Sunday, May 20, 2018

OPARESHENI YA KUTAFUTA NA KUOKOA KILICHOPOTEA


  
GROLY OF CHRIST TANZANIA CHUCH (GCTC)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA –MOROGORO
PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA

JUMAPILI MAY 20, 2018


Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akiwa tayari kutafuta na kuokoa kilichopotea.



UTANGULIZI
Kwa miaka mingi jamii za watu, kabila na lugha wamekuwa chini ya utumwa wa shetani, maisha yao yakiongozwa naye. Wametawaliwa kimwili na kiroho, wamenaswa kwenye mashimo, wamekuwa mawindo, wamezamishwa kwenye misitu ya uovu, wameibiwa mali na vitu vyao na wamekosa msaada, lakini Mungu kwa upendo wake akamtoa mwanae mpenzi ili watu waokolewe. Kwakuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

“Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.” (Luka 19:10)

Mwana wa Adamu ni Yesu Kristo mwenyewe (Yoh 1: 14). Hapo mwanzo Yesu alikuwa ‘Neno’, alikuwa kwa Mungu, naye ‘Neno’ akavaa mwili akakaa kwetu (Yohana 1:1-3).  Ndiye aliyekuja kama Imanueli [Mungu pamoja nasi] akazaliwa na mwanamke, akautoa uhai wake ili kupitia huo awaokoe wanadamu ambao ni mimi na wewe kutoka katika mikono ya shetani.
Baadhi ya makutano haya wakifuatilia neno la Mungu kuhusu Oparesheni kutafuta na kuokoa kilichopotea

Yesu Kristo alizaliwa kama mwanadamu wa kawaida, aliishi kama mwanadamu wa kawaida. Ulipofika wakati wake wa kuitenda kazi ya Mungu aliingia hekaluni, akisha kupewa kitabu,  akafungua unabii uliokuwa umetabiliwa na nabii Isaya, akasoma maandiko yafuatayo kudhihilisha lile alilojia hapa dunia.
“Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,  Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.  Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”  (Luka 4:17-21)

Maneno ya Bwana huwa yana andikwa na kutunzwa kwa wakati wake, ukifika wakati wa utimilifu wa maneno hayo matakatifu ya Mungu, Mungu humtuma mjumbe wake kuyatimiza. Unabii wa nabii Isaya uliandikwa miaka mingi sana iliyopita, lakini wakati wa kutimia kwake ulikuwa hujafika bado, ndipo Kristo alizaliwa baada ya muda kutimiza unabii huo.
“Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;” (Isaya 61:1-2)

Tangu wakati wa nabii Isaya watu walikuwa wanachukuliwa mateka, waliwekwa chini ya utawala wa giza na kumezwa na mwovu pasipo msaada wowote. Ndipo mwana wa Adamu akaja duniani kutafuta na kuokoa kile kilichochopotea, kuwafungua waliofungwa na kuonewa chini ya utawala shetani Ibilisi.

Yesu anapokuja kutafuta kwenye maisha ya wanadamu, huwa hatafuti lile linalo onekana, hutafuta ambalo limepotea, limefichwa, limeibiwa na kuwekwa mahali pa siri. Ikiwa kuna kitu ambacho ulikiweka mahali fulani ukategemea kesho ukichukue na ulipoenda siku inayofuata ukakikosa ujue kuwa kimeibiwa. Mungu aliwaweka wanadamu duniani wakiwa kamili, lakini watu hao wamepotea, wamepoteza mali zao, ndoa, mazao yao yameibiwa na kufichwa mahali. Ndipo sasa Mungu akaja ili kuokoa na kutafuta kilichopotea.

Baadhi ya Makutano wakijifunza kwa habari ya kutafuta na kuokoa kilichopotea.

Bwana uingia kwenye mashamba, kwenye mapori, mapango, nyumba za watu, juu ya dali. kwenye ofisi za watu, n.k, kutafuta na kuokoa kile ambacho kimeibiwa na kufichwa mahali. Yapo mambo mengi na vitu vingi vyako vimehamishwa mahali pake na kupelekwa sehemu nyingine. Mfano, amani yapasa kuwako ndani ya ndoa na familia lakini inaibiwa na kufichwa mahali hatimaye ndoa imekua uchungu, ndipo sasa anakuja kuitafuta ili kuirudisha mahali pake. Mchungaji mwema akiwa amepoteza kondoo mmoja ndani ya kundi la kondoo mia, huwaacha hao tisini na kenda na kuenda kumtafuta mmoja aliyepotea na akisha mpata anafurahi sana.

Biblia inataja habari za Mwana mpotevu aliye omba mali na fedha kutoka kwa baba yake , kwa kuwa baba yake alimpenda akampa, akenda nchi ya mbali, akatapanya mali hizo kwa uzinzi na uasherati. Njaa ikaingia kwake hata akaamua kujilisha pamoja na nguruwe, kwa mateso hayo akapata akili na akawaza kurudi kwa baba yake, aliporudi baba yake akafurahi sana kwa kumuona mwanae, (Luka 15:11-20). Hakika kuna furaha katika kurudisha, leo Bwana anataka kuokoa na kurudisha vitu vyako vilivyofichwa na mwovu kwa jina la Yesu.

Biashara yako iliyokufa, kazi yako iliyokufa, elimu iliyokufa, Bwana amekuja kuiokoa na kuirudisha mahali pake. Mara nyingine unajikuta wewe ni mama, siku zako zimepotea; mwezi wa kwanza, wapili hata watatu yamkini wamezipoteza ili hukose mtoto. Yesu Kristo amekuja ili urudishe kile ulichopoteza kwa jina la Yesu.

Macho ya Mungu yanaona kila mahali, huenda ukawa umechukuliwa kwa namna ya rohoni na kuweka kwa siri kwenye mkoba wa mtu, kwenye uvungu wa mtu. Mara nyingine unaweza kuibiwa na kuchukuliwa vitu vyako halali na kuwekwa mahali. Mfano, unaweza kuibiwa soksi moja ikapelekwa mahali na tangu siku hiyo umekuwa unatabia mbaya, mambo hayaendi kwakuwa umechukuliwa kwa namna ya kichawi.

Platform wakiongoza kipindi cha sifa na kuabudu.

Nguo, nywele, kucha au kitu chako chochote ni kiwakilishi chako. Yusufu alipomkimbia mke wa Potifa aliacha sharti, na kupitia sharti hilo alikamatwa na kuweka gerezani. Hivyo mali yako au sehemu yako inaweza kuchukuliwa na watu waovu ikapelekwa mahali na ikawa kiwakilishi chako katika kutesa maisha yako yote. Leo Bwana anataka kurudisha kile kilicho ibiwa, kurudisha kazi, ndoa,n.k.  kwa jina laYesu.

Akili ya mtu pia inaweza kuibiwa, kutekwa, upendeleo wako unaweza kuchukuliwa, kibali chako kinaweza kutekwa mahali ili tu uharibikiwe. Kwakuwa Yesu alifahamu haya ndipo akaja kutafuta na kuokoa kile kilicho potea.

Mtu aweza kuchukuliwa na kutekwa, mali na mambo yako yanaweza kuchukuliwa na kutekwa. Vile vitu vyako vinavyo haribika mara kwa mara ni kwasababu kunamtekaji amekuja kuvichukua na kuviteka. Mtu anapochukuliwa mateka, na kwakuwa mtu huyo huwa haonekani wanamwita msukule na mara nyingi huwa anakufa kabisa katika hali ya mwili na ndipo wanamchukua na kumteka anakosa uhuru, na utumiwa kama anavyotaka mtekaji wake kwakukosa maarifa.
“Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.” (Isaya 5:13)

Nabii Isaya alionyeshwa na Mungu kwamba watu hawa wanao onekana; wanakula, wanatembea, walala na kumka, kuoa na kuolewa, wameibiwa na kutekwa, wamechukuliwa na kunaswa kwenye mashimo. Chanzo kikubwa cha kuchukuliwa kwao ni kukosa maarifa, kutokujua kamaa kunawachawi, kuna waganga, majini. Kushindwa kufahamu kuwa kwa jina la Yesu ataokolewa. Shetani siku zote anafanya kazi kwa siri sana ili asionekane, anapata nguvu ikiwa anachomfanyia mtu hakijulikani.
“Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.” (Isaya 42:22)

Shetani alijaribu kumwibia Ayubu mali, ndoa, kazi zake akashindwa kwakua Bwana alimzingira Ayubu pande zote kwamaana alimtumikia Mungu kwa mwaminifu (Ayubu 1:1-3). Ndipo shetani akaenda mbele za Mungu akamwambia atoe mikono yake ya ulinzi kwa Ayubu (Ayubu: 10), Mungu alipotoa mikino ndipo mambo yakaharibika, mali zikaharibika na kila alichokuwa nacho (Ayubu 1:13-20).  Watoto wa Ayubu na mali zake ziliibiwa na watu au mipango ya shetani si kwaajili ya Mungu. Kuna wakati shetani anavaa mwili akatenda kazi kama binadamu ili aibe mali na vitu vya wanadamu.

Maranyingine waweza kumuona mtu mwenye afya nje, cheo na mali lakini ametekwa, ameibiwa fedha, mali, kazi n.k. Wamefungiwa huko hata hawawezi kujiongoza wenyewe, wamewekwa kwenye nguvu za shetani na utawala wake hata hakuna msaada. Wakati mwingine mtu anaweza kuibiwa tumbo, akili, moyo n,k vikawekwa mahali kifungoni.
Baadhi ya Makutano waliamua kumpa Yesu maisha yao ili waweza kutafuta, na kuokoa kilichopotea.

Unaweza kuibiwa sura yako au akili yako. Wanaenda  kwa waganga nakuchukua kile wanacho kitaka kwako, sasa yule aliye ibiwa anakuwa katika kundi la kukataliwa, hakuna anaye msemesha, hakuna anaye mtaka kwakuwa sura au kibali chake kimeibiwa. Leo Bwana arudishe kibali chako kwa jina la Yesu.

Jambo la kushangaza chini ya nchi nikuwa wale walio ibiwa na kutekwa ni wengi sana kuliko walio huru. Mtumishi wa Mungu Stephano alipigwa kwa mawe hadi kufa (Matendo 7:59), wengine walichomwamoto, na kukatwa vichwa (Marko 6:24-25). Kimsingi si wote wanaokufa, wanaopotea, wanaokaa kifungoni ni mapenzi ya Mungu, hapana! ni kazi za wovu. Ndipo bwana anasema siwezi kukaa ikiwa watu wake wanatekwa, wanauawa, wanapelekwa utumwani ndipo akasema.
“basi sasa, nafanya nini hapa, asema Bwana, ikiwa watu wangu wamechukuliwa bure? Hao wanao watawala wanapiga yohe, asema Bwana, na jina langu linatukanwa daima mchana kutwa”(Isaya 52:5)

Mwanadamu ni kazi ya Bwana, lakini wachawi wanamtumia binadamu huyo kama ndondocha na kuwatumia wanavyotaka, kwa kufanya hivyo jina la Bwana linatukanwa (Zaburi 138:8).

Watu wanaweza kuchukuliwa mateka kwa namna tatu. Kumbuka mtu ni roho anaka kwenye nyumba inaitwa mwili.  Kwakuwa mtu ni roho anaweza kuchukuliwa kwa namna tofauti kuwekwa kifungoni kama ifuatavyo;
1.Anaweza kuchukuliwa mzima kabisa. Wachawi wakimuona mtu anafaa kwenye mambo yao, wanakuja wanafanya uchawi wao kisha wanamchukua kwa kumtoa kwenye mwili wake kisha wanaleta gogo likavaa sura ya mtu huyo. Wakati watu wanahangaika na gogo ili walizike wao wanakuwa wamemchukua mtu huyo kumfanya watakavyo.

Sikumoja Askofu mkuu, Dr. Josephati Gwajima alikwenda msibani mahali, alipokuwa anapita kuaga mwili wa marehemu akaona mgomba umevalishwa suti umewekwa kwenye jeneza, akapita mara ya kwanza na ya pili, akasimama akawambia watu wote walikuwa mahali hapo huyu simtu bali mgomba, wakambishi ndio akasema ‘kwa jina la Yesu’ yule kijana akatoka ndani ya nyumba na kwenye jeneza ukaonekana mgomba kabisa.
Binti huyu alifunguliwa kutoka alikokuwa ametekwa, hakika amewekwa huru kwa jina la Yesu

Jana msavu stendi Morogoro alionekana kijana anaumwa mguu, watu wa stendi wakaamua kuchanga ili kumpeleka hospitali, wakati wanampeleka akatokea mtu anasema jamani mtu huyu si alikufa tanga? Wakamkatalia, lakini walipokwisha mpeleka hospitalini akapotea katika mazingira ya kutatanisha hadi leo hayupo.

Kwa mifano hiyo jifunze kuwa watu wanaweza kuchukuliwa na kufichwa, katika mwili akaonekana amekufa na wakamzika kabisa na kuandika jina lake kwenye msalaba, kumbe mtu huyo amechukuliwa amepelekwa mahali kufanya kazi kichawi. Wanaweza kumchukua mtu na mara nyingine wakamzika kumbe yuko Uganda anafanya kazi benki.

2. Mtu anaweza kuchukuliwa na kupotea kabisa, asife wala asionekane mahali kumbe amechukuliwa kwa namna ya kichawi wakamtowesha kumpeleka sehemu kufanya kazi. Tunajifunza mfano wa Yusufu aliyeuzwa na ndugu zake wakasema kuwa amekufa kumbe wamemuuza misri. Hivyo inawezekana mtu kutoweshwa katika mazingira ya kutatanisha kisha akapelekwa mahali pasipo julikana.

3. Mtu anaweza kuchukuliwa kwa namna ya rohoni. Kwakuwa mtu ni roho wanakuja kiuchawi na kumtoa ndani ya mwili kisha kumpeleka wanako taka (Yohana 6:63). Roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu, kwakua mwili bila roho umekufa, wanapochukua roho yake wanapanda roho ya mashetani ndani ya mwili. Ndipo matatizo kadha wa kadha yanamtokea mtu huyo.

Ndiomaana tukimrudisha mtu toka msukuleni anasema nilikuwa Tanga nalima mashamba ya katani, unapo muuliza sasa nani alikuwa kwenye mwili wako? Anasema jini, au paka au mbwa. Unaweza kuona mtu ndani ya familia anasababisha shida, ugomvi kwakuwa si mtu bali ni pepo aliye ndani ya mwili wake.
Mchungaji Dr. Godson Issa akimfungua binti huyu na kumweka huru.

Kuna wakati unaweza kumwona mtu anasumbua kwenye mtaa, mwingine anaacha kazi anatumia fedha vibaya, pia unaweza kuzaa mtoto kwenye familia hatari mno anasumbua sana ukaamua kumchapa kila siku, usimwaribu mtoto huyo kwamaana anaweza kuwa si mtu. Kristo alikuja kuokoa na kurudisha kile kilochotekwa na kuibiwa na leo amekuja ili wewe uokolewe kwa jina la Yesu.

Ulifunga ndoa na mume wako alikuwa safi, mtulivu, mpole lakini gafla anaanza kurudi usiku amelewa, anatoa maneno ya ajabu, unamuuliza umekuwaje? Hana jibu, mtu asiye na maarifa akiona mume wake yuko hivyo anaenda kwa mganga. Usifanye hivyo, mchawi hawezi kukusaidia, acha kwenda kwa mganga wa kienyeji tena mganga wa kienyeji ni mbaya kuliko mchawi, yeye anajua kuweka na kutoa uchawi.  Njoo kwa Yesu, yeye amekuja kuokoa na kurudisha kile kilichopotea, kuna uwezo wako umepotea, kibali chako kimepotea hata huwezi kufuatilia mambo yako, ndoa yako imepotea lakini Kristo amekuja kukuoka wewe kwa jina la Yesu.

Biblia inasema usimwache mwanamke mchawi kuishi (Kutoka 22:18), si kama Mungu alikosea bali ni kwasababu hawa wachawi ni wabaya wanaweza kumchukua mtu, mali yake na uwezo wake wakautumia watakavyo. Siku moja niliwahi kumkuta mtu kwenye kibao cha kanisa, nilipomwoji akawa mkali mno, nikamchukua nikamleta kanisani kisha nikamwombea, baada ya siku mbili mama yake akaja anataka mtoto wake, akasema kuwa alikuwa anapata msaada kupitia mtoto huyo, kumbe walimchukua wanamtumia kichawi. Leo Bwana anataka akutoe kwenye utumwa wa kichawi kwa jina la Yesu.
Showers of Glory Morogoro wakiimba na kucheza mbele za Bwana.

Sababu zinazo sababishwa mtu achukuliwe msukule ni kukosa maarifa, biblia inasema watu wangu wanapotea kwa kukosa maarifa (Hosea4:6), sababu nyingine inasabaibisha mtu kuchukuliwa mateka ni wivu (Matendo 5:17-21), sababu ya tatu ni dhambi. Dhambi inamfanya mwanadamu kukosa ulinzi wa Mungu na kuwa rahisi kwa shetani na mawakala wake kumchukua.
“nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo.” (Ezra 9:6-7)

Ili uweze kuwekwa chini ya ulinzi wa Mungu lazima umkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, ukisha mpokea Yesu utajifunza maarifa ya Neno la Mungu kwa namna hiyo unakuwa chini ya ulinzi wa Mungu na shetani hawezi kukuchukua mateka wewe kihurahisi, watoto wako na kile ulicho nacho. Mungu akubariki kwa moyo wako uliyo tayari kumfuata Kristo na kuwawaokoa waliotekwa. Ameni.

Share:
Powered by Blogger.

Pages