GLORY
OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
KANISA
LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI:
03 SEPTEMBA, 2017
MHUBIRI: MCHUNGAJI BARAKA NJAMASI (Snp) MAHENGE
Mchungaji kiongozi wa mahenge akihubiri katika ibada ya leo |
Damu
ni kimiminika ambacho kipo ndani ya mwili na kazi yake ni kusafirisha chakula,
hewa (oxygen) ndani ya mwili au kiumbe hai. Damu kwa asili ndio inayobeba UHAI
wa mtu. Waebrania 12:24 Imeandikwa, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile
ya Habili. Hii ni damu ya Yesu ndio inenayo mema.Mwanzo 4:10 Imeandikwa,
Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya
ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Hawa ni watoto wa Adamu waliokuwa wakimtolea
Bwana sadaka za kuteketezwa. Kaini na Habili walikuwa wakulima na wafugaji.
Habili alimtolea Bwana sadaka ya ng’ombe walionona kutoka kwenye zizi lake.
Bwana akazitakabali sadaka zake na ndugu yake Kaini akaona wivu na akamuua.
Ndipo Bwana akamuuliza Kaini umefanya nini, maana damu ya ndugu yako
inanililia. Tunajifunza ya kwamba Damu inaweza kusema au kunena. Lakini baada
ya agano jipya ndipo Bwana akamtoa mwanae wa pekee afe msalabani. Kwa kufa
kwake damu yenye uhai ilimwagika, na ndio maana neno linasema ya kwamba damu ya
Yesu ni Damu inenayo mema.
Walawi
17:10-11 Imeandikwa, ‘Kisha
mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati
yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo
alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa mwili u
katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya
upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa
sababu ya nafsi.’ Damu ndio inayobeba uhai wa mtu. Tangu agano la kale
mpaka sasa damu inaleta upatanisho. Yesu alikufa msalabani ili aondoe laana juu
yetu. Damu yake ikamwagika kichwani kwa miiba ili akili zetu ziweze kuwa sawa.
Mathayo 27:29 Imeandikwa 29 Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake,
na mwanzi katika mkono wake wa kuume;
wakapiga magoti mbele yake,
wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!. Damu yake
ikamwagika kwa misumali ya mikononi. Yohana 20:27 Imeandikwa 27 Kisha akamwambia
Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako
uutie ubavuni mwangu, wala usiwe
asiyeamini, bali aaminiye. Alitokwa damu mikononi ili kutupa uwezo wa
kugusa na kupata, kwa sababu mikono inabeba sehemu kubwa ya maisha yetu. Yawezekana
ukishika pesa zinapotea, ukianza miradi haiwezi kuendelea. Leo iko damu ya Yesu
ili kurudisha uweza wako wa kushika kwa mkono wako na ukala matunda ya kazi
yake.
Damu ya Ubavuni.
Yohana 19:33-34 Imeandikwa 33 Lakini walipomjia
Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; 34 lakini askari
mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Hii ni damu
iliyomwagika ili kuturudishia uhai wetu.
Hii ndio damu inayobeba uzima wa ndoa zetu. Hii ndio damu inayozuia mabaya
juu na kila aina ya mauti juu ya maisha yetu. Itumie damu hii kutamka uzima juu
ya ndoa, kazi, biashara, elimu na kila kilichokwama na utakuwa mzima tena kwa
damu ya Yesu. Damu inasema asome,
amiliki, atawale, ashinde, azae, aoe, aolewe na kushinda kuliko kawaida.
Damu ya Mgongoni.
Yohana 19:1 Imeandikwa 1 Basi ndipo Pilato
alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Hii ni damu iliyomwagika
kwa sababu ya mijeredi 39 aliyopigwa mgongoni. Alipigwa baada ya Wayahudi
kumtafutia visingizio vingi sana lakini hawakupata hata sehemu yoyote. Isaya 53:5-5 Imeandikwa, ‘Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. 5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona.’ hii ndio damu inenayo mema dhidi ya
magonjwa, balaa na taabu juu ya maisha yetu.
Ni kwa kupigwa kwake tunapokea uzima kwa jina la Yesu.
Damu ya Usoni.
Luka
22:42,44 Imeandikwa ‘akisema, Ee Baba,
ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali
yako yatendeke. 44 Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba;
hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.’ Hii ni damu iliyomwagika pale msalabani
Getsemani. Ni kwa sababu Yesu alikuwa akiomba kwa kumaanisha akizibeba dhambi
zetu. Hii ndio damu iliyotuondolea mapigo juu yetu. Hii ni damu inayoleta
Kibali kwa sababu Uso ndio sehemu inayomtambulisha mtu katikati ya wanadamu.
Hii ndio damu inayonena kung’aa, kukubalika, kupendelewa na kupokea fulsa. Waebrania
9: 29 Imeandikwa, ‘Na katika Torati karibu vitu vyote
husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.’ Hii ndio
damu iliyomwagika ili kutupatanisha na Mungu. Kumbe tukipatanishwa na Mungu
basi tunakubalika hata kwa wanadamu.
Damu
ya Miguuni.
Luka
10:19 Imeandikwa ‘ Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu
zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.’ Hii ilimwagika
baada ya kupigiliwa misumali miguuni. Hii ni damu iliyomwagika ili kutupa uweza
wa kuzikanyaga falme za giza. Kama damu
ya Yesu inanena mema basi ipo damu inayonena mabaya juu yako. Kwa kawaida damu
ikinena mabaya basi mashetani ufuatilia na kutenda mabaya katika maisha yako.
Kwanini watu wanashida, wamekwama kibiashara, hasara, matatizo, ni kwa sababu
wapo waliotoa damu kwa waganga na hata sasa inanea icho kinachokukabili leo
maishani mwako. Ufunuo 12:11 Imeandikwa,
‘Nao
wakamshinda kwa damu ya MwanaKondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao
hawakupenda maisha yao hata kufa.’ Sasa nenda kwa damu ya mwanakondoo
na uzinyamazishe kafara zote zinazonena mabaya kwenye ulimwengu wa rohoni. Damu
ya Yesu inatupa uweza wa kupambana na nguvu za shetani na kupokea ushindi
kamili. Nguvu ya damu ya Yesu haijalishi mashetani hao ni wa ngazi gani. Hapa
duniani wapo mashetani wa aina nne. Majini ni mashetani wanaotegemea sana mila
za Kiharabu. Majoka hawa ni wale wenye asili ya nyoka, wakimng’ata mtu umwchia
sumu ya uharibifu. Majoka ndio Miungu wanao abudiwa katika maeneo mbalimbali
duniani. Mizimu ni mashetani ambao ni roho za watu waliokufa zamani ambao
hawakuwa katika Kristo. Na mapepo ni wale malaika walioasi pamoja na shetani
wakatupwa shimoni.
Kwa
kawaida shetani anatenda kazi kuptia mashetani. Ili mapepo au majini watende
kazi lazima wapewe Damu au kafara. Yaweza kuwa damu ya mwanadamu, mnyama, au
ndege. Ukubwa au wingi wa damu ndio ukubwa wa tatizo. Kinacholeta madhara ni
sauti ya damu iliyomwagwa. Damu ikisha mwagwa, mashetani wanakunywa ili
walisimamie tatizo. Lakini leo lazima unyamazishe izo damu au kafara zao kwa
DAMU YA MWANAKONDOO. Damu ya Yesu ikinyunyizwa juu ya maisha yako utamiliki,
utatawala na utatiisha. Tembea na neno ili upokee ushindi wako kila mahali kwa
damu ya mwanakondoo. Ufunuo 12:11 Imeandikwa,
‘Nao
wakamshinda kwa damu ya MwanaKondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao
hawakupenda maisha yao hata kufa.’
========== AMEN ========
KWA MSAADA ZAIDI
NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM:
pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE:
pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro