Monday, June 20, 2016

Somo: SABABU ZA KIFO CHA GHAFLA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI:  19 JUNE 2016

 

Na: STEVEN NAMPUNJU (RP)

 

Tunakumbuka kwamba ili mtu ithibitishwe kuwa amekufa, lazima mwili wake utengane na roho yake. Na kama hivi ndivyo, lazima apatikane kitu cha kutenganisha kati ya 'roho na mwili'. Yesu akasema, "Nautoa uhai wangu ili niutwae tena". Ndiyo  kusema, ni Yesu pekee ndiye aliyeweza kuutoa uhai wake mwenyewe na kuutwaa tena, na wandamu wengine wote uhai wao hutolewa na yule anayeutoa uhai.

 

 

Imeandikwa katika UFUNUO 6:7-8.... “Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! 8 Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.”.   'Kuzimu na mauti' ni roho pacha, wanaofanya kazi moja lakini tofauti. Kuzimu huutesa mwili na ndiyo maana inatamba kwa kuutesa mwili wa mtu. Kuzimu italeta kukonda, kuugua, uchovu na kila udhaifu wa kimwili. Kwa upande mwingine, Mauti kazi yake ni kuufukuza uhai, kwa kuua. Hata hivyo ili mauti na kuzimu waweze kuua, lazima ziwepo sababu za kuua: Kama hapa sababu iliyotajwa ni TAUNI,  HAYAWANI, NJAA na UPANGA. Kwamba tauni inapewa mamlaka ya kusababisha kifo!!!. Njaa kali katika kijiji au  taifa yaweza kutokea lakini sababu yake ni kuuondoa uhai wa watu mahali hapo.

 

 

Kwa maandiko hapo juu tunajifunza kuwa mauti ina uwezo wa kupanda gari, farasi, bodaboda n.k. Mauti huandaa tukio la kuharibu ndoa, kazi, biashara, kwa kupanda usafiri wa aina yoyote ili kufuatilia na mwishowe kuundoa uhai. Mauti yaweza kusafiri toka Tanga, Songea n.k. na kwenda ilikotumwa ili kusababisha 'tukio la kifo'. Nyakati nyingine, unaweza kumuombea mtu mwenye mashetani ndani mwake, na kushangaa yakitamka kuwa yametumwa ili  kumuua. Swali la kujiuliza je, kwa nini muda wote haya mashetani hayajamuua? Jibu ni kwa sababu yanakuwa yanasubiria muda uliopangwa kwa tukio hilo kufanyika.

 

 

UKIRI
Nailazimasha kila roho ya mauti  iliyopandwa ndani  mwangu iniachie kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

Mungu hawezi kuruhuusu mtumishi wake kuangamia bila kumpa taarifa. Hezekia alipata taarifa ya kifo chake hata kabla ya kifo hicho kutokea, na akambiwa atengeneze mambo ya nyumbani mwake. Imeandikwa katika ISAYA 38:1Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona”. Maana yake, kama Hezekia alikuwa na watoto bado anasomesha, basi ahakikishe  anamalizia kuwasomesha shuleni kabla ya kifo chake n.k.

 

KIFO CHA GHAFLA KINATOKEA WAPI?

 
Kifo chaweza kuingia katika biashara, ndoa n.k. HOSEA 13:14... “Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu.”... Mungu hapa anasema atatuokoa na nguvu za mauti. Yapo mapigo yanayoambatana na kifo. Katika UFUNUO 6:8Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.”.... Matukio yenye kusababisha kifo yanatajwa, kama vile upanga, njaa, hayawani na tauni. Kuzimu hutekeleza matukio yaletayo kifo, mfano kuanguka kwa majengo, ajali za aina zote n.k.

 

MAMBO MUHIMU YA KUFAHAMU KUHUSU KIFO / MAUTI
 

1.      Kifo kinaweza kupanda gari ili kwenda kwa mtu. Tumesoma katika UFUNUO 6:7-8. Kama mauti na kuzimu zimepanda farasi, maana yake zinaweza kuendesha farasi. Hata katika maisha ya leo, mauti yaweza kupanda gari, au bodaboda ili kufika sehemu husika kwa haraka.  Lengo  ni kufika haraka na kuleta uharibifu. Ndiyo maana kuna watu wanajikuta kupoteza nafasi zao za kazi hata baaada ya kuahidiwa kupatiwa, ni  kwa kwa sababu mauti  inakuwa imetangulia kwa maboss wa maeneo hayo kwa kupanda usafiri wa haraka kabla ya mhusika.

 

2.      Mauti yaweza kuwa ndani ya sufuria au ndani ya chakula. Mauti ni roho, na kawaida roho yaweza kukaa na kugeuka kitu chochote.

 

2WAFALME 4:38 - 39  ...... “Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii. 39 Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtangomwitu, akayachuma matangomwitu,  hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasuapasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.”.... Katika matango  mwitu hapa, ni  kwamba huyu mtu hakuyajua. Katika ndoa, waweza kujikuta una umri miaka 37 au zaidi na kuona mtu ghafla amekuja  kwako na wewe bila kujua ukadhani huo ni muujiza wa Bwana,  kumbe ni matango mwitu (Mtu wa kuharibu maisha yako.)

 

2WAFALME 4:40 – “Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.” ....... Mauti haitoki hadi upige kelele. Walipiga kelele kusema mauti ipo sufuriani. Kumbe unaweza kuichemsha mauti sufuriani hadi ikaiva, na hata ukaanza kuila. Mauti yaweza kuingia sufuriani au hata kwenye chakula chako.

 

3.      Kifo kina chanzo chake. Kabla ya dhambi kuwepo duniani, mauti ilikuwa haipo. Baada ya Adamu na Eva kuasi, ikawa chanzo cha mauti kuwepo duniani. 1 WAKORINTHO 15:21...... Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu”.

 

2WAFALME 2:21-22 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. 22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena”.  Neema waliyokuwa nayo watu wa mji huu ni ile  kubaini au kuiona shida ya tatizo  lao. Watu wengi hata leo hii wanakuwa na matatizo lakini hawajui chanzo cha matatizo  yao ni kitu gani!!!!. Ina maana katika hayo maji, hata mama wajawazito wakiyanywa maji ya mahali hapo, watoto hufia matumboni mwao, n.k, na ndiyo kuzaa mapooza. 

 

Mauti hutengeneza uhalali wa kifo. Mathalani katika biashara, mauti ikiingia hutengeneza sababu ya wateja wa biashara yako kukukimbia, na mwishowe biashara hufa.

 

 

UKIRI
Ewe mauti uliyetengeneza sababu ya kufanya kazi ndani ya maisha yangu leo nakushinda kwa Jina la Yesu. Amen
 
 

 

 

 

4.      Kifo kinaweza kuptia dirishani. Imeandikwa katika YEREMIA 9:21.... Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu.”.... Yaani mauti yaweza kuingia madirishani, hata kama umefunga milango ya nyumba yako kila kona. Hata walinzi majumbani mwetu hawakai madirishani bali kwenye milango kulinda. Ndiyo kusema mauti ikipandia dirishani hata walinzi hawasaidii chochote!! Leo lazima tuikamate mauti inayovizia kuingia maisha mwako, kwa Jina la Yesu, na tutafunga milango na madirisha pia. Lengo  kuu la mauti  kuingia ndani ni  kukukatilia mbali. Mauti ina akili  ya kupanda kuelekea ndani.

 

5.      Mauti inaweza kuzungumza. Yaani mauti ina kinywa cha  kusema,  na kupanga bajeti kabisa. AYUBU 28:22... Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu”. Mahali hapa kuzimu inatajwa kama 'uharibifu', kwa sababu ya kazi yake ya kuleta uharibifu. Kumbuka tumesema, 'mauti na kuzimu' ni roho pacha. 

1 WAKORINTHO 15:26 ... Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.”.... Kwa kawaida, adui wa mwisho ndiye mwenye nguvu kupita wote waliomtangulia.

 

MITHALI 18:21..“Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;  Na wao waupendao watakula matunda yake”.... Mauti na uzima zipo katika mamlaka ya ulimi, na tena uzima au mauti vyatoka katika ulimi. Ndiyo maana wapo watu kusema kwao ni uvuvio wa mauti tu. Ni rahisi kumgundua mtu ambaye ndani mwake ipo roho la mauti. Siyo rahisi kumjua mtu kabla hajaongea chochote. Neema ya aina hii ni  muhimu sana kuwa nayo. Wapo wanaosema “Kwa ugonjwa  nilio nao siwezi  kupona‼‼”. Maana yake ni  kuwa, anayezungumza mambo kama hayo ni 'roho la mauti' ndani ya mtu husika. Uzima nao huletwa kwa kinywa, kwa kuongea. Hata Yesu kabla ya kufufua alikuwa anaongea, na ndiyo maana akamwita Lazaro na kumwambia "NJOO".

 

Mauti inaweza kusikia. Mauti inayo masikio. Kuzimu na Mauti wanaposikia  kwa masikio yao, huanza kupanga vita na mipango ya uharibifu. Imeandikwa katika AYUBU 28:22... Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu”. Mauti inaweza kuwa ndani mwako, ukatembea nayo bila wewe kujua. 

 

 

UKIRI
Naulazimisha ulimwengu wa roho ulioandaa masikio, leo nayatoboa masikio yote ya kishetani yaliyotegwa katika ofisi yangu na katika familia yangu, leo nayatoboa masikio yao. Roho ya Mauti aliyetumwa apande farasi ili anifuatilie, leo nayatoboa masikio yake kwa Jina la Yesu. Amen

 

Nduguze Yusufu walitengeneza sababu ya kuhalalisha kifo chake kwa baba yao (Mzee Yakobo). Ingawa mzee wao Yakobo aliziamini taarifa zile baada ya kuona ile nguo iliyolowa damu, hata hivyo ukweli ni kuwa Yusufu alikuwa utumwani, na hakuwa amekufa!!!!. Leo tutapigana na wale waliohalalisha kifo chako kwa kukupeleka utumwani kwa Jina la Yesu.

 

Bila Yesu mauti haiwezi kuondolewa katika jamii au familia yetu. Ukimwamini Yesu leo, yeye pekee anao uwezo  wa kuikamata mauti na kuiondoa kwako kwa Jina la Yesu.


Leo ni  nafasi pekee kwako  ambaye hujamwamini Yesu kufanya hivyo kwa kuokoka. Imeandikwa katika WAEBRANIA 2:14-15 .....Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, 15 awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa”. Ukimwamini Yesu leo ataiharibu nguvu ya mauti maishani mwako.

 
 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH

 

 

 

 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages