GLORY OF
CHRIST TANZANIA CHURCH,
KANISA LA UFUFUO
NA UZIMA MOROGORO
JUMAMOSI -:- 31
DESEMBA 2016.
MHUBIRI: HAPPINESS GODSON ISSA ZACHARIA
(RP -
MOROGORO)
Salamu za Mwaka Mpya zikitolewa na Mama (Happiness Godson Zacharia), RP - Morogoro usiku wa 31/12/2016. |
Katika KUMBUKUMBU
11:10-12 imeandikwa …(Kwa kuwa nchi mwingiayo kuimiliki, si mfano
wa nchi ya Misri mlikotoka, uliyokuwa ukipanda mbegu zako humo na
kuinywesheleza kwa mguu wako, kama shamba la mboga; 11 lakini nchi mwivukiayo
kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua ya
mbinguni; 12 nayo ni nchi itunzwayo na Bwana, Mungu wako; macho ya Bwana Mungu
wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka.)
Mwaka wa 2017 ni mwaka tunaouanza huku tukiamini
“MACHO YA MUNGU YAKO JUU YETU”. Imeandikwa
katika ZABURI 1:1…(Heri
mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki;Wala hakusimama katika njia ya
wakosaji; Wala hakuketi barazani pa
wenye mizaha. 2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,Na sheria yake
huitafakari mchana na usiku. 3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya
vijito vya maji,Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake
halinyauki;Na kila alitendalo litafanikiwa.). Na hizi ndizo salamu za mwaka mpya 2017,
zilizogawanyika katika maakundi matatu:-
1. SALAMU ZA KWANZA ZA MWAKA MPYA NI KWA
KANISA LOTE
Kila mmoja
wetu atambue kuwa kama jicho la Mungu litakuwa juu yako, hakikisha kuwa kila
siku unatembea katika Neno la Mungu, na
kwamba Neno la Mungu lisitoke moyoni mwako. Maana ya Kuokoka ni kutengwa na
hivyo hakikisha kuwa kwa mwaka mzima wa 2017 unajiepusha na kwenda katika
shauri la wasio haki, yaani wanapokuwepo watu waovu wewe huungani nao katika kuutenda
uovu huo; Biblia inasema pia
kuwa mtu huyo mwenye heri “Wala
hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala
hakuketi barazani pa wenye mizaha”. Kama kanisa hatupaswi kushindana na shetani
kwa njia za kimwili kwa sababu vita vyetu si juu ya damu na nyama. Wewe haupaswi
kumjibu shetani kwa wigi ulizovaa, wala nguo uliyoivaa, wala chochote kile bali
kitu utakachokifanya kwa mwaka 2017 ni kulitumia “Neno la Mungu”. Mwaka wa 2017 ni mwaka wa kumwambia shetani “Imeandikwa”.
2. SALAMU ZA PILI ZA MWAKA MPYA NI KWA
VIJANA WOTE
Tunaposoma katika 1TIMOTHEO 4:11-13, maneno ya Mungu
yanasema hivi:… (Mambo
hayo uyaagize na kuyafundisha. 12 Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali
uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na
imani na usafi. 13 Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na
kufundisha.). Mtume Paulo anakuasa wewe kama kijana kuwa mtu ye yote
asiudharau ujana wako. Umri wa kijana ni hadi miaka 35. Wewe kama kijana ukitaka
ujana wako usidharauliwe na mtu mwingine yeyote hakikisha kuwa unayasikiliza
maneno haya kisha uyatende.
Kivipi? Kijana unatakiwa uwe na maisha ya kuwa
kielelezo kwa watu wote watakaookoka leo, watakaookoka kesho na kwa wale
watakaookoka mwaka mzima wa 2017. Uwe kikelezo katika maneno yako: Yaani hata usemi wako usifanane
na usemi wa watu wasiokoka. Kumbuka kuwa Usafi
na Imani vinaendana pamoja. Je, upo na Bwana Yesu muda wote? Je, ukiwa
shuleni wewe kama kijana unamdhihirisha Kristo kwa maneno na matendo yako?
Ukiwa shuleni au mahali pengine popote, je watu wamekuwa wanakutumia kama
mnyama wa majaribio (test animals)
kwa mambo yasiyofaa? Kwani wewe umezaliwa ili utumike kama mnyama wa maabara ilihali
wewe siyo kama panya? Watu wote wafanyao mambo ya aina hii ni mithili ya panya
kwa sababu kila anayetaka kujifunza mambo machafu huwatumia vijana wa hii. Kijana unapaswa kuwa kielelezo kwa wenzako
katika kuvaa, unavyotembea, unavyosema n.k.
Tukisoma tena kwenye kitabu cha 1TIMOTHEO 4:14-16, maneno ya Mungu
yanasema hivi: …(Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na
kwa kuwekewa mikono ya wazee. 15 Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili
kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. 16 Jitunze nafsi yako, na
mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa
nafsi yako na wale wakusikiao pia.). Wewe kama kijana usitoe nafasi kwa
watu kutia mashaka juu ya wokovu wako kwa mwaka wote wa 2017. Nyakati nyingine namna ya uvaaji wa nguo
hutoa nafasi hizi kwa wasioamini kukejeli wokovu wako. Kwa upande wa mabinti kuvaa vizuri ni jambo
zuri, sawa ili kuitunza miili yenu kwa sababu ni ya thamani
sana. Mtume Paulo anasema ujitunze nafsi yako na mafundisho yako. Uistumie
kitu kingine bali tumia mafundisho haya ya Neno la Mungu uitunze nafsi yako.
Sherehe za Kuukaribisha Mwaka Mpya 2017 kwa Kuwasha Mishumaa, Usiku wa 31/12/2016 (Ufufuo na Uzima Morogoro) |
3. SALAMU ZA TATU ZA MWAKA MPYA NI KWA
WAMAMA WOTE
Imeandikwa katika LUKA 2:36-37 (Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti
Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya
uanawali wake. 37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika
hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba.). Biblia
inamtaja huyu Nabii mke, Ana, binti Fanueli. Mama huyu aliishi na mume wake kwa
miaka 7 tu, na alidumu hekaluni kwa miaka 84 akifunga na kuomba, hii ikimaanisha
kuwa alikuwa mjane kwa miaka 77 mizima. Hata hivyo, baada ya miaka yote hii ya
kuomba na kufunga, akampokea Yesu mikononi mwake siku ile ya Yesu ya kuwekwa
wakfu.
Majeshi ya Bwana Yesu wakishangilia na kumshukuru Mungu baada ya Kuvuka salama kuingia Mwaka Mpya wa 2017. |
Leo hii wapo watu ambao huyapangilia maisha
yao kwenye mawazo yao, wakizijenga picha zote nzuri nzuri za maisha ya ndoa zao
yatakavyokuwa pale watakapoolewa. Pengine wanapoangalia sinema za waigizaji wa
maisha mazuri ya ndoa, watu hawa hutamani kuwa au kuishi kama wao. Bila shaka
hii ni picha ambayo hata Ana binti Fanueli aliijenga mawazoni/akilini mwake: “Kwamba
niolewapo, nitakuwa natembea na mume wangu barabarani tumeshikana mikono namna
hii au ile, tutakuwa tunafanya hivi na vile, tukifurahia ndoa yetu hivi na
hivi.” Hata hivyo mama huyu alidumu na mume wa ndoto yake kwa miaka 7
tu ya ndoa. Hata baada ya hayo, Biblia
inasema mama huyu hakutoka hekaluni kwa kipindi chote cha miaka 77, na hatimaye
akampokea Yesu siku ile ya kuwekwa wakfu. Unaweza kujiuliza swali, hivi kwa
miaka yote hii, je huyu mama alikuwa
akifunga na kuombea kitu gani? Wakati ukitafakari jibu la swali hilo, cha
msingi tu kumbuka “Huyu ni mama
aliyeishi Ng’ambo ya ndoto zake”!!!. Cha kukusihi hapa na kukutia moyo wewe
mama ni kuwa usitoke hekaluni mwa Bwana, bali “ishi ng’ambo ya ndoto zako” (live beyond your dreams). Hata kama
uliota ndoto na kwa sasa hiyo ndoto haielekei kutokea, bado endelea kuishi ng’ambo
ya ndoto yako.
© Media and
Information Ministry
Glory of Christ Tanzania Church,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +25571765979866 / +255713459545
|