GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO
JUMAPILI: 31 JULY 2016
Na:
STEVEN NAMPUNJU (RP - MOROGORO)
RP Steven akifundisha kuhusu "Magereza ya Kichawi" Jumapili 31/7/2016 Katika Nyumba Ya Ufufuo na Uzima - Bonde la Maono Mkundi (Morogoro) |
Magereza ni sehemu au makao ya wafungwa ambako wanaishi. Wapo watu
wamepindishiwa maisha yao kwa sababu tu ya kuwekwa katika magereza. Yumkini
unaishi jinsi ulivyo lakini sivyo ungependelea kuishi. Unatamani kula vitu
vyenye ladha ya sukari lakini gereza la Kisukari linakuzuia kula vitu hivyo.
Kuna maisha fulani unayatamani uishi lakini umejikuta unaishi ndivyo sivyo.
Chanzo cha yote haya ni magereza. Na magereza haya yapo ya aina mbili: Magereza ya mwilini na Magereza ya rohoni.
Je, yale uliyokuwa unayatafuta miaka mingi iliyopita umeshayapata? Kama
bado ujue lipo gereza ambalo limefungia
vitu vyako ulivyomuomba Bwana. Leo tutashughulika na magereza yote ya rohoni na
kuwaweka watu huru kwa Jina la Yesu.
Katika WARUMI
7:21-25 Imeandikwa.....(Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi
nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. 22 Kwa maana naifurahia sheria
ya Mungu kwa utu wa ndani, 23 lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo
mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria
ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. 24 Ole wangu, maskini mimi! Ni nani
atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? 25 Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana
wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya
Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.). Kwa maandiko haya tunaziona
sheria za aina mbili zikitajwa:
1.
Sheria ya mauti na
2. Sheria ya uzima (Sheria
ya Mungu).
Wapo watu kama akina Paulo ni wale ambao moyoni
wanasikia furaha lakini mwilini hakuna furaha. Kwa kawaida, mfungwa hana uwezo
wa kuchagua chochote kile akiwa gerezani. Gereza na mkuu wa gereza ndiyo
wanaoamua mfungwa ale nini au alale saa ngapi. Silaha kubwa anayoitumia shetani
ni kuwaweka watu katika magereza. Magereza yapo
ya aina nyingi sana. Haya yaweza kuwa ni magereza ya umaskini, magereza
ya magonjwa, magereza ya njaa, magereza ya utasa n.k. Hapo ndipo shetani
anawaamulia wafungwa wake kwamba leo wale nini nini au waishi vipi na wapi.
Imeandikwa katika ISAYA 42:22....(Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na
kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa
mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.).
maandiko yansema “Wamefichwa katika “magereza”,
siyo “gereza moja”. Yapo magereza ya
magonjwa, utasa, umaskini n.k.. Endapo mtu haujawekwa kwenye gereza mojawapo,
utakuwa umewekwa katika gereza la aina nyinginne.
Mafuriko ya watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro - Bonde la Maono - Mkundi wakimwabudu Bwana Yesu Jumapili 31/7/2016 |
Magerezani ni mahali ambako watu waliofungwa
huwekwa ili kutumikia vifungo au adhabu zao kwa muda uliopangwa. Pengine ni
kuendana na kosa ulilolifanya. Hauwekwi gerezani bila kuwa na kosa. Askari wa
kiroho hutumwa na kuwatia watuhumiwa magerezani kwa muda uliopangwa.
Wapo watu wengine husema “huu ni mwaka sasa umepita bado ugonjwa wangu unaendelea”. Wengine
hufungwa magerezani kwa miezi sita, wengine miaka miwili au zaidi n.k. Wengeine
hukumu zao ni kufungwa gerezani na mwanzoni kuchapwa viboko wakati wa kuingia
na viboko vingine wakati wakutoka. Ndiyo maana wapo mtu wa aina hii akikumbuka
jinsi shida yake ilivyoanza, ni kwamba yalikuwepo matukio ya mikosi au misiba mfululizo nyakati fulani, shida zikaendelea
na mwishowe balaa au msiba mingine ikatokea tena kabla ya tatizo hilo kuisha.
Wapo wengine wamehukumiwa vifungo vya maisha.
Maana yake mtu amehukumiwa afe na shida aliyokuwa nayo. Leo hii tunaye Mungu
wetu ambaye ni Mungu wa kuokoa tutaingia
katika gereza lako na kukutoa humo kwa
Jina la Yesu.
Yesu yule yule aliyetembelea gereza la Petro na
kumtoa leo atawatoa wote walioshokiliwa magerezani kwa Jina la Yesu. Samsoni
aliwahi kuwekwa gerezani na kutumikishwa kazi ya kusaga ngano. Katika WAAMUZI 16:23-24 Imeandikwa...(Kisha wakuu wa Wafilisti
wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana
walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. 24 Na hao watu
walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi
mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni
mwetu.)... Shetani anatumia silaha ya kutoboa macho ili wewe usione
msaada hata kwa wenye kutaka kukusaidia. Wanajua Samsoni anaweza kuokota angalau
hata jiwe akawaua wengi kama kipindi kile alichotumia taya kama silaha na kuangamiza
maelfu ya adui zake.
UKIRI
Leo Ninataka macho yangu kwa Jina la Yesu.
Wewe uliyeniweka katika gereza la kutokuona fursa maishani mwangu niachie kwa
Jina la Yesu. Amen
|
Platform wa Ufufuo na Uzima - Bonde la Maono Mkundi Morogoro wakiongoza Watendakazi kwa Nyimbo za Kusifu na Kumwabudu Bwana Yesu Jumapili 31/7/2016. |
Imeandikwa katika WAAMUZI 16:25-26.... (Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema,
Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani,
akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. 26 Samsoni akamwambia
yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii
inazikalia, nipate kuzitegemea.). Ukeshawekwa gerezani unawekewa na
watu wa kukushika mikono. Leo tutazikamata nguzo zile ambazo magonjwa yako
yanazitegemea na kuwa huru kwa Jina la Yesu. Hata hivyo tutawalazimisha vijana /
watu wale wanaokushika wakuache huru kwanza kwa Jina la Yesu. Mtu yeyote aliyekuweka gerezani anazo nguzo
anazozitegemea. Pengine ni hirizi,pengine ni majini yake n.k. na ikiwa ni
waganga wa kienyeji, leo wote tutawafyeka na kuwaangamiza kwa Jina la Yesu.
Yesu alimponya yule mama siku ya Sabato, lakini
wakuu wa makuhani (Dini) walimkemea yule mama kwa sababu amepata uponyaji
siku ya Sabato. Kwamba zipo siku 6 za kupata uponyaji, na siku ya 7 ni
Sabato. Hata hivyo, siku ya kutoka katika gereza ni siku yoyote bila kujali ni
sabato au la katika Jina la Yesu.
Imeandikwa katika YOHANA 8:34...(Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila
atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.). Mtenda dhambi ni mtumwa wa
dhambi (maana nyingine ni kuwa mtenda dhambi ni mfungwa wa dhambi katika ulimwengu wa roho). Unapotenda dhambi unajiingiza
mwenyewe katika gereza mara moja, na kifungo
hiki chaweza kuwa cha maisha au cha
muda fulani.
Imeandikwa katika ZABURI 103:3-4...(Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa
yako yote, 4 Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya
fadhili na rehema,)...Ili Mungu amkomboe mtu na kaburi atamsamehe maovu yake
yote, na pili atamponya magonjwa yake yote. Shetani humfanya mtu atende dhambi
ili kifungo cha magonjwa yake kiendelee
siku zote.
Katika LUKA
4:18 Imeandikwa....(Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana
amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu
kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa.). Yesu alipoumaliza ule mfungo
wake wa siku 40, na kutangaza rasmi kazi yake, alianza kwa kusema macho ya
vipofu yafunguliwe tena ili waone. Ni kama yale yaliyotokea kwa Samsoni. Macho
yakeshatobolewa huwezi kuona fursa zozote wala hatima yako siyo rahisi kufanikiwa.
Ili utoke ndani ya gereza ni lazima upaze sauti
yako kwa Bwana.
1. Barthmayo alikuwa gereza la upofu, na aliposikia habari za Yesu kuwa anapita mahali
pale ilimbidi apaze sauti yake. Ingawa wapo watu waliokuwa katika msafara na
Yesu, ambao walimkazia macho kumkataza, lakini Barthmayo hakunyamaza. Hata
wewe, magonjwa yakija kwako usinyamaze, umaskini ukija kwako usinyamaze kimya.
2. Petro alipowekwa gerezani yeye alikaa kimya, akakubali kunyamaza.
Hata hivyo Kanisa (wapendwa) waliokuwa nje walifululiza maombi bila kuacha
kunyamaza, hadi Petro akachiwa huru. Wapo
watu wanaovunjika moyo wakeshayaona magereza yao ya HIV/AIDS na hata kusema
hapa hakuna uponyaji, au wakipatwa Kisukari, au BP, Umaskini, Ndoa kukosa amani
n.k.
3. Paulo na Sila kwa upande wao walikuwa gerezani lakini
hawakukubali kukaa kimya. Wafungwa wenzao waliwashangaa kwa nini wanaimba
mapambio ya kumsifu Mungu wakati wapo
katika taabu za gerezani. Wapo watu wanalala njaa, hawana fedha, hawana viatu,
hawana afya lakini bado wanamsifu Mungu, wanaenda makanisani wakati wengine wakiwaona
wanashangaa‼ Kilichotokea ni Paulo na Sila kuachiwa huru na wafungwa wenzao ambao
hawakuwaunga mkono katika kusifu, walibaki gerezani.
4. Shedraki, Meshaki na Abednego waliwekwa katika
gereza, na moto ukaandaliwa wakatupwa ndani ya tanuru ya moto. Wao waliendelea
kuomba na kusifu, na moto haukuwadhuru kamwe kwa Jina la Yesu. Mfalme alipokuja
alishangaa kuona kuwa ndani ya tanuru wapo watu
wanne badala ya watu watatu waliotupwa mle. Ili uweze kumstaajabisha mfalme, uskiubali
kukaa kimya.
.RP Steven na Watendakazi wa Ufufuo na Uzima - Bonde la Maono Morogoro wakiombea watu mbalimbali waliokuwa kwenye Magereza ya Kichawi Jumapili 31/7/2016. |
Imeandikwa
katika LUKA 5:17-25...(Ikawa
siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati
walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi,
na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya. 18 Na tazama, wakaja
watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na
kumweka mbele yake. 19 Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya
lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu,
wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. 20 Naye alipoiona
imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. 21 Basi, wale
waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye
maneno ya kukufuru? N'nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?
22 Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu?
23 Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka,
uende? 24 Lakini, mpate kujua ya kwamba
Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza).
Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. 25 Mara
hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani
kwake, huku akimtukuza Mungu.).. Kutoka gerezani inabidi uwe na juhudi
binafsi. Ukisema ufuate utaratibu wa kibinadamu utaendelea kubaki gerezani.
Hao
marafiki zako ndiyo waliokufanya uwe jinsi ulivyo. Kuwa makini na marafiki zako,
kwa sababu wengine mara yao ya kwanza kupelekwa kwa waganga wa kienyeji ilikuwa
kwa kupitia marafiki zao. Magereza mengine ni “mavazi ya aibu”, ambayo watu huyavaa na hayasitiri miili ya wale
wanayoyavaa. Endapo ukimuona mfungwa amevaa mavazi yake usidhani huwa anayafurahia. Mfungwa
hulazimika kuvaa hayo mavazi kwa sababu mkuu wa gereza kalazimisha avae hivyo.
Vivyo hivyo, wapo wakuu wa magereza ya
kusabisha watu kuvaa mavazi ya aibu, kwa
vijana wa kiume na kike.
Katika YEEMIA
52:33 Imeandikwa....(Naye akabadili mavazi yake ya gerezani,
akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake.). Ni
sharti ubadilishe hayo mavazi ili ijulikane
wazi kuwa wewe siyo mfungwa tena, kwa sababu ukiendelea kuyavaa bado watu
watakudhania wewe bado ni mfungwa. Imeandikwa
katika 2WAFALME 25:29...(naye
akambadilishia mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku
zote za maisha yake.). Huwezi kula chakula mbele ya Yesu hadi
ubadilishe mavazi ya magerezani. Biblia inasema sisi ni barua. Endapo unaenda
kushuhudia haushuhudii rohoni bali
mwilini.
Imeandikwa katika KUMBUKUMBU 21:13...(avue na mavazi ya uteka wake akae nyumbani
mwako, awakalie matanga babaye na mamaye mwezi mzima, kisha uingie kwake uwe
mumewe, naye awe mkeo.)... Kumbe yapo “Mavazi ya uteka”. Mavazi hutoa
tafsiri halisi, kuwa huyu mtu ni nani. Vazi la mtu laweza kumtambulisha kama
yeye ni hakimu, mchungaji, Sspika wa Bunge, askari polisi, mwanajeshi au raia.
Hata hivyo, wapo waliotupwa magerezani na
kuandikiwa kufa. Imeandikwa katika ZABURI 102:20....(Ili akusikie kuugua kwake
aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.).. Mungu aweza kuwasikia
wenye kuugua. Na wapo watu shida zao zitaishia kwenye kifo, kwa sababu tayari
wameandikiwa hivyo na mkuu wa gereza. Leo tukatae kukaa magerezani kwa Jina la
Yesu.
Imeandikwa katika ISAYA 14:17....(Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji
yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?). Familia zilizotiwa
magerezani, zinaishi maisha ya kifungwa. Magereza yameshikilia watu, na kufanya watu wakae katika
ukiwa. Wapo waliotamani wazae lakini
wamekwama. Leo tuwakamate mabwana jela wote na kuwafyeka kwa Jina la Yesu.
Katika 1PETRO
3:18-19 Imeandikwa...(Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa
ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu;
mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, 19 ambayo kwa hiyo aliwaendea
roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;). Wapo watu wanamdharau Yesu hata
pale wanapoonywa ingawa bado wapo vifungoni magerezani. Wengine wakihubiriwa
hukataa kusikia kama vile enzi za Sodoma na Gomora ilivyokuwa. Wengine husema
haya ni maneno maneno tu ya wachungaji.
Imeandikwa katika UFUNUO 2:10....(Usiogope mambo
yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili
mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami
nitakupa taji ya uzima.). Maandiko yansema
ibilisi atawatupa baadhi magerzani. Kwa kawaida, anayetupa haweki kwa
utaratibu, na maana yake ni kile kisicho na thamani kwa atupaye. Ibilisi
anatupa watu magerezani siyo kuwaweka.
Siri kubwa ya kutoka gerezani ni
kuwa mwaminifu. Jitihada zako binafsi
na wewe kuwa mwaminifu ndiko kutamfanya Mungu akutoe gerezani.
MIFANO
YA WATU WALIOWEKWA GEREZANI NA JINSI
WALIVYOTOKA.
1.
YUSUFU:
Imeandikwa katika MWANZO 41:8-14....(
8 Hata
asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na
watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna
aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.
9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema,
Nayakumbuka makosa yangu leo. 10 Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia
nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. 11 Tukaota ndoto
usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. 12 Na
huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari,
tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama
ilivyokuwa ndoto yake. 13 Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea;
mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. 14 Ndipo Farao
akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa,
akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.). Yusufu hata akiwa
gerezani hakuacha kuombea watu. Hakuacha kuwatafasiria wengine ndoto zao. Wapo
waliopo magerezani leo hii lakini hawaombei wengine, eti kwa kisingizio cha kuumwa. Wapo wengine
wamekwazwa na matukio fulani na kuacha
hata kuja kanisani kabisa.
UKIRI
Gereza lolote lililoshikilia maisha yangu achia, Nakuomba
Bwana Yesu leo unisikie tena na kunitoa niwe huru kwa Jina la Yesu. Amen
|
2.
DANIELI
Imeandikwa katika DANIELI 6:19-21...(Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa
haraka mpaka penye lile tundu la simba. 20 Naye alipolikaribia lile tundu,
akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee
Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima,
aweza kukuponya na simba hawa? 21 Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme,
uishi milele.). Kuna magereza ambayo ili utoke, unamhitaji Mungu peke
yake. Umainifu wa Danieli ulimfanya atoke gerezani. Wapo wanaosema mimi
namwangalia Mungu pekee simwangalii mwanadamu. Danieli alikuwa mwamnifu kwa
Mungu na kwa Mfalme (mtu). Endapo wewe unashiriki ufisadi, maana yake siyo
mwaminifu. Na siyo rahisi kutoka
gerezani.
NAMNA YA
KUTOKA GERZANI
(a) Njia ya Kuwa mwaminifu mbele za Mungu na watu. Hii ni njia
aliyoitumia Danieli, na hata wewe na mimi yafaa tuitumia kila wakati.
(b) Njia ya Kutoroka: Hii ni njia ya kuondoka bila kufuata
utaratibu halali. Siyo kila siku yafaa kutoroka. Ile siku ambayo walinzi
wamesinzia ndiyo yafaa kuwatoroka na kuachana nao kwa Jina la Yesu.
Kama ilivyoandikwa katika ISAYA 14:17...(Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji
yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?). Aliyetakiwa aolewe,
leo hajaolewa. Aliyetakiwa azae leo hii ni
tasa. Je, unaweza kumuaga mtu wa aina hii? Hapana. Njia sahihi ni
kumtoroka kwa Jina la Yesu.
Leo wewe ambaye hujaokoka ni sharti uokoke
kwanza kabla ya kupokea na uwezo wa kutoroka kwenye magereza uliyowekwa kwa
Jina la Yesu. Amen
© MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T)
CHURCH
==GCTC==
Tel: +255765979866 / or +255713459545
MOROGORO CHURCH
|