Wednesday, November 9, 2016

KUVUKA BAHARI YA SHAMU


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI -:- 06 NOVEMBA 2016.

 

MHUBIRI:          MCHUNGAJI KATSU (TOKA JAPAN).

& DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP - MOROGORO).

 
Mch. Katsu (Kushoto) akihubiri kwa Kijapani na kutafsiriwa na Mrs. Yuka Mwakyusa (Kulia)
 
Imeandikwa katika KUTOKA 14:1-10… (Bwana akasema na Musa, akamwambia, 2 Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari. 3 Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke. 4 Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi wakafanya hivyo. 5 Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? 6 Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; 7 tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. 8 Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. 9 Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. 10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana).

 

Wana wa Israeli walipokuwa wakienda Kanaani, walikutana na vikwazo vya aina  mbalimbali. Upande wa nyuma lilikuwepo jeshi la Misri, na mbele yao ilikuwepo Bahari ya Shamu. Walijiuliza maswali mengi  sana kwa nini  haya yote yatupate?  Kwa nini Mungu ameruhusu haya yote yatokee?

 

Hata katika maisha yetu ya kawaida,  twaweza kukutana na vikwazo vya aina nyingi. Yamkini yapo matatizo ya magonjwa, uchumi n.k. yamekupata. Ingawa tunamwamini  Mungu lakini matatizo bado yanaendelea kuwepo. Uonapo hayo ujue kuwa MUNGU anataka kukufanya uishi kwa kumwamini yeye peke yake. Wakati mwingine Mungu anayaruhusu majaribu yatokee ili tuweze kumwamini yeye peke yake. Mungu anatufundisha pia jinsi ya kupigana. Haikuwa bahati mbaya kwa wana wa Israeli waiendee ile Bahari ya  Shamu. Ndyiyo maana ilikuwepo Nguzo ya moto na nguzo ya wingu iliwaongoza wana wa Israeli hata kuifikia Bahari ya Shamu, kuonesha kuwa Mungu alikusudia jambo hilo kutokea.

 
Timu ya Wageni Kutoka Japani katika picha ya pamoja na SNP-Morogoro (Dr. Godson Issa Zacharia)
 

Je, unahisi wewe pia umeachwa na Mungu? Kwa kupitia wana wa Israeli, Mungu anataka tujifunze jinsi anavyotupenda na umuhimmu wa sisi kumtegemea yeye peke yake. Wakati mwingine mtu unaweza kupatwa na ugonjwa mkubwa, na akajiuliza kwa nini nipate ugonjwa kama huu wakati:

Ø  Kila mara naenda kanisani

Ø  Kila mara nafanya maombi

Ø  Kila mara nampenda Mungu.

 

Mbaya zaidi watu wengi wakipatwa na mambo kama hayo humlalamikia sana Mungu, na hata kumlaani Mungu. Inabidi ukumbuke kuwa huo ni  mtego wa shetani,  na anataka umkosee Mungu. Pale mtu akeshamwacha Mungu, shetani hufurahia sana kwa sababu mtu huyo huwa rasmi ni mali ya shetani. Petro alizama hata baada ya  kupiga hatua chache za kutembea juu ya  maji. Pengine Petro alijiona kama Yesu aliyekuwa anamwita siyo Bwana, au pengine alikuwa anaota ndoto tu au ni maono tu!! Kitendo cha Petro cha kusitasita, hata wakati Bwana alivyomwambia atembee juu ya maji, ndicho kilimfanya aanze kuzama.

 

Wakati mwingine majaribu/ au matatizo yakitokea huwa njia nzuri ya mtu kuomba, kwa sababu bila uwepo wa majaribu / au matatizo watu huwa hawamuombi  Mungu. Musa alipokumbana na yale majaribu, kwa nyuma akiliona jeshi la Misri na Bahari ya Shamu mbele yake, hakumlalamikia Mungu wala kulaani. Badala yake alimuita Bwana, na Bwana akamjibu kuwa aiinue fimbo yake mkononi mwake na kuipiga Bahari ili kuiamuru igawanyike. Musa alipofanya hivyo upepo mkali ulivuma, na Bahari ya Shamu ikagawanyika. Kuanzia pale, wana wa Israeli walipita pakavu katikati ya Bahari ya Shamu. Ndiyo maana Jina lingine la Mungu ni “MUUJIZA / MAAJABU”, kwa sababu ni Mungu afanyaye vitu ambavyo kwa akili  zetu hatukutegemea.

 
Umati wa Watendakazi wakisikiliza kwa makini mahubiri ya Mch. Katsu (Ufufuo na Uzima Japan) 6/11/2016

Endapo katikati yetu  yupo mtu mwenye ugonjwa wa aina yoyote ataenda kupata uponyaji wake siku ya  leo kwa Jina la Yesu. Mtu binafsi unapaswa kuchukua hatua ya imani kwa Mungu. Siyo imani ya mchungaji wako wala mtu mwingine yeyote. Wewe pekee ndiye unayepaswa kumwamini Mungu na kupokea uponyaji wako katika Jina la Yesu. Kumbuyka kuwa hatima yako itachaguliwa na wewe binafsi.

 

Mungu husikia maombi pale tumuombapo. Kwa kulitumia Jina la Yesu, unaweza kuamuru  kitu chochocte nacho kikatimia. Kwa Mfano,  kule Japan katika Mji wa Kagoshima ninapokaa kwa miaka zaidi ya 20  sasa nimekuwa nikiomba na typhoon (kimbunga) kinapotokea huwa nakiamuru kipite juu ya mji huu mita 150 juu bila  kuleta madhara na hutokea. Ni muda sasa wa kuamuru mashetani yote yaondoke katikati yetu kwa Jina la Yesu. Amen.



© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +255765979866 / +255713459545








 
Share:
Powered by Blogger.

Pages