JUMAPILI: 25 JANUARY 2015
- UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
Utangulizi: Jumapili ya leo 25/01/2015 Somo letu linaitwa “Kupata kwa Kuchelewa”. Bwana anataka upate vile
unavyomuomba. Mungu ni Mungu wa kutimiza ahadi zake kwetu. Hata hivyo, ingawa tunataka tupate kwa wakati
wa maombi yetu, kitu ulichokiomba kinachelewa kupatikana. WAGALITA 4:4…[Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu
alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,]… Mungu hufanya kazi kwa wakati wa
utimilifu. Upo uwezekano wa kuahidiwa jambo na Mungu na ukalipata kwa kuchelewa
au usilipate kabisa, kutokana na kuwepo kwa watu waovu ambao wanalizuia. Leo ni
siku ya kupita katikati ya watu hao kwa
Jina la Yesu. Leo tutapita katikati ya madeni, katikati ya magonjwa na katikati
ya umaskini kwa kuwa tumejengwa juu ya
mwamba ambaye ni Yesu Kristo, na malango
ya kuzimu hayatatushinda kwa Jina la Yesu.
JOSHUA 15:5-15 ….[Vile vile kama Bwana
alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo
nchi. 6 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu,
mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana
alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari
zako wewe, tulipokuwa katika Kadeshbarnea. 7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka
arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka
Kadeshbarnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama
ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. 8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda
pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu,
kwa utimilifu. 9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi
ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako
milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. 10 Sasa
basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na
mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli
waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini
na mitano umri wangu. 11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama
nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati
huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia
ndani. 12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo;
kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji
ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami
nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. 13 Yoshua akambarikia, akampa
Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. 14 Kwa hiyo Hebroni
ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama
Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu. 15 Basi jina la Hebroni hapo kwanza
uliitwa Kiriatharba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika
hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.]…. Kalebu na Joshua ndio pekee
waliosimamia imani yao kusema Bwana anaweza kuwavusha salama Israeli yote
kwenda nchi ya ahadi. Ingawa wale wapelelezi wengine 10 walikatisha tamaa
waisraeli, lakini katika Mungu, demokrasia haisemi wengi wape, bali wale wenye
imani kwa Yesu hushinda kwa Jina la Yesu. Mungu amekaa ndani ya Joshua ili
kuwavusha watu kwa Jina la Yesu. Katika
wale walioianza safari kuelekea Kanani (zaidi ya milioni sita), ni watu wawili
tu ndio waliofanikiwa kuingi Kanani (Joshua na Kalebu). Wengine wote walioingia
Kanani ni wale waliozaliwa njiani.
Mji wa Hebroni (ambao kabla uliitwa Kiriatharaba), vita ilikoma
pale tu Kalebu alipopewa huo mji. Ahadi ya Mungu kwa Kalebu ilitimia baada ya
miaka 45. Ahadi ya Bwanani kamilifu.
Wapo watu wanaomsubiria Bwana kwa
kipindi kifupi tu na papo hapo wakakata tamaa. Kumbuka "Mungu si mwanadamu hata aseme
uwongo". Anapoahidi jambo atalitimiza.
MWANZO 15:13-14 ….[Bwana akamwambia
Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake,
watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. 14
Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali
mengi.]…..Kuna wakati
ukifika, mateso yako yatakoma. Mungu ni
Mungu wa majira na nyakati. Mungu ameweka kipimo cha mateso na kuonewa. Mwaka
huu wa 2015, kwa kila anayemtumaini Mungu ni ‘mwaka wa kutoka’ kwa Jina la Yesu. Wakati huu Mungu
akiongea na Abramu, ni kipindi hicho hicho ambacho Abramu na Sarai walikuwa
hawana mtoto. Je,ahadi hii kwa wana wa Israeli ilitimia kwa wakati wake au
haikutimia?
KUTOKA 12:40-41…[Basi wana wa Israeli
kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na
thelathini. 41 Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku
ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri.]…. Je, miaka 430 ni sawa na 400 aliyoahidi Mungu kwa
Ibrahimu? Ahadi ya Mungu kwao ni kuwa ilitimia lakini kwa kuchelewa. Mungu
anaposema amesema, lakini mtekelezaji ni wewe ili Mungu afanye sehemu yake.
Mungu hufanya kazi pale alipokubaliwa.
"Maandalio ya moyo ni ya
mwanadamu, lakini jawabu la ulimi ni la Bwana"...[MITHALI 16:1]. Waisraeli walipaswa kutunza
muda walioahidiwa na Mungu, kwa kuwa muda huu ulipotimia Mungu alikuwa kazini kuwasubiria wana wa Israeli atekeleze
ahadi yake kwao ya kuwatoa nchi ya utumwa huko Misri. Matokeo yake, Mungu
alisababisha kitu kitokee, kwa kumuinua mfalme mpya huko Misri asiyemjua
Yusufu. KUTOKA 1:8…[Basi
akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.]…. Israeli walijisahau, wakakaa Gosheni wakifikiri ile
ni nchi yao. Mfalme asiyemjua Yusufu husababisha mateso na kuzifanya akili za watu zianze kufanya kazi.
2 KORINTHO 12:7-9…[Na makusudi nisipate
kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili,
mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. 8 Kwa ajili ya
kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. 9 Naye akaniambia, Neema
yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia
udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.]… Paulo katika udhaifu aliowekewa mwilini
mwake, alimsihi Mungu mara 3 lakini majibu ya Mungu kwake yakawa "neema
yangu yakutosha"….Mungu
anaweza kusababisha uwepo wa miiba ili kumfanya mtu ajirudi, na tabia za maisha
ya mtu huyu zibadilike.
Wana wa Israeli walipoanza kuomba na kumlilia Bwana, ndipo ambapo Mungu alimuinua Musa ili
awatoe Israeli kutoka Misri,nchi ya utumwa (KUTOKA 3:7-8….[Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu
wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao;
maana nayajua maumivu yao; - 8 nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya
Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo
maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na
Mhivi, na Myebusi.])…
wakati mwingine mtu anaweza kuwa kwenye tatizo lakini likachukua muda kuisha
kwa sababu huyo mtu hajachukua hatua ya kumuomba Mungu. Wana wa Israeli
walichelewa kutoka Misri kwa sababu ilipotimia ile miaka 400, walijisahau bila
kumuuliza Mungu awatoe kama ahadi yake kwao
ilivyokuwa. Siyo mpango wa Mungu kuchelewesha kutoa vile alivyoahidi
bali huo ni mpango wa mashetani.
Danieli alifunga na kuomba, lakini
akachelewa kupata majibu ya Mungu.
DANIELI 11:12-14 ….. [Ndipo akaniambia,
Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako
ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami
nimekuja kwa ajili ya maneno yako. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi
alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao
wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa
Uajemi. 14 Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika
siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.]….Unapoona unapata majibu kwa
kuchelewa,ujue kuna kitu kinachokuzuia,
na kitu hicho si Mungu.
MUNGU (JEHOVHA) HAWEZI KUSEMA UONGO:
Ushahidi wa Kimaandiko (Kibiblia)
(a)
HESABU 23:19….[Mungu si mtu, aseme
uongo; Wala si mwanadamu, ajute;Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena,
hatalifikiliza?]….
(b)
MALAKI 3:6…[Kwa kuwa mimi, Bwana,
sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.]…. Mungu wetu (Jehovha) hana kigeu geu.
(c)
TITO 1:2…[katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu
asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;]…
(d)
YAKOBO 1:17…[Kila kutoa kuliko
kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa
mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.]….
Sehemu tu ya Majeshi ya Bwana - Bonde la Maono Morogoro hapo Jumapili 25/1/2015 |
WATU WALIOCHELEWA KUPATA AHADI ZAO KUTOKA KWA MUNGU KATIKA BIBLIA
(a)
Wana wa
Israeli walichelewa kutoka Misri, badala ya kutoka huko baada ya miaka 400, kwa
kutojua majira ya kujiliwa kwao walitoka kule baada ya mmiaka 430.
(b)
Danieli
vivyo hivyo, alicheleweshewa majibu ya maombi yake na aliyefanya hivyo ni
Mfalme wa Uajemi.
(c)
Sara
alichelewa kupata mtoto wake (Isaka) kwa wakati, na akampata akiwa na umri wa miaka 90.
(d)
Raheli
naye alikaa katika hali ya utasa kwa muda mrefu, na baadae akampata Yusufu - MWANZO 30:22-24…[Mungu
akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo. 23 Akapata mimba, akazaa
mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu]…
(e)
Mke
wa Manoa alimpata Samsoni lakini kwa kuchelewa (WAAMUZI 13:1-2;…24 …[Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya
Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. 3
Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa,
huzai; lakini utachukua mimba, nawe
utamzaa mtoto mwanamume….. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita
jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia.]…
(f)
Hana
alimpata Samweli lakini kwa kuchelewa (1
SAMWELI 1:2 …. 19-20)….[naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja
akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na
watoto, lakini Hana hakuwa na watoto….. 19 Wakaondoka asubuhi na mapema,
wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama;
Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. 20 Ikawa, wakati ulipowadia,
Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli,
akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.].
(g)
Elizabethi
alimpata Yohana Mbatizaji lakini kwa kuchelewa (LUKA 1:7 … 24-25)…..[Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti
alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana… . . 24 Hata baada ya siku zile
mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, 25 Hivi ndivyo
alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu
mbele ya watu.].
1 THESALONIKE 2:17-18….[Lakini sisi, ndugu,
tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani
kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu. 18 Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam,
mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.]…. Mtume Paulo, mtu wa vita ndiye
anayeongea maneno haya. Ndiye aliyesema ‘ingawa naenenda katika
mwili, lakini sifanyi vita kwa jinsi ya
mwili’. Paulo anawaambia Wathesalonike kuwa alitamani kwenda kwao,
lakini hata hivyo shetani akamzuia zaidi ya mara tatu (3). Shetani
anaweza kukuchelewesha usipate, lakini
hawezi kukuzuia usipate.
UKIRI
Bwana Mungu,katika Jina la Yesu, nawarudisha nyuma yangu wote
walio kikwazo, leo nawakamata, kwa
Damu ya Mwanakondoo, warudi nyuma yangu, aliyekaa kwenye njia ya mafanikio yangu, nawakamata kwa Jina la Yesu, kila
kikwazo cha ushindi wangu, nakiondoa leo kwa Damu ya Yesu. Ninafanya vita na
yeyote, awe ni ndugu, au kiongozi, leo
namshughulikia kwa Jina la Yesu, kwa kuwa imeandikwa, ‘shetani akamuingia Yuda ili amsaliti Yesu’,
nami nawashughulikia, mashetani mliowaingia wanadamu ili wanizuie, kwa
Jina la Yesu. Amen.
|
Katika Biblia, tofauti kubwa iliyopo kati ya Musa na Joshua ni
kuwa, Musa alikuwa anaomba kwanza na baada ya maombi anagawanyisha Bahari ya
Shamu. Joshua kwa upande wake, alikuwa anatanguliza Makuhani kwanza katika Mto
Jordani wakiwa na Sanduku la Agano na baada
ya hapo maji yakagawanyika. Hii ilianza
baada ya Mungu kumwagiza Musa aweke mikono yake juu ya Joshua na roho wa Mungu
aliyekuwa ndani ya Musa akahamia kwa Joshua. Kwa hiyo, upako wa Joshua ni upako
uliorekebishwa.
DANIEL 9:1-5….[Katika
mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa
kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; 2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki
kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo
neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani,
miaka sabini. 3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na
dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. 4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama,
nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao
wampendao, na kuzishika amri zake; 5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi,
tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;].. Kuna nyakatiyingine ibabidi usome nyakati. Baada ya Daniel kujua siri
iliyopo kwenye vitabu aliomba na kupata majibu yake. 2 NYAKATI 36:21-22 …[ili
kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia
sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka
sabini. 22 Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili
kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana
akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme
wake wote, akaiandika pia, akisema,]…na pia katika YEREMIA
25:11…[Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu
cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.]… Wapo watu ambao hata sasa wanamtumikia
Mfalme wa Babeli, wakijua au bila kujua.
SABABU 10 ZINAZOMFANYA MTU APATEKWA
KUCHELEWA
(i).
Kutokujitambua: Mtu anayefanya vitu visivyo sawa lakini binafsi anaona ni sawa
ujue hajitambui. Ipo nguvu ya kujitambua, ambayo shetani hutumia hila za
kupofusha akili za wanadamu ili wasijitambue. Matatizo mengine yapo na wala
hayahitaji kufanyiwa maombi. Pindi hayo yakifanyika,mtu anawekwa huru.
(ii).
Kutokujua unatakiwa kuwa wapi: Pale ulipo kwa sasa sipo ambapo unapaswa
kuwepo. Wana wa Israeli wakiwa Gosheni kule Misri, walidhani kuwa pale ni
mahali alipokusudia Mungu wakae, kumbe
lilikuwepo eneo zuri zaidi alilokuwa amewaandalia Mungu.
(iii).
KutokujuaMadhara ya yale uyafanyayo leo na
athari zake baadae: Kila
jambo ulifanyalo leo, sirini au nuruni,
lina mshahara wake baadae (furaha au
kilio). Yona yalimkuta haya,
badala ya kwenda Ninawi yeye alichepuka kuelekea Tarshishi. Wakati watu ndani ya ile merikebu wanamuomba Mungu ili
dhoruba itulie, Yona yeye alikuwa chini, amelala usingizi. Ogopa sana mtu
ambaye wakati wengine wanaomba, yeye anakuwa amelala. Mtu anaweza kujificha ili
watu wasimuone, lakini siku ikifika Bwana atamtoa kwenye maficho yake, na siri
zote kufichuka. Ili Bahari iwe shwari,
lazima Yona wa maisha yako atupwe baharini kwa Jina la Yesu. GALATIA 6:7…[Msidanganyike,
Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.]…
(iv).
Kukwepa Gharama: Ukikwepa gharama kunaweza kukusababishia
upate kwa kuchelewa. Kila Baraka ina
Jaribu lake, na kila Jaribu lina Baraka yake. Usiwe mwepesi kumuomba Mungu alipunguze
jaribu lako, kwa sababu akifanya hivyo na Baraka iliyoambatana nalo itapungua.
Maandiko yanasema,mtu atakula matunda ya kazi yake. Kataa vyepesi vyepesi, lipa
gharama.
(v).
Kutokujua wakati sahihi: WARUMI 13:11..[Naam, tukiujua wakati,
kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu
wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini]…
Mungu akupe akili ya kujua siri za mafanikio yako kwa Jina la Yesu. 1 NYAKATI 12:32….[Naam,
tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa
maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini]…Ni akili pekee ya kujua majira na
nyakati itakayofanya mtu kutenda kwa wakati.
(vi).
Mtu wa kulalamika na manung’uniko kila wakati: Mtu wa aina hii, hawezi kuona jema hata
moja analotendewa. Wana wa Israeli walikuawa wote jangwani kutokana na shida
hii. Hii ni roho ya kuona makosa tu, na yale mema hayaonekani. Usiwe mwepesi kuona kibanzi kwenye jicho la
mwenzako, wakati boriti kwenye jicho lako hujalitoa. Soma katika Biblia katika ZABURI 106:25; 1 KORINTHO 10:10; EBRANIA
3:18.
(vii).
Kubweteka kusubiri kupewa kila kitu, hauko
tayari kuonesha uwezo wako binafsi: Ukiwa kazini kwenye nafasi yako,
onesha ubunifu wa kazi ile, ili iwe rahisi kupewa cheo. Wanawake vivyo
hivyo, wanapaswa wawe wabunifu katika ndoa zao, kwenye mapishi yao.
(viii).
Utoto wa Kudumaa na kutokuwa
tayari kuwa mtu mzima: Mtu anakuwa ni mtu mzima, lakini maamuzi na mambo yake ni ya utoto bado. GALATIA 4:1-2…[Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote
awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; 2 bali yu chini
ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.]…. Kuna vitu vingine umekosa kuvipata
kwa Bwana kwa sababu bado u mtoto. EBRANIA
5:12-14….[Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana
wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya
maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. 13 Kwa
maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto
mchanga. 14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa
kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya..]….Ukiwa mtu mzima, unapata unavyostahili
kwa wakati wake.
(ix).
Kukosa mtu sahihi wa kukuongoza
kwenye hatima yako: Kuna kipindi cha kutoka kwenye tatizo lako
huko Misri (Musa), lakini pia anahitajika mtu sahihi wa kukuingiza kwenye nchi
ya ahadi (Joshua). Unahitaji mtu sahihi, wa kukutoa dhambini na kukupeleka
kwenye Baraka zako.
(x).
Dhambi humgharimu mtu akapata
alichoahidiwa kwa kuchelewa: Muujiza na baraka zako zinaweza kucheleweshwa kutokana na dhambi.
Ibrahimu aliahidiwa ampate Isaka akiwa na miaka 86, lakini kitendo chake cha kuzaa
na mjakazi wake Hajiri, kilimfanya ampate
Isaka akiwa na umri wa miaka 100 (miaka 14 baadae). Dhambi ukiifanya
leo, huifanya ahadi ya Mungu kwako
isogee mbele zaidi. HESABU 14:34…[Kwa
hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku
kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua
kufarikana kwangu.]…Dhambi
inaweza kuimeza ndoto yako. Yusufu alijua siri hii, akagoma kulala na mke wa Potifa, ili asiikose ahadi ya Mungu maishani mwake.
Showers of Glory Bonde la Maono Morogoro wakiimba na kucheza wimbo wa 'Majeshi Majeshi' wa Flora Mbasha siku ya Jumapili 25/1/2015. |
UKIRI
Bwana Yesu,nimejifunza haya ili nisije kupata vile
nilivyoahidiwa wakati nimechelewa, ili nipate kwa wakati uliokusudiwa. Naomba
neema yakuzitambua njia zangu, na nijue jinsi ya kuishi kulingana na mapenzi
yako, Kwa Jina la Yesu. Amen.
|
© Information Ministry
(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi,
(Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
/or
Contact our Senior
Pastor:
Dr. Godson Issa Zacharia
(Ufufuo Na Uzima – Morogoro)
Cellphone: (+255) 757
550878 / +255 719798778