Wednesday, November 30, 2016

SOMO: ROHO YA USINGIZI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

JUMAPILI -:- 27 NOVEMBA 2016.

MHUBIRI: STEVEN NAMPUNJU (RP - MOROGORO) &

Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP - MOROGORO)

"Na Mataifa yote Watahubiriwa Injili kabla ya ule mwisho kuwapo"!! Pichani ni baadhi ya watu waliompa Yesu Kristo
Maisha yao kwa Kuokoka katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima Mkundi - Morogoro, hapo Jumapili 27/11/2016.


 
Kimsingi Roho ndiyo iletayo uhai maishani mwetu. Imeandikwa katika YOHANA 6:63… (Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.). Kumbe roho ndiyo itiayo uzima ndani mwetu. Roho ikiingia ndani ya maisha ya mtu inawezesha atembee, afanye kazi, afanye mambo yote, na endapo roho ya usingizi ikiingia ndani ya mtu itamfanya ashindwe kufanya hayo yote. Roho ya usingizi ina nguvu ya kumlaza mtu asiweze kufanya jambo lolote. Kwa kawaida mtua wapo usingizini hawezi kufanya maamuzi yoyote, na ili aweze kufanya kazi lazima kwanza aitwe.  Usingizi ni "nusu ya kifo". Imeandikwa katika LUKA 8:52…(Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu.). Hata sasa Yesu anasema usilie kwa sababu matumaini yako yaliyopotea jibu lake lipo kwa Yesu pekee anayeweza kukuamsha tena ili utoke usingizini kwa Jina la Yesu.

 
Mhubiri wa ibada ya Jumapili, 27/11/2016 - RP Steven Nampunju akifundisha kuhusu
ROHO YA USINGIZI
 

Kila penye usingizi, nyuma yake kuna malengo. Madaktari hutoa dawa za usingizi kwa wagonjwa wao ili  waweze kumtibu na mgonjwa akeshaamka kutoka usingizini anajikuta tayari kidonda cha operation ile kipo. Ni kweli ulilazwa lakini Yesu amekuja kuyaponya majeraha yako ili  uendelee na shughuli zako. Adui zako wanafanya hivyo  hivyo, kwamba wanawalaza watu usingizini kwanza ili waweze kufanya uharibifu wao. Yu wapi aliyetoka katika upasuaji na kuanza kubeba zege? Hawezi kwa sababu ya mshono uliopo. Adui ili wapate baadhi ya vitu kutoka kwako hukulaza usingizini kwanza. Baada ya kuamka kutoka usingizini huwezi kufanya baadhi ya shughuli ulizokuwa unazifanya kipindi cha nyuma.

Baba na Mama Dr. Godson Issa Zacharia katika ibada ya Jumapili 27/11/2016.

 

JE, KATIKA BIBLIA WAPO WATU WALIOWAHI KULAZWA USINGIZINI?

Ipo mifano mingi ya Kibiblia ya watu waliowahi kulazwa usingizini. Mifano hiyo ni kama ifuatavyo:

1.     Adamu

Imeandikwa katika MWANZO 2:18-23…(Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. 19 Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. 20 Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. 21 Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, 22 na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. 23 Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.). Mungu alikuwa na malengo ya kumtengeneza msaidizi wa Adamu, na ndipo akamlaza Adamu usingizini. Hilo ndilo lilikuwa lengo la Mungu la kumlaza Adamu usingizini. Tunajifunza kuwa, USINGIZI unaweza kutumwa kutoka sehemu  moja  kwenda nyingine. Kama Mungu anaweza kuuleta usingizi kwa mtu, maana yake ni kwamba hata adui yetu shetani anaweza kufanya hivyo hivyo. Cha kufanya ni kumruhusu Mungu leo akulaze usingizini ili baadae utakapoamka uifanye kazi yake katika Jina la Yesu. Wapo watu ambao ukiwaambia waokoke hawataki na hujitetea kuwa wanazo dini zao nzuri. Ni kweli, lakini hata hivyo watu wa aina hii mambo yao yakeshaumana huko ulimwenguni walipo hujikuta wanarudi kwa spidi kubwa wakiomba msaada ili waokoke.

 
Umati wa Watendakazi wakisikiliza kwa makini somo la ROHO YZ USINGIZI katika ibada ya Jumapili 27/11/2016.
 

2.     Sauli

Imeandikwa katika 1SAMWELI 26:7-12…(Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. 8 Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. 9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa Bwana, naye akawa hana hatia?10 Daudi akasema, Aishivyo Bwana, Bwana atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. 11 Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa Bwana; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. 12 Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia.). Tunajifunza kwamba 'Usingizi waweza kumwangukia mtu'. Kama upo usingizi kutoka kwa Bwana unaoweza kumwangukia mtu, basi ujue kuwa hata adui zetu (mashetani) wanaweza kufanya hivyo  hivyo. Ukilazwa usingizi, unaweza kunyang’anywa fumo lako (Vitu ulivyopaswa kuvitumia ili kujikinga). Wale wote waliochukua vitu vyetu tutawalaza usingizini, nakuchukua fumo zetu walizo nazo kwa Jina la Yesu. Leo usingizi ukija, hata wale waliokuwa majemedari watalazwa  tu katika Jina la Yesu. Kwa mtu  aliyelazwa, pigo lake ni mara moja tu, kama  alivyosema Abishai.

 

Wachawi wanachokifanya ni kuwalaza usingizini watu wote na kuyatesa maisha yao. Wanachokifanya ni kuituma roho la usingizi kwa waombaji kuwafanya wasiombe tena na matokeo yake kazi ya Bwana inakuwa haifanyiki tena.

 

UKIRI
Leo nakataa kwa Jina la Yesu. Nayaamsha maisha yangu kutoka kwenye mikono ya Iblisi anayelaza watu usingizini kwa Jina la Yesu. Amen

 

3.     Sisera

Huyu alikuwa shujaa na amiri jeshi wa jeshi lake,  ni shujaa aliyekuwa anashinda vita siku zote. Hata hivyo kupitia usingizi aliweza kuangushwa.

 

WAAMUZI 4:1-3….(Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana. 2 Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake. 3 Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini.). Sisela alikuwa na magari ya chuma (Kwa sasa ni  kama Vifaru) mia tisa, na aliwaonea wana wa Israeli kwa miaka 20 nao wakaendelea kumlilia Bwana ili awasikie. Je, kilio chako kimedumu miaka mingapi? Yamkini unacho kilio cha miezi michache tu na umeanza kukata tamaa ya kumlilia Bwana. Hupaswi kufa moyo kwa sababu yupo Mungu mwenye uwezo. Daudi aliwahi kumwambia Goliath kuwa "unanijia kwa silaha kali lakini mimi ninakujia kwa Jina la Bwana wa Majeshi Mungu wa Israeli ambaye unayatukana majeshi yake".

 

Katika WAAMUZI 4:17-21 imeandikwa….( Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni. 18 Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti. 19 Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika. 20 Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana. 21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.). Kumbe usingizi unaweza kumshika mtu na kumlaza. Aliyelazwa usingizi haendewi haraka, anaendewa polepole. Shujaa aliyekuwa akiogopwa sana ameuawa na mwanamke kwa kutumia kigingi cha hema. Leo hii utakitoa kigingi cha hema (ambacho kwetu ni Kitabu cha Maombi ya Kushindana / Kitabu cha Damu ya Yesu, n.k.) na kumwendea polepole adui yako na hakika utamuua kwa Jina la Yesu. Usimuogope yeyotoe ambaye ni shujaa. Wachawi wamegundua kuwa usingizi ndiyo  silaha kwao ya kuwalaza watu. Wapo watu ambao zamani walikuwa washuhudiaji  wazuri sana lakini kwa sasa hiyo huduma hawaifanyi tena, kwa sababu wamelazwa usingizini. Waliolazwa rohoni tayari na wapo tayari kufundisha washirika wapya kwa sababu hawapo macho tena.

 

UKIRI
Kuanzia leo  maisha yangu lazima yaamke kwa Damu ya Yesu. Ninaamuru kila roho zilizotumwa kuyalaza maisha yangu, nawapiga wachawi walionilaza usingizini,  ninawashinda wote kwa Jina la Yesu. Amen

 

 

4.     Samsoni

Imeadikwa katika WAAMUZI 16:15-20 …(Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. 16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. 17 Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. 19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. 20 Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha.). Mwanamke huyu Delila alitumia silaha ya usingizi na kuweza kumshinda Samsoni. Nywele za Samsoni zilizomtoka baadae alijikuta hana nguvu  tena. Samsoni hakujua kuwa baada ya kulazwa usingizi, vipo vitu vilimtoka pale pale. Mwanzoni ulikuwa unafunga mara kwa mara, lakini leo hii umebaki na hoja kuwa unaogopa kupata vidonda vya tumbo. Ulikuwa muombaji mzuri lakini leo hii maombi hakuna tena.

 

Shetani anapouleta usingizi maishani mwako anakuwa na malengo yake. Shetani akileta usingizi, huondoa vile vitu ambavyo ni "vihatarishi" kwake vilivyopo maishani mwa mtu (Kuondoa hamu ya kuomba, kuondoa hamu ya kumtumikia Mungu n.k.). Kile kilichomo ndani mwako ndicho kinachowafanya wachawi  wakuwinde kwa sababu ndicho kinachowapa shida siku zote.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 13:24-30….(Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; 25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. 27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? 28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? 29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. 30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.). Vyanzo vya mapando mbalimbali maishani mwa watu hutokea baada ya kulala  usingizini. Mapando haya yaweza kuwa magonjwa, mafarakano, kuchanganyikiwa, hasara, ajali, n.k. Hayupo adui anayeweza kupanda mapando haya wakati mtu yupo macho. Ndiyo maana tunasema usingizi ni sawa na nusu kifo. Kwa hiyo adui anaweza kufanya jambo lolote pale anapokuwa amemlaza mtu usigizini kwa sababu aliye usingizini hawezi kufanya maamuzi. Leo ni siku ya kuwaamsha wote waliolazwa usingizini kwa Damu ya Yesu.

 

UKIRI
Ninawakabili walioniletea roho ya usingizi kwenye maisha yangu. Ewe roho wa usingizi uliyekaa katika maisha toka kwa Damu ya Yesu. Leo nazikataa roho za usingizi zilizotumwa kutokea baharini, na kutokea angani, ninazishinda zote kwa Jina la Yesu. Amen

 

ROHO A USNIGIZI NI KITU GANI?

Kimsingi haya ni mashetani yanayotumwa na adui na kuufunika kabisa ufahamu wa mtu ili kumfanya mtu huyo awaze maisha ya kukata tamaa, na kumfanya mtu wa aina hii asifanye maamuzi sahihi katika maisha yake. Roho hizi huweza kumfanya mtu asikubali kuoa/kuolewa, asikubali uponyaji, asikubali kuokoka, akatae kuzaa watoto n.k. Wewe kimsingi siyo mtu wa kawaida,  ila kinachokusumbua leo hii ni ule usingizi uliowekewa na adui zako.

 

Wapo walazaji wanaolaza maisha yako ili uendelee kuwa mtu wa kawaida. Leo tutaenda kudai kutoka kwa Mungu wetu ili watu wajitambue kwa Jina la Yesu. Hata hivyo inabidi mtu kutambua kuwa ili Mungu akuisaidie ni sharti umpokee Yesu Kristo maishani mwako kwa kuokoka. Leo tutawaamsha wote waliolazwa usingizini, ili wakiamka waanze kumtumikia Mungu tena kwa Jina la Yesu.

 

© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +25571765979866 / +255713459545


 

SWAHILI















ENGLISH


 
Share:
Powered by Blogger.

Pages