Tuesday, May 17, 2016

KUOKOLEWA KUTOKA KWENYE NYUMBA ZA MASHETANI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI:  15 MAY 2016

 

Na: Dr. GODSON ISSA ZAHARIA (SNP)

 


 

Zipo nyumba zenye kumilikiwa na mashetani, na ndani yake wapo  wakazi yaani watu wanaoishi humo.  Nyumba ni mahali ambapo mtu aweza kuishi na kufanya shughuli mbali mbali. Nyumba ili iiywe nyumba ni lazima iwe na sakafu, kuta na paa.

 

Imeandikwa katika ISAYA 42:6-7.... (“Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; 7 kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa).... Hapa tunaiona nyumba maalum ya kufunga watu. Nyumba za aina hii ni za mashetani, walizoandaa ili kuwafunga watu  wakae humo ndani.

 

NYUMBA HIZI ZIKO WAPI?


ZABURI 119:85 Imeandikwa hivi.....(Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.)..... Yapo mashimo yaliyochimbwa kwa ajili yako. Siyo  mashimo ya kuchimba kokoto. La hasha. Ni mashimo ya kuwekea watu wakae katika mateso.

 

Imeandikwa pia katika ZABURI 35:7.... (Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.).....Kumbe waliochimba shimo kwa ajili  yako na  kukuwekea wavu, hawana sababu.  Siyo  kwamba uliwahi kuwaibia au kutenda dhambi, hapana. Bila sababu wanakuchimbia mashimo ili uangamie. Na hao wanaokuchimbia mashimo, siyo majini, ni  wanadamu wenzako.

 

Imeandikwa katika YEREMIA 5:26-29.....(Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu. 27 Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali. 28 Wamewanda sana, wang'aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji. 29 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?)...... Ndani ya mashimo haya yaliyoandaliwa na wanadamu, vipo vyumba (apartments) vilivyoandaliwa humo humo ndani. Wanadamu hawa wameshirikiana na mashetani kuifanya kazi hii katika ulimwengu wa roho.

 

ISAYA 42:22 Imeandikwa hivi....( Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.).... Anayechimba shimo,ameweka vyumba na nyumba za magereza, na watu wakiingia humo hunasa.


Wachawi, kwa mfano wanao uwezo wa kuchukua hata macho yako tu au miguu yako tu!!!. Wapo watu ambao kwa macho yao tu husababisha mambo yatokee. Wengine ni vinywa vyao, wakiongea lazima wakubalike. Kinywa au macho ya aina hii huibiwa na  wachawi na kuvipeleka mashimoni. Leo ni siku ya kuingia kwenye hivyo vyumba vya mashetani na kuwaachilia huru walioshikiliwa humo kwa Jina la Yesu.

 

Imeandikwa katika MITHALI 7:27.....( Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti).......Mauti na kuzimu hufanya kazi pamoja, kama ambavyo imeandikwa katika UFUNUO 6:8...( Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye.)... Kwa hiyo, unaweza kuiona nyumba,lakini kumbe ni nyumba yenye vyumba vya mauti ndani yake.

 

Imeandikwa katika MITHALI 5:5....( Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu;)...Wewe waweza kuiona miguu ya mtu kuwa ya kawaida, lakini miguu yake tu ukishikamana naye yaweza kukupeleka kuzimu. Kumbe unayeshirikiana naye aweza kuwa na miguu, kwa nje  waweza kumuona mtu wa kawaida lakini kumbe siyo mtu, kwa sababu miguu yake  imeshikamana na kuzimu.


Bwana Yesu alikuja ili kuvunja nguvu za aina hii. Yamkini hata leo, yupo mtu aliyekuwa anakushawaishi usije kanisani siku hii ya leo kwa kukuletea dharura za aina aina. Huyo bila shaka ni mjumbe wa shetani, kwa sababu miguu yake ni maalumu kwa kupeleka watu kuzimu.

 

Tulishafundishwa kuwa kuzimu haishibi. Kama ambavyo Yesu alisema nyumbani mwa Baba yake kuna makao mengi, na Yesu alienda ili kutuandalia makao,  shetani naye ana vyumba vya aina hiyo anakoweka misukule na kuwatesa. Leo tutaingia kwenye vyumba hivyo vya mashetani na  kuvipasua pasua kwa Jina la Yesu.

 

MITHALI 27:20 Imeandikwa...(Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi.).... Je, uliwahi  kuisikia kuwa malaria imeisha? Hapana. Na Uharibifu je? Hii ni kuthibitisha kuwa,  kuzimu inaendelea kuachama mdomo wake wazi ili kupokea watu kupitia magonjwa kama malaria na uharibifu mbali mbali.

 

Imeandikwa katika MITHALI 30:16......(Kuzimu; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!)... Na pia katika MITHALI 9:18 imeandikwa....( Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.)...... Kuna mambo mawili hapa: Kuzimuni kuna wageni, na wafu wamo humo ingawa wewe hujui.

 

Kuna watu au mtu ukiwa unatembea naye unajikuta imani yako inatetereka, na hata kumpenda Mungu kwako kunapungua. Hii ni kwa sababu mtu wa aina hiyo ana miguu ya kuelekea kuzimuni.  Hata nyumba, zipo ambazo kila ukiingia humo, hata kuomba inakuwa ngumu. Hii ni kwa sababu baadhi ya nyumba kama hizi zimeshikamana na kuzimu. Leo kwa mamlaka ya Jina la Yesu Krsito, tunavibomoa hivyo vyumba na kuvipasua ili waliomo humo waje kwa Bwana Yesu.

 

Yeyote anayechukuliwa kwenye hivyo vyumba vya mashetani ni wale wenye vitu (kibali, akili sana, uwezo wa kielimu, biashara n.k.). Mtu asiye na kitu hawezi kupelekwa au kupokelewa huko. Hata hivyo, Vyumba hivi havionekani  kwa macho ya kawaida. Wachawi wanapokiona kibali ulicho nacho hufanya mbinu na mipango ya kukuiba ili kukipata hicho kibali.

 

Yamkini kuna mtu umeonekana kuwa na tumbo ambalo laweza kumzaa Waziri,  au Mwanariadha maarufu Tanzania, au tumbo hilo  kuwa litamzaa mtu maarufu sana. Wachawi huiba matumbo ya aina hii, na kuyafungia kwenye vyumba maalumu. Endapo watakuja wahitaji wa matumbo  ya aina hii, waganga wa kienyeji  huwataka wanaohitaji matumbo ya aina hii,  watoe kafara kwanza. Hata hivyo, waganga huhitaji kafara za damu. Haijawahi kutokea mganga wa kienyeji kumtaka mteja wake akamletee kafara ya matunda, au mbogamboga au mchele. Mara zote waganga huagiza kuletewa kafara ya wanyama ili kuipata damu za kuimarisha nguvu zao za giza (Kwa sababu kwenye  damu kuna uhai). Matokeo yake,  wewe uliyeibiwa tumbo la aina hii,  utaendelea kuzaa watoto wasio kuwa na akili au wasio na kibali chochote.

 
Imeandikwa katika YEREMIA 50:33......(Bwana wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.)..... Biblia inasema wanaokuchukua mateka wanawashika sana na hawataki kuwaachia. Vivyo hivyo imeandikwa pia katika ISAYA 14:17.....(Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?).

 

UKIRI
KWA JINA LA YESU, YEYOTE ALIYENIFUNGIA KWENYE CHUMBA CHA GIZA LEO NINAKATAA KUKAA HUMO  SHIMONI, NATOKA KWA JINA LA YESU. AMEN

 

Bwana anasema hivi: Vile vyumba vilivyojengwa na kufungia watu kwenye nyumba za aina hiyo,  hata kabla ya jina la Morogoro kuwepo, leo vimefungwa kwa Jina la Yesu Kristo.

 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH

 

 

 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages