GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA
UZIMA → MOROGORO}
JUMAPILI: 9 APRIL 2017
MHUBIRI: PASTOR Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Tunaposema gereza tunamaanisha nini?
Gereza ni
nyumba ya kufunga watu, na kuwazuia watu. Ni kizuizi kinachowaweka watu fulani
mbali na jamii yake kwa kipindi fulani kwa
sababu ya usumbufu wao. Gereza ni mahali
pa kumuondolea mtu uhuru wake, ili asiweze kufanya jambo lolote alilotaka
kulifanya kwa hiari yake. Gereza siyo
lile jengo tu la kuonekana. Ndiyo maana
kuna watu wengine wanakuwa wamefungwa kifungo cha nje, na kwa maana hiyo mtu wa
aina hii hawezi kwenda nje ya eneo alilokatazwa kwenda. Mtu akiwa gerezani,
hata ratiba yake ya kula inakuwa inaratibiwa na waliomfunga. Mtu akiwa gerezani
hawezi kuchagua aina ya chakula, hawezi kuamua muda wa kuomba hata kama angekuwa
mlokole.!! Gerezani unanyang’anywa uhuru wako wa kutenda mambo. Yapo magereza
ya mwilini na magereza ya rohoni (katika ulimwengu wa roho).
Yamkini wewe hapa unajiona upo huru mwilini lakini
rohoni unaweza kuwa umefungwa bila kujijua. Kwa maana hiyo ipo misingi pia ya
magereza haya ya rohoni. Endapo upo ugonjwa fulani unakuwa umewekewa misingi,
siyo kwa kutumia matofali ya kuonekana, bali kwa njia ya KAFARA ZA DAMU. Na kwa maana hiyo, msingi unapokuwa imara, shida ya
mtu inakuwa kubwavile vile. Ndiyo maana kuna watu wanaweza kuwa wenye shida ya
kufanana, mathalani ni ukosefu tu wa kazi. Lakini, endapo katika kuwaombea watu
wa aina hii utalitaja Jina la Yesu, mmoja wao anapata kazi mara moja. Mwenzake anaweza
kuchukua hata zaidi ya mwaka hajapata kazi. Kwa nini? Tofauti hii husababishwa
na ukubwa wa kafara iliyotumika kumfunga huyu mtu. Wanaoshirikiana kujenga
misingi ya aina hii ni mashetani, majoka na majini. Kwa kuwa msingi bado upo,
tatizo nalo linakuwepo. Ndiyo maana leo lazima tuingie rohoni na kuangusha kila
misingi ya matatizo maishani mwetu kwa Jina la Yesu.
Kuna mtu akiombewa anapata nafuu pale pale. Lakini
baada ya muda tatizo lake linajirudia
tena. Hii ni kwa sababu, wakati wa maombi yale, pepo aliyekuwa katika
msingi wa tatizo hilo huondoka, lakini
pepo huyu huenda kutafuta mapepo mengine ili kuongezea nguvu kuimarisha upya ule
msingi wa tatizo la mtu. Ndiyo maana sasa, katika ISAYA 42:22 imeandikwa hivi “Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na
kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa
mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.”.
Hayo magereza ya rohoni yanayotajwa hapa yamejengwa katika msingi ambao ndiyo
unaoleta shida. Endapo utaushughulikia huu msingi na kuudondosha chini, unakuwa
salama kwa sababu unakuwa umepata suluhisho la tatizo lako.
Majeshi ya Bwana yakisikiliza kwa makini jinsi ya kutoka katika magereza ya mateso jumapili ya leo 09/04/2017 |
Katika ZABURI
137:7 imeandikwa hivi “Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya
Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini!”. Kuna msingi
wa kila tatizo ulilo nalo leo. Upo msingi wa kushindwa kwako. Upo msingi wa
kukufanya uache kazi. Ule msingi ni wa kishetani, ulioandaliwa ili upate
mateso. Msingi ukibomoka, taabu zako zinaisha. Leo tuitikise misingi yote ya
kishetani inayosababisha mateso kwetu kwa Jina la Yesu.
Yamkini yupo mtu anajifikiria kuwa hajafungwa. Kwa
kawaida, mfungwa hana uhuru wa kuchagua chochocte. Waliokufunga ndiyo wanaosimamia
kila jambo maishani mwako. Katika ulimwengu wa roho yapo magereza kama yalivyo
magereza ya mwilini kama vile Segerea au Ukonga au Kingolwira. Wewe ambaye
unatamani kula chakula fulani lakini kipato chako hakikuruhusu kukinunua ujue
umefungwa tu!! Wewe ambaye unatamani kuvaa nguo ya aina fulani lakini kipato chako
hakikuruhusu uinunue ujue umefungwa katika kifungo cha kipato!! Leo ni siku ya kuitikisa
hiyo misingi ya hilo gereza linalokushikilia kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Nakataa kuwa mfungwa kwa Jina la Yesu. Wewe gereza
uliyenishikilia niachie kwa Jina la Yesu. Gereza la mateso niachie kwa Jina
la Yesu.Gereza la utasa niachie kwa jina la Yesu.
|
Platform wa Ufufuo na Uzima Morogoro, wakiongoza nyimbo za sifa katika ibada ya leo 9/04/2017 |
Ipo Mifano mingi ya Magereza na Wafungwa wake katika Biblia. Tunaposoma katika MATENDO 16:16-18… (Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. 17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. 18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.). Huyu kijakazi alikuwa ana mapepo ya uaguzi na hivyo alitumia huu mwanya kuwadanganya watu kwa njia ya uaguzi wake, na hivyo kutengeneza faida kwa bwana zake. Kitendo hiki cha Paulo kuwatoa haya mapepo kiliwafanya mabwana zake kuwafitini. MATENDO 16:19-24.. (Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji; 20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; 21 tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi. 22 Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. 23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. 24 Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale). Pamoja na kwamba Paulo na Sila walishughulikia hili jambo kiroho, lakini tunawaona makadhi na wakuu wa mji waliwakamata na kuwatia gerezani. Tunajifunza kuwa endapo utayashughulikia mashetani na mambo yao rohoni na kuyashinda, mashetani haya na mawakala zao huinua vita vya mwilini. Hii ni kwa sababu kushindana kwetu siyo kwa damu na nyama. Na ndiyo maana endapo misingi ya kishetani itatikiswa rohoni na kuwashinda, mashetani hawa huja kwa njia za kimwili.
Leo tutayabomoa magereza yote ya rohoni na misingi
yake, ili walioyajenga wakose mahali pa kutesea watu wengine kwa Jina la Yesu. Na
hiki ndicho kilichotokea, tunaposoma MATENDO
16:25-28 imeandikwa “(Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila
walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine
walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi
ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote
vikalegezwa 27 Yule
mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka,
alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. 28 Ila
Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote
tupo hapa.).”.
Mtu aliyeokoka
akifungwa gerezani anakuwa mfungwa maalumu. Mlokole anapokuwa kwenye shida
anakuwa na maombi ya bidii. Ndicho walichokifanya Paulo na Sila katika shida
yao, hawakupoteza muda bali waliomba kwa bidii na maombi yao kusababisha misingi
ya gereza kubomoka ghafla. Hata hivyo, maombi yetu leo tutaamuru aliyekuwa
msimamizi wa gereza la mateso yako atakapoona misingi ya gereza imebomoka na
wafungwa wake kuachiliwa huru, kufa na afe kwa kuwa imeandikwa “Ategaye
mtego mtego utamnasa mwenyewe” kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Natikisa misingi ya gereza la Ukimwi, Natikisa
misingi ya gereza la kuachwa, Natikisa misingi ya gereza la kukosa kazi kwa
Jina la Yesu. Aliyekufunga apate gharama na azilipe gharama hizo mara saba
kwa Jina la Yesu.
|
Hata hivyo kwa wewe uliyeokoka unapokuwa unakuwa haupo peke yako. Ukifungwa unakuwa na Yesu ambaye tayari yupo ndani yako. Usiogope. Omba kwa bidii, mshukuru Bwana, Msifu wakati wote unapokuwa unaomba. Kumbuka kuwa wapo malaika maalumu wa kutikisa magereza, makaburi n.k. na ndiyo ambao Paulo na Sila waliwatumia. Tunajua je haya? Tunasoma katika KUTOKA 19:16-18 (Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. 17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. 18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.). Ukimuomba Mungu na akishuka, lazima hapo mahali patetemeke. Na pia katika MATHAYO 27:51-53 imeandikwa (Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; 52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; 53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.). Ukipaaza sauti yako kwa maombi utasababisha tetemeko. Yesu alikuwa amefungwa msalabani lakini hawakukifunga kinywa chake. Paza sauti yako ili upate ukombozi kwa Jina la Yesu.
Showers of Glory Morogoro na majeshi ya Bwana wakimshangilia na kumwimbia Mungu |
Katika MATHAYO
27:62-66 imeandikwa (Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya
Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, 63
wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai,
Baada ya siku tatu nitafufuka. 64 Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata
siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka
katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. 65 Pilato akawaambia,
Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. 66 Wakaenda, wakalilinda
kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.).
Tunafahamu kuwa kaburi ni mahali pa kuzikia. Kwa kawaida Mtu akishawekwa
kaburini huwa ndiyo mwisho wa kila kitu kinachomhusu mtu huyo. Ni ajabu kuona
kuwa kaburi la Yesu linaendelea kulindwa na maaskari hata baaada ya kuwekwa mle
ndani. Hii ni kwa sababu Yesu Kristo alikuwa wa thamani sana. Ndiyo kusema
kwamba ukiwa mlokole, kifungo chako
kinakuwa maalumu sana kiasi kwamba hata kaburi lako linakuwa linaendelea kulindwa.
Akiombewa na kutolewa katika gereza la mateso. |
Imeandikwa katika MATHAYO
28:2-4 (Na tazama, palikuwa na tetemeko
kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja
akalivingirisha lile jiwe akalikalia. 3 Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi
yake meupe kama theluji. 4 Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa
kama wafu). Malaika alishuka
toka mbingnui na kuliviringisha jiwe. Hata wewe utatoka mautini na kuingia
uzimani. Waliokutesa na kukuweka kwenye makaburi ya mateso leo ni siku ya
kuwashughulikia kwa Jina la Yesu.
Leo tunaamuru malaika ashuke kama umeme kwenye ndoa
yako, biashara yako, kwenye kazi na maisha yako na kutetemesha wale
waliokulinda kwenye mateso kwa Jina la Yesu. Leo tutaitumia Damu iliyomwagika
kutoka ubavuni mwa Yesu baada ya kuchomwa mkuki, na kuwashinda watesi wetu wote
kwa kuwa imeandikwa “Nao wakamshinda shetani kwa Damu ya
Mwanakondooo na kwa neno la ushuhuda wao ambao hawakuapenda maisha yao hata
kufa” Lipo gereza linalozuia maisha yako, lakini Bwana amesema ingawa
umelindwa sana, leo atasababisha waliokulinda watetemeke na kuwa kama wafu kwa
Jina la Yesu.
Kama wewe hujaokoka, leo mpe Yesu maisha yako, ili
utengeneze upya kwa maana ya kuokoka ili ukiwa upande wa Yesu ufanyike kiumbe
kipya na hivyo iwe rahisi kutoka kwenye magereza ya mateso kwa Jina la Yesu.
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: 0719 798778 (Sms
only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/