GLORY OF
CHRIST TANZANIA CHURCH,
KANISA LA UFUFUO
NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI -:-
09 OKTOBA 2016.
NA: RP
HAPPINESS GODSON (MOROGORO)
&
DR. GODSON
ISSA ZACHARIA (SNP - MOROGORO)
Baba (Dr. Godson Issa Zacharia) akiwa anamkaribisha Mama (RP Happiness Godson) ili kuhubiri Jumapili 9/10/2016 Ufufuo na Uzima Morogoro, Bonde la Maono Mkunndi |
SOMO:
WIVU WA BWANA UMENILA (UNANITAFUNA)
Bwana Yesu alikuwa hana
mchezo kabisa kwa habari ya kazi aliyotumwa na Baba yake. MATHAYO 21:12-14…(Yesu
akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua
hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza
njiwa; 13 akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali
ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. 14 Na vipofu na viwete wakamwendea
mle hekaluni, akawaponya.) Kumbe kuna kipindi katika nyumba ya Mungu
miujiza ilikuwa haiendelei, na watu walikuwa hawaponywi kwa sababu ya mauza
uza yaliyookuwemo humo. Kumbe hekalu likibadilika, miujiza inatokea. Yaani
kuna mtu anakuja kanisani lakini anaendelea na utaratibu wake wa maisha. Yesu
anataka leo aje kwa hasira ile ile ili awatimue tena na miujiza ianze
kudhihirika tena katika Jina la Yesu.
YOHANA 2:13-17…. ( Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa
karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. 14 Akaona pale hekaluni watu
waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.
15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na
ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; 16 akawaambia
wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu
kuwa nyumba ya biashara. 17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu
wa nyumba yako utanila.) Katika Biblia ya kiingereza, imeandikwa “wivu
wa nyumba yako utanitafuna”. Wakati huu Yesu alikuta hekaluni biashara
zikiendelea, na hasira au wivu wa nyumba ya Mungu ukaanza kumtafuna kwa ndani.
Alishangazwa kuona nyumba ya Mungu imegeuzwa matumizi yake. Yesu alitamani sana aone vikundi vya watu wakiwa wamekaa
wakiisoma Biblia na wengine wakifundishana neno la Mungu lakini ikawa kinyume
chake. Leo Yesu ataingia ndani ya hekalu tena kufumua fumua kila mpangaji
haramu aliyeingia humo katika Jina la Yesu. Kwa habari ya Mungu wake, Yesu
hakutaka mchezo. Yesu alikuwa na moto wa
Mungu ndani yake, akitamani kuiona kazi
ya Mungu ikienda mbele lakini wakawepo hawa waliokuwa wakimrudisha nyuma.
Platform wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiongoza nyimbo za sifa na kumwabudu Bwana Jumapili 9/10/2016 |
Tukisoma kitabu cha MWANZO
1:1-14 tunaiona Asili ya Mungu kuwa ilikuwa
ya kutenganisha vitu. Hata leo hii,
kanisani panapaswa kuwa mahali ambapo tofauti ionekane kati ya wale wa Mungu na wale wasiomtii Mungu. Mungu hakuwa akitaka kuchanganya mambo. Katika
mstari wan nne, Imeandikwa kuwa “Mungu alitenga nuru na giza”. Tunaona
kuwa Asili ya Mungu ni kutenga vitu.
Akisema ndiyo yake ni ndiyo, na hapana yake ni hapana.
Hata kwa wachungaji hawako salama. Makanisani leo hii, utamkuta
mchungaji mmoja anamsema vibaya mchungaji mwenzake wa kanisa lingine, wakati
Biblia inasema upendo huvumilia. Makanisani waumini wanataka mahubiri ya mafanikio, kupokea magari, kupokea pesa
n.k na habari ya kukemea dhambi haipo.
Watu mliokooka mnapaswa mtengwe, na siyo kujichanganya na mambo ya dunia hii. Wapo watu waliookoka na zikiwepo sherehe
za kipepo kama vile AROBAINI bado wanashiriki mambo haya ambayo hayafai kwa mtu
uliyeokoka. Wanafunzi vyuoni au sekondari wanakuwa na staili zao za maisha, na
wewe uliyeokoka hupaswi kuiga mitindo yao ya maisha kama uvaaji wa nguo au
sherehe za madisko wanazokuwa nazo. Mungu hapendi moto wako wa wokovu kupoozwa
na barafu za dunia hii. Mbona kipindi cha zamani ulikuwa unaomba na kufunga, na
sasa unashindwa?
Imeandikwa katika UFUNUO
3:14-17…(Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi
aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. 15 Nayajua matendo
yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au
moto. 16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika
utoke katika kinywa changu. 17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha,
wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka,
na maskini, na kipofu, na uchi 18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu
iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya
uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. 19
Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu..).
Watu wamefikia mahali na kuzoea mambo ya
kanisa na maana yake ni VUGUVUGU.
Kuna kipindi ulikuwa unaomba mpaka unajua hakika anga limekoma, lakini kwa sasa
ukiomba unajiona kama unajiongelesha. Kama Mungu aliwahi kututapika kwa sababu
ya vuguvugu, basi leo tunamuomba aturudishe tena kwa Jina la Yesu. Ili uanze
kuona uhalisia wa wokovu, Yesu anasema atakupaka dawa macho yako. Ifike wakati
umwambie Yesu kuwa “nakupenda jinsi ulivyo na siyo
kwa sababu ulinibairiki kwa vitu
kadhaa kadhaa maishani”. Siyo kwamba tunampenda Yesu ili atupatie yale
mahitaji yetu, la hasha!!!
Yesu alipokuwa anaenda Jerusalem aliulilia ule mji. Shetani
kuna wakati anagonga hodi kwenye milango ya watu. Kitakachokuponya wewe ni neno la Mungu ambalo utakuwa umeliweka akiba
moyoni mwako. Wakati ukiwa na afya nzuri ndiyo wa kumtumikia Mungu zaidi,
kwenda kanisani usipoteze muda kabla haujaja ule muda wa kujiliwa kwako. Laiti
ungejua elimu uliyo nayo leo hii ni kwa ajili utukufu wa Mungu!! Laiti ungejua
yakupasayo kutenda sasa hivi!! Yamkini unajiona una kila kitu na mavazi yako,
lakini Yesu akikuona anakuona mtupu. Upendo wako kwa Yesu ndiyo ukulete kanisani,
siyo kwa sababu wachungaji wako wamekupigia simu au kukutembelea.
Wapo watu waliokwazika kwa sababu waliugua na kutotembelewa na
wachungaji wao, na hatimaye wakatamani kurudi Katoliki!!! Hilo siyo jibu kwa
sababu kinachokufanya uje kanisani siyo mchungaji bali ni Yesu.!!! Kama
mahitaji yako yote unadhani yatatimizwa na mchungaji wako, basi ujue humhitaji
Mungu tena bali mchungaji wako ndiyo 'mungu' wako!! Wapo watu wanaokuja kanisani
ili wapate wachumba, lakini swali la kujiuliza ni usipompata mchumba itakuwa
je?
Tukisoma katika EZEKIELI
33:31-32 Imeandikwa…(Nao
huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia
maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo
mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. 32 Na tazama, wewe umekuwa kwao
kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda
vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi.). Mungu
anashangaa kuliona kanisa watu wanaenda lakini wakitoka na Biblia zao,
wanapitia bar na kunywa pombe. Mchungaji akihubiri watu wa aina hii huona kama
wimbo tu!!. Imefika mahali watu wamelizoea neno la Mungu mno. Endapo sisi
tuliookoka tutajichanganya, ni nani atakayeenda kuwahubiria wale wa mataifa
mengine wasioamini?
MATHAYO 5:3-6… (3 Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. 4 Heri wenye
huzuni; Maana hao watafarijika. 5 Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana
hao watashibishwa. 7 Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.)
Maskini wa roho ni wale watu wanaojiona bado wanyonge wanapomkaribia Mungu
zaidi.
Kwa habari ya wokovu,
kila mmoja anapaswa awe ana mahusiano binafsi na Mungu. Siku ya kwenda
mbinguni kila mmoja ataenda kivyake. Endapo unakwazwa na washirika kwa sababu
tu hawajakutembelea ulipokuwa unaumwa, uje bado hujawa imara katika waokovu wako.
Katika UFUNUO 3:1-2-3 Imeandikwa…(Na
kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika;
Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota
saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. 2 Uwe
mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona
matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. 3 Basi kumbuka jinsi
ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha,
nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako.). Yesu anasema anayajua hata matendo yetu. Kumbuka
ule upendo wa kwanza uliokuwa nao ulipookoka, ukatubu!!
Tukisoma katika UFUNUO
2:2-5 Imeandikwa…(Nayajua matendo yako, na taabu yako, na
subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu
wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; 3 tena ulikuwa na subira
na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. 4 Lakini nina neno juu
yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. 5 Basi, kumbuka ni wapi
ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo,
naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.).
YESU anafahamu ulipookoka hali haikuwa hii. Yesu anataka kila siku tunakuwa
kama watoto wachanga, ambao ni rahisi kupokea neno la Mungu. Wapo watoto wa
rohoni ambao wakati wa kuwafundisha hawalipokei neno, na pale ukimsomea neno
yeye atakupa mstari unaofuata!!
Ifike mahali kazi ya Mungu katika maaisha yako ifufuliwe tena
kwa Jina la Yesu. Ifike mahali tusione
aibu kuwaombea watu wagonjwa kwa sababu annayeponya siyo sisi bali ni Bwana
Yesu. Iweje walokole wawili hawelewani na kanisani wote wanakuja? Au mlokole
mmoja kumsema mwenzake vibaya hata
kumkwaza mwenzake? Linda sana moyo wako kuliko vyote uvilindavyo kwa maana humo
ndimo zitokapo chemchemi ya uzima.
Imeandikwa katika ISAYA
52: 1-2…(Amka, amka, jivike nguvu zako, Ee Sayuni; Jivike mavazi yako mazuri, Ee Yerusalemu, mji
mtakatifu; Kwa maana tokea sasa hataingia ndani yako Asiyetahiriwa, wala aliye najisi. 2
Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya
shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa.). Binti Sayuni ni Kanisa. Mungu anasema amkeni. Vile vitu
vilivyokurudisha wewe nyuma achana navyo, anza kukung’uta mavumbi!!! Wapo
wanoogopa kumtumikia Mungu eti kwa sababu ya mambo yao mabaya ya zamani,
historia ya kuwachukua wanaume za watu!! Historia ndiyo hiyo lakkini Mungu
anasema ukeshatubu dhambi zako unakuwa kiumbe kipya. Cha kufanya ni kendelea
kumtumikia Mungu kwa kuzikung’uta vumbi zako.
Umati wa Watendakazi na watu wengine waliohudhuria ibada, wakimsikiliza Mama Happiness Godson (RP), Ufufuo na Uzima Morogoro, Bonde la Maono Mkundi, wakati wa ibada Jumapili 9/10/2016 |
Yesu anataka tuwe na moyo wa kumtumikia yeye. Hakuna cha
kuututenga na upendo wa Kristo kama alivyosema Paulo. Yamkini dhiki, au
magonjwa, au familia lakini leo tuanze upya tena na kuachana na maisha ya
uvuguvugu!
Endapo wewe hujaokoka, kwa maana ya kumpokea Yesu maishani mwako,leo ni nafasi
yako kufanya hivyo.
© Media and
Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +25571765979866 / +255713459545
|
================== AMEN ======================