Sunday, September 10, 2017

MAPANDO YA KISHETANI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA – MOROGORO

JUMAPILI: 10 SEPTEMBA, 2017

MHUBIRI: MCHUNGAJI, Dr.  GODSON ISSA ZACHARIA (Sn)

Mchungaji Godson Issa Zacharia akihubiri katika ibada ya leo.
Mathayo 15:13 Imeandikwa, Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. 14 Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.   Katika neno ili tunajifunza kwamba kuna mahali pa kupanda ambapo ni kama shamba. Pia tunajifunza kwamba kuna Mpanzi aweza kutokea mbinguni au shetani na mawakala wake.  Maana yake ni kwamba Mungu aweza kupanda kutokea mbinguni, shetani na wanadamu wanaweza kupanda pia. Yohana 15:2-3 Imeandikwa, Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.

Mwanzo 1:27-28 Imeandikwa,  Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu anaweza kupanda. Kwa hiyo Mungu wetu ni mkulima  mwenye uwezo wa kupanda. Mwanzo 2:7-8 Imeandikwa, Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.

Kwa hiyo kama Mungu anaweza kupanda basi anaweza kuvuna pia. Galatia 6:7 Imenadikwa, “chochote apandacho mtu ndicho atakachovuna”. Yawezekana kuna mambo huyaoni kwa usahihi wake kwa sababu ya mapando ya kishetani. Shetani anaweza kupanda balaa, umasikini, mateso na mauti juu ya maisha yako. Kwa kawaida shetani anatumia wanadamu ambao wanaweza kuja kwako kama rafiki au mtu wa msaada. Unaweza kupanda kwa maneno ya kinywa chako. Mithali 18:21 Imeandikwa, “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;  Na wao waupendao watakula matunda yake.” Kwa hiyo ulimi unao uwezo wa kutumika kupanda mauti au uzima. Tumia vizuri ulimi wako kwa sababu  kwa maneno ya kinywa chako unaweza kupanda uharibifu, mauti, kukataliwa. Mfano, huwezi kujikataa mwenyewe alafu watu wengine wakakukubali. Maneno hasi unayotamka juu yako yana madhara sana kwa sababu kwa kutamka kwako unakuwa umepanda. Kinywa chako ni kifaa cha kupandia, Yawezekana akawa ndugu wa karibu. Huyu ni mtu anayeweza kupanda mabaya juu yako. Yanawezekana ndugu yako amekupandia roho ya kujipangia au uharibifu. Kuna mabaya yamekupata kutokana na maneno ya kinywa cha ndugu yako. Mfano; mtu anakutamkia, hautafanikiwa, utachelewa, huwezi kufanikiwa, huwezi kuanza, kwa maneno haya mtu kashakupandia mabaya. Pia kuna maneno yaliyozoeleka mitaani kama chizi wangu, masikini wa Mungu, mzuka na mtu anagonga, maana yake umepandiwa mabaya na umekubali.


Maneno haya ni mbegu. Kuna siku yataota na yatachipuka kwa kasi sana, amini haya utayapokea. Jitamkie Baraka, uzima, biashara, kazi, maendeleo maana neno ilo ni mbegu ambayo imepandwa. Mbegu ikiwa ndani ya ardhi kuna mambo ya kibiologia yanafanyika na hatimaye mche unachepuka na mwishowe kuzaa matunda. Panda leo kwa kinywa chako asema Bwana wa Majeshi.

Yeremia 4:3 Imendikwa, Maana Bwana awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba. Hii ni kanuni ya Mungu ya kupanda. Siku zote hapendi kupanda mbegu mahali ambapo kuna magugu tayari. Mungu anasema penye miiba usipande apo. Ulimeni udongo na upande mbegu yako. Mwili ni udongo na hivyo waweza kupandiwa kutoka kwa Mungu au shetani. Miiba hii ni shida, magonjwa kama Ukimwi, kichaa au kansa. Hii ni miiba itokayo kwa shetani. Miiba hii inaweza kuwa roho za majini, mizimu au vibwengo vimekaa ndani ya  mwili wako. Yeremia 1: 10 Imeandikwa, “angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Bwana ameweka maneno kwenye kinywa cha Yeremia. Maneno ndio mbegu sasa, konde ni biashara, kazi, ndoa yako. Kama kuna miiba hawezi kupandiwa Baraka hiyo ni lazima kwanza miiba iondolewa ndio mbegu ipandwe kwenye konde lako. Unaweza kumwambia mchungaji niombee biashara yangu ifanikiwe lakini nyuma yake kuna hirizi kwa hiyo Mchungaji lazima kwanza ang’oe hirizi ndo Baraka za Bwana zitaonekana kwako. Kama haujaokolewa dhambi ni miiba. Lazima kung’oa kwanza ndipo tupande. Mungu alikuwa ameweka maneno yake kwenye kinywa cha Yeremia lakini anamwambia Yeremia nimekuweka leo juu ya mataifa na falme ili kung’oa, kuharibu, kubomoa na kuangamiza. Kabla ujapanda ni lazima kwanza kung’oa.
Showers of Glory wakiimba na kucheza mbele za Mungu katika ibada ya leo.
Mathayo 13:24-30 Imeandikwa, Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. Bwana Yesu anatoa mfano wa mwenye konde alipanda mbegu baada ya kupanda wakati amelala akaja adui naye akapanda magugu. Wasaidizi wa Yesu wanamuuliza mbona ulipanda mbegu njema, konde limepataje magugu? Yesu aliwaambia wasaidizi wake haya magugu hayajapandwa na baba yangu wa mbinguni yawezekana aliyepanda ni adui. Shetani akipanda mbegu/magugu ile nyota yako haiwezi kufanya kazi tena. Mfano; Ndani yako kuna neema ya kufanya kazi ya Mungu, kuimba, kuonya, kufundisha lakini unakuwa ukifanya kazi ya Mungu kwa ulegevu, ukiona mtu anafanya kinyume na kusudi la Mungu jua ni kwa sababu ya magugu ya ibilisi. Unampenda Yesu lakini ndani yako kuna uongo, tama, uzinzi haya ndio magugu yenyewe. Kulala ni kama hivi ulipofika kanisani ukaokoka ukaanza kunena kwa lugha baadaye ukapunguza kwenda kanisani, ukapunguza kusoma neno la Mungu. Wakati huu ndio wakati wewe umelala uwezo wako wa kuomba haupo tena yule adui ndio muda wake wa kupanda magugu. U nani wewe unayelala unashindwa kufunga, unashindwa kuomba amka tena Bwana akuamshe kwa jina la Yesu unaweza ukasababisha shehena zetu zikatupwa baharini. Hatari ya pili ya kulala unaweza ukamezwa, Yona alipotupwa baharini  akamezwa na samaki.
Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu katika ibada ya leo.
Aliyepanda mbegu njema ni mwana wa Adamu na konde ni wewe na vitu vyote ulivyonavyo. Magugu ni wana wa yule mwovu, mwana wa mwovu ni wachawi, waganga, wasoma nyota, mawakala wa kishetani. Ibilisi na mawakala wake watakufanya uache kuomba, kuja kanisani hatimaye wanaanza kukupandia     magonjwa, Presha, kansa, unafukuzwa kazi. Wanaopanda wale ni wana wa uovu. Wavunao ni malaika wanajua hawa ndio tutakaowatuma. Sio mapenzi ya Mungu mtu kupatwa na mabaya, kumbe kuna mashetani yamekunuizia magonjwa. Kumbuka kila pando asilolipanda baba yangu wa mbinguni litang’olewa konde lazima lisafishwe tutuoe miiba kwanza. Kuna Baraka lakini haziwezi kuja kabla hatujang’oa miiba. Bwana anapanda ngano lakini shetani ndiye anayepnda magugu. Hauwezi kujenga wala kupanda mpaka magugu yameondoka.
Share:
Powered by Blogger.

Pages