Pages

Sunday, August 6, 2017

NGUVU YA KURUDISHA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

JUMAPILI: 06 AUGUST 2017

MHUBIRI:  PASTOR GODFREY MWAKYUSA (SNP-SHINYANGA)


Mchungaji Godfrey Mwakyusa akifundisha katika semina ya Saa ya ufufuo na Uzima.
Yawezekana wewe umekuwa na ndugu yako aliyepotea katika mazingira tata, na ungetamani akarudi na umuone tena. Kila jambo linawezekana kama unayo imani kwa kuwa imeandikwa katika WAEBRANIA 11:6 (Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.). Je, unaamini kuwa Mungu yupo?  Je, unaamini kuwa Mungu huwapa thawabu wale wamtafutao?


Katika 1WAKORINTHO 15:26 imeandikwa (Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.). Kwa nini Biblia inasema kuwa adui wa mwisho  wa atakayebatilishwa ni mauti? Hii ni kwa sababu MAUTI NI ROHO, na wala siyo tukio. Na kama mauti ni roho ujue kuwa inaweza kusikia, inaweza kutembea n.k. Katika familia mbalimbali yapo matukio ya vifo vya aina tofauti tofauti vinavyotokea na watu kufikiria hayo ni matukio tu.  Wakati mwingine matukio haya yanasababishwa na ndugu, kama ilivyoandikwa katika MATHAYO 10:36 (na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.). Leo ni  siku ya kurudisha vyote vilivyoibiwa au kufa kwa namna ya mauti katika maisha yako kwa Jina la Yesu. Imeandikwa pia katika HOSEA 13:14 (Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu.). Kumbe tunajifunza kuwa kaburi lina nguvu, na mauti inayo mapigo yake. Leo tutaangamiza nguvu ya kaburi na mapigo ya mauti kwa  Jina la Yesu.


Katika MITHALI 8:17 imeandikwa (Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.). Kumbe ukimpenda Mungu naye pia atakupenda, lakini  ni kwa wale wanaomtafuta Mungu kwa bidii tu. Je, ipo bidii gani kwa mtu anayefanya maombi yake akiwa ndani ya chandarua kitandani? Kwa hali ya maombi rahisi kama hayo siyo rahisi kuifukuza mauti inayonyemelea maisha yako. Fahamu kuwa Mauti anatenda kazi. Katika ulimwengu wa roho, wavunaji kwa njia ya mauti huangalia ule mtu  waliyemlenga katika TV zao za kichawi na kuweka mtegoili kumnasa. Nyakati nyingine yawezekana mtu akategwa kwa njia ya chakula kama vile ndizi mbivu, na baada tu ya kula mauti inamfuatilia. Biblia inasema kuwa mwenye nguvu anapolinda mali zake zinakuwa salama!!”. Leo tunaamuru kwa jina la Yesu, kila mauti iliyotumwa katika maisha yako kuwa mithili ya ugonjwa, itatoweka mara moja kwa Jina la Yesu. Wapo watu wenye elimu zao lakini elimu hizo haziwasaidii kupata kazi ya kufanya. Maana yake ni kuwa ipo mauti inayokuwa imetumwa katika  maisha yao ya kielimu, kuwafanya wasome tu  lakini  elimu hiyo  isiwasaidie. Mauti inaweza kuwa katika viatu, pindi tu ukivivaa unakuwa unaandamwa na mauti. Wakati mwingine wapo watu walipewa Zawadi ya nguo katika harusi nao wakafurahia, lakini kumbe ndani ya nguo hizo ipo mauti iliyonuiziwa kuwa mtu huyu atakapoivaa nguo hiyo kamwe asifanikiwe!!!. 


UKIRI
Leo chochote kilichomezwa na mauti NJOO, iwe ni biashara, NJOO, iwe ni safari NJOO katika Jina la Yesu. Ninakataa kila mauti yaliyotumwa kwangu kunizunguka, ninayaondoa kwa Jina la Yesu. Amen


Makutano ya watu wakisikiliza Semina ya Saa ya Ufufuo na Uzima leo. 
Imeandikwa katika 2 SAMWELI 22:5 (Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu). Kumbe mauti anayo mawimbi, na hivyo mauti ikianza kumfuatililia mtu ataona mawimbi mawimbi tu.  Pengine kuna mtu anakuwa ameokoka lakini muda wote anakuwa akihisi watu kuwa wanamsema vibaya, kwa kuwa mtu huyo anakuwa amepandiwa roho la kujikataa au kujihukumu mwenyewe. Tukisoma katika AYUBU 38:17 imeandikwa (Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu?). Kumbe mauti anayo malango na kuzimu pia anayo malango yake. Kumbe mauti anapovuna, kuzimu yeye hupokea mavuno. Ndiyo maana mauti na kuzimu ni ndugu pacha, na hufanya kazi kwa kutegemeana. Ukisoma tena katika ZABURI 89:48 imeandikwa (Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?). Tunajifunza kuwa kuzimu inao mkono. Kwa hiyo, kama mauti ina mkono, inao uwezo wa kukamata vitu na kuvishikilia.  Leo tutaikamata mikono  ya  kuzimu kwa Jina la Yesu.


Leo tunazifuta kafara zote ulizofanyiwa kwa Jina la Yesu. Yamkini ulipokuwa mdogo ulichanjwa chale bila wewe kujijua. ISAYA 66: 9 (Je! Mimi nilete wana karibu na kuzaliwa, nisizalishe? Asema Bwana; mimi nizalishaye, je! Nilifunge tumbo? Asema Mungu wako).  Kwa maana hiyo, ukiona mambo yako hayafanikiwa siyo kwa shauri la Bwana bali wapo adui wanaofanya ukae katika hali hiyo, na hivyo lazima ufanye vita vya rohoni kuwashambulia na kuwashinda kwa Damu ya  Mwanakondoo. Imeandikwa katika YONA 2:2 (Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu.) Yona alimlilia Bwana,  siyo kilio  cha  kulia la hasha!!. Alichofanya Yona ni Kuomba.!!. Kumbe kuzimu ina matumbo yake. Wachawi wanaweza kumweka mtu katika vyungu na wakikuona unapokuwa unatembea wakakujjeli jinsi ulivyo!!!. 

Katika ISAYA 5:14 imeandikwa (Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.). Yamkini katika maisha yako, kuna mtu aliwahi kukutamkia kuwa “Hautaolewa wewe!!” au “Hautafanikiwa wewe!!” Ujue kuwa kuzimu ilishafungua kinywa chake na kupokea maneno hayo ili kuyatendea kazi za uharibifu!!.  Inawezekana wewe unatembea barabarani lakini kumbe kuna adui alishakutumia “roho la kukataliwa na mauti” na unajikuta kila mahali unapokuwa watu wanakuzomea!!. Hapo ujue kinachofanya hayo yatokee ni yale mashetani ya kukataliwa yaliyotumwa kwako. Ni hadi pale mtu wa ina hii atakapokataa hiyo  hali na kuanza maombi ya kushindana na hizo roho  ndipo tu atakapofanikwa.


Platform Ministry wakiongoza sifa na Kuabudu.

Kumbe katika ulimwengu wa roho yapo mashimo. Imeandikwa katika ISAYA 42:22 (Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.). Tunajifunza kuwa mashimo haya yanaweza kuficha masiha ya mtu, au biashara  ya mtu,  au  kazi n.k.  Na endapo atapatikana mtu wa kusema NJOO, vitu hivi lazima virudishwe kwa Jina la Yesu. Kwa sababu Mungu alimfanya mtu kwa mfano wake, maana yake ni kuwa utakachosema ni kama vile  Mungu amesema!!. Endapo utasema “kwetu sisi watu hawaolewi”, umemsema vibaya. Endapo utasema “kwetu watu hawasomi”, ujue umesema. Leo  ubatilishe hizo  semi kwa Jina la Yesu. Ndiyo maana katika 1WAKORINTHO 15:49 imeandikwa (Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.). Unaposema umeokoka maana yake unachukua ule uwezo wa kimungu na kufanya chochote utakacho kama vile Mungu anavyofanya.


Imeandikwa katika AYUBU 20:15 (Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake.). Lazima apatikane mtu wa kusababisha shetani apatwe na kichefuchefu hata atapike vile alivyotuibia. Katika ulimwengu wa roho tumepewa vitu vingi sana, cha kufanya ni kumtiisha shetani aliyemeza vitu vyetu vyetu kwa Jina la Yesu. Leo  tunarudisha vitu  vyetu vyote, kama ambavyo wana wa Israeli  walipomwambia Farao kuwa wataondoka na kila kitu  chao,ndivyo itakavyokuwa kwako katika Jina la Yesu.


UKIRI
Mali zangu, iwe elimu,  iwe safari, iwe biashara, leo lazima utapike kwa Jina la Yesu. Leo mniachie, utasa uniachie, laana iniachie, mauti  iniachie, mikosi iniachie. Fedha zangu mali zangu leo, NJOO kwa Jina la Yesu. Mali zilizomezwa kwenye nyumba za wachawi, achia. Natuma moto wa radi  mahali popote walipochukua unyayo wangu, au walipochukua mikono yangu au walipochukua kucha zangu,  au walipochukua nywele zangu, au walipochukua nguo  yangu,  leo natoka  kwa Jina la Yesu. Natoka katikati yenu kwa Damu ya Mwanakondoo. Amen


Katika UFUNUO  18:11-14 neno la Mungu linasema hivi (Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena; 12 bidhaa ya dhahabu, na fedha, na kito chenye thamani, na lulu, na kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na hariri, na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, na kila chombo cha pembe, na kila chombo cha mti wa thamani nyingi, na cha shaba, na cha chuma, na cha marimari; 13 na mdalasini, na iliki, na uvumba, na marhamu, na ubani, na mvinyo, na mafuta ya mzeituni, na unga mzuri, na ngano, na ng'ombe, na kondoo, na farasi, na magari, na miili na roho za wanadamu. 14 Na matunda yaliyotamaniwa na roho yako yamekuondokea; na vitu vyote vilivyo laini na vitu vya fahari vimekupotea; wala watu hawataviona tena kamwe.). Kumbe kuna uwezekano wa mtu kuuzwa mwili wake na roho yake.  Na pia kuna uwezekano wa mtu kuuzwa roho yake bila mwili wake. Biashara zipo na zinaendelea katika ulimwengu wa roho. Kumbe basi mtu anaweza kufa hapa Morogoro lakiniakuzwa Nairobi au Mbeya au mahali popote pale.  Leo ukatae biashara za aina hii kufanyika katika familia yako katika Jina la Yesu. Leo kataa ndugu zako  kuibiwa na kuuzwa kwa Jina la Yesu.


Kama yupo mtu ambaye hujawahi kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi binafsi wa maisha yako, leo amua kuokoka na kumwamini Yesu Krsito maishani kwako. Wewe ambaye umechoka kuishi maisha ya kuonewa na shetani, leo mkubali Yesu Kristo maishani mwako kwa kuokoka.


Showers of Glory Morogoro wakimsifu Mungu.


========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia

Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson

Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson

TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/