Pages

Sunday, March 25, 2018

VIKAO VYA UHARIBIFU


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI: 25 MACHI, 2018

   
Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha somo la vikao vya uharibifu katika ibada ya leo.
Utangulizi: Vikao ni mikutano ya wanadamu wanapokutana ili kuamua jambo liwe kwa wema au kwa ubaya. Katika kila maisha mtu anapoenda  chini au juu panakuwa na kikao cha kumpandisha au kumshusha katika ngazi. Maamuzi ya vikao ndio yanayosababisha mtu apande au ashuke kutoka ngazi Fulani. Pia hata katika maisha ya kawaida huwa kuna vikao. Hata mbinguni huwa kuna vikao. Kwa mfano, kabla Yesu hajatumwa kuwaokoa wanadamu duniani, kwanza kilikaa kikao mbinguni.

 AINA 3 YA VIKAO
  • VIKAO VYA MBINGUNI
  • VIKAO VYA BINADAMU
  • VIKAO VYA KISHETANI

·         VIKAO VYA KIMBINGU.
 Hivi ni vikao vya utatu Mtakatifu kule mbinguni. Hivi ni vikao kati ya Mungu baba kama kiongozi, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu. Pia kinaweza kuwa kikao baina ya malaika watakatifu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya ufalme. Mungu aliwahi kukaa kikao ili kuwachafulia usemi watu wale waliokusudia kujenga mnara wa Babeli. “Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.” Mwanzo 11:5-7
Pia kuna wakati ambao Ahabu aliwatenda udhalimu wana wa Israeli Mungu akapanga kumwangusha. Kabla ya anguko lake kwanza kilifanyika kikao kule mbinguni. Baada ya kikao akatokea pepo akasema ataenda na kuingia vinywani mwa Manabii na kuwa uongo. 1 Wafalme 22:19-22
Ili vita ipiganwe lazima kuwe na kikao. Kwa hiyo kabla ya vita lazima kulikuwa na kikao kwa ajili ya vita hiyo. Ufunuo wa Yohana 12:7

·         VIKAO VYA KIBINADAMU.
Hivi ni vikao vya wanadamu kabisa. Hivi hufanyika kulingana na taratibu za kitaifa, mashirika, mikoa, familia au ukoo. Hivi hufanyika kwa ajili ya ustawi wao. Kwenye vikao hivi huwa vinapanga nani afanikiwe au asifanikiwe. Kupitia vikao hivi watu ufukuzwa kazi au apate kazi. Vikao hivi vinaweza kuwa halali au visiwe halali. Vikao hivi vinaweza kupitisha mipango ya kumwangamiza mtu Fulani. Wanaweza kuweka mikakati ili kumwondoa mtu kwenye nafasi yake ili waingie wao. Hivi vikao vinaweza kumpa mtu kitu asichostahili. Matokeo ya vikao hivi kwa desturi huwa ni mtu mmoja akalia na mwingine akacheka.
Platform Ministry wakioongoza sifa na kuabudu katika ibada ya leo.
·         VIKAO VYA KISHETANI.
Hivi ni vikao vilivyovuviwa na nguvu ya shetani. Vinaweza kuwa vikao vya wanadamu lakini vina nguvu ya shetani nyuma yake. Shetani Anaishi kuzimu na ana mawakala wake duniani. Anatumia wasihiri, wasoma nyota, wachawi na waganga ili kujadili maisha ya watu. Baada mijadala maamuzi ya mabaya ufuatia ili mtu aangamie. Wachawi hawa huwa na maeneo maalum ya kukutania na kupanga uharibifu wao. Vikao vya Kishetani ndio

“Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.” Yohana 12:31

·         LENGO LA VIKAO VYA UHARIBIFU
 Lengo mama la vikao vya uharibifu ni kuhakikisha kwamba mtu anaharibikiwa katika maisha yake au kuhakikisha mtu anakufa.
WAJUMBE WA VIKAO; lazima wawe watu wanaokufahamu vizuri. Hawa huwa watu wa karibu sana na wewe, mzazi, ndugu, rafiki au mke/ mume wako. Wajumbe hawa wanayafahamu vizuri maisha yako. Kwa hiyo kupitia hawa ni rahisi sana kukuangamiza. Wajumbe huwa wanakujua kwa undani zaidi. Vikao hivi hufanywa na watu wanaokufahamu vizuri.

·         AGENDA ZA VIKAO.
Agenda za vikao hivi haziko mbali na lengo mama. Agenda zao zinalenga uharibifu juu ya maisha ya mtu. Hizi huwa ni agenda ambazo misingi yake ni kuharibikiwa. Agenda zinaweza kuwa mtu apate ajali, kazi iharibike, elimu, uchumi udolole. Agenda zote nyuma yake zimejaa chuki na wivu. Walikuwepo watu wa dini walioona wivu juu ya kazi walioifanya mitume wa Yesu Kristo. “Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;” Matendo ya Mitume 5:17

Agenda za vikao hivi hujadiliwa na wajumbe wanaokufahamu vizuri. Wajumbe wa vikao vya uharibifu lazima wawe watu wanaokufahamu. Kwa desturi mtu wa kukuangamiza lazima awe mtu wako wa karibu. Kumbuka Ibilisi alikuwa Kerubi afunikaye kule mbinguni lakini akamwasi Mungu. Absalomu alimwasi baba yake Daudi lakini alikuwa baba yake. Samsoni alifungwa kamba na ndugu zake wa karibu. Kama haitoshi Yuda alikuwa mwanafunzi wa karibu sana na Yesu lakini ndiye aliyemsaliti Yesu.

Kwenye vikao hivi mabaya huamuliwa na kuwekewa mikakati. Kwenye vikao hivi wachawi hupeleka mashitaka. Wachawi wanaandika majina ya watu kwa damu za wanyama,ndege na wanadamu na kuyaweka kwenye madhabahu zao. Jina likipelekwa kwenye kikao chao lazima lijadiliwe ili upatwe na mabaya. Mtu anapojadilika kwenye kikao utaanza kusikia misiba, mimba imeharibika, hawezi kuoa lakini alikuwa anajiandaa, anasoma lakini hawezi kufaulu, biashara inadolola, ndoa na uchumi vinayumba. Leo lazima uwavunje wajumbe wa vikao hivi kwa jina la Yesu. Yeye aliyejadili ili usiolewe, usipate kazi, ndoa, mitaji nawashambulia kwa jina la Yesu. Unayo damu na jina la Yesu ambavyo ni silaha za kuvunja vikao vya uharibifu.
Jifunze jambo kwamba hakuna kinachotokea ambacho hakikupangwa mahali. Hakuna kilichotokea kwenye maisha yako ambacho hakikupangwa mahali. Huzuni, hasara, majuto, matatizo na hasara zinazokupata zote zinatokana na vikao vya uharibifu. Wao wamekaa kikao cha uharibifu lakini mbingu imekaa kikao cha uzima kwa jina la Yesu. Hakuna mabaya yanayotokana na Mungu tunayemtumikia. Maombolezo 3:33
Maelfu ya watu wakiabudu katika ibada ya leo  katika nyumba ya Ufufuo na Uzima Morogoro.

·         MIFANO YA VIKAO KWENYE BIBLIA
Kikao cha uharibifu dhidi ya Danieli. Danieli aliwekewa kikao cha uharibifu kwa sababu ya Sifa zake. Danieli alikuwa amepata sifa kwa Mfalme kwa sababu ya Roho aliyekaa ndani yake. Danieli alikuwa na hekima ya Mungu ndani yake. Lakini kikao cha kumwangamiza kilikaa kwa sababu walisikia tetesi kuwa mfalme Dario anakusudia kumwinua Danieli. “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.” Danieli 6:1-3


Kikao cha uharibifu kinakaa kwa sababu maalum. Wakuu hawa walitafuta sana namna ya kumpata. Waliangalia wapi katenda makosa wala hawakupata. Lakini kutokuwa na hatia au kosa sio sababu ya wajumbe kuacha kumpangia mabaya mtu. Mawaziri na maamiri waliamua kutafuta njia mbadala ya kumwangamiza. Hata Danieli alitafutwa kupitia mambo ya Mungu wake. Unaweza kutafutwa kwa sababu ya Imani yako. Lakini yupo Yesu upande wako kukupigania. ”Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.” Danieli 6:4-6


Wajumbe wa kikao cha uharibifu wanaanzia watu wawili na kuendelea. Kupitia vikao vyao maazimio mbalimbali upitishwa na kuwekewa namna ya kutekelezwa. Wajumbe wa vikao lazima wafanye (shauri) maamuzi kwa pamoja. Na kwa desturi wajumbe wa vikao hivi hukutana kwa siri. Mfano hapa Danieli alikuwa miongoni mwa Mawaziri lakini hakushirikishwa kwenye kikao. Maana yake Danieli hakuwa kwenye kikao lakini yawezekana jina lake lilikuwa kwenye orodha ya waliohudhuria. Huu ulikuwa kama mtego ambao umewekewa muda maalum. “Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.” Danieli 6:7-8
Lakini kumbuka maadui zako watakusanyana kwa ajili yako lakini hawatafanikiwa. Na wote watakao kusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako kwa jina la Yesu. “Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.” Isaya 54:15

Maelfu ya watu wakisikiliza somo la vikao vya uharibifu katika ibada ya leo.
Baada ya maazimio lazima waandae hati za mashtaka. Wajumbe wa vikao hivi wanaorodhesha makosa yako na mabaya wanayokusudia yakupate. Danieli aliandaliwa mashitaka kuhusu imani yake. Kuna mashtaka yameandaliwa kupitia taratibu za kawaida lakini kumbe kuna mtu analengwa ili aangamie. Danieli alipogundua hila zao  akaanza kuchukua hatua kwa kufanya maombi mara tatu zaidi. Lengo la mashtaka ni kumdhoofisha mtu lakini Danieli hakudhoofika. Bali Danieli aliomba kwa bidii ndio maana hata alipotupwa kwenye tundu la simba hakumezwa na simba. “Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku. Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Danieli 6:9-13


Ni vizuri umjue Mungu unayemtumikia. Hata mfalme Dario alitambua uwezo wa nguvu za Mungu wa Danieli. Wewe unaye Mungu anayeweza kuokoa yuko upande wako. Kuna matatizo yanayokukabili lakini Yehova anajua namna utakavyookolewa kwa jina la Yesu. “Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lolote lililo marufuku, wala amri yoyote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.” Danieli 6: 14-16

MADHARA YANAYOWAPATA WAFALME WALIODANGANYWA NA WAPITISHA SHERIA
  1. Kukosa Usingizi
  2. kufunga mfungo wa lazima yaani hakuna kula.
  3. Hakuna starehe wala furaha
Mamia ya watu waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa masiha yao.

Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.” Daniel 6:18 – 22
 Hawawezi kula kwa hiyo wanalazimika kufunga bila kupenda. Kabla Danieli hajafika kwenye shimo mfalme akalia kwa huzuni. Maana yake alihuzunika kwa sababu alijua amedanganywa na mawaziri wake.

HUKUMU YA WAJUMBE WA KIKAO.
Wajumbe wa kikao au mshtaki lazima ahukumiwe. Na mshtaki wa ndugu ni shetani anayeshitaki usiku na mchana. Na hukumu ni kwamba yaleyale mabaya waliyokusudia juu yako ndio yatakayowapata. Kumbuka mawaziri ndio walioamua kwamba asiyemwabudu mfalme lazima atupwe kwenye tundu la Simba. Lakini tundu lilelile ndilo walikotupwa wao na wakaangamizwa kwa vinywa vya simba. Leo naagiza wale walipanga mabaya juu yako yawapate wao kwa jina la Yesu. “Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba. Basi Danieli huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi. ” Danieli 6:23-28
Kuna watu waliokaa kikao ili uangamie lakini wataangamia wao kwa jina la Yesu. “Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.” Mithali 26:27
Mtu akifunguliwa kutoka katika vifungo vya uharibifu.
Kila mauti iliyopangwa juu yako itampata aliyeipanga kwa jina la Yesu. Na waovu huchimba shimo kwenda chini sana. Kuna mabaya ambayo yanaandaliwa kwa ustadi mkubwa. Wengine wamechimba mashimo tena wamechimba sana kwenda chini. “Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.” Zaburi 35:5
Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya!
16 Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.” Zaburi 7:15-16
Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!” Zaburi 57:6
Showers of Glory wakicheza kwa Bwana katika ibada ya leo.


KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro       http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/