Monday, December 1, 2014

WALIOKUFA KWENYE MAZINGIRA YA KUTATANISHA-Na: ADRIANO MAKAZI (RP)

JUMAPILI: 30 NOVEMBER 2014 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO


Utangulizi: Somo la leo linaitwa Waliokufa Kwenye Mazingira ya Kutatanisha”. Imeandikwa katika WARUMI 14:7-9….[Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. 8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. 9 Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.]… Yesu ndiye mmiliki  wa walio hai na waliokufa. Biblia inaongelea kwa habari ya kifo. Lakini Je,  kifo ni kitu gani? Kifo (au mauti) ni 'roho', tena kimsingi ni ule utengano kati ya mwili na roho. Kutoka kwenye mavumbi ya ardhi, Mungu alimuumba mtu, na akampulizia puani mwake pumzi ya uhai, na mtu huyu akawa ‘nafsi-hai’. Kwa hiyo mtu anapokufa, ni ishara ya ule uhai kutoka ndani ya mwili wake.  


RP Adriano akifundisha Somo leo 30/11/2014
katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima -
Bonde la Maono Morogoro 
Wachawi wanao uwezo wa kumchomoa mtu ndani yake na kuondoka naye,  au kuweka roho ingine ndani yake na kwa namna hii mtu huyu anakuwa sehemu ingine akifanyishwa kazi mbalimbali kwa matumizi ya huyo mchawi. Unapoona ajali duniani leo hii, mara nyingi unakuta kuwa dereva akidai aliona kitu chenye kumzuia njiani na kupelekea gari  liingie porini na kusababisha vifo vya watu. Maeneo mengine unasikia watu wanajitoa mhanga, wafe kwa ajili ya vitu au  imani za dini zao au makusudio yao. Watu wa aina hii siyo kwamba wao wanapenda kufanya hivyo, ila shetani alishageuza miili  yao,  na kuweka roho za wanyama wengine kwa kuondoa ile roho halisi ya mwanadamu ndani mwao. Leo tutatapeleka maombi yetu mbele  za Bwana kwa sababu ya kuwepo  kwa watu waliokufa katika mazingira ya kutatanisha. 

Children Ministry wakiimba na kumchezea Bwana Yesu leo 30/11/2014 katika Bonde la Maono - Morogoro.


Katika YOHANA 6:63…[Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.]… Kwa hiyo, unapoona biashara yako haiendi, kwa mfano, ujue ipo roho nyuma ya hiyo roho ya hasara. Katika  mahusiano ukiona mambo yameharibika,  ujue ipo roho  kinyume na hayo mahusiano yenu. YAKOBO  2:26…[ Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa….Hata hivyo, Uhai waweza kutolewa na kurudishwa tena. 

Majeshiya Bwana ya Bonde la Maono Morogoro wakifuatilia maaandiko ya somo la leo 30/11/2014
liitwalo "WALIOKUFA KWENYE MAZINGIRA YA KUTATANISHA"


UFUFUKO KATIKA AGANO LA KALE

Kibiblia, katika 1 WAFALME 17:17…[ Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. 18 Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? 19 Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. 20 Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. 21 Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. 22 Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.]…. Lengo la shetani kuweka ugonjwa ndani ya mtu ni ili kuutoa uhai wa huyo mtu. Mtu kufa siyo jambo rahisi kihivyo. Mungu anapokuwa amemuumba mtu, anakuwa amempangia maisha marefu ya kuishi. Mungu hajamuumba mtu asiishi kwa muda mrefu. Wafu wanafufuka. Yeyote anayekataa kuwa wafu hawafufuki ujue huyo ni mchawi kwa sababu atakuwa na misukule wake na anaogopa endapo wakifufuka, itakuwa je wale misukule wake?


MAOMBI:
Natangaza ndoa iliyoparaganyika irudi tena kwa Jina la Yesu. Natangaza biashara iliyoharibika irudi tena kwa Jina la Yesu. Natangaza kwa Jina la Yesu, afya iliyodhoofika ikurudoe tena kwa Jina la Yesu. Amen



2 WAFALME 4:18-20 …[Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao. 19 Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake. 20 Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa….Elisha naye  anafufua kama ambavyo boss wake Eliya naye alifufua. Ikumbukwe kuwa, mtoto huyu alipatikana kwa miujiza, baada ya wazazi  kukaa muda mrefu bila kuwa na watoto, na sasa baada ya kupata mtoto, anakufa muda si mrefu. Mungu akeshakupa kitu hakunyang’anyi, na hiyo ni kanuni yake. Hata Lucifer, vile alivyopewa na Mungu alienda navyo shimoni, hakunyang’anywa na Mungu.


2 WAFALME 4:21-37…[Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka. 22 Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja,  ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena. 23 Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno. 24 Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia. 25 Basi akaenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu, katika mlima wa Karmeli. Ikawa, yule mtu wa Mungu alipomwona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, Tazama, Mshunami yule kule. 26 Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo. 27 Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na Bwana amenificha, wala hakuniambia. 28 Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?  29 Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto. 30 Na mama yake yule mtoto akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata. 31 Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu.    Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka. 32 Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake. 33 Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba Bwana. 34 Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake,    na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake;    mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto. 35 Kisha akarudi, akatembea nyumbani, huko na huko mara moja; akapanda, akajinyosha juu yake;    na yule mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake. 36 Akamwita Gehazi, akasema, Mwite yule Mshunami. Basi akamwita. Na alipofika kwake, Elisha akasema, Haya! Mchukue mwanao. 37 Ndipo akaingia, akamwangukia miguu akainama mpaka nchi; kisha akamchukua mwanawe, akatoka.]… Mara 7 ni utimilifu wa Mungu. Biblia inasema kuwa huyu mtoto alipiga chafya mara 7 na ndipo akafufuka.


UFUFUKO KATIKA AGANO JIPYA

Matukio hayo  mawili hapo juu ni ya Agano la Kale. Katika Agano Jipya, Yesu alifufua wafu wanne kama kielelezo, na wanafunzi wake pia walifanya hivyo hivyo. 


LUKA 8:40-42;49-55….[Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote. 41 Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake; 42 kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga….49.Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia,    Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu. 50 Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa. 51 Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye. 52 Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. 53 Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. 54 Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. 55 Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula.]…..Kama ambavyo  waombolezaji hawa walikuwa 'wakilia' na baadaye 'kucheka', hata katika maisha ya  kawaida, wapo  wanaoijifanya wanakuhurumia lakini  kumbe wanakucheka. Ole wake akuchekaye leo, kwa sababu siku yake ya kulia nayo inakuja katika Jina la Yesu.


LUKA 7:11-18…[Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. 12 Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. 13 Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. 14 Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. 15 Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. 16 Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. 17 Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.  18 Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote.]… Wale waliokuwa wamelibeba jeneza walisimama na msafara wao‼


MAOMBI
Naamuru kwa Jina la Yesu, msafara wa watu waliojiandaa kuchukua akili, msafara wa watu waliojiandaa kuchukua damu nyakati hizi  za Krismasi tunazoziendea, msafara wa watu waliojiandaa kuchukua nyota, msafara wa watu waliojiandaa kuchukua ufahamu, msafara wa watu waliojiandaa kuchukua akili yako, wote wasimame kwa Jina la Yesu. Naagiza katika nchi, bahari na anga waliojiandaa kuchukua wanao  wasimame kwa Jina la Yesu. Anayetumia nyota kwa shughuli zake, leo nasimamisha msafara wake kwa Jina la Yesu. Naamuru   mkono wa Bwana uguse biashara yako, ndoa yako, elimu yako, uzima wako kwa Jina la Yesu. Amen



YOHANA 11:1-44, Biblia inazungumzia Ufufuo wa Lazaro. Kumbe yapo  mambo yanaweza kukushika lakini  kumbe siyo ya mauti bali ni kwa utukufu wa Mungu.  Aliyelala sharti aamshwe. Kunapoenda 'utukufu', na 'aibu' iende huko huko. Kwa maana hiyo, hatuna sababu ya kuogoopa kuombea ‘maiti’ kwa sababu maiti akifufuka, huo ni ‘utukufu’ kwa Yesu, na  asipofufuka, ‘aibu’ pia ni kwa Yesu. Yesu anakuambia leo mwanaume kwa mwanamke,  ya kwamba “Ndugu yako atafufuka”….. Ukimwamini Yesu,  mambo yako  yaliyokufa yatafufuka. Ukimwamini Yesu,  Ndoa yako iliyokufa, itafufuka. Ukimwamini Yesu,  biashara yako iliyokufa itafufuka.


Yesu akitaka kuja kufufua hukutaka uliondoe jiwe kwanza. YOHANA 11:39…[Yesu akasema, Liondoeni jiwe.]… Leo ni siku ya kuondoa jiwe ili Yesu afufue mambo yako  kwanza. Liondoe jiwe la mashaka na hofu, liondoe jiwe lile la kutoamini kwa Jina la Yesu. wengine wanalamika kwamba hawaolewi, hawapati kazi, hawafanikiwi n.k. Ujue kwamba lipo  jiwe lenye kuzuia, na ni muhimu hayo mawe yaondolewe kwanza. Lipo jiwe wamekuwekea waganga wa kienyeji katika maisha yako. Kuondoa jiwe siyo kazi ya Yesu. hilo ni jambo  lililo juu yako. Kazi ya Yesu ni ya kufufua tu.


MAOMBI:
Naliondoa  jiwe lililowekwa lilinizuia nisifanikiwe, Aliyekaa kama jiwe, nakuondoa kwa Jina la Yesu. Leo naponda mawe yote yaliyokaa mbele yangu kunizuia kwa Jina  la Yesu. Amen



Kufufua ni mpango wa Mungu, wala huhitaji maombi mengi sana kusababisha ufufuo. YOHANA 11:41-43…[Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. 42 Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. 43 Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.]…Kumbe waliochukuliwa siyo wa kuombewa bali ni  wa kuitwa. Waliokufa wanasikia. Aliyekufa anasikia. YOHANA 11:44…[Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.]


Katika MATENDO 9:36-41... [Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. 37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. 38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. 39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. 40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. 41 Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.]….Petro  ambaye ni mwanafunzi wa Yesu, ndiye alihusika katika kufufua Dorkasi.


MATENDO 20:7-12…[ Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. 8 Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika. 9 Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. 10 Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. 11 Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake. 12 Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.]… Ni mbaya kusinzia wakati neno la Mungu linahubiriwa.  Hii ilikuwa ni ajali ya kuanguka toka kwenye jengo lakini Paulo akamfufua.


EBRANIA 9:35…[Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;]…Hapa ni idadi kubwa tu ya wanawake, Biblia haisemi ni mwanamke mmoja, bali wanawake, na kwamba siyo  mfu mmoja, bali ni wafu wengi walifufuliwa.


1 KORINTHO 15:12-19...[Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? 13 Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; 14 tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. 15 Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. 16 Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. 17 Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. 18 Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. 19 Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.]…. Mtume Paulo anasisitiza kwamba kama wafu hawafufuki, basi kuhubiri kwetu kote  ni bure.


Showers of Glory wa Bonde la Maono - Morogoro wakionesha vipaji vya vya kumuimbia Bwana Yesu leo 30/11/2014


Wapo wanaoamini kuwa wafu wanafufuliwa siku ile ya mwisho. YOHANA 5:25…[Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.]… Neno hili limesimama kwa 'nyakati mbili',  zile zijazo (nyakati za parapanda) na nyakati za sasa hivi. 


YOHANA 5:28-29…[Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. 29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.]… Aina hii ya ufufuo  unahusu wakati wa parapanda ya mwisho Yesu atakapokuja kuhukumu wazima na wafu.


MATHAYO 10:8...[Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.]….Wengi  wa wahubiri duniani leo hii, hawazungumzii kabisa habari ya kufufua wafu. Wengi hufanya kazi ya kupoza wafu, lakini huruka mambo ya  ufufuo, na kurukia ukoma na kutoa pepo.  Neno hili  la kufufua wafu siyo la wahubiri au mitume tu, ni kwa kila mtu amwaminiye Yesu Krsito maishani mwake anaweza kufanya hivyo.


© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
 /or
Contact our Senior Pastor:
 Dr. Godson Issa Zacharia
 (Ufufuo Na Uzima – Morogoro)

Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778
Share:
Powered by Blogger.

Pages