Sunday, October 15, 2017

INUKENI ENYI MALANGO YA MILELE

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI TAREHE 15.10.2017.

MHUBIRI: MCHUNGAJI. STEVEN NAMPUNJU (Rp)

Mchungaji Mwandamizi akihubiri katika ibada ya leo.
Mlango ni sehemu iliyoachwa wazi ili kuingia, au kupitishia vitu kuingiza ndani. Ni kizuizi ambacho kinazuia vilivyoko ndani visitoke nje bila utaratibu.Mathayo 16:18 Imeandikwa, “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda”. Hizi ni habari za mtume Petro, alijibu jibu ambalo lilimshangaza Yesu. Yesu akasema ni roho amekufunulia haya. Ndipo Yesu akasema juu yako nitalijenga kanisa wala malango ya kuzimu hayatakushinda. Kumbe kuna milango ya kuzimu.Kwa kawaida katika maisha yetu tunajenga kuta au uzio na kuweka mlango wa kuingia na kutokea

 Ufunuo 21:9 Imeandikwa, “Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibiarusi, mke wa MwanaKondoo”. Yohana aliuona mji wenye milango mitatu kila upande. Hii inatufundisha kuwa hata mbingu ina majina.Ezekieli 48:31 Imeandikwa, “na malango ya mji yatatajwa kwa majina ya kabila za Israeli, malango matatu upande wa kaskazini; lango la Reubeni, moja; lango la Yuda, moja; na lango la Lawi”. hata wana wa Israeli walikuwa na malango. Kabila kumi na mbili za Waisraeli walikuwa na mlango wao.

MJI WA SODOMA NA GOMORA
 Mwanzo 19:1-10 Imeandikwa, “Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha. Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala. Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote. Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua. Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake. 

Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi. Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu. Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, anataka kuhukumu! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango. Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango. Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango”.

Makutano ya Ufufuo na Uzima wakisikiliza kwa makini katika ibada ya leo.
Neno linasema Rutu alikuwa langoni pa mji wa Sodoma. Wenyeji wa mji walizingira nyumba ya Rutu. Watu hawa walizingira pande zote ili kuwatenda mabaya. Hii ina maana mtu aweza kuzingirwa na kufungiwa lango ili asifanikiwe. Watu hawa walikuwa wakali hata wakataka kuuvunja mlango wa Rutu. Malaika wakaufunga mlango ili asiharibiwe mtu wa Mungu.  Kila mlango wa mafanikio yako una malaika wa ulinzi. Katika habari hizi malaika wa ulinzi waliwapiga upofu watu wa mji ule. Wenyeji waliutafuta mlango wala hawakuuona tena. Upofu unaozungumziwa hapa ni upofu wa akili zao. Maana yake ni kwamba Mungu huwaondolea akili au fahamu adui zako ili wasifahamu na kukutenda mabaya.
MJI WA YERIKO.
Yoshua 6:1 Imeandikwa, “Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia”. Mji huu ulifungwa milango yake kwa ajili ya wana wa Israeli. Mji huu ulifungwa kwa sababu ya historia juu ya maisha ya wana wa Israeli. Waliogopa habari za miujiza na maajabu ambayo Mungu aliwatendea watu wake. Yoshua 5: 1 Imeandikwa, “Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng'ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hata tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli”.

 Mji wa Yeriko ulifungwa baada ya kusikia taarifa za ukuu wa Mungu. Watu wa nchi hii walijua kuwa wana wa Israeli walikuwa ni hatari tupu. Hata sasa songa mbele maana wanaokuzuia na kukufungia milango ya Baraka ni kwa sababu wamejua wewe ni hatari tupu. Kuna mahali umekosa kazi, umekataliwa, umetukanwa na kunyimwa ruhusa kuingia ofisi Fulani, si kwamba huna sifa bali adui amekujua kwamba ukipata wewe ni hatari tupu kwenye ufalme wa shetani. Amua leo kuchukua hatua uvunje malango yote ya ibilisi na walinzi wake, nawe utamiliki Baraka zako.

Wenyeji wa Mji walisikia kwamba Mungu wa Israeli alivyowatendea wana wa Israeli. Wakajua jinsi Mungu alivyowapa Maana kule jangwani, jinsi alivyowapa maji matamu katikati ya jangwa na hata habari za miujiza ile ya kuigawanya bahari. Hata leo lipo neno la Mungu ambalo ndio fimbo yetu. Waliposikia miujiza hii wakawekwa walinzi ili kulinda malango ili wana wa Israeli wasiingie. Kwenye maisha haya tuna safari kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. Wanadamu wanapoona mtu anabarikiwa wanaanza kuona wivu. Kwa kawaida wachawi wakikuona wivu huchukua hatua ya kuanza kukuzuia usifike kwenye hatima yako. Silaha yao ni kufunga milango ambayo ungepita na kuifikia hatima yako. Shetani anatumia kizuizi cha muda au cha milele kuzuia. Leo lazima uamue kung’oa malango ya uovu ili umiliki Baraka zako.

Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu.
Mashetani waweza kuingia ndani ya maisha ya mtu na kuwa chochote. Mashetani wanaweza kugeuka na kuwa mlango wa kuzuia Baraka zako. Jini anaweza kuingia ndani ya mtu na anakaa kama mmiliki wa mwili. Wengine wanabadiliksa na kuwa matukio ya kifo. Haya yanatokea kwa sababu kuna waliokaa kama malango ya kuzuia Baraka zako. Yako majini yameelekezwa kuzuia au kuhakikisha huwezi kuingia ofisi fulani. Hii ni kwa sababu wanajua kwenye ofisi hiyo kuna mtu ambaye ana Baraka zako. Amua leo kutia ufahamu na kuomba kwa bidii ili kumwondoa mlinzi au kila anayezuia usizifikie Baraka zako.

Zaburi 24:1-10 Imeandikwa, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila. Atapokea baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake. Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita. Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu”.

Malango yaweza kuwa kizuizi cha kielimu, kazi, biashara, Kiuchumi na familia. Malango haya haya yana wekwa kwa namna ya kutokuwa tayari kuondoka. Haya ndiyo malango ya milele ambayo tumepewa mamlaka kuyaondoa leo kwa jina la Yesu. Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao Bwana na Mungu wa Yakobo. Kwa kuwa unamtafuta Bwana naye atakupa nguvu ya kuyainua malango ya milele. Waliokuzuia wote watakimbia kwa jina la Yesu. Ewe umtafutaye Bwana unayo mamlaka ya kuyainua malango. Jifunze jambo kwamba KUINUKA NI ISHARA YA KUONDOKA.

Showers of Glory wakisifu na kucheza katika ibada ya leo.

Malango haya ni mashetani yanayoweza kuhoji. Shetani na mawakala wake hawaondoki kwa kuombwa ila kwa amri kutoka kinywani mwa wale wamtafutao Bwana. Maana Bwana wa utukufu akiingia shetani hawezi kukaa. Bwana wa Utukufu ndiye Mfalme wa Utukufu. Nenda kwa neno la Bwana ukalikabili lango na kulibomoa kwa jina la Yesu. Lazima uyaondoe malango yaliyoko mbele yako ili Baraka zako ziwe dhahiri. Kama malango hayajatoka basi kuna mambo hutoyapata.

KWA MSAADA ZAIDII NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798 778
(WhatsAssp & SMS only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogorohttp://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages