GLORY
OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
KANISA
LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
PASTOR
DR. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI:
10 MACHI, 2018
Utangulizi:
Neno muhula lina maana
ya muda au wakati uliokubalika kwa ajili ya jambo Fulani kufanyika. Ni majira
yaliyokubalika kwa ajili ya kitu Fulani kufany ika. Linaweza kuwa jambo jema au
baya lakini haya yote yana muhula wake. Muda huu ukifika kama ni wakati wa
kucheka au kulia lazima mtu ama alie au acheke. Muhula wa jambo Fulani huwezi
kushindana nao. Kama kuna vitu mtu hatakiwi kushindana nao ni muhula wa jambo Fulani
kwenye maisha ya mtu. Hata neno la Mungu linazungumza kwa habari ya muhula wa
mtu.
Mungu alimwambia
Ibrahimu kwa hakuna neno gumu la kumshinda Bwana. Aliambiwa kwa sababu mke wake
alikuwa hapati mtoto. Malaika akamwambia kwa muhula wake atazaa mtoto. Mama huyu
alikuwa hajapata mtoto kwa sababu muhula wake ulikuwa haujafika. Mama huyu
muhula wake ulipotimia alizaa mtoto wa kiume katika uzee wake. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda
Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata
mwana wa kiume.” (MWANZO 18:14)
Mhula ukifika unapata kile ambacho
amekuahidi Mungu ukipate, biblia inasema Sara alipata mtoto kwa muhula ule ule aliopangiwa
na Mungu.
“Sara akapata mimba akamzalia
Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.” (MWANZO
21:2)
Sara alikuwa hana
watoto lakini muhula ulipotimia alipata mtoto. Anna alikuwa hana mtoto na
akasumbuliwa sana na Penina. Mama huyu akaliitia jina la Bwana mpaka akapata
mtoto. Mtoto Samweli akazaliwa na mafuta ya Unabii. Kinachozaliwa kwenye muhula
huwa kinastawi sana.
Mungu anatufundisha
kwa habari ya muhula ili tuyatambue majira. Kuna wakati wa kila kusudi chini ya
nchi. Mungu akamwambia Mhubiri kuna wakati wa kupanda na wakati wa kung’oa. Kuna
wakati wa kucheka, kulia, kucheka, kufurahi, kukataliwa na kutumikishwa. Yako majira
mengi nay a kutisha lakini yuko Bwana wa kuokoa. Anasema kuna wakati wa kung’oa
yale Bwana hakuyapanda kwenye maisha yako. Kuna mapando yaliyopandwa kwenye
kazi, biashara, ndoa na uchumi wako, lazima yote yang’olewe kwa jina la Yesu.
“Kwa kila jambo kuna majira
yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya
mbingu.Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa;
Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na
wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na
wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa
kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na
wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa
kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa
kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa
kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa
kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati
wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.” (MHUBIRI
3:1-8)
Kuna wakati
Yesu alikuwa anasema na kuwauliza wale waliokuwa wanakuja kwake; je unaamini? Wakijibu
ndiyo anawaambia pokea sawasawa na ulivyo amini. Pokea leo kibali, uwezo,utajiri sawasawa na
ulivyo amini kwa jina la Yesu. Bwana Yesu aliwahi kutoa mfano mmoja kuhusu
mpandaji. Mkulima alipanda ngano na alipo lala usingizi adui akaja akapanda
magugu ndani yake. Wafanya kazi wakenda kwa bosi kumweleza kilichotoke hivyo
akawaambia wayaache magugu na ngano pamoja ili ukifika wakati wa kuvuna atayatenganisha
magugu na ngano. Shetani ukiwa umelala anaweza kukupandia mabaya na uhuribifu
kwenye maisha yako; atapanda shida taabu, dhiki, mikosi na balaa, lakini haya
ni mapando ya kishetani ambayo ni lazima kuyang’oa kwa jina la Yesu.
Kuna wakati
na muhula wa kuwaangamiza mashetani na wote wanao tesa maisha yetu. Siku moja
Yesu alipovuka ng’ambo alipita katika njia akakutana na watu wawili waliokuwa
na mapepo, wakali mno waliokuwa wanawazuia watu kupita njia hiyo. Yalitamba kwa
namna nyingi sana lakini Kristo alipofika yaliona nguvu yake hata wakapiga
kelele wakisema wataka kutuangamiza kabla ya muhula wetu.
“Naye
alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana
naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na
tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja
kututesa kabla ya muhula wetu?” (MATHAYO 8:28-29)
Kwa habari
ya wagerasi na mashetani yaliyo tesa watu huko yalikuwa na muhula wa
kuangamizwa na aliipofika Yesu yakaondolewa. Vilevile mashetani wanaolinda
hatima yako, wanaotesa maisha yako, wanao haribu kazi yako na kusumbua ndoa
yako hata hakuna furha tena. Bwana ameleta muhula maalumu wa kuwaondoa wale
walio kutesa maishani mwako kwa jina la
Yesu. Shetani kwa asili ni muonezi; mawakala wake yani majoka, mizimu na
wachawi, waganga na wasoma nyota wamewaonea watu kwa mda mrefu, amewachukua
watu misukule, anaanawazui katika mipango ya maisha, analeta mgonjwa, anazuia
watu wapate kazi, wasisome na kila wanalotaka kulifanya.
“habari za
Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” (MATENDO
YA MITUME 10:38)
Shetani akifunga
watu huwa hataki kuwaruhusu kupiga hatua
katika maisha yao. Anawaweka katika kifungo na kuwahusuru humo na kuwajengea
ngome, anaweka ulinzi mkali wasitoke, hataki wapate msaada. Lakini leo Bwana
amekuja kuwafungua watu kutoka katika vifungo mbalimbali, amekuja kufungua
biashara yako, haki yako, elimu yako, biashara yako, pokea vyote kwa jina la
Yesu.
“Aliyeufanya
ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?
” (ISAYA 14:17)
Biblia imeweka
wazi kwa habari ya uonevu wa shetani kwa wanadamu. Naye Mungu amechungulia
katika ulimwengu wa roho ameona jinsi wanadamu walichukuliwa na wachawi,
walivyowekwa katika vifungo na kuwaingiza katika balaa na magonjwa. wengine
anawasomba na kuwaweka shimoni, nyumba za kufungwa.
‘Basi sasa nafanya nini hapa asema
Bwana ikiwa watu wangu wamechukuliwa bure? Hao wanaowatawasla wanapiga yowe
asema Bwana, na jina langu linatukanwa daima mchana kutwa.’ (ISAYA 52:5)
Uonevu wa
shetani ni kila mahali; matatizo yote unayo yaona leo yanasababishwa na
shetani, japokuwa matatizo yana tofautiana. Mfano mzuri, ukiamka tu asubuhi
kichwa kinaanza kuuma unashindwa kufanya mambo ya msingi hatimaye mambo yako
yanakwama. Unapata pesa kwa ajili ya kufanya mambo muhimu yeye anakuletea
mikosi, magonjwa na dhiki hata hufanikishi lile ulilo kusudia kulifanya kwa
pesa zako. Anapoteza malengo na kupindisha hatima za watu kwa uonevu wake.
“Kwa sababu
hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao
wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.” (ISAYA 5:13)
Baadhi ya makutano wakifuatilia kwa makini Mchungaji akifundisha |
Vita kati
ya watakatifu na shetani ilisha isha tangu mbinguni.Malaika watakatifu walimwondoa
mbinguni na kumtupa shimoni, kama vile shetani alivyotupwa toka mbinguni tunao
uwezo wa kumtupa nje ya maisha yetu kwa jina la Yesu. Biblia inasema
wakamshinda shetani kwa damu ya Kristo tunao uwezo wa kumshinda shetani. Inuka
leo mshinde anaye haribu mipango yako, anayekula ndoa yako, anayeharibu watoto
wako kwa jina la Yesu.
“Kulikuwa
na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka
naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao
hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa
pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na
nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa
chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na
usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya MwanaKondoo, na kwa neno la ushuhuda wao;
ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu,
nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu
mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” (UFUNUO12:7-12)
Yesu
alikuja duniani kwaajili ya kuwaokoa wale walionewa na kuwafungua waliofungwa;
kazi kubwa aliyokuja kufanya dunia ilikuwa ni kuzivunja kazi za shetani dunia,
kuwakomboa walio na taabu, shida na matatizo kadha wa kadha. Alikuja kutupatia vile ambavyo shetani
kimsingi alivizuia tusivipate maishani mwetu, tulipangiwa utajiri lakini tu
maskini. Alikuja ili wewe utoke katika uonezi wa shetani kwa jina la Yesu.
“atendaye
dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi
hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi”.(1YOHANA3:8)
Hujafikia
kiwango kizuri cha maisha kwa maana amekuzuia mahali. Ulipangiwa uwe mmliki wa kiwanda kikubwa leo
ni mfugaji wa kuku, ulipangiwa kuwa mwanasiasa mkubwa leo ni fundi viatu. Ukiona
hayo jua shetani anakaa mbele yako na kuweka mipango ili ufukuzwe kazi, ili
usisaidiwe lakini Bwana amekuja ili utoke kifungoni katika jina la Yesu.
Shetani
anaweza akakaa ndani ya mtu akakuzuia katika mipango yako. Anaweza kuwa kaka, rafiki,
shangazi au ndugu wa karibu au mtu yoyote. Biblia inasema wafanyakazi wenzake
na Danieli walimchongea ili Danieli afe, lakini yeye alimtii Mungu akawa
anamwomba kwa bidii mara tatu kwa siku. Kwa sheria ya waajemi alikuwa amevunja
sheria nao wakamtupa katika tundu la simba lakini Bwana akamwokoa na midomo ya
simba kwa jina la Yesu. Kuna watu wameonewa sana na watu walio waonea
hawajaguswa bado; mwingine ameshindwa kusoma laikini yule alimzuia kusoma bado hajaguswa.
Kuna mwingine ameonewa katika matatizo, afya ,kazi maendeleo na wale walikuonea
bado hawajaguswa kwakuwa muhula wao ulikuwa bado. Leo muhula wao umefika na
wataangushwa kwa jina la Yesu.
Mashetani wanatetemeka mbele za
Mungu:
Shetani anajua
uwezo wake na mamlaka yake, hawawezi kukaa palipo na nguvu ya Mungu. Mashetani
yakimwona Yesu yana ogopa. Tumia jina la Yesu kumshinda shetani na ataondoka
maisha ni mwako, kwa maana kwa nguvu za Mungu shetani ameshindwa kwa jina la
Yesu.
“Wewe
waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na
kutetemeka.” (YAKOBO 2:19)
Ndugu mmoja
aliyekuwa na mapepo walipomwona Yesu kwa mbali alipiga mbio akapiga magoti
mbele za Yesu, kuashiria kuwa alikuwa amesalimu amri mbele ya nguvu ya Mfalme
Yesu. Kila mwenye pepo husalimu chini ya mamlaka ya Kristo , je mwanadamu aliye
umbwa na Mungu? Leo upate hofu unyenyekee chini ya mkono wa Mungu kwa jina la
Yesu. Kwa unyenyekevu wako mashetani watawekwa mbali na wewe kwa jina la Yesu.
“Na
alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti
kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa
Mungu usinitese.” ( MARKO 5:6-7)
Mtu akifunguliwa kutoka muhula wa mateso aliyokuwa amewekewa na mashetani. |
Shetani ni mwoga sana akishajua muhula wake wakumwangamiza umefika anaanzisha lugha za kujitetea tetea, anaanza kufanya mambo fulani ya kujionesha kuwa mtakatifu. Lakini Bwana hakuruhusu shetani azungumze mbele yake. Pokea uwezo wa kumwangamiza mashetani kwa jina la Yesu.
“akisema,
Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani,
Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo
mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.” (MARKO 1:24-26)
Ukimwamini
Yesu, Yesu anakaa ndani yako. Mashetani wakija kukuangalia wanamwona Yesu. Ili
kumwangamiza shetani na mapepo wabaya lazima uwe na nguvu ya Mungu ndani yako kwa
maana kile aliye na Yesu ananguvu ya Mungu ndani yake. Leo upokee nguvu ya
Mungu ndani yako ukafukuze mapepo kwa jina la Yesu.
“Mimi ni
mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;
maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (YOHANA
15:5)
Tunayo amri
au kibali cha kuwaondoa mapepo maishani mwetu. Kwa kumpokea Yesu tunao uwezo wa
kufukuza mashetani yanayotutesa kwa jina la Yesu. Alipowaita wanafunzi wake
akwapa amri ya kuwatoa mapepo na kushinda nguvu zote za adui na hakuna kila litakalo
wadhuru. Hivyo ukiwa na amri ya Kristo hakuna nguvu ya shetani itakayo kudhuru
kwa jina la Yesu.
“Akawaita
wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na
kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.”(MATHAYO
10:1)
Children Ministry wakiimba na kucheza mbele za Bwana wakati wa Ibada ya Leo. |
Ukisha kuwa na mamlaka ya Mungu ndani yako Roho yake inakaa ndani yako nawe unakuwa na mamlaka ya kuangusha nguvu zote za shetani na kutoa mateka wote. Sisi tuliokoka tunayo nguvu ya Mungu ndani yetu na Yesu anafanya kazi yake kupitia sisi, kwa nguvu hiyo tutaangusha maadui wote wanao tuzuia kuingia na wanotutesa kwenye muhula wetu kwa jina la Yesu
“Roho ya
Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri
wanyenyekevu habari njema; ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka
uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa
Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;” (ISAYA
61:1-2)
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA
NASI KUPITIA
FACEBOOK:
Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL:
+255 719 798 778