JUMAPILI: 23 NOVEMBER 2014 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
RP Adriano akiomba kwa ajili ya somo la leo "KIFUNGO CHA AKILI" tarehe 23/11/2014 |
KUTOKA 35:30-35….[Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; 31 naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; 32 na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba, 33 na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina.34 Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. 35 Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.]…. Kama tunavyojua, Mungu alimuandaa Musa kuwatoa wana wa Israeli kutoka Misri walikokuwa wanakaa kwa hali ya utumwa. Wanadamu tumeumbwa ili tumwabudu Bwana. Kazi kubwa kuliko zote mbinguni ni ya kumwabudu Bwana. Hata shetani naye anataka sana kuabudiwa. Wakati wakiwa njiani jangwani, Mungu alitaka wana wa Israeli wawe wanamuabudu. Hata hivyo Musa hakuwa na ujuzi wa uandisi au ufundi wa ujenzi wa nyumba ya Bwana. Mungu akawa anamwambia Musa kuwa wapo watu ambao wameshaandaliwa tayari na amewawekea akili ndani yao kwa hiyo kazi.
Kila mtu anatumwa kuja duniani kwa makusudi maalum. Imeandikwa
katika YOHANA 1:6-7...[Palitokea
mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7 Huyo alikuja kwa ushuhuda,
ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye.]…. Kwa hiyo Yohana tunaona hapa kusudio
la kuja kwake duniani. Haipaswi kukaa hapa duniani kama mtalii.
Yamkini umepewa akili uwe
waziri mkuu siku moja katika taifa hili. Lakini wajanja wachache
wameichukua akili yako na leo hii
upo tu mtaani bila chochote cha kufanania na hiyo nafasi. Pengine umepewa akili ufanye
biashara lakini leo hii huwezi chochote na wajanja wachache wanatumia akili yako
kufanyia biashara zao. Mungu alimpa ‘akili’ Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri,
wa kabila ya Yuda, ili kumwezesha
kufanya kazi ya werevu kujenga hema ya Bwana (KUTOKA 35:30-35). Kuna namna ya kutenda itokayo kwa
Bwana na ambayo inakuwa tofauti na utendaji wa watu wengine. Hata katika
uimbaji, siyo wote huvutia kwenye kuimba, bali wale ambao Bwana ameweka kitu
cha tofauti ndani mwao, utendaji wao
huwa tofauti kabisa. Kama umepewa kazi na huna akili, hutaweza kufanya hiyo kazi.
Showers of Glory - Bonde la Maono Morogoro wakimwimbia Bwana katika ibada ya leo Jumapili tarehe 23/11/2014. |
Yamkini Mungu amekuwekea akili ya kuleta majibu kwa mambo yaliyopo katika jamii yako. Katika
Biblia, 2 SAMWELI 14:19-20….[Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio
pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho
yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kuume, au kwa
kushoto, kukana neno lo lote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumwa wako
Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi
wako; 20 mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na
bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote
ya duniani.]…. Yoabu
alikuwa anajua siri mbalimbali za ufalme wa Daudi. Yoabu alimtumia huyu mama
ili akabadili mawazo ya mfalme ili amwachie Absalomu urithi wa ufalme wake badala ya Sulemani. Mtu mwenye akili hawezi kuletewa mambo mlango wa nyuma naye akayakubali.
Shetani huwa anatumia mtindo huu wa kugeuza akili za watu wafanye kinyume na
makusudio ya Bwana. Jambo hili la Yoabu la kumjaza maneno huyu mwanamke hata
hivyo lilishindikana.
MAOMBI
Kwa Jina la Yesu, Mungu akupe akili ya kuona mambo miaka mitano ijayo kwa Jina la
Yesu. Mungu akupe akili ya kufanya mambo makuu kwa Jina la Yesu. Ninaamuru
kwa Jina la Yesu, kila aliyekuja kwako amelishwa maneno, ashindwe kwa Jina la Yesu. Amen
|
Usikubali kuwa kituo cha kupokea kila neno mtaani mwako. Watu wa aina hii, wenye kuja kwako
wakiwa na maneno, usiwape sikio lako ili wasikuharibu. Kama Yesu angesikiliza
yale watu wanayoongea juu yake, asingeweza kuhubiri. Ndiyo maana aliwauliza wanafunzi wake
kule nje watu wanasema yeye ni nani. Huko
nje, watu walikuwa wanamwita Yesu ni nabii ajaye, wengine Eliya, wengine Yohana
Mbatizaji. Lakini wanafunzi wake, wale wa ndani walikuwa wakimuita Yesu kuwa ni
“Kristo, mwana wa Mungu aliye Hai”. Ni
vizuri sana uwe na Jina zuri kwa wale wa ndani. Kwa sababu, wale wa ndani
wanakuita sawa na Mungu anavyokuita. Wakati wale wa nje wanakuita wewe ‘maskini’, Mungu
anakuita tajiri.
MAOMBI
Baba Mungu wa Mbinguni, naomba unipe akili ya kujua jinsi ya
kutenda katika Jina la Yesu. Amen
|
1 NYAKATI 12:32….[Na wa wana wa Isakari,
watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa
vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.]…. Hawa wana wa Isakari walikuwa na akili ya kujua mambo
ya kufanywa kwa nyakati na majira yake na wana wote wa Isreali, na
Israeli yote iliwategemea sana hawa ili kufanikiwa.
Sehemu ya umati wa Majeshi ya Bwana waliokuwa wanafuatilia somo la leo 'Kifungo cha Akili' Bonde la Maono-Morogoro |
Ipo hatari kubwa sana ya kutoijua majira, na kinachoweza kumfanya
mtu ayajue majira ni akili. Imeandikwa LUKA
19:40….[Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, 42
akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini
sasa yamefichwa machoni pako. 43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako
watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; 44
watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya
jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.]….. Yesu Kristo kabla ya kuja
duniani alitabiriwa na manabii
mbalimbali, Musa, Eliya, Isaya na hata Yohana Mbatizaji. Ilipaswa watu wazisome
alama za nyakati kama ilivyoandikwa katika YOHANA
1:11-12…[Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.
12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake;]…
Msaada unaweza kuja lakini kwa kuwa hujui
majira, ukaukataa. Wokovu
unaaweza kuja lakini kama umefungwa akili, hutajua. Watu wengi hupenda kuziona
ishara. Maandiko yanasema ‘wana heri wale wanaoamini bila kuona ishara’. Yamkini uliwahi kuwakataa watu kwa
macho yako kukudanganya, na sasa unajutia.
Kuna watu leo hii unawaona wanapitia maisha yasiyo yao lakini kumbe Bwana
anawatengeneza. Usipende sana kufurahia wale ambao wameshatengenezwa na wengine. Hata kama unayemuona leo hii awe ni kijana au binti hajavaa vizuri kama unavyotaka, bado unayo nafasi ya kuja kumtengeneza mbele ya safari ili apendeze au aonekane kama unavyotaka. Hata 'cake' hupitishwa kwenye 'oven' yenye moto mkali kwanza na kuokwa kabla ya kuliwa, na
ikeshatoka huko hupendwa na watu wote.
Majeshi ya Bwana yakifurahia kwa shangwe Mafudisho ya Somo la "Kifungo cha Akili" leo tarehe 23/11/2014 |
MAOMBI:
Bwana unirudishie akili yangu. Roho ya uchungu roho ya kutopenda kusamehe niiachie kwa
Jina la Yesu. Naomba nguvu ya kusamehe kwa Jina la Yesu. Amen
|
Hakuna jambo gumu sana kama kusamehe. Mara zote, kila unapokumbuka
jambo ulilotendewa na mtu fulani ni rahisi sana hali ya uchungu kujirudia. Neno
la kuleta msaada kwako ni ‘kuachilia’. Unapomshikilia mtu moyoni mwako
huyo mtu hawezi kufanikiwa. Imeandikwa ‘laana
isiyo na sababu haimpati mtu’, lakini kwa kuwa ipo sababu, kile ulichotamka kwa huyo mtu kinampata. Pengine uliwahi kutamka
maneno au wewe kutamkiwa maneno na mtu maishani mwako, na matokeo yake hayo
yaliyotamkwa yamekuwa yakiyadhuru maisha yako. Leo ni siku ya maachilio. Lazima uachilie kwanza ili
Mungu aweze kukusamehe.
'Huwezi Kupigana Ukiwa Umekaa Chini Namna hii', ni maneno ya RP Adriano alipokuwa akifundisha mbinu za kupigana na Wanaozifunga Akili, leo 23/11/2014 |
WARUMI
10:9….[Kwa
sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni
mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.]…. Kumbe kinywa cha mtu chapaswa kifanye ukiri. Kukiri kunaenda na
kuamini, na kuamini huendana na kukiri. Huwezi kufayiwa ukiri na mtu mwingine.
Lazima imani iendane na matendo. Unapofanya hivyo, wale wenye akili timamu
watakucheka. Mfano, unakiri kuwa lazima mwaka huu niolewe, na unaanza kufanya
mazoezi ya jinsi ya kutembea na shela yako au jinsi utakavyokuwa siku ya ndoa yako. Unapokiri, kuna vitu vinaachilia katika ulimwengu wa
roho. Waweza kuendesha mfano wa gari hewani tu,
na kuonesha jinsi utakavyoendesha gari lako. Wenye akili wakikuona jinsi
unavyoendesha hilo gari hewani ambalo halipo watakucheka, lakini katika ulimwengu wa
roho yatakuja kutimia jinsi hiyo hiyo.
MAOMBI
Maneno niliyomtamkia na mtu yeyote leo nayavunja kwa Jina la Yesu. Maneno niliyotamkiwa na mtu yeyote nayo yakanipata, nayavunja maneno
hayo kwa Jina la Yesu. Amen
|
Wachawi wana uwezo wa kujua akili ya mtu hata kabla mtu huyo
hajazaliwa. Kawaida, mtu anapokuwa
amefanikiwaa kisiasa, kiuchumi, kimasomo au kibiashara ujue kuna nguvu nyuma yake inayomfanikisha kuwa hivyo.
KUMBUKUMBU 8:18…[Bali utamkumbuka
Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye
imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.]… Kumbuka Bwana Mungu maana
ndiye akupaye nguvu za kupata mume, Bwana Mungu ndiye akupaye nguvu za kupata mke, na Bwana Mungu ndiye akupaye nguvu za kupata ndoa n.k. Shetani
hana uwezo wa kufanya jambo lolote jipya.
© Information Ministry
(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi,
(Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
/or
Contact our Senior
Pastor:
Dr. Godson Issa Zacharia
(Ufufuo Na Uzima – Morogoro)
Cellphone: (+255) 757
550878 / +255 719798778