Monday, June 13, 2016

Somo: MISHALE YA MAUTI-Na: Dr. GERSHOM (RP)


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI:  12 JUNE 2016

 
 

 

Shetani asili yake ni kuwaonea watu. Shetani huifyatua mishale ya kuwapiga watu, inayokuwa imetegwa na wachawi na waganga wa kienyeji wakishirikiana na shetani katika kuwaonea watu. Hiyo mishale hawakupigi eti  kwa sababu umekosea lolote, lahasha, bali ni kwa sababu kiasili shetani huwaonea watu, kama ilivyoandikwa katika MATENDO 10: 38  ...“habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye”.

 

Mauti ni nini? Mauti ni roho ambayo inaweza ikatumwa na ikimwingia mtu inaweza kumsababishia kifo.Mauti sio tukio bali ni roho ambayo hata katika kazi, ikiingia humo husababisha kifo cha hiyo kazi. Mauti inaweza kupanda farasi,  au bodaboda,  au gari n.k.  Imeandikwa katika UFUNUO 6:8 ... Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.”

 

Roho ya mauti huweza kutengeneza tukio.  Mathalani yapo magonjwa ya mlipuko ambayo nyuma yake ni roho za mauti zinazogeuka na kuwa ugonjwa fulani kama vile kipindupindu na mwishowe kuishia kuwa tukio la kifo. Mauti yaweza kuingia katika masomo, na kusababisha ukosefu wa ada ili kuua kile ambacho Mungu alikiweka kwa ajili ya hatima ya huyo mtu ya kusoma na kuwa mtu mkubwa sana katika jamii. Biblia inasema kuwa, mauti ndiyo silaha ya pekee anayoitegemea shetani. Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 15:26...”Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.” Shetani huwafanya watu waanze kumiliki baadhi ya magonjwa, na hata kusikika akisema “pumu yangu, malaria yangu, kifaduro changu n.k.

 

Katika Biblia, zipo aina 2 kuu za mauti:

1.     Mauti ya Mwili na Mauti ya Roho. Mwili  unapotengana na roho, mauti  ya mwili hutokea. YAKOBO 2:26... “Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.”. Ni kweli kuwa imani pasipo matendo imekufa, na pale Roho ikitoka ndani ya mwili ndiyo watu tunasema mtu fulani amekufa. Imeandikwa katika YOHANA 6:63  ... “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”.  Hii inamaanisha kuwa Mwili pasipo roho hakuna kitu.

 

2.     Mauti ya  pili ni  pale roho itakapotupwa Ziwa la Moto (Jehanamu). UFUNUO 20:14... “Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.”.... Tumeona kuwa Mauti siyo tukio, na ndiyo maana mauti na kuzimu vyaweza kukamatwa na kutupwa katika Ziwa la Moto.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 10:28 ... Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.”........ Hao watu wenye kuweza kuua mwili ni  wachawi,  wafuga majini, wasoma nyota,  waganga wa kienyeji n.k. hawa wanaweza kuua mwili, kwa maana yakutenganisha mwili na roho. ZABURI 124:7.... “Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.”. Hii mitego ianweza kutegwa na hawa wasoma nyota na wenzao, ili kumwingia mtu kama mshale, na mwishowe kusababisha tukio.

 

Imeandikwa katika EZEKIELI 13:17-19... “Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, 17 Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, 18 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? 19 Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo”... Wapo hawa wenye mishale ya mauti ndiyo hao hao wanaowinda maisha ya watu ili kuzuia wengine wasifanikiwe.  Kuna watu walipaswa kuwa hai, lakini wamekufa. Na wapo wengine walipaswa kuwa wamekufa lakini bado wako hai.Kuna mishale ya magonjwa inaweza ikatumwa ndani ya mtu na mtu huyu akaugua hadi kufa,mishale inapotumwa kwa mtu inakua na sumu ikiingia kwenye ndoa inakufa,roho ya mtu inaweza kuwindwa kuna watu wanafunga hirizi kumbe hirizi hizo ni mishale kwa ajili ya kufunga watu na kuwinda roho za watu

 

Imeandikwa katika EZEKIELI 13:20Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege.”... Kuna kazi zilipaswa kuwa zimekwisha kufa laknni wapo watu wanazifanya hizo kazi ziendelee kuwa hai.

 

Imeandikwa katika ZABURI 64:3 - 5 ... “Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu, 4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi. 5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona? 6 Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa.” Waganga na kundi lao, hutega mitego kwa kutumia hirizi zao n.k.  msahale wa mauti unaweza kutumwa katika biashara yako na kugeuka kuwa majambazi wakaiba pesa zote biashara yako ikafa. Mshale wa mauti pia waweza kutumwa katika kazi yako na kugeuka kuwa roho ya kuacha kazi. Mshale waweza kumuingia mtu na kugeuka kuwa kifo. Mchana wa leo tunaifyatua mishale yote kwa JIna la Yesu.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 17:15-18 “Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. 16 Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. 17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. 18 Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.”....  Pepo ni roho. Ndiyo maana lilimwingia huyu kijana na kuweka mazingira hatarishi ili akifa ijulikane kilichomuua ni kifafa. Yesu alipomuangalia akasema nakuona ewe mauti akaikemea ile mauti yule kijana akawa mzima.Hapa tunaona Yesu  hakushughulikia kifafa bali ile roho iliyojificha nyuma ya kifafa, yaani pepo. 

 

Katika WAEBRANIA 2:14-15 Imeandikwa... “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, 15 awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.” .....

 

Wanadamu wanaiogopa mauti kuliko  vitu vyote. Yesu aliinyausha nguvu ya mauti tokea shinani. Yesu angeweza kuiepuka ile mauti,tunaona Bwana Yesu walivyomsulubisha msalabani alikua kwenye hatua ya kwenda kuikabili mauti,baada ya kufa msalabani alitoka ndani ya mwili akashuka hata kuzimu akamnyang,anya shetani ufunguo wa mauti na kuzimu.Kristo alishinda mauti baada ya kukaa kaburini siku tatu,  lakini alitaka afe msalabani ili baadae aingie mahali anapokaa shetani, na kuangamiza silaha yake  ya mauti na kumharibu tokea kwenye chimbuko lake. Kwa siku  zote tatu, kaburi la Yesu lililindwa na maaskari wengi wenye silaha,  wakizuia wanafunzi wake wasije kumuiba,na wakitaka kumzuia Yesu asifufuke. hata hivyo, malaika  aliposhuka mahali pale, wale maaskari walitetemeka, na kuwa kama wafu, na Yesu akatoka kaburini mzima.

 

UKIRI
Mchana wa leo tunawatuma malaika kuvitoa vyote vilivyofungwa katika maisha yako kwa Jina la Yesu. tunamtuma malaika akaliondoe jiwe lililozuia masomo yako. Waliofungwa kaburini, katika jina la Yesu kila mishale wa mauti uliotumwa kwenye maisha yangu, mishale ya magonjwa,kushindwa naing,oa kwa jina la Yesu,nakanyaga nguvu ya mauti,mauti kwa ajali naifunga kwa jina la Yesu…….Amen.
 

 

Mauti ilishindwa pale msalabani. ZAURI 38:12 ...’” 12 Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa.”

 

YEREMIA 5:26 - 27 .... “Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu. 27 Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali. 28 Wamewanda sana, wang'aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji. 29 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?  ”...  Mungu anajiuliza, hivi  kwa hali kama hii nisijipatilize kwa watu wa aina hii?

 

ZABURI 91:3-4... “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.”... Mtego wa mauti ni ule ambao adui anakutumia, akijua tayari una sumu ili apate kukuangamiza au kukuua. Wapo watu hata sasa hivi, ameshategwa tayari. Kila mtego huwa na mtu ambaye aliutega. Iwe ni mitego ya magonjwa, iliyotegwa njiani, iliyotegwa katika vyakula, na mahali popote pale, leo tunaing,oa kwa Jina la Yesu.

WAEFESO 6:11-15 ...“Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka,  juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.”.... 

Adui anaweza kukuvamia na mishale hii ya moto pindi akikukuta hauna Roho wa Kristo ndani mwako. Leo ni vyema kumpa Yesu maisha yako, kwa wewe ambaye hujaokoka.

 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH

 

 

 

 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages