Pages

Sunday, November 5, 2017

KUNG’OA ROHO YA KUPATA NA KUPOTEZA

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI: 5, NOVEMBA, 2017.

MHUBIRI:MCHUNGAJI, Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha neno la Mungu kuhusu Roho ya kupata na kupoteza wakati wa Ibada ya Leo.

Yeremia 1:10 imeandikwa, “angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Mungu amekuweka leo juu ya mataifa ili kubomoa na kuharibu. Mungu amekuweka juu ya kazi, elimu, shamba, ofisi na miradi yako ili ubomoe na kuharibu kazi za ibilisi. Kuna roho inaweza kupandwa juu ya mtu ambayo ikimpata mtu, kila akipata kitu lazima apoteze. Waweza kupata mtaji, nyumba, mchumba au ndoa ikavunjika baada ya miaka mitatu. Hii ndio tunaita roho ya kupata na kupoteza. Mathayo 15:13Imeandikwa, “Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia,Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.” Yawezekana ni kwenye kazi, shamba, familia, biashara au uchumi kuna pando ambalo halikutoka kwa Mungu. ndipo Yesu akasema kila pando ambalo halikupandwa na Baba yangu wa mbinguni lazima ling’olewe.

Mapando mengi huwa yanapandwa wakati mtu amelala. Unaweza kupandiwa roho ya uvivu, magonjwa ya kila namna, uvimbe, utasa, umasikini. Mapando haya kwa kuwa hayatokani na Mungu, lazima uyang’oe kwa jina la Yesu. Ukiyang’oa mapando haya lazima maisha yako yatabadilika. Ayubu 2:4 – 7 imeandikwa, “Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa” Hapa tunamwona Ayubu akiwa mgonjwa lakini neno linasema shetani amempiga Ayubu na magonjwa. Kumbe kuna vitu vimewapata watu si kwa sababu Mungu amependa bali yamepandwa na shetani. Unaweza kumwona mgonjwa ametajiwa jina refu na dawa isiyopatikana jua hilo ni pando.

Roho ya kupata na kupoteza ni sawasawa kabisa na roho ya mauti au kifo. Roho inayosababisha upoteze kile ulichokipata tena kwa ugumu, au uchungu hiyo inafanana au inalinganishwa na roho ya kifo au mauti. Utasikia watu wanasema, Fulani ametutangulia mbele ya haki, hatukonaye tena, ametutoka au tumempoteza ndugu yetu. Kwa hiyo roho anayesababisha kifo ndio roho yuleyule anayesababisha kifo na mauti. Unakumbuka ulivyopata kazi, uchumba, ndoa, shule au miradi lakini vyote vilipotea. Kumbe shida sio kupata ila kupoteza. Unajua nyumba ulikuwa nayo ikaungua, duka ulikuwa nalo lakini likaliwa, mchumba ulimpata lakini uchumba ukaharibika.
Baadhi ya Makutano wakisikiliza somo wakati wa Ibada.

Kifo sio tukio bali ni roho. Hii ni roho na inaweza kukaa nyumbani, kwenye mradi, dukani, ofisini au kwenye gari. Ufunuo wa Yohana 6:8 Imeandikwa “Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.” Mtu wa Mungu Yohana alionyeshwa roho ya mauti ikiwa kwenye gari. Waebrania 2:14 Imeandikwa, “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,” lakini usiogope maana Yesu alitumwa ili kumwaharibu Yule mwenye nguvu ya mauti. Kumbe unaweza kuwa darasani, nyumbani, kitandani, kwenye gari lakini mauti ipo. Unaweza kupata kazi, mimba, watoto, shule lakini ukapoteza hii ni kwa sababu roho ya mauti/kupata na kupoteza ilikuwepo.

KIFO AU KUPOTEA KABLA YA KUZALIWA. Hivi ni vifo vinavyotokea kabla ya kuzaliwa. Hivi ni vile ambavyo utasikia mama alipata ujauzito lakini mimba ikatoka. Mtu aliitwa kwenye Usaili, ukaitwa kazini lakini wakati umefika ofisini unaambiwa tulikosea kukuita kwa sababu nafasi hii haikuwa yako. Mbaya zaidi unapewa na nauli ya kukurudisha mpaka nyumbani. Mfano, shangazi anaamua kukupa kiwanja kama zawadi kabla hajakukabidhi nyalaka za umiliki shangazi anafariki. Matukio kama haya maana yake iko roho ya kupoteza kabla ya kuzaliwa. Hii ni roho maalum ambayo inapandwa maalum kwa ajili ya kuhakikisha jambo halitokei. Mama amebeba mimba miezi nane lakini kabla ya wiki mbili kujifungua, mtoto anazaliwa akiwa amefariki. Mwingine ameomba kusoma nje ya nchi kwa kufadhiliwa, siku ya kupewa Visa unagongewa mhuri wa KUKATALIWA. Maana yake alikuwepo roho wa kuharibu kabla ya kuzaliwa au kuanza. Lazima uzing’oe roho za kupata na kupoteza.
Platform wakiongoza sifa na kuabudu katika Ibada ya leo.

KIFO WAKATI WA KUZALIWA. Mashetani walikuwa wanakuwinda uharibikiwe kabla ya kuzaa ila kwa maombi yako ukawashinda. Mashetani wataendelea kukufuatilia na kuhakikisha kama ni mtoto anakufa siku ya kuzaliwa. Mama anafanikiwa kujifungua kwa kawaida baada ya muda mtoto anaaza kubadilika ghafla anakufa. Utasikia mama anaambiwa imekuwa bahati mbaya. Wakati wa kuzaliwa inakuwepo timu maalum ya wachawi, waganga na wasihili kuhakikisha kwamba hata kitu kikizaliwa kisiishi. Ulikuwa unatafuta shule au chuo, umepata chuo ila siku ya usajili unajikuta huna nakala halisi za vyeti vyako.
Ufunuo wa Yohana 12:1-4 Imeandikwa, “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.”
Jifunze kuna vifo ambavyo ni roho ya kupata na kupoteza. Shetani anaitwa malaika wa kuzimu kazi yake ni kuharibu wakati mambo yanapoanza. Joka jekundu ni shetani na leo linawakilishwa na wachawi na waganga. Wachawi wanaweza kusababisha kifo wakati wa kujifungua. 1Korintho 10:10 Imeandikwa, “Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.” hapa shetani anaitwa mharabu. Yohana 10:10 Imeandikwa, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” shetani ni mharibifu. Pambana nao kwa jina la Yesu maana imeandikwa Yesu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea.

KIFO BAADA YA KUZALIWA kitu kikianza au mtoto akizaliwa uharibifu unaingia. Hii ni roho inayohakikisha vitu vinakufa wakati wa uchanga. Mfano wakati wa uchanga wa ndoa, elimu, biashara, masomo, mradi au huduma. Ufunuo wa Yohana 12:5-6 Imeandikwa, “Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi. Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini”. Hiki ni kifo wakati wa uchanga. Kwa kawaida kwenye uchanga vitu vinaharibika kwa wepesi sana. Huyu ni mtoto aliyeokolewa wakati wa kuzaliwa lakini shetani anamtafuta wakati wa uchanga. Biashara inapoanza unapewa kusimamia unatoa chenchi bila utaratibu hatimaye mwenye kazi anakufukuza.
Showers of glory wakimsifu Mungu

Ufunuo wa Yohana 12:13 - 15 Imeandikwa, “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo. Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule. Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.” Tunaona Mungu anamwondoa mtoto karibu na shetani lakini nyoka hakukubali. Shetani anamfuatilia na akaachilia maji kama mto. Lakini nchi ikamsaidia mwanamke kwa kumeza maji.

Mfano wa Farao alipopanga kuwauwa watoto wachanga. Hii ilikuwa ni kwa sababu alikuwa anamtafuta Musa ili kumwuua. Ezekieli 29:3 Imeandikwa, “nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.” Kutoka 1:15-17 Imeandikwa, “Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi.

Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.”

Add caption


Mfano wa tatu, Mfalme Herode alitaka kumuua Yesu wakati wa uchanga wake. Mungu akamwotesha Yusufu ili ampeleke Misri. Mathayo 2: 13-15 Imeandikwa, “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”

KIFO AU KUPOTEZA BAADA YA KUIMARIKA. Hii ni roho inavamia vitu wakati mtu ameaza kitu na kimeimalika au kustawika. Yawezekana ndoa imedumu kwa miaka mitatu alafu wanandoa wakaachana au biashara baada ya miaka miwili mtaji unaharibika. Maana yake ipo roho ya kupata na kupoteza. Lazima uamue kuwaondoa wote kwa jina la Yesu.
========== AMEN ========
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro
http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/