KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI YA PASAKA: 1 APRIL, 2018
Mchungaji kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha somo la kuhamishwa toka utumwani kwa njia ya pasaka |
Utangulizi
Pasaka sio kuvaa nguo nzuri, wala
kula chakula kizuri, wala sio kujipaka majivu, bali pasaka ni kuhamishwa kutoka utumwani,
kutoka katika utumwa wa gereza la mateso, kukataliwa, kuugua, kuteswa na majini
mahaba, kifungo cha kuzaa, mapooza n.k. Ukiwa utumwani unaonewa sana, utumwa ni
mateso, biblia inasema katika kitabu cha Isaya
54:14 utathibitika katika haki utakuwa mbali na kuonewa, kumbe kuna watu
ambao wanateswa na kuonewa utumwani wanateswa na vifungo mbalimbali na
wanaowafunga ni watu kabisa yawezekana ni ndugu kabisa anaweza kuwa kaka,
mjomba au mtu yeyote yule lakini leo hii Yesu anaenda kukufungua kutoka
utumwani kwa njia ya pasaka. Ukihamishwa kutoka utumwani unahamishwa na vitu
vyako vyote vilivyo shikiliwa utumwani, ikiwa ni afya, elimu, kazi, kibali,
ndoa n.k.
Sio kwa sababu ya fedha ulizo
nazo, au kwa kua wewe unaelimu au una kitu chochote cha thamani bali ni kwa
sababu umembeba Yesu. Ukimbeba Yesu akiingia nyumbani mwako nyumba yako inapona,
akiingia kazini kwako kazi yako inapona, akiingia kwenye biashara yako biashara
inapona hivyo leo hii unatakiwa kumbeba Yesu ili upone utoke katika utumwa wa
magonjwa, kukataliwa, kutokuoa au kuolewa n.k. watu walipomuona Yesu akiwa juu
ya punda walishangilia sio kwa sababu ya yule punda bali ni kwa sababu yule punda
alimbeba Yesu hivyo na wewe leo unatakiwa kumbeba Yesu ndani yako ili uonekane kuwa
ni wathamani machoni pa Bwana na mbele za watu wengine pia.
”Maana mimi ni Bwana, Mungu wako;
Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa
Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na
mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili
yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.” (Isaya 43:3-4)
Yesu alichagua punda wa kupanda
walikuwepo punda wengi sana Yerusalemu lakini Yesu alichagua punda wa kupanda
kwa sababu ya uthamani wa punda yule, hata wewe leo hii Yesu amekupenda na
kukuona kuwa wewe ni wathamani sana na ndio maana amekuokoa kwa damu yake ya
thamani, Yesu ana haja na wewe, ana haja na kazi yako, anahaja na elimu yako,
anahaja na biashara yako, anahaja na ndoa yako, afya yako kwa kuwa amekuona
kuwa wewe ni wa thamani machoni pake hivyo unatakiwa kumbeba yeye Yesu ili naye
akupende na kukuheshimu na kutoa watu kutoka pande mbalimbali za dunia ili waje
kwako kukusaidia, atatoa watu kwa ajili ya kazi yako, elimu yako, biashara
yako, afya yako ili waje kukusaidia katika mambo mbalimbali.
“Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta
wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;” (Isaya 43:5)
Mungu anasema usiogope kwa kuwa
atakuwa pamoja na wewe ili akusaidie, pengine kuna mambo ambayo unayapitia
ambayo kwa akili yako unaona unashindwa Yesu anasema usiogope kwasababu yupo
kila mahali, ukiwa bafuni yupo, ukiwa mahali popote yupo kwa ajili ya
kukusaidia hivyo usiogope Yesu yupo kila mahali amefufuka yupo tayari
kukusaidia mahali popote na muda wowote, usiogope asema Bwana.
“nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie;
waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.” (Isaya
43:6)
Kuna kaskazi ambayo inatakiwa
ikuletee kazi, mchumba, elimu, au kitu chochote lakini kuna nguvu inayotaka
kuzuia leo hii kwa msaada wa jina la Yesu aliye hai natangaza kila anayetaka
kuzuia kazi, elimu, ndoa, biashara kutoka kaskazini ninamfyeka kwa jina la Yesu
aachie kila kitu chako unachotakiwa kumiliki na ninaiamuru kusi isizuie kwa jina la Yesu
Kristo aliye hai.
Watu mbalimbali wameshindwa
kutafsiri vizuri maana ya pasaka wanadhani kuwa siku ya pasaka ni kucheza
disko, au kukaa nyumbani na kupika vyakula vizuri na kufanya sherehe, wengine
wanadhani kuwa pasaka ni kwenda beach na kustarehe huko lakini kumbe pasaka ni
kuhamishwa kutoka utumwani. Kwenye katiba ya ufalme ambayo ni biblia imeeleza
juu ya kuhamishwa ambapo Yesu alifanywa kama kondoo aliyewekwa tayari kwa
kuchinjwa, akajeruhiwa, akachubuliwa, akafa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu
ili mimi na wewe tuwe huru kutoka utumwani, alifanya vyote hivi yaani alikubali
kupata mateso haya makali ili wewe na mimi tuhame kutoka mautini na kwa sababu
hiyo Mungu akamkirimia jina lipitalo majina yote ili kwa kupitia yeye kila goti
lipigwe mbele zake.
“ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha
fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye
sura yake Mungu.”( 2 wakorintho 4:4)
Watu wanaweza kuangamia na
kupotea kwa sababu mungu wa dunia hii ambaye ni shetani anakuwa amewapofusha
fikra zao, amepofusha fikra zao ili wajue kuwa pasaka ni sherehe tu, ni siku ya
kula chakula kizuri, kufanya starehe na kusheherekea, utaona hata katika biblia
mama yake Yesu alishawahi kumpoteza Yesu
kwenye siku kama hii ya pasaka, walidhani kuwa pasaka ni sherehe wakasherekea
sana mpaka Yesu akapotea.
Makutano ya Bwana wakisikiliza neno la Mungu. |
“Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila
mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na
alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya
sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto
Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na
wazee wake walikuwa hawana habari. Nao
wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa
wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku
wakimtafuta.”(Luka 2:41-45)
Hata leo watu wengi wamepotea
katika siku hizi za sikukuu wamepotea kimwili na kiroho kwa sababu ya kukosa
kutambua kuwa pasaka sio kusheherekea au kuvaa nguo nzuri bali ni kuhama kutoka
utumwani.
“Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya
kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?”( Luka 2:49)
Pasaka ni siku ya kukaa kwenye
nyumba ya Bwana kama ambavyo Yesu alikaa kwenye nyumba ya Baba yake, unatakiwa
uwepo kwenye nyumba ya Bwana kusikiliza neno la Bwana, kutafuta uso wa Mungu
kwa kuomba, kufurahi pamoja katika nyumba ya Bwana. Yesu aliona dunia yote
imejaa utumwa, watu wanalia kutoka katika vifungo mbalimbali na ndio maana
alikuja kuwatoa watu kutoka utumwani, kuna watu wao wanawaza kuwa sio watumwa
kwa sababu wana kazi nzuri, ndoa, biashara nzuri lakini wamesahau kuwa mtu
anaweza kuwa na kazi nzuri lakini ni mtumwa, anaweza kuwa mbunge, rais, waziri
au mtu anayemiliki makampuni makubwa lakini bado akawa ni mtumwa, bila kumpokea
Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako wewe unakuwa bado ni mtumwa kwa
maana damu ya Yesu pekee ndio iwezayo kukutoa katika utumwa kwa njia ya wokovu.
Damu ya mwanakondoo ni damu
inayonena mema, damu hii inaweza kuja juu ya mtu na kufanyika uzima unaona hata
pilato alipokuwa anaambiwa na watu kuwa Yesu asulubiwe alikataa na kunawa mikono
ikimaanisha kuwa asiwe na hatia juu ya damu ya Yesu, watu wote wakajibu damu ya
Yesu iwe juu yao na watoto wao wenyewe.
“ Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote,
bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano,
akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya
ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu
ya watoto wetu.”( mathayo 27:24-25)
Unaona kuna mambo ambayo unaweza
ukapitia kwenye familia kwa sababu ya damu inayonena mabaya juu yenu ambayo
ilisababishwa na mtu yeyote kwenye familia, hivyo unahitaji damu ya Yesu
inyamazishe kila damu zinazonena mabaya juu yako na familia yako damu hii ya
Yesu unaipata kwa njia ya wokovu peke yake yaani kwa kumpokea Bwana Yesu kuwa
Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Pia damu ya Yesu inaweza kunena
mema juu yako na kunyamazisha kila damu za makafara ndani ya jina la Yesu imo
damu na leo hii naituma damu ya Yesu ije juu ya ndoa yako, damu hii itembee juu
ya maisha yako, juu ya kazi yako kwa maana ndani ya damu hii umo uzima, pokea
damu ya Yesu kwenye maisha yako kwa jina la Yesu.
Kijana huyu anaitwa ISAYA STEPHANO. Kijana huyu aliokotwa kutoka makaburini hapo Kihonda na sasa anaendelea vizuri. nguvu ya kufufua wafu inatenda kazi hata sasa. |
”na Yesu mjumbe wa agano jipya,
na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili” (Waebrania 12:24)
Damu hii ya Yesu ina tabia mbalimbali,
inatabia ya kusema, inatabia ya kulia, inatabia ya kunyamazisha kila damu za
kafara zilizotolewa juu yako. Kuna nguvu katika jina la Yesu kwa maana ndani ya
jina la Yesu imo damu inenayo mema, wanaotaka wewe ufe kwa kukuendea kwa mganga
wa kienyeji na kutoa damu ya kafara ili iseme, inene usiolewe, usizae, usisome,
ufe, ukataliwe n.k. nikweli wamemwaga damu zao ili zinene mabayo juu yako
lakini leo tunayo damu ya Yesu pekee iwezayo kunyamazisha damu hizi za kafara
na inauwezo wa kukuhamisha kutoka utumwani, tumia damu hiyo kunyamazisha kila
damu zote za kafara zinazonena uhalibifu juu yako.
“Naye alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika
yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa
wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa
katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi,
vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi,
au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu
vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye
kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza
katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.”( Wakolosai 1:13-18)
Ndani ya jina la Yesu vitu vyote
vinashikamana, huyu Yesu ambaye alipigwa akafa na kuzikwa na siku ya tatu
akafufufka ukiwa naye vitu vyako vyote hushikamana yaani wewe na mke wako
mtashikamana, wewe na elimu yako mtashikamana, wewe na kazi yako mtashikamana
n.k. alikuja kutuhamisha kutoka utumwani wewe na vitu vyako, Bwana Yesu
alipokuwa msalabani alikuja kutuhamisha kutoka kwenye mateso alipigwa na kuning’inizwa
msalabani wajaribu walikuja na kujaribu kama kweli amekufa wakamchoma mkuki
ubavuni damu na maji vikatoka roho yake ikatoka na roho ilipotoka ikaenda mpaka
kuzimu kumnyang’anya shetani ufunguo wa kuzimu na mauti na kwa kupitia hiyo
wewe na mimi tumepewa mamlaka ya kumkanyaga nyoka na ng’e kwa jina la Yesu,
kila silaha ya shetani iliyoinuka juu yako, juu ya ndoa yako, n.k.
haitafanikiwa kwa kuwa amekwisha kunyang’anywa ufunguo wa kuzimu na mauti mahali
popote ambapo shetani amekaa kwenye maisha yako, ndoa yako, elimu yako, mponde
kichwa chake kwa jina la Yesu kwa maana hana nguvu kwako tumia jina la Yesu
jina lenye nguvu na mamlaka mponde shetani aachie vitu vyako kwa jina la Yesu.
“Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa
ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu;
mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho
waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu
wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu,
safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane,
waliokoka kwa maji.” (1 petro 3:18-20)
Yesu hakuja duniani kwa ajili ya
watakatifu bali alikuja kwa ajili ya wale wenye dhambi ili wawe huru kutoka
katika vifungo vya dhambi. Roho ya Yesu aliteremka mpaka kuzimu kwa sababu
alijua kuna kundi la watu ambao walikuwa wapo shimoni akaenda na kuwahubilia
ili wapate wokovu.
“Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya
nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu
akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona
umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita
Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio,
akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama
Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa
roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande
viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;” (Mathayo 27: 45-51)
Yesu aliitoa roho yake yeye
mwenyewe na roho yake ikaenda mpaka kuzimu kufanya kazi maalumu, matukio
mbalimbali yalitokea mara baada ya Yesu kuitoa roho yake, pazia la hekalu
likapasuka, tetemeko kuu la nchi likatokea, pazia lilipasuka ili kisiwepo
kizuizi chochote cha wewe kwenda kwa Mungu Yesu alikuja kwa ajili ya wenye
dhambi ili wasamehewe na kuwa na haki watu mbalimbali wanaweza wakaleta vizuizi
mbalimbali vya watu kwenda kwa Yesu wanaweza kumsema mtu kutokana na tabia
yake, mavazi yake, au namna alivyo lakini Yesu alikuja kuondoa mapazia yote
yana vizuizi vyote ambavyo mtu anavipata ili asimfikie Yesu au asipate wokovu.
MAOMBI
“Kwa jina lenye nguvu la Bwana
wangu Yesu Kristo leo ninapasua kila pazia lililowekwa mbele yangu ili
kunitenga mimi na kazi yangu, kunitenga mimi na ndoa yangu, biashara, mume au
mke wangu, kunitenga na baraka zangu, wewe pazia nakupasua kwa jina la
Yesu.......( endelea kupasua kila pazia lilowekwa kukutenga na baraka zako)”
Tetemeko la nchi lilitokea ili ikiwa
kuna mtu yeyote aliyeshikilia kazi yako, ndoa yako, elimu yako, biashara yako,
n.k. ukiitumia damu ya Yesu na kusema kuwa unaitumia damu ya Yesu kutetemesha
kila walioshikilia vitu vyako wanatetemeshwa kwa jina la Yesu na kuachia vitu
vyako kwa jina la Yesu.
MAOMBI
“Baba katika jina lenye nguvu la
Bwana wetu Yesu Kristo ninatetemesha kila mashimo yaliyonifungia, yaliyoshikilia
kazi yangu, ndoa yangu, elimu yangu, afya yangu, ninaamuru jina la Yesu
liwatetemeshe zaidi ya mtu atetemeshwavyo na umeme na kisha waviachie vitu
vyangu kwa jina la Yesu. Amina ”
“makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;” (Mathayo
27:52)
Aliposhuka kuzimu aliwaendea roho
za watu waliopo shimoni, makaburi yakafunguka na watu wakatoka. Kuna watu ambao
walikuwa wamechukuliwa msukule na kuwekwa shimoni lakini Yesu aliposhuka kuzimu
alizitoa roho za watu waliokufa, alihubiri kwanza na watu waliopo shimoni
wakasikia na kisha wakafufuka. Inawezekana na wewe kuna vitu vyako ambavyo
vimefichwa makaburini, ndoa yako imefichwa makaburini, nyota imefichwa
makaburini, elimu, kibali n.k. vimefichwa makaburini leo ninatangaza mahali
popote ambapo vitu vyako vimefichwa makaburini njoooooo toka nje ya kaburi kwa
jina la Yesu Kristo.
MAOMBI
“Kwa mamlaka ya jina la Yesu
Kristo jina lililo hai na lenye nguvu ninatikisa makaburi yote ya kichawi
yaliyonishikilia kwa jina la Yesu, makaburi yaliyokamata afya yangu, mikono
yangu, moyo wangu, kazi yangu, watoto wangu, mume au mke wangu au kitu changu chochote
nakuamuru wewe kaburi upasuke na unitapike na kuachia vitu vyangu vyote kwa
jina la Yesu. Amina ”
” Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;
mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yohana 10:10)
Kuzimu ni wezi, wanawatumia watu
mbalimbali kama wachawi, waganga, wasoma nyota ili kuiba vitu vyako na kisha kuvifungia
katika jeneza chini kuzimu au mahali popote. Wanaweza kukutengenezea jeneza ili
wewe ukataliwe, usifanye vitu vile ambavyo unatakiwa kufanya. Inawezekana hapo
mwanzo ulikuwa unapendwa na watu lakini ghafla ukaanza kuchukiwa hata na ndugu
zako wa karibu ni kwa sababu ya kufungiwa kwenye jeneza la kuzimu. Wachawi wanaweza
kutengeneza janeza kukufungia wewe na kazi yako, na ndoa yako, biashara yako,
wanaweza kuiba macho yako, moyo wako yaani hapo mwanzao ulikuwa na moyo mzuri
moyo wa kumpenda Mungu na kufanya kazi ya Bwana lakini leo hii moyo umeibiwa na
kufungiwa kwenye jeneza mahali Fulani na ndio maana husikii kuomba tena,
kufunga tena, ni kwa sababu
MAOMBI
“Leo katika jina la Yesu
ninakuamuru wewe shimo mwenye jeneza ambalo limefungia hatima yangu, akili
yangu moyo wangu, kibali changu leo ninaamuru wewe jeneza na kaburi pasuka kwa
jina la Yesu, wewe joka unayenilinda kwenye jeneza leo ninakufyeka na
ninakuamuru achia kila kitu changu, achia mchumba wangu, kazi , ndoa, achia
uwezo wangu, ule uwezo wa kufanya kazi, wa kuhubili, kusoma neno la Mungu,
kuomba, n.k. nakuamuru achia kwa jina Yesu, ninakuponda leo kwa jina la Yesu na
ninavunja nguvu ya kaburi na jeneza na mauti kwa jina lenye nguvu la Yesu
Kristo. Amina.”
“nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake,
wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa
pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo
yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” (Mathayo
27:53-54)
Kuna mambo yamekaa kwa namna ya
kufika katika maisha yako lakini leo hii mambo hayo yatatoweka kwa sababu ya
kutetemeshwa kwa kufufuka kwake Yesu. Huyu mfalme Yesu anapotoka kwenye mwili
wake ardhi inatetemeka lakini pia anaporejea kwenye mwili wake ardhi
inatetemeka pia.
“Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya
kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda
kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu
malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe
akalikalia.” (Mathayo 28:1-2)
Inawezekana kuna watu wanakulinda kwenye tabu
uliyonayo, wanafurahi kukuona upo kwenye utumwa na hata akitokea mtu wa kukutoa
wanakasirika na kuzuia mtu yeyote asikutoe katika kifungo, yaani hawa ni
walinzi wanaokulinda ili usitoke katika kifungo ulichonacho kama ambavyo
walinzi walilinda kaburi la Yesu lakini leo ninaamuru tetemeko kuu la nchi
litokee mahali ulipofungwa na walinzi wote watetemeshwe na wawe kama wafu kwa
jina la Yesu na kisha wewe utoke mahali ambapo umefungwa kwa jina la Yesu.
Showers of Glory Morogoro wakicheza mbele za Bwana Baada ya kutoka utumwani ilikuwa furaha ya ajabu wakati wa Ibada ya leo. |
“Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi
ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote
yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na
wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya
kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi
tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha,
wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata
leo.” ( Mathayo 28:11-15)
Baada ya Yesu kufufuka wazee wa
mji wakakutana kwenye kikao chao wakafanya shauri wakapanga maneno ya uongo ili
waseme Yesu hajafufuka bali wezi wamemuiba, wakakusanya hela ili wawalipe
walinzi waseme uongo na ndio maana uongo huwa unatenda kazi sana mpaka leo. Mungu
leo hii akuhamishe kutoka katika maneno ya uongo kwa jina la Yesu. Kuna mtu
mwingine leo hii ukimuhubilia kuwa Yesu anaishi Yesu anaokoa kimsingi mtu huyu
huwa haamini kabisa anaona kama ni uongo lakini wewe leo hii unatakiwa kuamshwa
kutoka katika usingizi huo wa kudanganywa na umwamini na kumpokea Bwana Yesu
Kristo kuwa Bwana na mwokozi wako. Usipoamini kuwa Bwana Yesu Kristo alifufuka
katika wafu imani yako ni bure kabisa.
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI
WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK:
Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us
on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us
on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255
719 798 778
BLOG:
Ufufuo na Uzima Morogoro