Pages

Sunday, July 9, 2017

SOMO: NDOA ZA KISHETANI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

JUMAPILI: 09 JULY 2017

MHUBIRI:  PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha katika ibada ya leo kuhusu Ndoa za Kishetani.



Ndoa ni muungano wa maisha kati ya watu wawili walioamua kushi pamoja. Mara nyingi ndoa ni mkataba wa hiari  baina ya hao watu wawili, lakini  pia kuna nyakatai zingine ndoa hufanyika bila hiari ya watu wawili. Ndoa ni mktaba pekee ambao, ukishafungwa hauwezi kuvunjwa tena. Katika kitabu cha MWANZO 2:24 imeandikwa “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”. Lakini pia imeandikwa katika MATHAYO19:5akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?” Kwa hiyo ndoa ni hali ya kutoka kwenye wingi  na  kuwa umoja.

Mashetani  wapo wengi na  wanajitahidi  kuunganisha uzao  wa kijini na uzao  wa wanadamu na hatimaye kuzaa watoto. Tunaposoma katika 1KORINTHO 6:16-17 neno la Mungu linasema (Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. 17 Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye). Shetani anayajua haya maandiko, na hivyo kuwafanya watu wafunge ndoa za kishetani bila wao kujua. Mume au mke wa kiroho ana uwezo wa kuoa au kuoelwa na mtu. Lengo la mashetani kufanya haya ni ili  kuongeza mawakala wa mashetani kuleta uharibifu duniani.

Ndoa za kishetani zilianza muda mrefu sana. Katika MWANZO 6:1-2 Imeandikwa (Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.) Katika maandiko haya, wana wa binadamu wanatenganishwa na Wana wa Mungu. Ndivyo pia tunaposoma katika AYUBU 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Katika kikao hiki cha mbinguni, shetani naye anajihudhurisha kwa sababu naye ni malaika. Ndivyo pia ilivyoandikwa katika 1WAFALME 22:19-21 (Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. 20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee RamothGileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo,akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.). Tunajifunza kuwa Wana wa Mungu katika maadiko ya AGANO LA KALE ni MALAIKA, bali katika AGANO JIPYA wana wa Mungu ni wale WATU WALIOKOKA (YOHANA 1:12).



Maelfu ya wana wa Ufufuo na Uzima Morogoro, wakisikiliza kwa umakini somo kuhusu Ndoa za Kishetani




Tunasoma katika Maandiko EZRA 9:2 “Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili.” Tunasoma pia katika DANIELI 2:43Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo”. Tunajifunza kuwa kumbe inwezekana kuwepo na mahusiano ya kindoa kati ya wanadamu na malaika (aitwae shetani). Kibiblia shetani ni malaika-mchafu, kwa sababu alimuasi Mungu na kutupwa  nje. Hii ndio sababu siku zote kazi yake ni kuharibu maisha ya wanadamu.

Katika YUDA 1:6 imeandikwa “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu,   amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.” Na Katika UFUNUO 9:11 imeandikwa “Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni.” Haya majini yanaweza kukuingia katika ndoto, na pale unapoamka hujikuta umeshajichafua bila wewe kupenda. Mara nyingine huwajia watu kama binadamu kabisa ndotoni ukadhani ni watu wa kawaida na hivyo ukajikuta umeoa au kuoelewa nao. Ndoto ni bayana. Hayupo mtu aliyewahi kuota ndoto na alichoota kisitimie. Wewe unayeota ndoto za kuvishwa pete usidhani ni ndoto tu za kawaida, unashiriki tendo la ndoa, jua yapo madhara yatokanayo na aina hizi za ndoto. Ndiyo maana hadi sasa maisha yako yamekuwa si ya mafanikio.

Malaika wachafu (fallen angels) na mashetani wanaweza kubadilika na kuwa chochote. Wapo malaika wachafu wanaweza kujigeuza na kuwa kifuu cha nazi, au gari au mti au chochote kile. Kwa maneno mengine shetani anaishi kwa kanuni ya rohoni ya kuvaa umbo.

MIFANO YA KIBIBLIA KUHUSU MALAIKA KATIKA UMBO LA WANADAMU
1.      Ibarahimu aliwahi kuwapokea wageni vijana waliokuwa malaika bila yeye kujua, akawaandalia chakula, wakala  na kunywa.
Kitabu cha MWANZO 18:1-8Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. 2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, 3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. 4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. 5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. 6 Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. 7 Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. 8 Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala.” Tunajifunza kuwa mgeni anaweza kuja kwako na ukamsaidia lakini kumbe siyo mtu bali ni malaika. Kwa hiyo kumbe malaika anaweza kuja kwako na kula chakula au kunywa, lakini kumbe siyo mtu. Kwa hiyo, malaika wazuri au malaika wachafu wanaweza kuingia nyumbani mwako, na kwa maana hiyo siyo kila chenye umbile la binadamu ukakidhania ni mwanadamu mwenzako!!
2.      Mfano mwingine ni wa Lutu, ambaye pia katika Biblia alikutana na malaika. MWANZO 19:1-5 Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. 2 Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu,   hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha. 3 Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala. 4 Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote. 5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua.” Tunajifunza kuwa Lutu aliwajua hawa si wanadamu bali ni malaika, pengine kwa sababu walitokea kwa Ibarahimu, nduguye. Malaika wanaweza kukaa ndani ya nyumba, wakalala, wakapiga hata mswaki. Tujifunze kuwa hata unapopokea mgeni mtendee vizuri na endapo ni malaika mchafu anaweza kukuletea uharibifu. Katika mstari wa 5 tunajifunza kuwa watu wa mji wanaweza kuwaona malaika na kuwapenda kwa uzuri wao, na hata wakataka kuingilia nao kimwili (kuwajua). Kama basi wanadamu wanaweza kuwajua majini, inamaanisha kuwa ndoa za wanadamu na majini zipo.

3.      Katika kitabu cha YOSHUA, tunajifunza eneo lingine ambalo malaika walikutana na wanadamu. Katika YOSHUA 5:13-15 Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? 14 Akasema, La, lakini nimekuja sasa, niliamiri wa jeshi la Bwana. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake? 15 Huyo amiri wa jeshi la Bwana akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya vivyo.” Kumbe tunajifunza kuwa, kama malaika wa Bwana anaweza kuuvaa mwili na kushika silaha, basi hata malaika wachafu wanaweza kufanya vivyo hivyo. Kwa hiyo majoka na majini yanaweza kufunga ndoa baada ya kuvaa mwili wa kibinadamu. Wapo watu wanaoota ndoto za kunyonyesha watoto, wakati bado hawajaolewa au kuwa na mume.


Showers of Glory Morogoro wakimtukuza Mungu kwenye Ibada ya Leo.


JINSI GANI MAJINI HAYA HUWAINGIA WANADAMU?
Wake au waume wa rohoni ni wa hatari sana. Ni bora kuoelwa na mume wa kibinadamu hata kama atakuwa anakutesa kimwili kuliko hao wa kiroho. Ili kuwaepuka unapaswa kuzijua njia anazotumia shetani kukutegahadi kujikuta umefunga naye ndoa za rohoni. Mara zote shetani hupenda sana kuwaingia watu kuendana na vile vitu ambavyo mtu husika anavyopendelea maishani mwake, Mfano:-
1.      Pengine mtu ni mpenzi sana na maua fulani fulani, na hivyo akipita njiani aweza kuokota ua la aina hivyo kumbe ni mtego, na papo hapo jini huyu hupata nafasi ya kumuingia huyo  mtu.

2.      Wakati mwingine kuna mtu anakuwa anapenda sana pete au mikufu, na hivyo akiokota vitu vya aina hiyo alivyotegeshewa, basi jini huyu humwingia huyo mtu.

3.      Unaweza kuwa na jirani mchawi au pengine ni ndugu au mtu  unayesoma naye au kufanya naye kazi. Endapo  kila siku mtu  wa aina hii utakuwa unamuota ndotoni akikuingilia mwilini,  ujue siyo  kwamba uliota ndoto bali  ni  hakika uliingiliwa.

DALILI KWA WENYE WAKE / WAUME WA ROHONI KABLA YA NDOA:
Kwa mtu ambaye kimwili hajaoa au kuolewa, zifuatazo ni dalili kufahamu kuwa una mume  au mke wa rohoni:
1.      Endapo utakuwa unaota ndoto za kuwa umeolewa au kuoa, ujue hiyo ni  mojawapo ya ndoto.

2.      Kama wewe ni binti utakuwa huwapendi wanaume. Na kama wewe ni  mwanaume, unakuwa huna muda wowote wa kusalimiana na watu wa  jinsi ya kike. Ndiyo aina ya watu ambao hujiita ni WAGUMU!!

3.      Dalili nyingine na hasa kwa wadada, mathalani ni pale kila baada ya kuchumbiwa uchumba huo huharibika kwa sababu kadhaa wa kadhaa zisizo za msingi. Hii ni kwa sababu mume wa rohoni aliye naye hataki kuruhusu uolewe na huyo mume mpya.

4.      Dalili nyingine ni kuwa, mtu huharibu mwenyewe kile kitu alichokianzisha. Pengine unalo gari lako mwenyewe na unaliharibu bila kulitunza. Hii ni kwa sababu wale wanaokumiliki kiroho wanataka usipate msaada kokote ili baadae uwafuate wao.

5.      Dalili nyingine ni kuwa hakuna kitu chochote kitakachokaa au kudumu. Hata kama watoto  watazaliwa hawataishi muda mrefu.

6.      Dalili nyingine ni kuwa hata ukiota ndoto nzuri namna gani, ndoto hiyo husahaulika mara moja uamkapo. Hii ni kwa sababu wanaomiliki huiiba hiyo ndoto ili mtu  huyo asifanikiwe.

7.      Kwa wadada wakiwa  kwenye siku zao (hedhi), husikia maumivu makali sana. Na mbaya zaidi hukaa zaidi ya muda wa kawaida.

8.      Wakati mwingine mtu anakuwa akiishi  kivyake vyake tu, anakuwa na mpangilio fulani wa kuweka mambo yake vizuri kwa utaratibu chumbani mwake, na endapo mtu mwingine akivuruga chochote atakuwa mkali  sana kama pilipili akitaka alichokipanga kibaki vile vile tu.


Mmoja wapo wa watu akiombewa ili kufunguliwa kutoka kwenye ndoa za Kishetani.


DALILI KWA WANANDOA WENYE WAKE / WAUME WA ROHONI:
Kwa walioolewa au kuoa, zifuatazo ni  dalili  za watu wenye waume  au wake wa rohoni:
1.      Dalili ya kwanza nikukosa furaha ya mahusiano yao. Mke huona karaha kumuona mume anapotokezea.

2.      Watu wa aina hii usiku ukifika mke atalala na jeans kitandani. Na kama ni mume mwenye mke wa rohoni, kuna wakati mume atakuwa analala sebuleni au kwenye kochi.

3.      Wakati mwingine mke au mume wa aina hii hafurahii tendo la ndoa, baada ya kujikuta wote kama vile wanalazimishana.

4.      Wanakuwa na Ugumu wa kuzaa au kupata watoto. Mke anapata wakati mgumu sana kupata mtoto na pia ugumu wa kujifungaua pale anapokuwa anajifungua. Wakati mwingine mimba huharibika.


Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akiwaombea watu ili kuwatoa kwenye ndoa za Kishetani.



Kama wewe haumjui Yesu wala hujawahi kumpokea kuwa BWANA NA MWOKOZI wa maisha yako,leo ufanye hivyo ili maombi yetu ya siku  ya leo yaweze kuleta suluhisho  la kudumu kuwatimua waume na wake wa kirho  wanaosumbua maisha yako.

========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/