GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
[UFUFUO NA UZIMA MOROGORO]
JUMAPILI: 29 JANUARI 2017
MHUBIRI: PASTOR HAPPINESS GODSON (RP)
Pastor Happiness Godson (Mama) akihubiri Somo la Kuomba kwa Bidii, Jumapili 29/1/2017 Nyuma yake (Kulia) ni Baba (SNP) Dr. Godson Issa Zacharia Ufufuo na Uzima Morogoro. |
Maana ya kuomba kwa bidii ni ile hali ya kung’ang’ana, na
kuomba kwa ufanisi (effective prayer). Neno “Bidii” ni ile shauku ya kufanikisha
jambo fulani. Inawezekana kuomba imekuwa desturi yetu, kwenye ibada na mikesha
mbalimbali ya kila siku. Kuomba kwetu huku kumekuwa kwa mazoea na kwa kawaida
sana. Mungu leo anataka kusema na mioyo
yetu, huku tukiwa siyo tu wasikiaji wa
neno bali watendaji wa neno hilo pia. Imeandikwa katika YAKOBO 5:16…(Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana,
akiomba kwa bidii.). Kuomba kwa bidii ni aina ya kuomba kwa shauku na
hisia. Mathalani Mfanyabiashara hufanya biashara yake kwa ufanisi ili
wapatikane wateja wengi zaidi. Mwalimu yeyote ni rahisi kumuona mwanafunzi wake
mwenye bidii, kwa jinsi anavyokuwa anajisomea, anavyouliza maswali na kutafuta
elimu kwa njia mbalimbali.
Mungu naye anataka kuiona bidii hiyo hiyo maishani mwetu. Ndiyo maana imeandikwa katika MITAHALI 8: 17… (Nawapenda
wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona). Yawezekana
unampenda Mungu naye anakupenda lakini ili umuone Mungu kinachokosekana katika
upendo wako na Mungu ni BIDII. Hata
katika biashara yako, usipoweka bidii ya kazi biashara hiyo yaweza kufa. Sisi
tuliompokea Yesu, twajua kuwa Mungu anatupenda sana, na ndiyo maana alimtoa
mwanae Yesu Kristo aje na afe msalabani kwa ajili yetu.
Imeandikwa katika WAEBRANIA
5:7…(Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na
kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi,
akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;). Bwana Yesu aliiiona
mauti mbele yake, akamtolea “Yule awezaye kumuokoa na umaskini”, akamtolea “Yule
awezaye kumuokoa na utasa”, akamtolea “Yule awezaye kumuokoa na magonjwa”, “Maombi
na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha
Mungu”. Yesu alipoiona ile shida aliyokuwa anaiptia hakumwendea mtu mwingine
yeyote, bali alimtolea “Yule awezaye
kumuokoa tena kwa kulia na machozi”!! Kumbe
kuna mauti inakuja kama ilivyoandikwa kaatika YEREMIA 9:21 (Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu,
imeingia majumbani mwetu….). Mauti imepanda dirishani. Kwamba wakati wa
uhai wake Yesu, aliomba kwa bidii na machozi yakatoka. Leo hii sisi tumekuwa wa kawaida kawaida tu.
Leo tumuombe Bwana Yesu atuhurumie, kwa sababu pamoja na ubinadamu tulio nao,
tumeendelea kuomba kwa kawaida kawaida tu. Yesu aliomba hata akasikilizwa ni kwa
sababu alitia bidii.
Katika MATHAYO
26:36-44 imeandikwa…(Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani
iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule
nikaombe. 37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika
na kusononeka. 38 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha
kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. 39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka
kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke;
walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. 40 Akawajia wale
wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja
nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i
radhi, lakini mwili ni dhaifu. 42 Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema,
Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako
yatimizwe. 43 Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.
44 Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.).
Hapa tuanona maisha ya maombi ya Bwana Yesu, baada ya kuiona mauti yake ile
aliyokuwa anaijua tokea akiwa mbinguni. Yesu alipoiona hii mauti yenye uchungu
na adhabu kubwa, alifikia wakati wa kutaka kuomba angalau hii mauti
ibatilishwe. Kitendo cha Yesu kuanguka kifudifudi ni ishara ya bidii katika
maombi yake. Kama jaribu la Yesu aliliona kama “kikombe”, basi lile jaribu
ulilo nalo wewe ni sawa na kulilinganisha na “kijiko cha chai” tu kwa sababu
hujawa na jaribu la kuchapwa mijeledi 40 kasoro moja, au kuangikwa msalabani!!!
Yesu alipoomba mara ya kwanza, aliona utulivu. Kumbe kuna
wakati Mungu ananyamaza tumuombapo!!. Hata mara ya pili, Yesu alipoenda kuomba
kwa umbali wa kurusha jiwe, bado ukimya uliendelea kuwepo. Yesu hakukata tamaa
baada ya kuona ukimya wa mara zote mbili. Yesu aliendelea kuomba hata mara ya
tatu bila kuacha, tena kwa bidii. Bwana
Yesu aliomba maneno yale yale, mara zote tatu huku akisema kwamba siyo kwa
mapenzi yake, bali kwa mapenzi ya Mungu. Leo hii wangapi wetu ambao hupenda kuomba
tu kidogo na kupendelea kuona Mungu
ameshawajibu.
Imeandikwa katika LUKA
22:44….(Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake
ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]). Swali tunaloweza
kujjiuliza ni hili, “Hivi kwa nini Yesu alipokuwa katika dhiki alizidi kuomba?”
Maana yake, kwamba kwa kadiri alivyokuwa katika dhiki, kwa kadiri alivyokuwa
katika mateso, kwa kadiri alivyokuwa katika umaskini n.k. ndivyo alivyozidi sana
kulia. Yamkini wewe pia kuna dhiki unayo, lakini pamoja na dhiki hiyo kuwepo
bado hujaomba hata matone ya damu kudondoka mwilini mwako, na umeanza kukata
tamaa. Yesu alipokuwa katika dhiki hakurudi nyuma. Unapaswa kutia bidii katika
Maombi. Lakini Sivyo ilivyo sasa. Ni kwamba wapo watu wengi leo hii ambao dhiki
yao ikizidi wanakuwa tayari kurudi Misri, kurudia yale maisha ya zamani ya
dhambi. Mume tu akikutaza kwenda kanisani upo tayari kuacha. Ukumbuke kuwa Mume
wako au mke wako hana mbingu ya
kukupatia mwisho wa maisha ya hapa duniani ukiwadia.
Pichani ni baadhi ya mamia waliohudhuria ibada ya Jumapili 29/1/2017 Ufufuo na Uzima Morogoro wakifuatilia Maandiko. |
Kuomba kwa bidii ni kuomba ambapo hauna nafasi ya kujua
anachokifanya jirani yako. YESU kwa vile
alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya
damu yakidondoka nchini. Mungu
anataka katika kuomba kwako, siku akikukomboa ujue hakika ni Mungu. Wakati
mwingine umeomba kwa habari ya kupata kazi, lakini kumbuka kwamba Mungu
angekupatia hiyo kazi baada ya kumuomba kwa mwezi mmoja tu pengine
usingeendelea na imani yako kwake. Mungu amekuacha ili uzidi kujua ukuu wake na
namna ya kuomba kwa bidii. Bidii ya mambo ya Mungu itakufaa sana kwa mazoezi ya
mambo ya rohoni.
Imeandikwa katika 1WAFALME
18: 41-46.. (Naye Eliya akamwambia Ahabu,
Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. 42 Basi Ahabu akainuka
ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu
kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. 43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea
sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu.
Naye akanena, Enenda tena mara saba. 44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama,
wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda,
umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. 45 Ikawa, muda si muda, mbingu
zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda
garini, akaenda zake Yezreeli. 46 Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya;
akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.).
Hebu waza kidogo, Eliya ndiye aliyefunga mvua isinyeshe, Lakini Eliya huyu huyu
ndiye anaomba mvua inyeshe, huku akiinama
uso wake mpaka magotini.
Pengine hata wewe mtumishi wa Mungu amekutabiria muujiza wako
maishani mwako, na baada ya hapo wewe umetulia kuusubiria muujiza utokee bila
hata kuomba. Eliya alienda mlimani kuomba. Hata wewe unapopewa utabiri wa
habari za muujiza wako, nenda mlimani ukaombe, tena kwa bidii kama alivyofanya
Eliya. Kumbe kuomba kwa bidii kunasababisha mambo yasiyowezekana kuja katika
maisha yako. Kwa kawaida wengi wa watu wasiopenda kuomba ndiyo hao hupendelea
kutabiriwa.
Mwanandamu ana vipande viwili, kimoja cha rohoni na kingine
cha mwilini. Unaruhusiwa kuwa mwilini lakini siyo kwa asilimia nyingi. Ukiweza
kuweka Maisha ya mwilini (20%) na ya rohoni (80%), utajikuta kuwa mambo yako
yakifanikiwa. Eliya alimpa Ahabu taarifa ya mvua kunyesha ingawa dalili za
mvua yenyewe hazikuwepo. Kuna mtu
akiambiwa baraka yake ya kuolewa ipo lakini bado atataka kuona dalili za
kutokea kwa baraka hiyo. Cha kufanya ni kuendelea kung’ang’ana kwa maombi.
Eliya alimtuma mtumishi wake kwenda kuangalia upande wa bahari hata mara zote
saba. Twaweza kujiuliza hivi kwa nini Eliya aliyeifunga hii mvua asingeomba kwa
kawaida tu na mvua hiyo ikanyesha?!
Pia Katika 1SAMWELI1: 9-18 Imeandikwa.. (Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli,
kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana. 10 Naye
huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. 11
Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la
mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi
mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za
maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. 12 Ikawa, hapo alipodumu
kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. 13 Basi Hana alikuwa
akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake
isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. 14 Ndipo Eli akamwambia,
Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. 15 Hana akajibu,
akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi
sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. 16
Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi
wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. 17 Ndipo
Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako
uliyomwomba. 18 Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi
huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana
tena.). Hana angeweza kuomba maombi ya kushindana na kumkemea
shetani kwa namna zote zile, lakini
isingemsaidia kwa sababu Biblia inasema aliyemfunga tumbo ni Mungu mweyewe, siyo shetani. Penina pamoja
na kuwa ni mke mwenza wa Hana, lakini ndiye aliuchochea ule uchungu wa Hana wa
kutokuwa na mtoto. Kumbe basi adui mkubwa wa mwanamke ni mwanamke mwenzake.
Penina ni mfano wa mtu anayeamua siku yako iwe nzuri au isiwe nzuri. Kuna watu
wanakuwa na Penina wengi katika maisha yao. Pengine Penina wako ni mumeo, au
mkeo, au boss wako kazini. Kwa upande wake Hana aliamuacha Penina na kuondoka kwenda
Shilo, penye Nyumba ya Mungu ambapo watu waliochoka wanaenda na kumuomba Mungu.
Akiwa hekaluni mle, Hana aliomba kwa bidii, midomo yake ikawa inacheza kiasi
kwamba hata mchungaji wake (Eli) akawa hamuelewielewi.
Kuna wakati umefika unapitia maisha ya kuitwa kila ‘jina baya’.
Watu walianza kukuita tasa kwa sasa wanakuita mgumba. Hali kama hii ilipofika
kwa Hana, alijitambua na kukimbilia Nyumbani kwa Bwana. Kumbe kuna wakati wa
kuamua kutoka na kujitenga na mazingira yanayokuzunguka ili uweze kuomba kwa
bidii. Uonapo watu wanasema mbona umeokoka lakini haijakusaidia, huo ndiyo
wakati wako wa kukimbilia zaidi kwa Bwana na kuumimina moyo wako kwa Bwana.
Biblia inasema “Ondokeni katia yao mkatengwe nao”. Kumbe kuna wakati wa kutoka
kati yao, ukijua kuwa majibu yako yapo kwa Bwana peke yake. Kuna wakati
unapaswa kuacha kitanda chako na kumuacha hata mume wako amelala ukimbilie
kanisani ili kuumimina moyo wako kwa Bwana. Ni hatua ya kuhama kutoka kwenye
maombi ya kushangaa shangaa, bila kuangalia mwingine anasema nini!!.
Pastor Happiness Godson (Mama) akiombea baadhi ya Watu wenye mahitaji mbalimbali Jumapili 29/1/2017 |
Kuomba kwa Bidii ni maombi ya mtu aliyeteswa na Penina. Ni
maombi ya kujikana. Ni maombi ya mtu ambaye akiitwa TASA ni KWELI NI TASA,
hajasingiziwa, ndivyo alivyo!!. Biblia
haijasema kuwa Eli alimshawishi Hana kwa kumpigia simu ili Hana aje hekaluni
kuombewa. Ukiona mtu anakumbushwa aje kanisani kuombewa kwa habari ya shida
yake, ujue huyo siye. Wenye mapito
hukimbilia Shilo wenyewe bila hata kukumbushwa.
Usidhani kwamba ukifunga na kuomba ukiwa kanisani jibu
litakuja papo hapo. Danieli aliomba kwa siku 21 lakini jibu la maombi yake
likazuiliwa na Mfalme wa Uajemi muda wote huo. Ukiomba kwa bidii hata kama
Mungu hajakujibu kwa dalili yoyote ile, lakini ndani mwako unakuwa na hakika
kuwa kile unachokiomba kimekwishakuwa. Kuomba kwa Bidii ni maombi ambayo shida
yake inajieleza yenyewe. Maombi ya kuomba kwa bidii ni maombi yasiyosubiri
kuwepo kwa semina au mikutano ya Injili.
Hali yako inakuwa inajieleza yenyewe. Ukija na kuyamimina maneno yako
mbele za Mungu, kwa kuwa maneno ni roho, kile ulichomwambia Mungu ni hakika
utakipokea kwa Jina la Yesu. Mtunga Zaburi akasema “Nitayainua macho yangu niitazame milima, msaada wangu utatoka wapi?”.
Nami nayaona maombi haya ya hisia yakizaa kitu kipya maishani mwako kwa Jina la
Yesu. Kuna wakati mwingine utaletewa mgonjwa kumuombea. Siyo maombi ya kuomba
kwa dakika mbili tu na kumaliza. Kuna nyakati
nyingine utatakiwa kumrudisha mtu aliyekufa, siyo maombi ya kuomba kwa muda
mfupi hayo.
Hata hivyo huwezi
Kuomba kwa Bidii endapo mtu hujampokea Yesu maishani mwako. Wewe ambaye
hujaokoka, leo hii ni nafasi yako kufanya hivyo kwa kukubali kuokoka na
kuwa kiumbe kipya ndani ya Yesu Kristo.
© Media and Information Ministry
GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +255719612874 / +255713459545
|