Pages

Sunday, August 27, 2017

KUIVUNJA MINYORORO YA UTUMWA

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA ---> MOROGORO}

JUMAPILI: 27 AUGUST 2017

MHUBIRI:  PASTOR GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)


Mchungaji Kiongozi akifundisha neno la Mungu katika ibada ya leo.

Tunaposoma katika YEREMIA 1:8-10 neno la Mungu linasema hivi “Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. 9 Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama,   nimetia maneno yangu kinywani mwako; 10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu,   na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”. Kusudi la Mungu kutuweka hapa duniani ni ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu,   na kuangamiza. Kumbe ipo pia minyororo iliyopo katikati ya maisha yako ambayo kwa wewe uliyeokoka unapaswa kuing'oa, na kuibomoa, na kuiharibu, na kuiangamiza. Minyororo hii ni ile ya rohoni. Minyororo ya rohoni ndiyo inayomfanya mtu kuwa mtumwa, kwamba hana uhuru tena wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Unafungwa rohoni lakini madhara yanathibitika mwilini. Tunajifunza kuwa mtu anaweza kufungwa na minyororo ya rohoni na ambayo kwa bahatimbaya huwa haionekani katika macho ya nyama.
Kwa kawaida minyororo ni kitu kama kamba ambazo ni za chuma, na siyo rahisi kuvunjwa.  Lengo la kutumia minyororo ni ili kumfanya mtu asiweze kufurukuta, kwa sababu ukitaka kujifungua kwa nguvu itakukuumiza. Katika ZABURI 105:17-18 imeandikwa hiviAlimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani. 18 Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.” Kwa hiyo hata Yusufu alifanyiwa mambo hayo, akafungwa na pingu na minyororo miguuni mwake. Na tukumbuke wale waliomfunga Yusufu walikuwa ndugu zake, na wala siyo watu wa mbali.



Platform wakimsifu Mungu katika Ibada ya leo.
Tunasoma pia katika ZABURI 149:8Wawafunge wafalme wao kwa minyororo, Na wakuu wao kwa pingu za chuma.”. Kwa wewe uliyeokoka ni mfalme, na kuna uwezekano  kuwa kuna waliofunga maisha yakjo kwa minororo ili usiweze kupiga hatua za maendeleo maishani mwako. Ingawa minyororo hii haionekani kwa macho ya mwilini, ukifungwa unakuwa mtu usiyeweza kufanya lolote utakalo maishani mwako (inacapacitated). Mwishowe unakuwa na maisha ya kusema “mimi ziwezi kuzaa, siwezi tena kula nyama, siruhusiwi kula vyakula vyenye sukari, siwezi kufanikiwa n.k”. swali la kujiuliiza hapa ni: hivi kwa nini hao  madaktari wa kukuzuia kula nyama wasikuzuie usile matembele? Shetani kwa kuwa ni roho, huwaingia watu na kufanya wasababishe hiyo minyororo ya utumwa iwafunge watu wengine. Shetani huyu huwafunga watu ili wasiondoke kabisa katika utumwa huo kama ilivyoandikwa katika ISAYA 14:17Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” Hata hivyo ipo habari njema leo kwako, kwa kuwa imeandikwa katika YEREMIA 40:4 kusema “Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko.” Mnyororo ukifunguliwa unatakiwa uondoke mara moja, siyo kubaki unashangaa shangaa tu. Leo Bwana Yesu anataka kuwachilia watu huru ili waende zao kwa Jina la Yesu.

Yesu akisema kitu na wewe ukikiamini kitakuwa chako. Imeandikwa katika MARKO 11:1-6 “Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, 2 akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. 3 Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. 4 Wakaenda zao, wakamwona mwanapunda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. 5 Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwanapunda? 6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.”. Tunaona kuwa hawa wanafunzi waliamini kile alichosema Yesu, na walifuata njia na kumkuta mwana punda akiwa amefungwa. Kuna watu hupenda kufanyiwa muujiza kwanza ili baadae waweze kuamini. Hiyo siyo sahihi!!!. Ni wangapi leo wamefungwa na minyororo ya kishetani? Wapo waliofungwa midomo yao ili wasiweze kufuata wachumba wao na kuwachumbia.  Wapo pia waliofungwa midomo yao ili wasiweze kuongea na wateja ili kufanya biashara. Vitu vilivyofungwa na minyororo havihitaji ruhusa ya kuvifungua. Aliyefungwa na akawepo mtu wa kufungua ujue tayari huo ni msaada kwako. Yamkini kazi au ndoa yako ipo mahali fulani na inahitaji mtu wa kuja kuifungua. Leo tutafuata mahali hapo ambapo kazi au  ndoa yako imefungiwa na kusababisha ushindwe kupiga hatua kama familia.

Kumbe ni lazima awepo mtu aliyefunga na wakitokea watu wa kufungua ndipo mashindano huanzia hapo. Wale wanafunzi walipomfikia yule mwanapunda waliwakuta watu waliomfunga na ndio waliowaliza maswali ya kwa nini wanamfungua huyo mwanapunda. Hawa huitwa walinzi wa rohoni. Leo tunafuatilia minyororo iliyofunga maisha yako, mahali popote ilipo. Tutaiendea minyororo iliyomfunga mtu kwa kansa, minyororo ya uzinzi, utasa, ububu n.k. na tutavunjilia mbali kwa Jina la Yesu. Leo Bwana Yesu ametupa neema ya kwenda popote ulipofungiwa na kuwafuata walinzi wanaosimamia taabu yako na kuwaaambia “BWANA ANA HAJA NAWE”. Katika LUKA 19:33-34 imeandikwa hivi “Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwanapunda? 34 Wakasema, Bwana ana haja naye.” Wapo adui zako waliokufunga na endapo wa mtu wa kukufungua atatokea ndiyo hao hao watajitokeza na kuanza kuuliza maswali ya “kwa nini mnamfugua mtu huyu!!” Wenye kufunga na walinzi wao ndiyo huuliza maswali kama haya: “Mbona umeanza kufanya kazi? Mbona umeanza kuzaa? Mbona umeolewa? Mbona unafanya biashara?

Zipo baraka tele ambazo Mungu alishaziweka mbele yako hata kabla hujazaliwa. Yamkini ulipaswa uwe mbunge mahali fulani lakini kwa kuwa umefungwa na minyororo umebakia jinsi ulivyo hadi sasa.  Kwa kawaida, mtu aliyefungwa kwa minyororo akitaka kufurukuta minyororo hiyo humuumiza. Ndiyo maana baadhi ya watu  wanapoombewa makanisani, huanza kusema “baada ya kuombewa ile shida yangu nikama vile imeongezeka”. Cha kufanya ni kukaa kanisani na kujifunza zaidi namna ya kupambana kiroho. Mashetani lazima yaambiwe ukweli, kuwa Bwana ana haja nawe. Kuna aliyekufunga mnyororo kwamba “Usianze kazi/ Usisome/ Usiolewe/ Usifanikiwe”. Mbaya zaidi, waliokufunga minyororo hawapo mbali, ni watu wa karibu. Ndiyo wale wanaokuzuia wewe usiende kanisani, na hasa wanafanya vita nawe kwamba usikanyage Kanisa la Ufufuo na Uzima. Watakuruhusu uende makanisa mengine kwa sababu wanajua fika kuwa ukija Ufufuo na Uzima, ukianza kupiga majeshi ile minyororo waliyokufunga itaachia!!!


Maelfu ya wana wa Ufufuo na Uzima wakijifunza somo la Kuivunja Minyororo ya Utumwa 

UKIRI
Ewe mnyororo nakuvunja kwa Jina la Yesu.   Minyororo yote iliyosimama mbele zako tunailegeza kwa Jina la Yesu. Aliyesema usianze kazi akuone ukianza kazi kwa Jina la Yesu. Amen


Leo tutafanya vita vya rohoni na kumshinda shetani na malaika zake, kama vile ilivyoandikwa katika 2WAKORINTHO 10:3-6 (Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; 6 tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.). Kama silaha zetu zina uwezo wa kuangusha ngome, ujue kuwa ndani ya ngome kuna ndoa zimefungiwa humo, kuna biashara zimefungiwa ndani ya ngome, kuna kazi zimefungiwa ngomeni n.k. Bwana anasema kuwa “sisi ni silaha za Bwana za vita”.  Ili ushinde unapaswa kuvaa SILAHA ZOTE za Bwana. Kumbuka kuwa tunazitumia Silaha Zote, siyo silaha moja au mbili tu.


mtu huyu akifunguliwa kutoka Minyororo ya Utumwa
UKIRI
Imeandikwa katika YEREMIA 40:4Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko”. Kuanzia sasa nataka nifuate yale Yesu aliyosema, kuwa ana haja na mimi.  Ingawa nilifungwa minyororo, mimi na familia yangu, mimi na kazi yangu, kuanzia sasa ewe mnyororo uliokaa kwenye kazi, miguu, ewe mnyororo uliokaa kwenye akili yangu, leo kwa Jina la Yesu nakataa kubaki kwenye kifungo hicho kwa Jina la Yesu. Aliyenifunga na anayenilinda ili nikae kwenye kifungo hicho leo namfyeka kwa Jina la Yesu. Leo nakataa kubaki kwenye kifungo. Ewe kifungo cha kansa, ewe kifungo cha umaskini leo fyekwa kwa Jina la Yesu. Naamuru mashetani wote mliokaa kama kifungo achia maisha yangu kwa Jina la Yesu Kristo.  Amen


========== AMEN ========
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro
http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/