Monday, February 2, 2015

KIPAWA HUFUNGUA MLANGO-Na: ADRIANO MAKAZI (RP)


JUMAPILI:  01 FEBRUARY 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 

Utangulizi: Jumapili ya leo 01/02/2015 Somo letu linaitwa Kipawa Hufungua Mlango”. Ipo milango ya aina nyingi sana hapa duniani. Ipo milango kuhusiana na ndoa,  uchumba,

 
RP  Adriano akifundisha  kwa mifano
 Somo  la 'Kipawa hufungua Mlango'
 

MITHALI 17:8….[Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa.]… Kipawa kinaweza kumuingiza mtu mahali ambapo hakutarajia Kufika.

MITHALI 18:16…[Zawadi ya mtu humpatia nafasi;  Humleta mbele ya watu wakuu.]… Unahitaji  kuwa na kipawa ili kuingia katika nafasi ambayo ulikuwa unaifuatilia. Katika Biblia,  Daudi  ingawa alikuwa mchunga kondoo wa baba yake, lakini alikuwa na kipawa chakupiga kinubi,  kiasi kwamba mapepo ya Mfalme Sauli yalikuwa yanatimka yanaposikia  sauti ya kinubi cha Daudi.

 

Paulo na Silla walikuwa gerezani wakiomba na kuimba, lakini ghafla tetemeko la nchi likatokea na misingi ya gereza ikapasuka, ‘milango ya gereza’ ikawaachia. Mwaka huu ni wa kuachilia vipawa vya watu  vilivyoshikiliwa na adui zetu kwa Jina la Yesu.

 

Yusufu mwana wa Yakobo alitupwa gerezani pamoja na kwamba alikuwa na kipawa  ndani yake cha kufasiri ndoto. Hata hivyo, haijalishi ni gereza la aina gani ambalo wanadamu wamekuweka (gereza la mikosi, madeni, magonjwa, umaskini n.k), lakini kupitia kipawa chako, ipo siku  ya kuondoka kwa ushindi  kutoka ndani ya hilo gereza kwa sababu Mungu anaweza kukutembelea humo gerezani kwa Jina la Yesu.
RP Adriano akiomba ibadani tarehe 1/2/2015


MWANZO 40:5-7….[Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. 6 Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. 7Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? ]… Kuna wakati mwingine unaweza kuwa na kipawa lakini usijue kuwa unacho kwa sababu hujakitendea kazi. Ukiona unaota ota ndoto sana, ujue upo gerezani. Kwa nini? Kwa sababu unakuwa hauna muda wa kukaa na Bwana na kuzungumza naye. Ndoto ni bayana, na yaweza kukaa muda mrefu kabla ya kutokea. Ni vizuri kuiombea ndoto yako, endapo ni nzuri uiombee itokee lakini kama ni  mbaya uikatae kwa Jina la Yesu.

 

MWANZO 40:8-14…[Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie. 9 Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. 10 Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. 11 Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. 12 Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. 13 Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. 14 Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. 15 Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani.]… Ni vizuri kumtaja taja Yule aliyekusaidia, usifunge vioo vyote hata kutomtendea mema mtu huyo.

 

MWANZO 40:16-17…[Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu. 17 Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu. 18 Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu. 19 Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako.]…. Kwa mkuu wa waokaji,yeye alifuata tu mkumbo kwa kuiga mwenzake alivyokuwa ametafsiriwa ndote yake na ambayo ilionnekana njema. Hukumu ya hawa maakida ilikuwa ifanyike baada ya siku tatu zijazo na ndoto wakaota siku moja wote kwa pamoja. Hata hivyo, Mkuu wa waokaji  alitundikwa kwenye mti na akafa.

 

MWANZO 41:1-7….[Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. 2 Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. 3 Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto.  4 Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. 5 Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. 6 Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. 7 Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.]…. Wale wanaoharibu maisha au afya au ndoa na kudhoofisha hutokea chini na kupanda. Mara zote ubaya hula kizuri (UFUNUO 13:1….[Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.])…

 

MWANZO 41:8……[Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.]… Mungu alilenga kuwa, akosekane mtu wa kuweza kufasiri ndoto, ili hatimaye amtoe Yusufu gerezani. Mawazo ya Mungu si sawa na ya wanadamu, kwani Mungu humwazia mema mwanadamu.

 

MWANZO 41:9-15…[Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. 10 Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. 11 Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. - 12 Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. 13 Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. 14 Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. 15 Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.]…. Wapo mashetani ambao hugeuza mambo ili habari mbaya zisikike kutoka kwako. Farao alisikiahabari za Yusufu. Je, ni  habari gani zako watu wanazisikia ukiwa nyumbani na ukiwa kanisani? Mitaani kwetu hata waliookoka huweza kukosa bahati zao za kuoa / kuolewa kutokana na taarifa zinazosikika juu yao. Ni vizuro kumpendeza Mungu pamoja  na wanadamu. Wapo wapeleka habari kwa boss wako,

 

UKIRI
Kwa jina la Yesu, Nawakamata watu wote wapeleka habari, wanaofautailia njia zangu, nawakamata kwa damu ya mwanakondoo, leo ninawapiga, nawashambulia enyi mashetani, enyi majoka, enyi miziumu mliokaa kuniharibia maisha yangu,  mnaogeuza maneno ili nionekane sifai, nawashabulia kwa Damu ya Yesu….Amen.
 

 
Showers of Glory wa Bonde la Maono Morogoro wakiimba na kumcezea Bwana Jumapili 1/2/2015

 

2 PETRO 2:11…[Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.]…. Mungu katika idara za utendaji wake ameweka idara mbali mbali.  Shetani naye ameigiza vivyo hivyo. Wapo malaika wa kupeleka taarifa mbaya, ili uonekane tofauiti. Ndiyo maana hata  Yesu aliwauliza wanafuzni wake kujua kule  nje huwa watu wanamuita kuwa yeye ni nani.

 

Baadhi ya watu wanavyo vipawa vyao lakni vimezuiliwa. Yamkini waweza kuwa na kipawa lakini anayekijua hicho kipawa chako ni wewe na mke wako tu. Yesu alisema hayupo mtu mwenye kuwasha taa na kuiweka chini ya kiango, bali hiweka juu ya paa ili iangaze ndani kote. Kataa kubaki pale ulipo kwa Jina la Yesu.

 

Kipawa cha Yusufu cha kufasiri ndoto kilimpeleka kwenye hatima yake. Ukeshafasiri ndoto ya Mfalme huwezi kurudi gerezani tena. Ukeshaitwa kuifasiri ndoto, utapewa majukumu ya kusimamia, na  ndiyo maana Yusufu alifanyika kuwa Waziri Mkuu wa nchi ya Misri  baada ya kutumia vizuri kipawa chake, na kuichukua nafasi ya Potifa,  yule aliyemshtaki. Kipawa hutengeneza njia ya kuifikia ndoto yako. Daudi alipoitwa kwa Mfalme kupiga zeze, alipewa na jukumu lingine la kuwa mbeba silaha za Mfalme. 

 

Ili ujue unacho kipawa unamhitajimtu wa kukushika mkono. Namuona Yoshua wako anakuja kwako kwa Jina la Yesu.  namuona Musa wako anakuja kwa Jina la Yesu. Yesu aliibadilisha nafasi ya Petro, badala ya kuwa mvuvi wa samaki na kuwa mvuvi wa roho za watu. Daudi hakuwahi kusomea maswala ya  utawala kwani alikuwa mchungaji wa kondoo, lakini baadae alifanyika kuwa Mfalme wan chi ya Israeli. Ndiyo maana, si jibu sahihi kujitetea eti unashindwa kufanya mambo makubwa kwa sababu hujasoma.

 

Ili uweze kufanikisha mambo yako,ni vizuri utambue na kuheshimu neema za wengine. Imeandikwa Katika GALATIA 2:9…[tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;]….. Tatizo la watu wengi  ni kuona kipawa au neema yamwingine na kuanza kutaka kuishambulia. Daudi baada ya kumuua Goliathi, wanawake walianza kuimba nyimbo za kumsifu Daudi. Matokeo  yake, Sauli alitaka kumuua Daudi.  Mwishowe, yuleyule  aliyetaka kumuua Daudi alikuja kuuliwa. Wape mkono wa shirika wale wanaofanya vizuri. Akina Yakobo, na Kefa, na Yohana walikuwepo tokea awali wakati wa huduma ya Yesu Kristo,  lakini kwa kuwa waliona kipawa alicho nacho Paulo na Barnaba, ilibidi wawaunge mkono.

NANI WALIOHESHIMU VIPAWA VYA WENGINE KATIKA BIBLIA?

a)      POTIFA:

Mwanzo  39:1-6…[1 Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. 2 Bwana akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. 3 Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake. 4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. 5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.]…. Ukimweka mtu wa Bwana na ukaona Baraka zinaongezeka kwenye nyumba yako, ujue huyo ni mtu sahihi mwenye kipawa. Vitumie vipawa walivyopewa watu  na Mungu, vitumie ili kufanikisha ndoto zako.

 
Majeshi ya Bwana ya Bonde la Maono Morogoro wakiomba ibadani Jumapili tarehe 1/2/2015.

 

b)     NEBUKADNEZA:

DANIEL 1:3-4…[Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; 4 vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.]… Huyu mfalme alikuwa hajaokoka, ni mpagani lakini alijua umuhimu wa kutafuta wenye vipawa.

 

c)      DARIO

DANEIL  6:1-2 …[Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; 2 na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.]…. Huyu ni mfalme, aliazimu amweke Daniel juu ya ufalme wake ili aspate hasara. Maana yake, ukitaka  kufanikiwa muweke mtu mwenye kipawa ili usipate hasara.

 

d)     FARAO

MWANZO 41:37-40….[ 37 Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. 38 Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? 39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. 40 Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.]…. Alimchukua Yusufu awe juu ya nyumba yake, na juu ya Misri yote ili ile ndoto yake iweze kutimizwa. Farao alimuamini sana Yusufu,  kijana Muebrania aliyewahi kuwekwa gerezani kwa kosa la kubaka.  Ni vyema umwamini mtu ili na wewe uaminike. Mtu asiyeamini wengine ujue naye ana tatizo. Maisha ya mke na mume vivyo hivyo, ni vizuri waamniane,kwa sababu nje ya hapo ni kujilietea magonjwa ya presha bure.

 

e)     LABANI

MWANZO 30:25-27…[Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu. 26 Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia. 27 Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako.]….Aina hii ya watu kama Labani, ni  wadhulumuji. Labani kwa kubarikiwa kote huku alipaswa amsaidie Yakobo, ili naye afanikiwe lakini Labani  aliikosa hiyo shukrani. Kwa  wewe uliyeokoka, majumbani kwetu vivyo hivyo, yamkini wapo wasaidizi wa ndani (house girls) na wanapaswa kupewa haki zao. Si vyema kuwanyanyasa na kuwanyima mishahara yao pale wanapodai ujira wao. Endapo hawa watanyanyasika,  wanaweza kufanya jambo lolote kwa wanao au hata kuweka vitu visivyofaaa kwenye vyakula wanavyowaandalia. Ni vyema kuwa na amani na watu wote.

Maombi katika Bonde la Maono - Morogoro, Jumapili tarehe 1/2/2015

 

UKIRI
Kwa Jina la Yesu, Nakataa kuanzia leo kuishi maisha yasiyo yangu kwa Jina la Yesu. Amen.
 

 

 

© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Senior Pastor:

 Dr. Godson Issa Zacharia

 (Ufufuo Na Uzima – Morogoro)

Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages