mwanao hafanyi vizuri darasani pamoja na kumpeleka tuition siku zote, ujue kuna kitu‼! Adui ndiye amekuingizia kitu hicho, na usikubali kusema eti hiki ni kitu cha kawaida katika familia au ukoo wako. Kila kitu kina chanzo  na mwanzo wake. Hakuna ugonjwa ambao utamwelezea daktari  halafu  aseme eti ni ugonjwa mgeni usio kuwa na chanzo chake.

 

Kila unachopambana nacho sasa hivi ujue kina mwanzo wake.  Wana wa Israeli walifahamu kabisa wapo watu wanaopambana nao kila wakati. Ndiyo maana wakamuuliza Mungu swali, kuwa kwa kuwa Yoshua amekufa, ni nani atakayewaongoza kwa ajili  ya kupambana na adui zao? Imeandikwa  WAAMUZI 1:1…[Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?]… Cha msingi  hapa ni kwamba wana wa Israeli  walitambua kuwa wana adui na adui yao ni nani‼ Hata wewe na mimi, kama Mkristo inabidi ufahamu kuwa katika  maisha ya kila siku, lazima uwe tayari kupigana na pia kumjua adui yako ni nani unayepigana naye.

 

Sihitaji kumtafuta adui yangu ni nani‼ Ninachotakiwa kufanya ni kulipiga tatizo, na nikimuona yupo anayelia  papo hapo nitafahamu kuwa ndiye chanzo cha tatizo  langu. Hii ni kwa sababu, ya ile kanuni kuwa ‘ukienda kumfungua punda aliyefungwa, atakayekuja kukuuliza kwa nini unamfungua ujue ndiye mwenye punda’.  Hatuhitaji kuwa kama wapiga ramli.  Sisi  kazi  yetu ni kupiga tatizo na atakayefungua mdomo kulia tutajua ndiye alikuwa mmiliki wa lile tatizo‼!

 

Pamoja na shida iliyosimama mbele yangu, Kanaani tunaingia. Pamoja na ugonjwa uliosimama mbele yangu, Kanaani nitaaingia.  Pamoja na Bahari ya Shamu iliyosimama mbele yangu, Kanaani tunaingia…. Tumechoka kwenda makanisani na kuagwa kwa kuambiwa “Amani ya Bwana iwe nanyi”…. Lakini hata hivyo, ukutanapo njiani na mganga wa kienyeji atakuwa anakucheka. Kwa nini? Kwa sababu huyo mganga wa kienyeji amefanikiwa kukuchezea usiku kucha, na hivyo amani uliyopewa kanisani hauna. Je, ni nani  mbabe kati yenu wawili? Ni dhahiri mbabe ni huyo mganga wa kienyeji. Inafaa ifike wakati ambapo hata mganga wa kienyeji awe anakiri mbele za watu kuwa “Mungu  unayemtumikia siyoMungu  wa kawaida‼” Leo ni siku ya kupambana na wale waliotutenda, nasi tuwatende vivyo hivyo.

 

Leo tumejipanga kupambana na adui yetu katika maeneo matatu:

1.      Kwanza ni  AFYA, kwa kuwa adui  anajua kuwa mwili wako ukiwa mgonjwa, hauwezi kupigana. Magonjwa siyo mpango wa Mungu. Kila ugonjwa umetengenezwa na shetani kuzimu. Lazima umnyang’anye shetani afya yako asiimiliki. Wapo wanaopata mishahara yao tena mikubwa tu, lakini  yote huishia kwenye matibabu  ya watu wa nyumbani mwao. Unaposikia  CHUMA ULETE,  siyo rahisi kuelezea kwa jinsi ambavyo magonjwa ya kutengenezwa yanapotokea, na kusababsiha fedha iishie kwenye matibabu‼‼. Shetani hana mamlaka ya kufunga kule mbinguni, ila uwezo wake ni wa kukufunga hapa duniani tu. Hata hivyo wewe unayo mamlaka  ya kufunga mambo yote ya shetani hapa duniani na hata mbinguni yawe  yamefungwa vivyo hivyo. Imeandikwa katika 2WAKORINTHO 10:4-5… [(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;]… Tunayo mamlaka ya kuangusha kila kazi za kishetani zipate kumtii Kristo.

 

UKIRI
Kila kiwanda cha kutengeneza magonjwa, leo  nakiunguza kwa Damu Ya Yesu. Kila  adui anayetaka kurudisha kiwanda hiki namtangazia kifo kwa Jina la Yesu. Amen

 

2.      Sehemu ya PILI ambayo shetani hufuatilia maisha ya watu ni  katika MAFANIKIO. Wapo watu wasiopendelea kuona mafanikio yako. Imeandikwa katika KUMBUKUMBU 4:40…[ Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.]…. Ni mpango wa Mungu ufanikiwe, wewe na uzao wako. Shetani kazi yake ni  kuzuia mpango wa Mungu usifike. Leo ni siku ya kudai chako, na vile  vya kwao, pia tunavidai view vyetu kwa Jina la Yesu‼‼ Wale walioiba kipato chako kwa muda wa kutosha, leo ni  siku  ya kuwafanya kama walivyokufanya wewe. Leo tunawagusa tu waliotugusa, ambao  hawajatugusa leo hatuwagusi kamwe kwa Jina la Yesu.

 

Mungu  alisema “Ahabu lazima afe”.  Hata hivyo, Ahabu aligoma akasema hatakufa. Walipoenda vitani, Ahabu alitumia ujanja/hila kwa kuyavua mavazi yake ya ufalme, na kumvisha Yehoshafati.  Wakiwa vitani, askari walikuwa wameagizwa wamtafute mfalme  Ahabu pekee na kumuua. Hata hivyo, Yehoshafati hakujua kitendo cha kuvaa mavazi ya Ahabu kingemfanya awindwe na kufa vitani. Walipomfuata Yehoshafati wamuue, ilibidi Yehoshafati apige kelele aseme yeye siye Ahabu. hata hivyo, Kijana mrusha mshale, alifanikiwa kuurusha mshale angani,  na ulipokuwa unarudi ili kutua ardhini ulienda moja kwa moja kumtafuta Ahabu alipo na kumuua‼‼! Hii ni saa ya kurudishiwa vilivyo vyetu.  Tena Biblia  inasema mwizi akikamatwa, atarejesha mara saba.

 

UKIRI
Ninakivunja kiwanda cha umaskini, Kwa Damu  ya  Mwanakondoo. Leo najiondoa kwenye orodha ya  maskini wa Taifa hili  Kwa Damu  ya  Mwanakondoo. Kwa Jina la  Yesu, leo naushika mshale,  maana imeandikwa Elisha alipokuwa anaumwa, Yehoashi mfalme wa Israeli akamwendea, naye Elisha akamwambia “Rusha mshale, na unapourusha sema hivi ‘Mshale wa Bwana, Mshale wa Kushinda” (2 Wafalme 13:14-19)…. na mimi  leo natangaza mshale wa Bwana mshale  wa kushinda. Na mimi leo naachia mshale wa kuangamiza kila kiwanda cha umaskini, leo nakishambulia kiwanda cha umaskini kwa Jina la Yesu. Ewe adui mwenye kiwanda nakutangazia kuwa sitakuwa maskini kamwe Kwa Damu  ya  Mwanakondoo.  Amen.

 

3.      Eneo la TATU la kushughulikia ni kwenye VIFUNGO,  ambavyo kwavyo  unakuwa unavipitia bila kujua. Maisha yanakwenda kwa ugumu kwa sababu ya vifungo maishani mwako. Hata Lazaro baada ya kufufuka, Biblia inasema alikuwa  amefungwa miguu yake na leso usoni mwake. Maana yake ni  kuwa,  unaweza kweli kuwa umeokoka,  lakini kumbe umefungwa na hivyo  maisha unayopitia ni ya ugumu ugumu tu. Leo ni siku ya kuwafanya kama walivyotufanya sisi. Kila aliyenifunga,  nami namfunga. Imeandikwa, “Nitakachounga hapa duniani na mbinguni kitakuwa kimefungwa

 

UKIRI
Kwa Damu Ya Yesu, leo nafanya  vita kukata kila kamba iliyonifunga viungo  vyangu  vya mwili. Ewe adui uliyenifunga leo nakuteketeza kwa moto wa Damu ya Mwanakondoo. Kuanzia sasa, nimetoka mautini naingia uzimani kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

Zipo sababu ambazo waganga wa kienyeji na wachawi huzitumia ili kufanikisha mambo yao ya kuwatenda watu wengine kaatika maisha. Mojawapo ni hizi sababu zilizoandikwa katika MALAKI 3:7…[Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi,  nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? ]… Mtu yeyote anayeampenda Yesu lazima akimbilie kwa Yesu. Huwezi kumtenda adui yako kama alivyokutenda kama hujamrudia Bwana  Yesu. Leo tunataka tumrudie Bwana Yesu ili tuweze  kuwapiga wale waliotuonea.

 

Pia imeandikwa katika MALAKI 3:8-9….[Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. ]… Kumbe  kitendo cha kumuibia Mungu kinaitwa ‘laana’.  Sasa ili  kuziepuka laana hizi, kila mmoja wetu anatakiwa  kulipa zaka na dhabihu zote kwa Bwana.

 

Kumtolea Mungu zaka na dhabihu ni njia mojawapo ya kumfanya shetani akose uthibitisho wa kukushtaki au  kukulaani.  Imeandikwa katika MALAKI 3:10-12…[Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi. 12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.]… Zaka ni kodi ya Mungu. Chakula katika nyumba ya Bwana siyo ubwabwa, ila ni neno la Mungu. Hivyo  kwa kutoa zaka, ni ili kuwezesha neno  la Bwana liweze kuhubiriwa kila mahali.

 

Kwa wewe ambaye hujaokoka, leo ni fursa muhimu sana kufanya maamuzi hayo ili uweze kuwatenda wale waliyotenda mabaya maishani mwako.

 

KWA SIKU TANO ZOTE WIKI NZIMA TUTAFUNGA NA KUOMBA

ILI KUWATENDA ADUI ZETU SAWASAWA NA WALIVYOTUTENDA SISI.

 

=== © Information Ministry ===

(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Church Leadreship:

 Bishop Dr. Godson Issa Zacharia

 (Glory of Christ (Tanzania) Church in Morogoro)

Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545
Share:
Powered by Blogger.

Pages