Monday, January 5, 2015

SOMO: MSINGI WA UTAWALA WA DUNIA-Na: ADRIANO MAKAZI (RP)


JUMAPILI: 04 JANUARY 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO


RP  Adriano akifundisha tarehe 4/1/2015
katika Bonde la Maono - Morogoro.

Utangulizi: Somo la leo linaitwa Msingi wa Utawala wa Dunia”. Dunia hii tunayoishi  na kuikalia ina mtawala wake, ambaye ameweka misingi ya aina fulani ili awe mfalme wake kwa wakaao ndani  yake. Huyu mtawala si mwingine bali ni 'shetani'. Leo ni siku ya kutoka kwenye hiyo misingi ya  mtawala wa dunia hii ili kutuwezesha kutawala, kumiliki na kutiisha kwa Jina la Yesu.
 

Mungu naye ana msingi wa utawala wake. Imeandikwa katika ZABURI 89:14…[Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako.].. Hata shetani naye alitamani kukikalia kiti cha Mungu ambaye ndiye alimuumba. Mungu Baba ameweka kiti chake cha enzi katika mbingu ya tatu.  Shetani hakuwahi kuingia katika mbingu ya tatu hata mara moja.  ISAYA 11:1-4…[Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. 2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; 3 na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; 4 bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.]…. Sisi wanadamu tunatoa hukumu kwa kuona au kwa kusikia au kuambiwa tu taarifa ya mtu mhusika. Lakini Mungu wetu hahukumu kwa namna hizi za kibinadamu,  bali kwa haki  yake.


Wokovu wa mtu  una watu watatu  ambao wanaweza kuujua, bila hata kujificha. Wa kwanza ni mtu mwenyewe, wa pili ni  shetani na wa tatu ni Mungu mwenyewe. Mungu anapokuangalia hakuoni wewe, bali humuona Yesu Kristo ambaye wewe umejificha ndani yake.

 
Makutano makubwa ya majeeshi ya Bwana Bonde la Maono  Morogoro wakifuatilia
Maandiko Jumapili ya terehe 4/1/2015 - Somo la Msingi wa Utawala wa Dunia.

Samsoni katika Biblia alipokamatwa na Wafilisti walimng'oa macho yake mawili na wakawa wanasherehekea. Wachawi na waganga wa kienyeji hufanya sherehe za kufurahia namna walivyokung’oa macho yako  mawili ya kiroho. Yamkini kuna mambo unayaona na kudhani  kuwa ndivyo ilivyo au ni ya kawaida lakini sivyo.  WAAMUZI 16:25-26 …[Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. 26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.]… Leo tunataka kijana aliyewekwa kukushika mkono akuache ili uzipapase nguzo mbili ambazo nyumba ya maisha yako inazitegemea.

 

WAAMUZI 16:27-31 …[Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. 28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. 29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. 30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. 31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.]… Shetani anaitwa mungu wa dunia hii. Maandiko yanasema katika 1 YOHANA 5:19...[Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.]… Maana yake,wewe unayempiga piga huyu ambaye dunia hii iko chini yake, kuna vitu atakunyima tu.

 

YOHANA 17:11-15…[Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. 12 Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. 13 Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. 14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.]…. Unapoona ulimwengu unakuchukia, au akiwepo mtu anayekuchukia, ujue wewe siyo kama wale, wa ulimwengu huu, na kwamba wewe upo ulimwenguni lakini umetengwa na huo ulimwengu wenye watu ambao hawajaokoka. Ulimwengu huu mfano wake ni wa 'mtu mbabe' anayeingia kwenye nyumba ya mtu mwingine na kuikalia hiyo nyumba, kufanya mambo yote apendayo sebuleni kwake na mwenye nyumba hawezi  kumfanya jambo lolote‼!

 

2 KORINTHO 4:4…[ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.]…

 

YOHANA 12:31…[Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.]… Mkuu wa ulimwengu huu yupo.

 

YOHANA 14:30…[Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.]… Yesu anamtambua shetani kama mkuu wa ulimwengu  huu.

 

YOHANA 16:11….[kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.]…. Shetani  nin mtawala wa ulimwengu huu. Na kwa sababu hiyo, kuna misingi  ambayo sheetani ameiweka ya utawala wake.

 
RP Adriano aakimuombea mmoja wa watu
waliohudhuria ibada ya tarehe 4/1/2015
 

WARUMI 12:2…[Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.]… Dunia hii ina namna yake,  jinsi ya kupata mali au umaarufu. Sisi tuliookoka, tunaonywa tusifuatishe namna ya dunia hii kwa sababu kuna hatari  ya nia zetu kugeuzwa au kuwa kinyume na  mapenzi  ya Mungu yenye kukuelekeza katika uharibifu. Usitamani utajiri wa wandamu unaokutana nao,  bali msubiri Bwana naye atakubariki. Usiambatane na watu ambao siri ya utajiri wao wala hauijui. Ndiyo maana baadhi ya watu ambao walinaswa na njia hizi za kishetani,  wanapotaka kutoroka kwenye hiyo mitego hufa vifo  vya  ghafla na huo huwa mwisho wa maisha yao.

 

Biblia pia inatukataza tusiipende dunia. I YOHANA 2:15-17…[Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. 16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. 17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.]… Hapa haimaanishi kuwa usivipende vile vilivyopo duniani (mathalani magari au majumba). Lakini, usihamishe upendo wako kwa Mungu na kuweka katika vitu vya dunia hii. Upendo wako na moyo wako usiweke kwenye vile vitu  alivyokupa Mungu,  bali upendo na moyo wako weka kwa Mungu wako. Biblia haisemi tusivitumie vya duniani, bali 'tunavyovitawala tusiviruhusu vikatutawala'. Vitu vya dunia hii vinayo nguvu ya kumtoa mtu kwenye  kumpenda Mungu.

 

YAKOBO 4:4…[Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.]…. Unapotaka kuwa rafiki wa dunia unafanyika adui wa Mungu.

 

ZABURI 18:15….[Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.]… Mtawala wa dunia anajenga misingi kwa lengo la kuwanasa wengi.  Maji  yalipopita, ile misingi  iliyokuwa imejificha, ikawekwa wazi. Maji yanapopita mahali hukangua udongo na kufichua vitu vilivyomo ndani ya ardhi. Endapo shetani amejenga msingi imara, kuubomoa si jambo rahisi.

 

1 KORINTHO 3:10…[Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.]… Inategemea wewe umejenga kwenye msingi wa  nani? Wakati wa ujenzi, msingi hutangulia kwanza. Shetani ambaye ni 'mungu  wa dunia hii' naye ni 'mjenzi lakini wa uharibifu'. Kila kilichojengwa katika  msingi wa Mungu hakiwezi kubomoka katika Jina la Yesu.

Majeshi ya Bwana  Bonde la Maono - Morogoro wakifuatilia somo 'Msingi wa Utawala wa Dunia'

 

MATHAYO 16:13-18...[Basi Yesu akaenda pande za KaisariaFilipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? 14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. 15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? 16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. 17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.]… Je, kanisa limejengwa juu ya mwamba upi? Yaani juu ya maneno  ya Petro kuwa ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai’. Kanisa limejengwa juu  ya yale maneno, na siyo juu ya Petro kama Wakatoliki wanavyofikiri, kwani Petro ni mwanadamu kama wanadamu wengine. Leo jenga ndoa yako, biashara yako, kazi yako na masomo yako - juu ya mwamba ambaye ni  Yesu Kristo.

 

UKIRI
Katika Jina la Yesu, Kanisa limejengwa juu ya Mwamba, na malango ya kuzimu hatalishinda. Nami leo Bwana najenga maisha yangu katika mwamba ambaye  ni  Yesu Kristo. Hakuna umaskini kwangu, hakuna ajali kwangu, hakuna vifo vya kutatanisha kwangu kwa  kuwa nimejengwa juu ya mwamba ambaye ni Yesu Kristo, na malango ya kuzimu hayatanishinda. Amen

 

Kama ni  kujenga kila  mtu anaweza kujenga. Cha muhimu, je, umejenga katika msingi gani? LUKA 6:46-49…[Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo? 47 Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. 48 Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. 49 Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.]… Mfano wa kwanza ni kwamba ukijenga vizuri nyumba yako na msingi ukauweka juu ya mwamba, mito na gharika zikija, hiyo  nyumba haiwezi kuanguka. Mfano wa pili ni wa watu ambao wanajenga nyumba juu ya udongo. Yesu katika mifano hii miwili alikuwa akiongea na wale watu wake ambao tayari wameshaokoka (wanafunzi wake). Hii ina maana kuwa,  hata kama umeokoka,  gharika na mito kutokea ni mambo ya kawaida. Kataa ‘wokovu wa spana mkononi’ – yaani haiishi  siku wewe bila kutenda dhambi. Toka katikati ya uovu. Shetani haogopi kuwa wewe umeokoka au unakuja kanisani. Shetani  anachoogopa kwako ni ule ‘utakatifu wako’. Ni heri leo kufanya  maamuzi ama ya kuwa 'baridi' au  'moto' na siyo kuwa 'vugu vugu'. 

 

UKIRI
 Leo Ninakataa  wokovu wa vuguvugu kwa Jina la Yesu. Ninakataa dhambi isinizinge mimi kwa  Jina la Yesu. Ninaomba neema ili kwamba ninapoyasikia maneno yako Yesu niyatende, ili niijenge nyumba yangu katika mwamba ambaye ni Yesu Kristo. Amen
 

 

Meshaki, Shedraki na Abednego walisimamia imani yao hata mbele ya Mfalme alipowahoji uso kwa uso kuhusu dhamira yao  ya kutoiabudu ile sanamu aliyoisimamisha Mfalme. Katika nchi nzima, walipatikana hawa vijana watatu tu ambao imani yao ilijengwa katika mwamba, ambaye ni Yesu Kristo.

 

1 WAFALME 16:34…[Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.]… Tatizo la mtu mmoja na mwingine laweza kufanana. Hata hivyo, kufunguliwa kati ya watu hawa wawili hutofautiana,  kwani kafara iliyopelekea kifungo chao nayo pengine imetofautiana. Mathalani  watu wapo wawili wenye 'shida ya kutozaa'. Lakini mmoja wao hazai kwa sababu alifungwa kwa kafara ya ng'ombe hamsini na mwenzake alifungwa kwa kafara ya kuchinja kuku. Ni dhahiri kuwa, huyu ambaye kuku alichinjwa kisha akafungwa asizae atakapo ombewa kufunguliwa kwake ni rahisi zaidi kuliko yule wa ng'ombe hamsini!!! Na mbaya zaidi,  wapo waliofunga wengine kwa kutoa kafara za damu za wanadamu!! Hiyo huwa na ugumu zaidi kufunguliwa kwake, lakini kwa Yesu Kristo hakuna jambo lisilowezekana.


 

UKIRI
 Kwa Damu ya Yesu Baba Mungu wa Mbinguni naomba unitakase kwa Damu yako ya thamani. Naamuru misingi yote ya umaskini na misingi ya balaa inayoshikilia akili yangu,  inayoshikilia nyota yangu, kule niliponaswa kwa kutokujua, ninaomba Damu ya Yesu  initoe kwenye balaa nilizowekewa, leo nitoke mahali  popote nilipofungwa.  Kwa maana imeandikwa 'Bomoeni bomoeni hata msingini', leo naibomoa msingi uliojengwa kwenye  kazi yangu, na kwenye ukoo wangu kwa Jina la Yesu. Amen 
 

 

© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Senior Pastor:

 Dr. Godson Issa Zacharia

 (Ufufuo Na Uzima – Morogoro)

Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778
Share:
Powered by Blogger.

Pages