Wednesday, April 19, 2017

NGUVU KUTOKA KATIKA KABURI LILILO WAZI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

 

JUMAPILI YA PASAKA: 16 APRIL 2017

 

MHUBIRI:  PASTOR Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

 
Pastor Dr. Godson Issa Zacharia akiomba siku  ya Pasaka 16/4/2017 kabla ya Kuhubiri

 
Leo watu duniani  kote wanaadhimisha siku ya Kufufuka kwa Yesu Kristo. Yesu Kristo hayupo kaburini tena, kwani alifufuka siku kama hii. Tunasoma katika MATHAYO 27:27-31 (Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. 28 Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. 29 Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume;    wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! 30 Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampigapiga kichwani. 31 Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.). Tunajifunza kuwa Safari ya Yesu kuelekea Kalvari iliandamana na dhihaka, matusi, kudharauliwa na mateso mengi. Yesu alidhihakiwa na watu wale wale aliowasaidia na kuwaponya. Hata wewe Ukiona watu wanakudharau na kukutemea mate, ujue ushindi wako uko karibu. Ukiona watu wanakuvua nguo zako (kukuaibisha) ujue kuwa ushindi wako uko karibu.



Ibada ya Kusifu na Kuabudu ikiongozwa na Platform wa Ufufuo na Uzima Morogoro siku  ya Pasaka 16.4.2017.

 

Wale waliokuwa wakimpiga Yesu ni wanadamu kama sisi. Imeandikwa katika MATHAYO 27:37–49 (Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. 38 Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. 39 Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, 40 Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. 41 Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. 42 Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. 43 Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. 44 Pia wale wanyang'anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile. Kabla ya haya kutokea, tukumbuke kuwa Yuda Iskariote ndiye aliyehusika kuratibu kukamatwa kwa Yesu. Lakini Yesu alisema “Ole wake atakayeisaliti Damu isiyo  na hatia”. Alichokifanya Yesu ni kuwaonya wanafunzi wake wasikubali kufanya usaliti ule.  Pamoja na onyo hilo, hata hivyo Yuda alidanganyika na kuchukua vipande vya fedha ili kumsaliti Yesu. Yuda Isakriote alikuja na kumbusu Yesu. Hili ni fundisho kwetu kuwa siyo kila atakayekubusu anafanya hivyo kwa nia njema. Hata hivyo, Adhabu ya mtu yeyote anayefanya usaliti kwa damu isiyo na hatia ni kifo.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 27:45-54 (Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. 46 Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani?  Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? 47 Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. 48 Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. 49 Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. 50 Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.  51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; 52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. 54 Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.). Kupitia sauti ya Yesu aliyoipaaza akiwa msalabani, miamba ilitikiswa, makaburi yalipasuka, na waliokuwemo ndani wakatoka nje na kuwatokea watu wengi.

 

Kupitia nguvu hii, iliyosababisha makaburi kupasuka, tunatangaza leo kuwa makaburi yanayozuia mahitaji yako, kazi yako, upendeleo wako, ndoa yako n.k, yote yapasuke mara moja kwa Jina la Yesu. Tunakutangazia wewe kuwa yupo mmoja tu aliyeishinda mauti, huyu ni YESU KRISTO. Wale watu walimchoma Yesu Kristo mkuki ubavuni, Damu na Maji yakamwagika.  Kwa nini walimchoma mkuki ubavuni? Hii ilikuwa njia ya kuthibitisha kuwa Yesu amekufa au la. Na kwa hiyo, kwa maji na damu ile, ni dhahiri kuwa siku ile Yesu alikufa kweli  kweli.  

 

Yesu akisema kitu lazima kinakuwa. Kwa kufufuka kwa Yesu, roho za mauti nazo tunazishinda. Pamoja na kuwa Yesu tayari alikuwa keshazikwa kaburini, lakini bado askari waliwekwa pale kaburini ili kuulinda mwili wa Yesu ili asifufuke. Katika MATHAYO 27:63-66 tunasoma (wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. 64 Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. 65 Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. 66 Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi). Ndiyo kusema kuwa, hata wewe wapo watu walioweka askari wa kishetani ili kukulinda usifanikiwe. Lengo la hao watu ni kuona kuwa ahadi za Mungu kwako hazitimii kamwe.

 

Katika MATHAYO 28:1-5 tunasoma maneno haya: (Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.2 Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. 3 Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. 4 Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. 5 Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa.). Kwa mara nyingine tena tunajifunza kuwa Yesu akisema jambo lazima linakuwa. Hapa tunamuona MALAIKA anawakumbusha wanafunzi wa Yesu kuwa waelekee Galilaya ili wakutane na Yesu kama alivyowaahidi hapo awali aliposema katika MATHAYO 26:32 kwamba “Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”.

 
Pichani ni sehemu tu  ya umati wa watendakazi na waumini waliojitokeza siku  hiyo  ya Pasaka 16.4.2017 - Ufufuo na Uzima Morogoro

 

Leo ni siku ya kukumbuka kuwa YESU WETU YUPO HAI, na kaburi lake lipo wazi. Kila kitu chako kilichokuwa makaburini lazima leo kiwe wazi kwa Jina la Yesu.

========== AMEN ========

 

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia

Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson

Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson

TEL: 0719 798778 (Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages