Thursday, September 29, 2016

SOMO: NGUVU YA MSALABA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO
JUMAPILI: 25/09/ 2016

Na: PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

Askofu wa Morogoro (SNP) Dr. Godson Issa Zacharia wakati wa Ibada,
Ufufuo na Uzima Morogoro - Bonde la Maono Jumapili 25/9/2016.

Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 1 :18... (Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.).. Ukiiongelea kazi ya msalaba katikati ya watu wataona ni upuuzi na watakudharau sana lakini kwetu sisi tuliokolewa ni nguvu ya Mungu ,msalaba una nguvu sana ,nguvu hiyo ndio inayoamua kila kitu cha maisha ya mtu.

Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 2:4
(Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu)…Nguvu hiyo ndio inayofanya watu wafanikiwe,watu wasonge mbele.

 

Imeandikwa katika 1WATHESALONIKE 2:5
(Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.)


Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 4:20
(Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu).

 
Mama (RP Happiness Godson) akilisalimia Kanisa wakati wa Ibada Jumapili 25/9/2016
Ufufuo na Uzima Morogoro - Mkundi, Bonde la Maono.
 

Imeandikwa katika WAEFESO 6:10
(Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake).
Hata Yesu alipokua akifundisha wanafunzi wake siku moja walimuuliza swali je mwalimu tuombeje?

 

Imeandikwa katika MATHAYO 6:9-13
Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.
Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele.Amina.
]

Hapa tunaona Yesu akawajibu yeye mwenyewe ni ufalme na hakuna ufalme bila mfalme, nguvu za Bwana zinapoonekana ni Utukufu ,Utukufu maana yake ni udhihirisho wa ile nguvu,na nguvu ni uweza wa kutenda.Msalaba wa Yesu ndio uliobeba nguvu zote za ulimwengu,nguvu za kuokoa ,nguvu za kuponya maisha ya watu.
Kuna matukio yaliyotokea Yesu alipokua pale msalabani yanayodhihirisha nguvu ya msalaba.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 27:45-54
(Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.)

Hapa tunaona Yesu alipokua pale msalabani alitoa kelele tatu au sauti kubwa tatu ,alikua akiongea na Mungu ,Yesu akawa analalamika Eloi Eloi lama sabakithani yaani Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?Yesu alimwambia baba yake kwanini umeniacha?maana dunia imejaa mateso ,taabu na mahangaiko mengi. Alikua anauliza hivyo ili ulimwengu upate majibu ,msalabani yapo majibu, majibu ya kazi yako ,majibu ya ndoa yako ,majibu ya watoto wako, kuna mambo mengi ambayo huyajui hata sasa lakini leo Bwana anasema uendee msalaba utapokea majibu yako.

 

Msalabani ni mahali pa kuvunja vizuizi,yako mapazia ya kichawi yanayozuia maisha yako ,lakini kwa nguvu ya msalaba ipo nguvu ya kuvunja mapazia yale yanayokuzuia ukitaka kusoma unazuiliwa ,ukitaka kuanza kazi unazuiliwa,yako mapazia, kuna watu wanatengeneza mapazia kabisa ili wewe usipite lakini leo msalaba unao uwezo wa kulipasua pazia la kuzuia maendeleo yako kwa jina la Yesu.


 

Tukio lingine nchi yote ikatetemeka ,Yesu akiwa msalabani nchi yote ilitetemeka na miamba ilipasuka ,nguvu ya msalaba inao uwezo wa kutetemesha nchi na kupasua miamba ,baada ya miamba kupasuka liko tukio lingine lilitokea pale, makaburi yakafunuka na miili ya watu ikaanza kutoka ,miili mingi ya watakatifu waliolala,wakatembea wakaingia kwenye miji ya watu.

 

Tukio lingine wale akida waliokua pale wakaogopa wote ,huyu akida alikua akimlinda Yesu ,walichukua mkuki wakamchoma wakamnywesha siki lakini baadae wale akida wakagundua Yesu alikua mwana wa Mungu. Msalabani pana uwezo wa kugundua vitu ambavyo ulipaswa kufanya lakini hukufanya umechelewa. Matukio yakaendelea kutokea pale msalabani ,utaona hata walipompeleka kaburini wakaweka na walinzi wakaamua kumlinda sana .

 
Umati wa Watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiwa ibadani Jumapili 25/9/2016

Imeandikwa katika LUKA 23 :44-46
(Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,
jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. 6 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu
.)


 

Imeandikwa katika YOHANA 19:30
(Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.)


Tunaona Yesu alipoipokea ile siki akasema kwa sauti kuu imekwishaaa…hii nayo ilikua ni sauti kuu, msalaba ukatoa sauti kuu sauti kuu ina uweza,Yesu aliposema imekwisha sio kwamba alikua ameuwawa hapana ,sauti kuu hii ya msalabani ina uwezo wa kushinda mauti ,ina uwezo wa kushinda sauti zote za wanadamu,sauti za waganga wa kienyeji,sauti za wasoma nyota ,sauti za waajiri,sauti za ndugu.Kwenye msalaba kuna sauti ambayo inanyamazisha sauti zingine


 

Yesu alipokua msalabani akapaza sauti moja tu miamba ikapasuka,na dunia ikatikisika,sauti ya msalaba ni kelele ya utakatifu na haiwezi kuvumilika ,na sauti hii ya Bwana Yesu ikisikika wachawi wote wanatawanyika kwa jina la Yesu. Ukiutazama msalaba ujue kuna majibu ,kuna jibu ambalo ulikua hulijui mjomba halijui,ndugu hawajui lakini leo uangalie msalaba, unapotafuta majibu kimbilia msalaba wa Yesu.
Unaweza kujiuliza maswali mengi mbona siolewi,mbona nikianza kazi inaharibika, mbona nikifungua mradi unakufa ? wewe utafute msalaba ulipo ,uangalie msalaba majibu yako yanapatikana msalabani ,kuna watu wanapokuona leo umekosa kazi wanafurahi wanasema amekwisha lakini ghafla wanashangaa umepata kazi tena umeongezwa mshahara wao wanafikiri wamekumaliza kumbe wamekupandisha ngazi.
Msalaba unao uwezo wa kurudisha vyote ,msalaba unafanya yale yote yaliyokua yamekufa kwenye maisha yako yarejee tena ,msalaba unanyamazisha taabu zote, magonjwa yote,utaona jua lilinyamazishwa kwa masaa matatu. Namba tatu ina maana kubwa sana kibiblia utaona hata Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki kwa siku tatu,utaona hata mbinguni kuna utatu mtakatifu,utaona Yesu alifufuka siku ya tatu. Kwahiyo utaona jua lilikaa kimya kwa masaa matatu mbele ya msalaba ili taabu iliyokutesa inyamaze kimya, magonjwa yakae kimya,kwenye msalaba kuna ukamilifu, utaona msalaba unainamisha ,leo inamisha kila waliokutesa kwenye maisha yako yako kwa jina la Yesu.

Showers of Glory wakiimba na kumwimbia Bwana Jumapili 25/9/2016.

 

Msalabani kuna nguvu ya kuongeza kama umepata pesa fungua biashara ,kama umepata kazi na ulikua huna mke sasa uoe.


UKIRI:
Kwa jina la Yesu nawakamata wachawi wote mlionitesa,mliofunga maisha yangu nawainamisha kwa jina la Yesu nawakanyaga wote kwa jina la Yesu,Imeandikwa utamkanyaga simba na mwana simba …. leo nakanyaga wachawi wote kwa jina la Yesu, kwa nguvu ya msalaba nakanyaga kila nguvu ya nyoka kwa nguvu ya msalaba nawakabili wasoma nyota waliofunga maisha yangu nawakanyaga wote kwa damu ya mwanakondoo,mipango ya giza nakanyaga,leo naivaa miguu ya chuma ya Bwana Yesu nakanyaga laana,nakanyaga magonjwa,nakanyaga utasa,roho za mauti nazikanyaga nakataa leo sitakufa kwa jina la Yesu…….. Amen.

 

© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima Mkundi - Morogoro)
Tel: +25571765979866 / +255713459545
 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages