Monday, September 19, 2016

SOMO: KUVUNJA VITI VYA ENZI VYA SHETANI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI -:- 18 SEPTEMBA 2016.

NA: DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)


 

Dr. Godson Issa Zacharia, Askofu wa Ufufuo na Uzima - Morogoro
 

 

Nini maana ya Kiti cha Enzi? Kiti cha enzi ni makao fulani, mahali fulani,  mtu fulani. Ni makao makuu ya mtawala fulani,  awe wa hapa duniani, wa mbinguni  au kuzimu. Kiti cha enzi chaweza kuwa mbinguni nacho kikaitwa kiti cha enzi cha Mungu au  kikawa kiti cha enzi cha shetani na ambapo  ndipo akaapo.  Kiti cha enzi ni maalumu sana kwa kutolea maamuzi au kuhukumu. Hata hapa duniani, katika taifa letu  la Tanzania,  kiti chake cha enzi kipo mahali panapoitwa Ikulu, au kama ni Marekani panaitwa White House, na kama ni Uchina kinaitwa Dragon House n,k. kwenye kiti cha enzi mambo yote mazuri au mabaya huamuliwa hapo na hayupo yeyote wa kuweza kuyatengua.


 

Imeandikwa katika ISAYA 66:1…(Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?).  Tunaona jinsi ambavyo Mungu anahukumua akiwa mbinguni katika kiti chake cha enzi,na hapa duniani ndipo pa kukanyagia. Shetani kama tujuavyo yeye hajawahi kuumba chochote, ila anachokifanya ni kudurufu (copying) kwa kutumia vile ambavyo Mungu ameviumba mwenyewe. Kwa hiyo,  shetani naye akiwa hapa  duniani  ametenenza kiti chake cha enzi, na kipo hapa duniani. Tunajuaje hili?

 

Tukisoma katika LUKA 12:5-6…(Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. 6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo.). Kunayo  tofauti ya uwa mmiliki wa kitu chako na kitu hicho kuwa mikononi  mwako. Kwa hiyo shetani anavyo vitu ingawa siyo vyake, na amekuwa akivigawia watu.

 

Imeandikwa katika UFUNUO 12:7-9…..(Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; 8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. 9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.). Kwa hiyo shetani alitupwa nje, na ambapo ni  duniani.

 

Shetani alipotupwa nje,  aliondooka pamoja na theluthi ya malaika waliokuwa naye mbinguni kipindi hicho. Tunajua je haya? Tukisoma katika UFUNUO 12:4….(Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.)

 

Kule mbinguni kilikuwepo kicheko na furaha kwa jinsi ambavyo shjetani alifukuzwa mbinguni. Hata hivyo, duniani alikotupwa ni  kilio.  Imeanidkwa katika UFUNUO 12:12…(Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.). huyu ibilisi ameshuka hapa hapa duniani,  na muda wake ni mchache sana. Akiingia katika biashara, huyu ibilisi anaharibu kila kitu kupitia majini yanayotumwa kutokea katika kiti cha enzi. Akiingia katika elimu, huyu ibilis anaharibu kila kitu kupitia majini yanayotumwa kutokea katika kiti cha enzi. Akiingia katika ndoa, huyu ibilisi anaharibu kila kitu kupitia majini yanayotumwa kutokea katika kiti cha enzi. Akiingia katika biashara, huyu ibilisi anaharibu kila kitu kupitia majini yanayotumwa kutokea katika kiti cha enzi. Leo  kazi yetu ni kukifuata kiti cha enzi na kukibinua na kukivunja kwa Jina la Yesu. Ndiyo  maana hayupo hakimu  anayetoa  hukumu bila kuwa amekalia  kiti chake cha enzi. Spika wa Bunge,  vivyo  hivyo anapotoa maamuzi yake utamsikia akisema “Kiti kimeamua yafuatayo!!!!

 

UKIRI
Ewe kiti cha enzi cha kishetani nakukabili na kuanzia sasa ninakukamata na kukuvunja kwa Jina la Yesu. Ewe kiti cha enzi uliyewekwa ndani yangu, ninakubomoa kwa Jina la Yesu. Amen.
 

 

Mamia ya watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro katika ibada ya Jumapili 18/09/2016
 

Kwa kuwa  kiti cha enzi cha shetani kipo hapa duniani,  basi anakuwa anatawala afya ya watu, ndoa zao, biashara,  elimu  n.k. Leo tukivamie na kukibomoa kiti cha enzi cha Yule anayekuzuilia usisonge mbele kwa Jina la Yesu.  Imeansikwa mimi ni rungu la Bwana, na kwa mimi nitavunja vunja farasi na mapanda farasi. Simama uende kama silaha na kukivunja kiti cha enzi kilicholeta taabu katika maisha yako kwa Jina la Yesu. Leo tutaviafuata viti vya enzi vilivyomo ndani ya watu. Hawa ni wale wanaotesa maisha yaw engine,  kwa kutoa maamuzi yanaoyathiri wengine kwa Jina la Yesu. Huwezi kupata  ushindi kama hujakivunja kiti cha enzi.

 

Wapo waliouza mali zao ili kuwasomesha watoto wao, na baadhi wameweka waalimu wa ‘tuition’ ila matokeo yanapokuja unamkuta mtoto anaambulia 3% kwa mia. Tunavikusanya viti vyote vya enzi, view vimekaliwa au kama havina mkaliaji, leo tunavovunja vyote kwa Jina la Yesu. Viti vya enzi vya kishetani vimewekwa ili kutesa maisha ya watu.

 

Imeandikwa katika UFUNUO 2:13….(Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.). Hii ni kudhihirisha kuwa, hata Mungu anapajua pale  akaapo shetani, penye kiti cha enzi cha kishetani. Mungu anasema pamoja na yote,  Kanisa la Pergamo ingawa lipo katikati ya hicho kiti cha enzi cha shetani, lakini watu wameendelea kuwa waaminifu. Yaani watu wamepigwa, wameteswa, wameumizwa lakini bado wameendelea kuwa waaminifu katikati ya shida kama alizopata Antipa.  Kuna wengine mnasema, watoto wapo vizuri, wanasoma shule na haipo shida yoyuote ila kwenye ndoa ni vurugu vurugu!!! Maana yake ni kuwa, penye hizo vurugu, ndipo penye kiti cha enzi cha kishetani, mni sharti ukivunje kwanza hicho kiti cha enzi cha shetani ili uweze kuwa na ndoa yenye amani.

 

Kiti cha enzi kikiwekwa ndani ya mwili wa mwanadamu, huyo mtu huitwa mwenye nguvu. Watu wa aina hii huvuruga hata mambo ambayo tayari yaliamuliwa na vikao vilivyopita, na matokeo yake mtu huyo atataka muanze upya kufanya maamuzi mapya. Cha kufanya ni kufanya mamombi ya kushindana na  mwenye nguvu huyu,  kwa  kukivunja kiti cha enzi anachokikalia.

 

Imeandikwa katika UFUNUO 12:1-… (Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. 2 Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa). Mimba ni shara ya kuongezeka. Maana yake,  mlikuwa wawili, na sasa wanakuwepo mwingine anayeongezeka.

 
Katika UFUNUO 12:3-4 Imeandikwa…(Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. 4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake ). Huyu joka hakai karibu na mwingine bali Yule anayekaribia kuzaa.  Ni kuonesha kuwa, joka huyu anakaa karibu na mtu mwenye kutaka kuzaa kazi, mwenye kuzaa biashara, mwenye  kuzaa ndoa n.k. Huyu joka anapokuona unataka kuzaa afya njema, msingi wa nyumba, wanatokea waharibifu. Uonapo haya  yanatokea ujue ibilisi yupo kazini kwa ajili ya kuharibu. Vitu vyote vizuri ambavyo Bwana anataka uvipate, anakuja joka ambaye ni ibilisi ili kuvila.

 

Imeandikwa katika UFUNUO 12:13-15...(Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. 14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo. 15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.). Kwa mamlaka ya Jina la Yesu, yeyote ambaye ni mjamzito (wa biashara, wa familia, wa kazi n.k) hakuna atakayemezwa na majoka ya rohoni kuanzia leo. Mito ya mafuriko ya hasara tunayakomesha kwa Jina la Yesu. Kiti cha enzi kinaweza hata kumimina maji,kwa mafuriko ya kila aina (udhaifu wa afya, udhaifu wa maombi n.k.).

 

Tabia mojawapo ya mwenye nguvu wa ulimwengu huu ipo  katika kutoa ushauri. Kiti cha enzi cha kwanza ni kile cha shetani alivyompa ushauri Yesu kwamba baada ya kufunga kwa siku zile 40 basi aligeuze jiwe liwe mkate. Yesu alishajua kuwa ukiwa umefunga kwa siku nyingi  vile na ukaanza kufungua kinywa kwa kula mikate, lazima ufe. Na ndiyo maana akamjibu shetani kwamba “imeandikwa Mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo kinywani mwa Bwana!!” (LUKA 4:4)

 

UKIRI
Leo Bwana Yesu umenijaza maarifa ya kuvivunja viti vya enzi vilivyosimama mbele yangu. Bwana Yesu nipe kibali cha kuvunja viti vya enzi, yawezekana kiti cha enzi kimewekwa ndani yangu, nami nakivunja sasa kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

Shetani akiwa hapa duniani, na kiti chake cha enzi anayo makao yake katika maeneo matatu:

1.      Kiti cha enzi kwenye mikusanyiko ya maji (bahari, mito, maziwa).

2.      Kiti cha enzi katika nchi (duniani) chenye uwezo wa kuzuia mapenzi ya Mungu yasifanye kazi hapa duniani. Hawa ndiyo wanaozuia kazi ya Kanisa kusonga mbele.  UFUNUO 13:11… (Kisha nikaona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka katika nchi; naye alikuwa na pembe mbili mfano wa MwanaKondoo, akanena kama joka.)

3.      Kiti cha enzi cha Angani: Mfano wake ni kile ambacho kilizuilia maombi ya Danieli kwa siku 21. Huko angani mwenye kiti hicho huitwa mfalme wa anga.

 

Wewe ambaye hujaokoka leo unayo nafasi ya kumpokea Yesu Kristo maishani mwako ili iwe rahisi kwako kukibomoa kiti cha enzi cha shetani, chenye kuyatesa maisha yako.

 



© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +25571765979866 / +255713459545
 
 
 
Share:
Powered by Blogger.

Pages