GLORY OF CHRIST CHURCH TANZANIA
UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI: 22
JANUARI 2017
MHUBIRI: ADRIANO MAKAZI (RP)
Baba (SNP) Dr. Godson Issa Zacharia katika Maombi mwanzoni mwa Ibada Jumapili 22/1/2017 |
Neno asili maana yake ni mwanzo, ni jadi ya kitu tokea kilipoanza. Jinsi ulivyo sivyo ulipaswa kuwa!!.Mungu leo anataka
urudi kwenye asili yako. Leo Kataa jinsi ulivyo na ukubali kurudi kwenye asili yako kwa Jina la Yesu. Katika 1SAMWELI 1:1-20
Biblia inasema hivi (Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa
nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu,
mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu 2 naye alikuwa na wake
wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye
huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. 3 Na mtu huyo
alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea
Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na
Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. 4 Hata siku ile ilipofika Elkana
alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume
kwa wake, sehemu zao; 5 lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda
Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 6 Ila mwenzake humchokoza sana,
hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 7 Tena mumewe
akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani
kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile
chakula. 8 Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula?
Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? 9
Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani,
alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana.
10 Naye huyo mwanamke
alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. 11 Akaweka
nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi
wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi
wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha
yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. 12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba
mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. 13 Basi Hana alikuwa akinena
moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa
hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. 14 Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa
mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. 15 Hana akajibu, akasema, Hasha!
Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala
kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. 16 Usimdhanie mjakazi wako
kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na
kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. 17 Ndipo Eli akajibu, akasema,
Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. 18 Naye
akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda
zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. 19 Wakaondoka
asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani
kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. 20 Ikawa,
wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina
lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.).
Hana anaonekana
akimwekea Bwana Nadhiri hata kabla ya kwenda nyumbani kwa Bwana. Mara nyingi sana akina mama
wanapochelewa kuzaa, hupenda kuongea maneno mengi sana ya kukata tamaa kwa
habari ya mtoto wanayemsubiria. Hana kwa upande wake alitumia maneno ya Biblia
katika kuweka nadhiri hii, na maneno
haya yanapatikana katika HESABU 6:1-5…(Kisha
Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu
mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke
wakfu kwa Bwana; 3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala
siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi
wala zilizokauka. 4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa
mzabibu, tangu kokwa hata maganda. 5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga,
wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo
alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani
mwake zikue ziwe ndefu..). Kwa hiyo maana ya nadhiri ni KUTENGWA KWA MAKUSUDI MAALUMU; ni mtu aliyewekwa wakfu kwa ajili ya
Bwana, na huyo mtu anaitwa Mtakatifu wa Bwana.
RP Adriano Makazi akifundisha kuhusu Somo "Narudi kwenye Asili Yangu" Jumapili 22/1/2017 Katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Mkundi - Morogoro |
Katika WAAMUZI 13:2-5 imeandikwa ..(Palikuwa
na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe
alikuwa tasa, hakuzaa watoto. 3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke,
akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe
utamzaa mtoto mwanamume. 4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala
kileo, wala usile kitu kilicho najisi; 5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe
utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo
atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na
mikono ya Wafilisti.). Maandiko yanasema “Mtoto huyu atakuwa mnadhiri
wa Mungu tangu tumboni”. Kwa hiyo asili
ya mtoto huyu ni kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Unaweza kuwa unafanya
biashara kwa ugumu lakini kumbe ugumu huo siyo asili yako kwa Jina la Yesu. Hata leo wapo watu
wanaofanya kazi ambazo siyo za asili yao.
UKIRI
Katika Jina la Yesu, Ninaomba
Bwana leo ile minyororo niliyofungwa ikabadilisha asili yangu, leo naivunja na kurudi kwenye asili yangu kwa Jina la Yesu. Amen
|
Katika MWANZO 25:21-25 imeandikwa….(Isaka
akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia,
na Rebeka mkewe akachukua mimba. 22 Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni
hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana. 23 Bwana akamwambia,
Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu
tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa
atamtumikia mdogo.). Tunakumbuka kuwa tatizo hili la utasa halikuanzia kwa Isaka. Ni tatizo
lililoanzia kwa Ibrahimu na mkewe Sara, kitendo kilichomfanya Ibrahimu kuzaa na mjakazi wake. Utaona tatizo hili
liliendelea kujirudia hata kwa Yakobo, ambapo mkewe Raheli hakuwa na watoto.
Raheli hata hivyo alimwambia mumewe Yakobo ampe watoto la sivyo atakufa!!! Leo
hii tatizo la utasa likitokea lawama zote hupelekwa kwa mwanamke, lakini kumbe
mwenye kutoa hao watoto ni mume kwa
mujibu wa Raheli.
Mwanadamu
kwa asili yake hana shukrani. Raheli pamoja na kuwa alikuwa hana watoto, lakini
alipokuwa mjamzito akaanza kulalamikia ile mimba. Hata hivyo, Raheli alipata
akili na kumuuliza Bwana!!. Unapopata matatizo hata kwenye ndoa yako, usilalamike tu bali nenda
kamuulize Bwana. Usijaribu kutatua tatizo lako kwa kuongeza tatizo lingine juju
yake bali nenda kamuulize Bwana. Hatimaye Jibu la Mungu kwa Raheli ni kuwa
mataifa mawili yapo tumboni mwake. Unapoiona misukusuko, ujue yapo mataifa
mawili ndani yako. Maana yake ni kwamba,
kuna kitu cha Mungu ndani mwako
lakini kinazuiliwa na mashetani.
Mungu
anaiona asili yako tangia tumboni. Mungu anaweza kuona kama una nguvu au huna
nguvu tangia ukiwa tumboni. Vipo vitu kama vitano ambavyo asili yake inaonekana tangia tumboni kwa maaandiko
tuliyosoma hapo juu:-
1.
Mungu
analiona taifa tangia tumboni mwa mama. Wewe kibinadamu unaiona ni mimba
tu, lakini Mungu anaona taifa tangia
tumboni. Taifa litakuwa hodari au la, linaoneka tangia tumboni.
2.
Mungu
analiona kabila tangia tumboni mwa mama
3.
Mafarakano
tangia tumboni mwa mama.
4.
Uhodari
huonekana tangia tumboni mwa mama. Mtoto huonekana kuwa hajawahi kushindwa na
adui zake tangia tumboni mwa mama.
5.
Mkubwa
atatawaliwa tangu tumboni. Kumbe unaweza kumzaa mtoto tayari alishatawaliwa akiwa tumboni.
Tatizo kumbe
huweza kuanzia tangia tumboni. ZABURI 22:10… (10 Kwako nalitupwa tangu tumboni,
Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.). na ZABURI 58:3…( 3 Wasio haki wamejitenga tangu
kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.). Asili inaonekana
tangu tumboni.
ZABURI
71:6…(Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama
yangu, Ninakusifu Wewe daima.).
ISAYA
46:3….(Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya
Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani;).
Yaani mtu unatembea lakini mimba yako ilishanunuliwa. Kwamba inawezekana mtu
ulinunuliwa ukiwa tumboni, na hivyo kufanyika kuwa mali ya wachawi au waganga wa kienyeji.
Ndiyo maana
tumesoma katika 1SAMWELI kuwa Hana hata kabla ya kuchukua mimba alishweka wakfu
mwanae kuwa mndahiri wa Mungu. Inawezekana hata wewe bila kujua mama yako
alipokuchukua mimba aliwekeana nadhiri na waganga wa kienyeji na sasa maisha
yako yamekuwa ya ugumu kwa sababu hizo. Samweli kwa mara tatu aliisikia sauti
ya Mungu ikimwita ingawa hakujua ni Bwana, akawa anamwendea Eli. Kitendo hiki
kinatufundisha kuwa, kama huyu mnadhiri wa Mungu anaisikia sauti ya Jmungu,
maana yake hata waliowekwa wakfu kwa wachawi wanakuwa na miunganiko na sauti za
kishetani (mizimu).
Katika jamii
zetu za Kiafrika, zipo mila na tamaduni
mbalimbali zinazofanya watu kuingia katika maagano ya kishetani. Mathalani,
kama umeokoka, ni vyema kujitenga na ibada za arobaini kwa sababu kupitia hizo,
mashetani hupata upenyo wa kukufuatilia maisha yako.
Mambo
mengi huanzi tumboni. Zipo baraka
zinaaznia tangia tumboni. Kuna utajiri unaanzia tangia tumboni. Kuna kushindwa
kunakoanzia tangia tumboni. Yususu
alizaliwa na asili yake ya kuwa waziri mkuu tangia tumboni, pamoja na
misukusuko yote aliyopitia.
Ufufuo na Uzima Tunafahamu Mungu kwetu ni Roho. Na tunapomwabudu Mungu, Tunamwabudu katika Roho na Kweli |
UKIRI
Asili
yangu ni kushinda wala siyo kushindwa. Asili yangu ni utajiri. Asili yangu
siyo umaskini. Ninaharibu kila mashetani yanayosimamia matatizo yangu kuanzia tumboni kwa Jina la Yesu. Ninarudi
kwenye asili yangu kwa Jina la Yesu. Amen
|
Asili ya mtu
huanzia tumboni. Kwa mfano: Mtume Paulo hapo awali alilitesa Kanisa ingawa
haikuwa asili yake. Kabla ya kuwa mtume alikuwa akifanya uovu mwingi sana akiitwa
Sauli. Ni Paulo huyuhuyu aliyesema “vita vyetu
si juu ya damu na nyama”, ingawa yeye alifanya mauaji ya
Wakristo. MATENDO 9:1-9…( Lakini Sauli, akizidi kutisha na
kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, 2 akataka ampe barua za kuenda
Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa
wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. 3 Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula
ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia,
Sauli, Sauli, mbona waniudhi? 5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi
ndimi Yesu unayeniudhi wewe. 6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo
kutenda. 7 Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti,
wasione mtu. 8 Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu;
wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. 9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala
hanywi.). Hakuna
mbabe aliye juu ya Yesu. Paulo pamoja na ukali wake lakini kwa Yesu ilibidi auache
ukali wake na kumgeukia Mungu na kuwa
kiumbe kipya. Yamkini mumeo au mkeo unamuona kama aliyeshindikana lakini ukimleta
kwa Mfalme Yesu atatulia na kugeuka kuwa
kiumbe kipya. Usikate tamaa kwa mwanao ambaye hataki kuisikiliza sauti yako, wewe
umkabidhi kwa Bwana naye atamgeuza kwa Jina la Yesu. Yamkini wapo watu
unaosafiri nao tangia umeokoka, lakini leo watasimama kimya wakiisikia sauti
wasimuone mtu. Leo tunaamuru magonjwa yanafuatana nawe yasimame kimya na
kuisikiliza sauti ya Mfalme Yesu kwa Jina la Yesu.
Tumeona kuwa
asili ya Paulo haikuwa ya uuaji. Ndiyo maana Bwana akaanza kumtengeneza. Imeandikwa
katika MATENDO 8:3…(Sauli
akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na
kuwatupa gerezani.). Sauli ni mharibifu, ndani yake likiwemo pepo
Mharabu (Napelioni). Hata leo hii wapo watu waharibifu kwa namna hiyo. Mashetani yanaweza kuingia ndani ya mtu na
kufanya mambo sivyo. Kuna watu wapo kwenye ndoa leo hii wanaishi maisha mabaya
tofauti na ndoa zao zilivyoanza hapo awali. Maana yake ni kuwa yameingia mapepo
ya kuharibu asili ya ndoa, lakini Yesu
aliyebadilisha wengine anaweza kuawabadilisha hata wanadnoa wa aina hii kwa
Jina la Yesu.
Imeandikwa katika LUKA
22:3-5…(Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale
Thenashara. 4 Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari,
jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. 5 Wakafurahi, wakapatana naye kumpa
fedha.). Kumbuka kuwa asili ya Yuda alikuwa ni Mtume, tena aliyekuwa
anatumwa na Bwana hata kwenye huduma za mapepo. Kumbe mashetani wanaweza
kumuingia mtu na kufunika asili yake na mtu
huyo kuwa tofauti. Yuda kuanzia hapa alipoingiwa na mashetani alianza kumuona
Yesu kama mtu wa kawaida tu, na wala siyo kumuona kama Mungu tena.
Katika WAGALATI 1:15 imeandikwa hivi…(Lakini
Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,
16 alipoona vema kumdhihirisha
Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri
na watu wenye mwili na damu;). Maswali ya kujiuliza ni haya: Imekuwa je Paulo huyu huyu
akawa muuaji hapo awali? Kumbe tangia tumboni mwa mama yake Paulo alitengwa kwa
kazi ya Bwana? Kwa hiyo Asili ya Paulo ilikuwa
ni kuhubiri Injili, lakini uuaji
uliletwa na mapepo maishani mwake.
Maandiko ni Muhimu Yafuatiliwe Ukiwa Ufufuo na Uzima Morogoro, ili Kuijua Kweli nayo Kweli ituweke Huru Kweli Kweli. |
Mungu ni Mungu
wa makusudi. Tunamuona mtu mmoja aitwae Rahabu, ambaye alikuwa kahaba lakini
Yesu alipitia katika ukoo wake huyu. Hii haikuwa asili ya Rahabu kuwa kahaba.
Ina maana kuwa unapomuona mtu leo hii akiwa na maisha ya ajabu ajabu fahamu
kuwa hiyo siyo asili yake mtu huyo.
Wachawi wana
uwezo wa kumuona mtu tangia akiwa tumboni mwa mama yake. Wanaweza kufunika
asili ake au kuiiba asili hiyo. Wanao uwezo kwa kuiona hatima ya mtu na
kuiharibu. Yamkini hata wewe kuna mambo unayopitia lakini hiyo siyo asili yako. Umewekewa asili ya magonjwa
lakini siyo asili yako. Mtu anaweza kuwa mgonjwa tangia tumboni. Mtoto
anapozaliwa, hutenganishwa na mama yake kwa kukikata kitovu. Wachawi wanaweza
kukifunga kitovu cha mtoto waliyemjuona tangia tumboni ili hatima yake
isitimie.
Kwenye
Biblia, kuna mtoto ambaye mbingu ilijua asili yake kuwa “ni shujaa” lakini yeye
mwenyewe hakugundua hilo. WAAMUZI 6:11-14
imeandikwa…( Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra,
uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta
ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea,
akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana
wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi
matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana,
aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono
ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe
Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?). Gideoni haoni ushujaa ambao mbingu
zinauona. Wakati Gideoni amekata tamaa na kuchoka, ndipo malaika wa Bwana alimtokea. Hata leo kuna
watu ukiwatia moyo kuwa Bwana yupo nawe, huweza kukataa kukubaliana nawe
kwani watu wa aina hii huangalia ugumu
wa maisha wanayopitia na ndipo huhoji: “kama
Bwana yupo nami kwa nini niendelee kuishi maisha ya aina hii?!!!” Saa ya
Bwana ikifika, Bwana atakupigania kwa Jina la Yesu. Malaika wa Bwana alimwambia
Gideoni kuwa anayezuilia maisha yake asionekane kuwa shujaa ni ile madhabahu
ya baba yake mzazi.
Shetani
anaweza kumzuia mtu asirudi kwenye asili yajke. Katika 1THESALONIKE 2:18 imeandikwa hivi (Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu,
naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia).
Kumbe shetani anapoona upo mbioni kuondoka kwenye asili yako anaweza kukuzuia.
Cha kufanya leo ni kumkubali Yesu
maishani mwako kwa maana ya kuokoka ili ukiwa upande wa Yesu ufanyike kiumbe
kipya na kurudi kirahisi kwenye asili yako kwa Jina la Yesu.
======== Fuatana nasi kwenye FACEBOOK kwa Kubonyeza Link Hapa Chini ==========
Somo: NARUDI KWENYE ASILI YANGU
© Media and Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
|