Sunday, December 17, 2017

MATEKA CHINI YA BAHARI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

MCHUNGAJI KIONGOZI: DKT. GODSON ISSA ZACHARIA

JUMPILI: 17, DISEMBA, 2017

MHUBIRI: MCHUNGAJI, DKT. HAPINESS MUHIMBULA (RP)

Mchungaji Mkaazi, Dkt. Hapiness Muhimbula (RP)
Kwa kawaida shetani ana maeneo matatu ya utawala. Maeneno hayo ni Bahari, Anga na Nchi kavu. Katika maeneo haya yote zina idara mbalimbali kwa ajili ya kufunga maisha ya watu. Anweza akawa mzima mwilini lakini rohoni katekwa na maefungwa chini ya bahari. Kupitia somo hili utajifunza kuhusu dalili za watu waliotekwa chini ya bahari na namna ya kuwafungua. UFUNUO WA YOHANA 12: 7-12 Imeandikwa, “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;  nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.  Nao wakamshinda kwa damu ya MwanaKondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.  Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Mwanzo 6:1-3 Imeandikwa, “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.”  Kuna maisha yanaendelea chini ya bahari.  Kuna kila kitu chini ya bahari, magari, nyumba na vyumba vyake na kila aina ya starehe. Hawa ni mashetani wa hali ya juu sana.
Tangu mwanzo maji yalichukua sehemu kubwa ya dunia. Hakukuwa na utengano kati ya maji na nchi kavu. Shetani alipotupwa chini alianzisha utawala wake huko chini. Makao makuu ya Ibilisi ni chini ya bahari ya Hindi. Hapa Mungu anafundisha kwa habari za kuzimu ya Baharini. Kuzimu ina mifumo ya kijeshi yenye ubunifu mkubwa kuliko majeshi ya serikali za wanadamu.
EZEKIELI 29:1-3 Imeandikwa, “Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote; nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.” Huu ni mto wa Farao lakini ndani yake kulikuwa na joka. Kuna wakati uliwai kupewa dawa na mganga wa kienyeji na ukaelekezwa kuoga maji ya mto fulani.
ISAYA 27:1 Imeandikwa, “Katika siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzongazonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.” naye atamwua Yule joka akaaye baharini. Maji ya bahari yana muunganiko na mashetani. Lakini maji haya kila aliyeyatumia kwa maelekezo ya waganga aliapatwa na balaa na mikosi.
Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu katika ibada ya leo.
UFUNUO WA YOHANA  10:1-6 Imeandikwa, “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.  Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike. Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;
Akaweka mguu wake juu ya bahari. Maana yake ni kwamba shetani anakaa baharini, angani na nchi kavu.  Kuzimu hii ya bahari ina malango, walinzi na mageti yaliyofungwa kwa ustadi wa hali ya juu. Vifungo vya kuzimu ni kama vile walivyokuwa wamefungwa wakina Paulo na Sila. Yawezekana kuna vitu au mtu aliyepelekwa kuzimu. Kuzimu hii ina vyumba vyenye walinzi wa aina mbalimbali kuhakikisha kila aliyefungwa hawezi kufunguliwa kutoka kuzimu. Vifungo vya namna hii havitoki isipokuwa kwa maombi ya mwenye haki.
ISAYA 49:24-26 Imeandikwa, “Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu.  Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.” Mungu wetu ni mwenye nguvu hivyo tukiomba kwa jina lake watafunguliwa. Kumbe kinachoweza kuwatoa watu baharini ni nguvu ya Mungu kupitia jina la Yesu.
Baadhi ya Makutano waliompokea Yesu wakiongozwa sala ya Toba.
ISAYA 42:22 Imeandikwa, “Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.” Ndio maana Mungu akamfunulia nabii Isaya kwamba kuna watu wametekwa, kufungwa au wameuawa isivyo halali. Ndio maana Mungu akamwambia Isaya lazima apatikane asemaye Rudisha. Mungu aliyasema haya kwa sababu anajua bahari, mito na Maziwa yamemeza watu wengi. Lakini maombi ya kumtoa mtu baharini ni maombi ya kivita ambayo yanahitaji kujikana.
UFUNUO WA YOHANA 17:1-2  Imeandikwa, “Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;  ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.”  huyu kahaba mkuu aketiye juu ya maji. Huyu ni shetani katika mwili wa wanadamu. Ndio maana leo kuna watu wanafanya ukahaba kwa sababu wote wamepandwa na roho za kishetani. Huyu ni shetani anayetenda kazi hadi kwa wachungaji. Shetani anavuvuia roho ya ukahaba na uzinzi hata kwa watu waliokoka. Lazima tusimame imara na kupambana kwa nguvu zako zote.
TABIA ZA WATU WALIOTEKWA BAHARINI
WANAKUWA NA KIBURI SANA. Ayubu 41:1 Ieandikwa, “Je! Waweza wewe kumvua mamba kwa ndoana?  Au, kuufunga ulimi wake kwa kamba?”  kuna watu walikuwa wanyenyekevu lakini leo wamekuwa na kiburi sana. Ukiona dalili kama hiyo faamu kuwa mtu huyo kashatekwa na mashetani wa baharini.
KILA BIASHARA ANAYOANZA INAHARIBIKA. Watu wa namna kila biashara atakayofanya huwa inaharibika kwa sababu mashetani wana tabia ya kusimamia biashara. Ndio maana kuna waganga wanaotoa ulinzi wa biashara kwa kuelekeza watu wakuge maji ya baharini.
KUVUNJIKA KWA NDOA. Watu waliotekwa chini ya bahari wana tabia ya kupenda kuoa wake wengi.  Katika maisha haya
Makutano wakifuatilia neno la Mungu wakati wa Ibada kuhusu mateka chini ya Bahari.
kuwa na mume mmoja na wake wengi  lazima vurugu zitokee. Ndio maana kuna talaka nyingi kwa watu wa mwambao wa Pwani. ISAYA 4:1 Imeandikwa, “Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.
NDOA ZA KISHETANI. Kuna mengi yanayotokea leo duniani kwa sababu ya watu wamemilikiwa na shetani.  Ndio maana mwanaume anaweza kufunga ndoa na mwanaume mwenzake. Hata walioana katika ulimwengu wa mwili bado ndoa zao zina matatizo makubwa. Ni kwa sababu kuna mashetani yanayotawala maisha yao na ndio maana hakuna furaha ya ndoa. Katika dalili kama hizi fahamu kuna mashetani kutoa baharini. Mashetani wa bahari wametumwa kuchinja na kuharibu. Mwanaume anaweza kumpa mkewe pesa kwa ajili ya matumizi lakini mke akanunua vitu kinyume na matarajio. Ugomvi unaanzia hapo.
WANASIMAMIA MAVAZI AU WANAONGOZA MITINDO. Haya mashetani wa baharini yana idara maalum inayohusika na kusimamia mitindo ya vitu mbalimbali. Kuna mashetani yaliyotumwa kwa ajili ya mitindo ya mavazi. Kuna mitindo ya mavazi, mawigi ya aina mbalimbali, namna ya kunyoa mfano Viduku. Staili mbalimbali za kusuka nywele.

Baharini kuna idara nyingi sana na zinasimamia matukio ya kutisha yanayotokea duniani. Kuna idara inayohusika na kuanguka kwa majengo yenye watu wengi ili wachinjwe na kupelekwa kuzimu. Idara nyingine inaratibu matukio ya ajali za moto.
Mchungaji Dkt. Hapiness Muhimbula (RP) akifungua mtu kutoka vifungo vya mashetani wa baharini.

SABABU ZA KUTEKWA CHINI YA BAHARI
DHAMBI. Hii ni sababu ya kwanza ili mtu aweze kutekwa na ibilisi. Kwa sababu kila atendaye dhambi upungukiewa na utukufu wa Mungu.
MATAMBIKO.   Haya ni matukio ya kimila yanayoambatana na kutoa vitu mbalimbali. Katika matambiko mtu anaweza kupeleka kitovu cha mtoto.
MUZIKI WA DUNIA. Muziki wa kidunia una uvuvio wa kishetani. Kila muziki na wanamuziki wake wengi wanategemea mashetani wa baharini.
Kuna sababu nyingi sana kama Mavazi. Wengine wametekwa kwa sababu ya kuazima nguo za watu wengine. Wengine walichukuliwa kwa sababu ya kuoga mtoni. Wengine ni kwa sababu ya sherehe za usiku na ngoma za kienyeji.
Ukiri: Nakataa kukaa chini ya baharini kwa jina la Yesu. Navaa uweza na silaha za Bwana za Vita na ninapambana na mshetani waliotumwa kutokea baharini, mtoni, ziwani na ninawaondoa wote kwa jina la Yesu. Ninaamuru malaika wa Bwana wavae sura yangu kwa uweza wa Roho Mtakatifu na kuvamia malango ya bahari kwa jina la Yesu. Ninavunja silaha zote ambazo majini ya baharini wamezituma kwangu, naziondoa leo kwa jina la Yesu. Nahama leo kutoka vifungo vya kuzimu kwa jina la Yesu.
Binti akifunguliwa kutoka vifungo vya mashetani ya baharini.
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
(WhatsAssp & SMS only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro       http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/




Share:
Powered by Blogger.

Pages