Monday, June 27, 2016

LAANA YA KUMUIBIA MUNGU ZAKA

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI:  26 JUNE 2016

 

Na: Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

 

Zaka ni sadaka. Ili tuweze kupata baraka za kimungu tunapaswa kumtolea Mungu sadaka. Unapotoa  unaleta vile  vya aasili vije kwako. Usipotoa sadaka au  zaka,  unafunga vile vya asili visieweze kuingia kwako. Kwa hiyo zipo baraka tele katika kutoa.

 

LAANA YA KUMUIBIA MUNGU ZAKA NDIYO NINI?

Hii ni laana impatayo mtu kwa kosa la kutomtolea Mungu zaka. Humfanya mtu aharibikiwe na kupata magonjwa na mateso ya aina mbalimbali kwa kutomtolea Mungu zaka. Nyuma ya laana zingine zote yupo shetani ISIPOKUWA laana ya kumuibia Mungu zaka kwa sababu Mungu mwenyewe ameiruhusu laana hiyo impate mtu. Huwezi kuiondoa hii laana kwa maombi ya kukemea.

 

ZAKA NI NINI?

Zaka ni sadaka au matoleao maaulumu ambayo ni tofauti na sadaka zinginme zote. Ni sehemu ya kumi (10%) ya vitu vyote ulivyobarikiwa navyo. Kwa  lugha ingne,  ni fungu la kumi la vitu vyote apatavyo mtu. Zaka hujulikana kama kodi ya maendeleo ya nyumba ya Bwana.

 

 

Imeandikwa katika 2 NYAKATI 24:9-10 ....(Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea Bwana kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani. 10 Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.)... Tunajifunza kuwa "Kodi" hii ni ya kufanya  watu wafurahi, siyo kuitoa huku umekunjamana au umenuna usoni.

 

Imeandikwa katika HESABU 31:37....(na kodi ya Bwana katika hao kondoo ilikuwa kondoo mia sita na sabini na watano.)..... Kodi ya Mungu/Bwana ni asilimia kumi  au fungu la kumi la mapato yako.

 

 

1.       UTOAJI WA FUNGU LA KUMI KATIKA AGANO LA KALE

 

IBRAHIMU ALITOA FUNGU LA KUMI KWA KUHANI MKUU AITWAE MELKIZEDEKI.

Imeandikwa katika MWANZO  14:18-20....(Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. 19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. 20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.)....

 

 

Imeandikwa katika WAEBRANIA 6:20.....(alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.). Yesu amefananishwa na Kuhani Mkuu aitwae Melikizedeki, aliyepokea zaka kutoka kwa Ibrahimu. Hata Yakobo ambaye pia ni uzao wa Ibrahimu, pia naye alitoa fungu  la kumi.

 

UTOAJI WA FUNGU LA KUMI WAKATI WA MUSA

 

Imeandikwa katika WALAWI  27:30-33..... (Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana. 31 Na kama mtu akitaka kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake. 32 Tena zaka yote ya ng'ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa Bwana. 33 Hataangalia kwamba ni mwema au kwamba ni mbaya, wala hatambadili; na kama akimbadili na yo yote, ndipo wote wawili, huyo na huyo waliobadiliwa watakuwa ni watakatifu; hatakombolewa.).... Mbegu katika andiko hili maana yake ni MTAJI. Kwa hiyo fungu la kumi katika mtaji lazima itolewe.  Matunda nayo yapaswa kutolewa zaka, yaani kile kinachozalishwa na mbegu / mtaji wako, kama ambavyo  imeandikwa katika KUMBUKUMBU 14:22.....( Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.).....

 

 
2.      FUNGU LA KUMI WAKATI WA AGANO JIPYA

 
Imeandikwa katika WAEBRANIA 7:4-7....(Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. 5 Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu. 6 Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. 7 Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa.)......

 

Pia imeandikwa katika WAEBRANIA 7:9... (Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi;)...

 

 

3.      UTOAJI WA FUNGU LA KUMI WAKATI WA MANABII

 

Imeandikwa katika 2 NYAKATI 31:5.....(Mara ilipotangaa amri, wana wa Israeli wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, na divai, na mafuta, na asali, na mazao yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta nyingi)... Hapa tunawaona wana wa Israeli wakitoa zaka kwa ya vitu vyote kwa jinsi ambavyo Mungu alikuwa amewabarikia katika mashamba, mazao na malimbuko ya vitu vyao vyote.

 

 

4.      KAZI YA WA FUNGU LA KUMI

 

(i).  Kuwepo Chakula Nyumbani mwa Bwana.

Imeandikwa katika MALAKI 3:10.... (Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.).... Mbingu zina madirisha ya kumwaga baraka tele kwa watu wanaokubali kutoa zaka kamili ghalani. Kwa hiyo kazi kubwa ya fungu la kumi ni kuwezesha chakula kiwepo nyumbani mwa Bwana, na siyo katika nyumba ya mtu fulani au mchungaji. Kwa lugha nyingine, ni kwa njia hii ya zaka hata hao wachungaji wataweza kuifanya kazi ya Bwana kwa ufanisi.

 

Nyumba ya Bwana ni kama jengo letu la kanisa. Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu yote, na kwa maana hiyo ni muhimu kwetu kumjengea Nyumba Kubwa kuliko zote kutokana na ukuu wake wa ajabu.

 

 

CHAKULA GANI KINAZUNGUMZIWA HAPA KATIKA MALAKI 3:10?

Imeandikwa katika YOHANA 4:34.....(Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.).... Kwa hiyo unatoa zaka ili kazi ya Bwana ifanyike na kuenda vizuri. Maana yake, tuifanye kazi ya Bwana iende vizuri, kwa kununua vyombo vya sauti, viti, muziki n.k.


Biblia inapoosema "mapenzi yake" maana yake ni ipi? Mapenzi ya Mungu ni Kuona watu wanawekwa huru, wenye mapepo wanaachiwa huru, wagonjwa wanapata uponyaji, viwete wanatembea, wafu wanafufuliwa  n.k.

 

Imeandikwa katika LUKA 4:18.....(Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,  Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.).... Haya yalikuwa  ni maneno ya kwanza kabisa ya Yesu (Abstract) wakati wa kuianza kazi / huduma yake duniani. Hii ndiyo kazi, ya Kuwafungua walio magerezani, kuwaachia huru waliosetwa kwa Jina la Yesu.

 

 

UKIRI
Kwa Jina la Yesu ninajifunza maneno kutoka kwako, unisaidie sasa kuujua ukweli kwa maana hiyo kweli ndiyo itaniweka huru kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

Imeandikwa katika LUKA 8:1-3...(Ikawa baada ya hayo alikuwa akizungukazunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, 2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, 3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao).... Yesu anahudumiwa na watu walioonesha shukrani baada ya kupata uponyaji wao. Watu hawa walitumia mali zao ili kuitegemeza huduma ya Yesu hapa duniani. Hata leo hii, ni wajibu wako kuitegemeza huduma ya Bwana katika Kanisa kwa kutumia mali na fedha zako kadiri unavyobarikiwa na Bwana.

 

 

Ukisoma katika HESABU 18:21...(Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania;)... Kumbe kwenye hema la kukutania, ni lazima lihudumiwe kwa kutumia  zaka.

 

 

FAIDA ZA KUTOA FUNGU LA KUMI

Bibilia haizungumzii faida za kutoa sadaka za kawaida. Ni zaka pekee ambayo Mungu ameitamkia maneno ya baraka kwa kuitoa.

 

MALAKI 3:10-12....(Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.
12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.)....... Kwa maandiko haya, tunaona kuwa, zipo FAIDA ZA KUMTOLEA MUNGU ZAKA, nazo ni kama ifuatavyo:-

 

(i).     Mungu atafungulia madirisha ya Mbinguni. Na kwa namna hiyo, mvua za Baraka zitafuatia. Kwa hiyo Baraka za Mungu huja kama mvua. Baraka humwagwa kama mvua. Na kwa maana hiyo, endapo mtu hatoi fungu la kumi, kinyume chake ni kuwa madirisha ya mbinguni yatafungwa kwa ajili yako.

 

 

(ii).  Mungu atamkemea shetani (adui alaye) mazao yetu.

Mazao ya mashamba yetu hayataharibiwa na shetani. Iwe ni katika biashara, kazi, masomo, mashambani n.k. shetania anayeharibu atakemewa kwa Jina la Yesu.

 

 

(iii).                  Mazao ya ardhi yetu hayataharibiwa

Mazao hapa ni kama kazi zetu, biashara yako,n.k. itakuwa salama na hakuna wa kuziharibu. 

 

(iv). Mzabibu wako hautaangamia wala kupukutisha mazao yake.

 
Hii maana yake ni: Unapokuwa katika Yesu unakuwa sehemu ya Mzabibu, kwa kuwa yeye ndiye mzabibu wa kweli na ulio bora. Kwa lugha ingine, haitakuwepo mapooza katika mazao yako. Hautaanzisha jambo nalo likashindwa kabla ya kufikia mwisho wake katika Jina la Yesu.

 

(v).   Mataifa yatakuita heri.

 

Maana yake, kila atakayekuona atakuwa anasema hakika wewe ni heri. Kuna wakati watu waklikuona jinsi ulivyobarikiwa, watakiri kwa vinywa zao kuwa hakika umebarikiwa.

 

 

NANI ANAYETAKIWA KUTOA FUNGU LA KUMI?

Fungu la kumi lazima litolewe na kila mtu. Hapana kusema eti fungu la kumi litatolewa na wale wakubwa tu wenye mali, HAPANA. Kwa kila sh.1,000 unayobarikwa nayo, hakiksiha kuwa sh.100 unaitenga ili kuwa fungu lako la kumi / zaka.

 

 

Katika 1WAFALME 17:10-16 Imeandikwa... (Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. 11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. 12 Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa,    na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. 13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee;    kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. 15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.).... Ukiwa mwaminifu mbele za Bwana, kile kidogo ulicho nacho hakitapungua kwako kawa Jina la Yesu.

 

 

Mfano mwingine ni pale ambapo Yesu aliwahi kuchungulia katika kikapu cha sadaka. Alikuwepo mwanamke mjane aliyekuwa na sadaka ndogo sana mkononi mwake, iliyokuwa ya mwisho kabisa kwa matumizi yake binafsi. Imeandikwa katika LUKA 21:3-4.... (Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; 4 maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo.)

 

 

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UTOAJI WA ZAKA ZAKO ILI ZIWE BARAKA

(i).  Peleka zaka katika nyumba ya Bwana ambapo Kweli ya Kristo inahubiriwa

 

Hapa ni  pale ambapo  watu wanahubiri kweli, na siyo wanaopinga au kuukataa wokovu. Endapo mahali uanpopeleka zaka wanakataa wokovu, maana yake ukiitoa zaka yako utakuwa unashirikiana nao katika kuudhoofisha wokovu.

 

(ii).        Usipeleke zaka nyumbani kwa mchungaji

 

Zaka ipelekwe nyumbani kwa Bwana, wala siyo nyumabni kwa mchungaji wako. Endapo utaipeleka zaka nyumbani kwa mchuungaji, kitendo cha kufanya hivyo maana yake ni kuwa unataka kumshawishi mchungaji naye awe mwizi pale atapoitumia kwa kujisahau.

 

(iii).      Peleka zaka zako mahali ambapo chakula chako cha rohoni unakula

 

Haifai kuwa unalishwa chakula cha rohoni mahali hapa lakini inapofikia katika kutoa fungu la kumi bado unaendelea kuitoa zaka kwenye Kanisa lako la zamani ulikotokea.  Imeandikwa katika WAGALATIA 6:6.... (Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.)..... Sisi ni wakufunzi wako, na wewe ni mwanafunzi wetu.

 

 

KWA NINI LAANA IWEPO?

Siri kubwa ni kwamba, vyote tulivyo navyo ni mali za Bwana. Imeandikwa katika MALAKI 3:8-9....(Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.)..... Hii ni laana ambayo hata kama utataka kuifyeka kwa maombi, siyo rahisi kuondoka.

 

Laana ya mwizi inao uwezo wa kuingia katika Nyumba. Imeandikwa katika ZEKARIA 5:1-4...... (Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo. 2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. 3 Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili. 4 Nitaituma itokee, asema Bwana wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.).... Laana kwa mwizi hutumwa na Mungu mwenyewe. Endapo umeiba, laana hutumwa na Mungu mwenyewe. Hata ungejaribu kuomba namna gani, haitawezekana.

 

 

JE MWIZI WA ZAKA AFANYE NINI ILI KUIONDOA HII LAANA?

1.       Njia kuu kuliko zote ni Kutubu. Hii ni kwa wale waliokuwa hawatoi zaka kabisa au walikuwa wakitoa pungufu isiyo kamili.

 

2.      Kuishi maisha matakatifu, na kutoa zaka kama ikupasavyo kufanya. Asiwepo mtu wa kuitumia zaka kama mkopo.  Na endapo mtu atakuwa ametubu na kuanza maisha mapya na Bwana kwa kutoa zaka, itakuwa  rahisi kufyeka mashetani na nguvu zote za giza.

 
 

 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH

 

 

 

 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages