Sunday, October 22, 2017

MIKONO YA KISHETANI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI: 22, OKTOBA, 2017

MHUBIRI:            MCHUNGAJI. Dr. GODSON ISSA ZACHARIA


Mchungaji Kiongozi Godson Issa Zacharia akihubiri katika somo la leo.
Utangulizi: Tunaposoma maandiko  katika Yohana 4:24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Mungu wetu  ni Roho, kwa hiyo hana mwili. Hata hivyo, ni Mungu mwenye mikono, vidole, macho ana pua  ana akili ambayo haichunguziki kwa mujibu wa neno lake!!!! Musa alimuona Mungu mgongoni, ikimaanisha kuwa kumbe Mungu anao mgongo. Mungu wetu ambaye ni roho bado neno lake linatufundisha kwamba ana akili, macho, mgongo, mikono na miguu.

 Zaburi 80:15 Imeandikwa, “Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.” Hapa tunaona Mungu anatumia mkono wake kupanda mbegu. Zaburi 88:5 Imeandikwa, “Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.”… wametengwa mbali na mkono wako Luka 11: 20 Imeandikwa, “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.” Mitume wa Yesu wanasema wao walitoa pepo kwa kidole cha Mungu. Zaburi 29:11 Imeandikwa, “Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.” Mungu atawapa watu wake nguvu za roho mtakatifu kwa ajili ya kazi yake.
 
Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu katika ibada ya leo.
Mkono wa Kichawi au kishetani, kama vilevile Mungu alivyo na mikono wakati yeye  ni roho vilelvile na shetani ana mikono pia. Kwa kawaida shetani hakuumba chochote bali anachukua nakala ya uumbaji wa Mungu. Kama Mungu anaweza kuokoa kwa mkono na shetani naye anaweza kuangamiza kwa mkono.

Kuna mwanadamu ambaye ni mchawi ambaye akigusa kitu kwa mikono yake, lazima uharibikiwe. Pili anaweza kuwa shetani akagusa mali zako na ukaharibikiwa. Kuna watu akigusa shamba, biashara au ofisi yako lazima ukose wateja. Habakuki 2:9 Imeandikwa, “Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu!” Mkono wa uovu ndio mkono wa shetani na  mawakala wake mchawi na waganga. Anaweza kuwa mtu wa kawaida lakini amevuviwa na nguvu za kishetani. Wapo baadhi ya watu ambao wakikusalimia au wakigusana na wewe kwa kutumia mikono yao basi kuanzia hapo mambo yako huanza kuharibikiwa.  Unaweza kuwa umeajiriwa ofisi fulani, mfanya kazi mwenzako akaamua kwa mkono wake akachomoa nyaraka muhimu kwa ajili ya kazi yako ili kazi yako iharibike. Pengine kuna mtu ambaye ulikutana naye siku moja na akakusalimia kwa kukupa mkono, na tangu siku hiyo mambo yako yakaanza kuharibika.

Mkono wa shetani au mchawi waweza kunyooshwa kwenye kazi, biashara, familia au afya n.k. Ndio maaana utaona mtu anafanya biashara lakini analia kwa sababu hajawai kupata faida. Wengine ameolewa lakini hajawai kupata mtoto ni kwa sababu kuna mtu alimgusa au amenyoosha mkono wa kishetani juu ya uzazi wake. Kama Mungu anasema kila tutakapokanyaga ametupa. Kwa hiyo shetani naye akikanyaga jua kazi, biashara, uchumba, miradi au ujenzi jua huwezi kufanikiwa.
Majeshi ya Bwana wakisikiliza Neno la Mungu katika ibada ya leo.

1.    
MIKONO YA WACHAWI AU WANADAMU
Wanadamu hawa wachawi wanaweza kukugusa moja kwa moja au kupitia bidhaa. Yawezekana ikawa ni nguo, wigi, kitenge au suti Fulani lakini kumbe iemenuiziwa manuizo ya kichawi nyuma yake.

Matendo ya Mitume 12: 1-6 Imeandikwa, “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne,   wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza”.

Herode alikuwa ni mwanadamu lakini alitumia mkono wake kuwatenda mabaya watu wa kanisa.  Huyu alikuwa mfalme lakini alinyoosha mkono ili watu wa Mungu wauwawe. Anaweza kuwa Rais, Waziri, Mbunge, Kaka, dada au rafiki lakini wakanyosha mkono ili wewe uharibikiwe. Pengine anaweza kuwa ni mwanadamu lakini akaiandika barua ya wewe kuachishwa kazi, au kufunga biashara au kusitisha mkataba. Wakati mwingine ukoo au familia wanaweza wakaandika maagano ambayo baadae yanageuka kuwa matatizo ya kiukoo au familia husika. Pengine yawezekana ilikuwa ni kwa sababu tu kwa mkono wako ulibeba kuku kwenda kwa mganga wa kienyeji kipindi kile kabla hujaokoka!!. Wapo watu ambao ukiwapa kubeba watoto lazima walie sana, ukiona hayo jua kuwa watu kama hao mikono yao ina uovu ndani yake.

Kazi uliyonayo leo hii ni kuuvunja mkono wa kichawi kwa jina la Yesu. Leo waendee wachawi kwa nguvu ya jina la Yesu, Damu ya Yesu na Roho Mtakatifu. Kumbuka kuwa Wewe ni silaha za Bwana za vita na kwa wewe Bwana atavunja wachawi wazee kwa vijana. Wachawi wamepanda uovu, mabaya, ajali, magonjwa kama Ukimwi, Kisukari na mengine lakini tumepewa mamlaka ya kung’oa yote na kuyaharibu kwa jina la Yesu.
 
Binti huyu akifunguliwa kutoka mikono ya Kichawi katika Ibada ya Leo.
2.     MIKONO YA KISHETANI
Hii ni mikono ya mashetani kama mizimu, majoka na majini n.k. Ayubu 1:1-3 Imeandikwa, “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.” Ayubu alikuwa mtu aliyebarikiwa na Yehova kwa mali na vitu vingi. Kwa maandiko haya tunauona wasifu wa rohoni wa Ayubu (kwamba ni mkamilifun  na mwelekevu), na wasifu wake wa wa mwilini (kuwa na mali nyingi, watoto 10 n.k.).


Hata hivyo shetani aliziona Baraka zote juu ya Ayubu akashikwa na wivu. Ayubu 1:6- Imenadikwa, “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako”.

Mungu alimzuia shetani asinyooshe mkono wake juu ya roho yake. Lakini alimruhusu shetani anyooshe mkono wake na kugusa mali na ustawi wa Ayubu. Kumbe shetani kwa kuwa anayo mikono anaweza kunyoosha mkono wake juu ya kazi, biashara, shamba au mali ulizonazo na kukuletea matatizo.

MADHARA YA KUNYOOSHEWA MKONO NA SHETANI.
Ni yapi madhara ya shetani kunyoosha mkono wake na kugusa maisha yako? Hebu tumuangalie mgusaji (shetani), ambaye anaweza kuingia hata katika familiayakona kuleta madhara mbalimbali!! Tunaposoma katika AYUBU 1:13-20, tunaona kwamba:

a)     DHARA LA KWANZA: Katika AYUBU 1:13-15 imeandikwa (Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 14 mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; 15 mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.). Je, huyu mjumbe namba moja wa kuleta taarifa alikuwa kajificha wapi kwa nini yeye asishambuliwe na hao Waseba? Inawezekana kuwa hata huyu mleta taarifa ni miongoni mwao.
 
Mchungaji Mwandamizi Happiness Muhimbula akifuatilia neno la Leo

b)    DHARA LA PILI: Katika AYUBU 1:16 imeandikwa (Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.). Swali la kujiuliza: Huyu mjumbe namba 2 naye alijuaje kuwa huo moto ulitoka mbinguni? Ni lini alienda mbinguni na kuukuta huo moto? Lazima watoa taarifa kama hawa tuwahoji, kwa sababu yumkini ni miongoni mwa wajumbe wa kishetani wanaowekwa ili  kutoa taarifa mbaya.

c)     DHARA LA TATU: Katika AYUBU 1:17 imeandikwa (Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.). Huyu mjumbe namba 3 wa kuleta taarifa naye ni wale wale,  kwamba haiwezekani aweze kuliona tukio lote kuanzia linapoanza hadi kumalizika, na mwishowe apate nafasi  ya kupeleka taarifa.

d)    DHARA LA NNE: Katika AYUBU 1:18 imeandikwa (Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa;). Huyu mjumbe namba 4 naye kama walivyokuwa watangulizi wengine, huyu naye siyo  mtu, bali  ni wakala wa kishetani. Kwa nini tuseme hivyo? Ni kwa sababu tunajiuliza, Aliwezaje kujua upepo ulikotokea, na mambo yaliyokuwa mle ndani kwenye karamu, na je, alijua je kule ndani kwamba hakuna aliyesalimika? Lazima tugutuke na kuwaaibisha watu wa aina hii, kwa kuwa watu wa aina hii nao ni sehemu ya hao  mashetani.
Showers of Glory Morogoro wakisifu na kumchezea Mungu wakati wa Ibada ya Leo
Tunajifunza kuwa shetani aliuvaa mwili na kutengeneza matukio katika nyumba ya Ayubu.  Kwa kuitumia mikono yake, shetani aliweza kugusa vitu vya Ayubu na kuleta uharibifu mkubwa. Leo tukatae kuguswa na mkono wa shetani, tumkaribie Mungu wetu ili yeye ndiye ayaguse maisha yetu. Pengine wewe ni mwanandoa, nasasa maisha unayopitia nis tofauti na maisha uliyoanza wakati mnaanza ndoa. Leo tutaikata mikono ya wachawi waliogusa ndoa au  maisha yako na kusababisha balaa na migogoro isiyoisha kwa Jina la Yesu.

Leo kupitia sadaka zetu tunamsihi Mungu kwa Agano kwamba Bwana akayazuie matukio kama yale ya kishetani yasitokee kwetu. Leo tutashambulia mikono ya akina Herode (wanadamu), na ile mikono ya mashetani wanaotuzuia na kuleta uharibifu maishani mwetu. Hata hivyo, ni sharti ukubali kuokoka kwanza kwa maana ya  kumpokea Yesu Kristo maishani mwako.


KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
(WhatsAssp & SMS only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages