Monday, October 24, 2016

SOMO: AKILI ILIYOLOGWA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI -:- 23 OKTOBA 2016.

NA: DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP - MOROGORO)

Umati wa Waumini na Watendakazi wa Ufufuo na Uzima  Morogoro wakifuatilia Neno la Mungu, wakati  wa ibada ya Jumapili 23/10/2016 iliyoongozwa na Dr. Goson Issa Zacharia (SNP - Morogoro)
 


Mchawi anaweza kuloga miguu yako na hatimaye ukashindwa kutembea. Mchawi pia anaweza kuloga chochote cha maendeleo yako na ukashindwa kupiga hatua yoyote ya   kimaendelea. Wachawi pia huweza kuloga mikono yako na ukashindwa kufanya kazi.

 

Imeandikwa katika WAGALATIA 3: 1.. (Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?). Paulo anawauliza Wagalatia hili swali, kuonesha kuwa akili ya mtu yaweza kulogwa. Akili ikilogwa,  mtu anakuwa hayupo vizuri. Iweje, watu waliomuona Yesu Kristo amesulubiwa msalabani,  lakini bado wanajivuta kwenda kanisani? Iweje watu walioshuhudia Yesu akifufuka leo hii wanasubiria kupigiwa simu ili waje kanisani? Lazima kwa watu kama hawa utakuta wamelogwa akili zao.

 

UKIRI
Bwana Yesu, ninamfuatilia mtu yeypte aliyeloga akili yangu, aniachie kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

Mungu alipomuumba mwanadamu, alimwekea vipande vitatu:

1.      Roho – ni ile pumzi aliyomwekea mwanadamua baada ya kumpulizia puani

2.      Mwili – huu ni kama jumba tu la kuihifadhi roho ya mwanadamu

3.      Nafsi – ni muunganiko wa roho na mwili. Hata hivyo, nafsi nayo ina vitengo/idara tatu,  ambazo ni:

·        Idara ya hisia

·        Idara ya utashi

·        Idara ya nia  - ni katika idara hii ambapo akili  hutunzwa. Wazungu husema kwamba “Mind is the department of thought”.

Katika idara ya nia ndipo ambapo mtu hunuia kufanya mambo kadhaa kadhaa. Mfano: mtu anaponuia kufanya biashara, huanzia katika idara hii ya nia. Mungu alipomuumba mwanadamu alimweka na akili. Sasa endapo akili ya mtu ikitoka, mtu anakuwa ahana lolote.

 

Wachawi huiloga nafsi katika idara hii ya nia.  Unaweza ukawa hujalogwa kabisa miguu yako, au tumbo lako, au sehemu nyingine ya mwili. Hata hivyo wachawai wakiiloga akili  yako utashindwa kufikia hatima ya maisha yako.

 

Biblia inasema kuwa,,”Enyi wanaume kaeni na wake zenu kwa akili”. Maana yake ni kuwa, Mungu alishaweka akili katika nafsi  zetu ili wanaume waweze kuishi na wake zao. Inaonesha kuwa ipo akili maalumu ya mtu  kuishi na mke wake. Na endapo akili ya aina hii imelogwa, ujue mtu wa aina hiyon hawezi kuimudu familia  yake.

 

Katika KUTOKA 35:30-31 Imeandikwa (Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; 31 naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; 32 na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba, 33 na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina. 34 Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. 35 Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.) Hili hema lilitengenezwa kwa AKILI siyo elimu ya watu kusomea uinjinia chuo kikuu.

 

Imeandikwa katika ISAYA 40:28…(Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.) Mungu ambaye ni roho pia ana akili zisizoweza kuchunguzika.

 

UKIRI
Na mimi niwe na akili sawasawa na Mungu aliyeniumba, kwa Jina la Yesu.  Amen
 

 

Tukisoma katika 1YOHANA 5:20 Imeandikwa..(Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele). Akili tuliyopewa ni ay  kumjua Yesu Kristo kuwa ni kweli. Kwa sababu ya ukweli ule, mtu utakuwa huru kwa sababu imeandikwa “Mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru

 

Imeandikwa katika  2 TIMOTHEO 2:7…( Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote). Walokole wengi sku hizi wanafunga na kuomba wakiwa milimani hata kwa siku 10 lakini wanapotoka huko,  kwa kukosa maarifa, wanaishia kuanguka. Kwa nini? Baadhi hujikuta wakati wa maombi ya aina hii huona maono, na baadae huwakubalia watu wasiookoka kwa mambo kama vile ya mwenzi wa ndoa ingawa wanafahamu kuwa watu hao hawajawahi kuokoka au hata kumwamini Yesu maishani mwao.

 

Katika 2KORINTHO 11:19 Imeandikwa  …(Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha.). Mungu ametupatia akili ya kuweza kiushi kwa amani na watu wajinga wajinga wasio  na akili. Si vyema kugombana na watu wa aina hii,

 

Imeandikwa katika 1PETRO 3:7….(Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.). Hauhitaji  upako wa kuishi  na mwanamke wako wa ndoa. Upako unaohitaji ni ile akili aliyokupa Bwana. Wachawi wanaffahamu kuwa ukiwa na akili utafanikiwa sana na kama utakuwa umelogwa akili,  hutaweza kutambua kipi ufanye!!.

 

Tukisoma katika WAEFESO 4:17-20 Imeandikwa…(Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; 18 ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; 19 ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.).. Akili ikilogwa inakuwa imetiwa giza. Maana yake unakuwa na akili sawa, laikini akili hiyo inakuwa na uzito.

 

Imeandikwa katika LUKA 10:27….(Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.).

 
Platform wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiongoza nyimbo za Kusifu na Kumwabudu Bwana Yesu Jumapili 23/10/2016

UKIRI
Kwa Jina la Yesu, enyi Wagalatia msiokuwa na akili, ni nani aliyewaloga? Akili yangu iliyofungwa mahali popote, iachwe kwa Jina la Yesu. Ewe akili yangu iliyoshikiliwa niachie, ewe ufahamu ulioshikiliwa iachiwe. Aliyeloga akili yangu nisije kanisani, ewe mchawi na ewe mganga leo kwa Jina la Yesu ninakupiga. Ninawaponda wanaologa akili, ninawasambaratisha kwa Jina la Yesu. Amen
 



 
© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +25571765979866 / +255713459545
Share:
Powered by Blogger.

Pages