Pages

Sunday, September 24, 2017

MANENO YAKO YANATAWALA MAISHA YAKO

GLORY OF CHRIST TANZAN IA CHURCH (GCTC)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA – MOROGORO

JUMAPILI: 24 SEPTEMBA, 2017

MHUBIRI: Mchungaji, Happiness Mhimbula (Rp)

Utangulizi.
Tunajifunza ya kwamba hakuna kinachoweza kutokea isipokuwa kimetamkwa mahali. kila kinachotokea leo kimeanzia kwenye ulimwengu wa roho na hatimaye kudhihirika kwenye ulimwengu wa mwili.Kwa hiyo kinywa chako ndio kimebeba uzima au mauti juu ya maisha yako. angalia sana kile unachokisema iko siku kitatokea aidha ni kizuri au kibaya. Maisha unayoishi leo ni matokeo ya maneno uliyoyatamka jana.
Mchungaji Mwandamizi Happiness Mhimbula akifundisha neno la Mungu katika ibada ya leo.
 Mithali 6:2 Imeandikwa, “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako.” Kumbe maneno ya kinywa chako yanaweza kukutega na kukukamata. Mtu kwa asili ni wa rohoni. Kwa hiyo unaweza kutumia maneno yako kuumba mema au mabaya juu ya maisha yako. Ulimwengu wa roho ni mpana sana na ni vigumu sana kuuelezea. Ndio maana Mungu alikuwa katika ulimwengu wa roho kutokea uko alitamka na vitu vikatokea. Kumbe kwa asili sisi ni waumbaji kwa vinywa vyetu. Jifunze kuongea neno la Mungu ambalo ndio silaha za uumbaji. Yale unayoyatamka ndio yanayotokea. Mtu aliyeokoka kwa Mungu wewe ni muumbaji. Unaweza kutumia neno la Mungu kuiumba kesho yako. Neno la Mungu ni roho linaloweza kuleta madhara kwenye ulimwengu wa mwili. Kile unachokiongea ndio kinatokea katika maisha yako.

Yakobo 3:3-9 Imeandikwa, “Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. 4 Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha. 5 Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. 6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. 7 Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. 8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. 9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu”. 

Baadhi ya maelfu ya wana wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakisikiliza neno la Mungu kwa makini.
Mtume Paulo anasema ulimi ni kiungo kidogo lakini unaweza kuongoza maisha yako. Ni kwa ulimi wako unaweza kwenda uzima au mauti. Ni lazima ujifunze kuuzuia ulimi wako kunena mabaya. Zingatia ni yapi unayoyatamka. Ishi kwa neno la Mungu. Kuna umuhimu wa kujifunza namna ya kutamka katika maisha yako. Mtu akitumia ulimi wake vibaya madhara yake ni mabaya. Lazima ulijaze neno la Mungu ndani ya moyo wako. Maana likiwemo neno la Mungu ndani yako ndilo utakalonena daima. Kuna mtu amejaa hofu na mashaka na anaishi katika hofu kwa sababu ya kinywa chake. Kila neno unaloliongea lina malaika wa kulitekeleza. Wako malaika wa Mungu kutekeleza mema unayoyatamka. Lakini pia wako mashetani amabao wamesubili unene mabaya ili wayatekeleze. Jifunze kwa Yesu maana aliishi kwa Imeandikwa. Neno Imeandikwa alilitumia Yesu kuonyesha namna ya kutumia neno la Mungu kama silaha. Nena ushindi nyakati zote bila kujali mazingira yanayokuzunguka.

Kumbe ulimi umejaa sumu iletayo mauti. Hapa tunajifunza kutoka kwa mtume Paulo kwamba Ulimi huu umejaa Uzima kwa jina la Yesu. Mithali 4:21 Imeandikwa, “Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako”. kumbe afya yako inategemea na neno la Mungu ndani ya moyo wako. Penye ugonjwa, balaa, shida wewe tamka uzima kwa jina la Yesu. Ayubu 38:12-13 Imeandikwa,“Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? 13 Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung'utwe wakawe mbali nayo” Lazima uongee na asubuhi yako. Baraka zako za siku zinategemea sana ulinena nini wakati wa maombi yako asubuhi. Mungu alijua kwamba wako wanaopanga mabaya juu ya maisha yako. Ni kwa kinywa chako umepewa mamlaka ya kuyapindua mabaya kwa jina la Yesu. Zaburi 119: 97-99 Imeandikwa, “Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.98 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote. 99 Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.” Ukiyashika mausia ya Bwana unaweza kutenda zaidi ya mawazo ya wanadamu. 
Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu katika ibada ya leo.

Neno linapozungumzwa ni kama unapoteza lakini neno la Mungu linakaa katika ulimwengu wa roho ili kutenda kazi. Mathayo 12: 34-36 Imeandikwa, “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. 35 Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. 36 Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu”. Tunajifunza kwamba yale unayoyatamka ndio yaliyoujaza moyo wako. Kumbe hata hukumu yetu inategemea ni kipi ambacho tumenena wakati wa uhai wetu. Ni mengi tumeongea ambayo yanasababisha chuki, karaha, mafarakano na kukatisha tamaa. Lazima tutubu ili neema ya Mungu itusaidie kutengwa mbali na hukumu ya maneno yetu. Maisha yetu yanategemea sana yapi unanena.
Mithali 15:4 Imeandikwa, “Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo,” Mithali12:8 Imeandikwa “Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa,” Mithali 18:21 Imeandikwa, “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;” Na wao waupendao watakula matunda yake. Kile unachokiri ndicho kinachokupata. Neno la Mungu ni roho tena ni uzima. Kama umekwama mahali, umetingwa na jambo, unaugua wewe tamka au jinenee uzima juu yako. Tumia Damu ya mwanakondoo mara nyingi na hatimaye utaona matokeo ya maombi yako. Kile ulichokitamka ndicho utakachokiishi. 

1Petro 3:10 Imeandikwa “Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila,” Kuna balaa na mikosi maishani mwako kwa sababu ya mabaya uliyoyanena. Kumbe maisha mema yanategemea mazuri uliyonena. Kinywa chako kimebeba uzima wako. Ufundishe ulimi wako kunena mema, weka malaika wa kulinda kinywa chako ili useme yatakayoleta uzima juu yako. Jifunze kwa mtumishi wa Mungu Daudi, mtu aliyekuwa mchunga kondoo za baba yake. Mtu huyu alikuwa amejaza neno la Bwana. Ni kwa neno la Mungu Daudi alimpiga Goliati aliyekuwa mtesi wa kabila la Israeli. Tumia neno la Mungu kuumba uzima juu yako. 
Showers of Glory Morogoro wakisifu na kucheza mbele za Bwana katika ibada ya leo.
Ebrania 11:3 Imeandikwa, “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.” Jifunze kuumba kesho yako kwa maneno katika ulimwengu wa roho. Anza kuchora ramani ya nyumba yako, anza kutamka mambo makubwa na ndivyo itakavyokuwa. Tengeneza mambo yako kutokea ulimwengu wa roho ili uyapokee katika ulimwengu wa mwili.
Mwanzo1:3,6,9,11,20,24 Imeandikwa, “Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.6 Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. . 9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. 11 Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. 20 Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. 24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.” Tunajifunza kutoka kwa Mungu maana aliumba kwa neno. Kumbe kile unachokisema kinatokea, hujapata kwa sababu hujatamka. Kumbe kila kiumbe kinaweza kuitii sauti yako kwa jina la Yesu. Katika Mwanzo sura ya kwanza tunaona kwa ujumla kwamba Mungu aliumba kwa kusema.


Mchungaji Happiness Mhimbula akimfungua mtu kutoka kifungo cha maneno.
Hesabu 14:26-28 Imeandikwa, “Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 27 Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo. 28 Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;” Mungu anasubili useme ili athibitishe kile unachotaka. Mungu hapendi manunguniko na malalamiko. Ndio maana Mungu akwaambia nitawatendea kama nilivyowasikia mnasema. Tamka mema ili Mungu ayatimize kwako. Kumbukumbu la Torati 30:19 Imeandikwa, “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Kumbe ukichagua uzima utapokea uhai na mauti itakuwa mbali na wewe.