Sunday, May 28, 2017

MSHALE WA USHINDI DHIDI YA WACHAWI

GLORY OF CHRIST TANANIA CHURCH [GCTC]
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI: 28. MAY. 2017.
MHUBIRI: PASTOR: DR. GODSON ISSA ZACHARIA



Mchungaji Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha katika Ibada ya leo.


Mshale ni nini? Mshale ni silaha yenye ncha kali. Ni silaha kama zilivyo silaha nyingine za kivita. Ni silaha yenye Sumu na kazi ya sumu hii huwa ni kuua na kuangamiza. Tabia nyingine ya mshale huwa ukiingia mahala hauwezi kutolewa kwa kuvutwa. Lengo la kutumia mshale huwa ni kuua. Ukitumwahuleta mauti.

“Mshale wa Ushindi”. Unaitwa Mshale wa Ushindi kwa sababu kuna makundi mawili. Kundi la kwanza ni mshale uletao Ushindi kwa wale walio upande wa Yesu. Na kundi la pili, ni Mshale wa uletao mauti kutoka kwa shetani.  Ufunuo wa Yohana 12:7-8 Imeandikwa Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; 8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Hapa kuna makundi mawili ya rohoni. Kundi moja linaongozwa na Malaika Mikaeli, analiongoza jeshi la Bwana. Na kundi la pili linaongozwa na Yule joka ndiye shetani na washirika wake. Malaika Mikaeli alitumia mshale wa Bwana na ndio maana shetani alipigwa na kutupwa nje na mahala pake hapakuonekana tena.

 Mshale wa ushindi huwa unatumika vitani. Wanaotumia mshale wa ushindi ndio wale wa timu ya mwanakondoo. Hii ndio timu yetu sisi waliookolewa. Na ndio maana Imeandikwa katika Efeso 6: 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Wanaoshindwa ni wale majini, majoka, wachawi walio upande wa shetani. Mshale wa kushinda huwa unaweza kushinda pasipo kujali ulikoelekezwa. Iwe umeelekezwa kuzimu ya angani, majini, nchi kavu, lazima mshale huu utenda kazi na kuleta ushindi.

Upande wa pili ni ule wa shetani. Upande huu huwa unarusha mishale ya Uovu. Kazi yao huwa inarusha mishale kila siku. Wakati mwingine huwa wanabahatisha na mshale unampata mtu na kumletea matatizo. Zaburi 64:3-6 Imeandikwa,  Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu, 4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi. 5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona? 6 Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa.


Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu.

 Hawa ni wanadamu wanaotumia ulimi wao kuwaangamiza. Hawa ndio mawakala wa shetani huwa wana tabia ya kuwavizia watu wakamilifu ili kuwaangamiza. Tabia yao huwa ni kuwategeshea watu wanao mtegemea Mungu. Na kwa kanuni ujifanya hodari katika kutenda mabaya. Yohana 10: 10 Imeandikwa, Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Ndio maana neno hili linasema kazi yao ni kuangamiza. Mishale hii ikitumwa mtu anaanza kurudi nyuma. Kama ni mwanafunzi utamwona anaanza kushindwa, biashara inadorora, ndoa inayumba na haimaye mauti. Hawa ni hodari wa kuharibu mimba, kazi, na mashamba. Hawa hawaangalii wewe ni nani, Hawajali wewe ni Mchungaji, Daktari au Profesa. Tabia yao huwa hawaogopi chochote ulichonacho. Kwanini, ni kwa sababu silaha zao zina nguvu rohoni. Wanajua huwezi kuwaona kwa macho ya mwilini. Jifunze jambo la furaha na Baraka, ya kuwa siri yetu ni kwamba Yesu akiwa upande wetu hawawezi kutupata. Yesu kwetu ni ngao inayoweza kuzuia mishale yao.

Isaya 54:17 Imeandikwa, Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana. Kwa kawaida mshale wa Bwana huwa unaakaili na hauwezi kuzuiliwa na mwanadamu.

MISHALE YA WACHAWI
Mishale ya wachawi huwa inakuja kwa gafla. Wanafanya vikao ili kumwangamiza mtu, kabla jambo halijatokea, kwanza wanakaa vikao na kufanya maamuzi. Wanashauriana ili kupata sehemu ambayo ukitegwa huwezi kuigundua kwa urahisi. Mara zote huwa wnatumia akili za ziada ili usiweze kutambua, wanatega mitego n.k. Lakini Bwana anasema atakuokoa na mtego wa shetani. Unaweza kuona mtu anakuwa msaada kwako kumbe anakuwinda. Zaburi 91:3-4 Imeandikwa, Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. 4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Baada ya vikao wanapanga na kuhakikisha wanakamilisha  mpango wao.  Na kanuni yao ni kuhakikisha mawazo yao yanakamilika kwa siri ili mtu asijue.


Makutano wakisikiliza somo la leo (Mshale wa Ushindi dhidi ya wachawi)

Ili mchawi aweze kuurusha mshale, lazima azingatie yafuatayo;
Moja; kumfanya mtu ajichanganye na wao. Mithali 4:14-15 Imeandikwa, Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Ili waweze kukupiga mshale ni lazima ufanye kama wanavyofanya, utende kama watendavyo. Neno la Mungu linaonya ya kuwa tusikaribie njia zao na tujitenge mbali nao.  Na ndio maana neno linasema tusiziendee njia za uovu. Ukiona mwovu anakwambia nakupenda, jua  moyoni mwake anakuchukia sana. Na ndio maana neno linasema tuache dhambi. Na pengine anasema Ikimbieni zinaa. Ukiona njia za uovu sharti ugeuke na kukimbia. Usikubali mtu kuchoma ubani kwenye nyumba yako au biashara yako. Usipende kusema uongo wala kusengenya watu. Unaweza kuona ni taratibu za jamii unayoishi. Utasikia mtu anaenda sherehe ya arobaini, au kusalia wafu na wewe unaungana nao. Jua hapo unatafutwa na mshale wa wachawi.

Ufunuo wa Yohana 3: 15 Imeandikwa, Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Utaona mtu anakuja kanisani lakini bado anaenda kwa waganga. Mungu wetu hapendi kujichanganya, unaenda kanisani uku una nyumba ndogo, Hawala au unafanya uzinzi. Mungu hapendi kujichanganya. Kwa sababu ukijichanganya ndio tiketi ya kupatwa na mshale wa uovu.  Vigezo vikiwepo tayari wanaweza kuurusha mshale na ukakupata. Wanaweza sasa kuurusha mshale kwenye biashara, shule, kazi, afya na hatimaye mauti. Unaweza kurushwa kwenye ndoa au uchumba ila sasa hakuna mawasiliano, jua tayari mshale wa wachawi umeisha ingia. Kudorora kwa biashara, shule, afya, kazi, ndoa, ni dalili ya kuwa tayari upo mshale wenye sumu za kichawi na tayari inatenda kazi ndani yako. Lazima kuyeyusha kwa jina na damu ya mwanakondoo. Maana nguvu ya msalaba ni upuuzi kwao wanaopotea na ni nguvu kwao wanaokolewa.

 Mithali  4: 14-16 Imeandikwa, Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. 16 Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Kumbe ujue hawa mawakala wa shetani hawalali isipokuwa wamemwangusha mtu. Kazi yao ni kuhakikisha mtu amepatwa na baya. Wakishatenda baya ndo wanaweza kupata usingizi. Kwanini, wanatumia muda wao mwingi kuangamiza, ndio nia ya shetani. Na pengine ni kwa sababu wakirusha kwa watu wengine mshale wao hauwezi kuwapata. Kwa sbabu hiyo ni lazima watafute wa kumpiga kwamshale wao. Huwa hawalali mpaka kusudi lao limekamilika. Lakini leo shauri lao lazima libatirike. Maana kwa mshale wa Bwana wamepgwa.



Mchungaji Dr. Godson Issa, akimwombea mtu.

MSHALE WA USHINDI.
Jinsi Mungu anavyowapiga wachawi kwa mshale wa ushindi. Zaburi 64:7 Imeandikwa, Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa. Ni kanuni ya Mungu kutumia mshale mmoja tu na wachawi uanguka. Zaburi 64:8-10 Imeandikwa, Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa. 9 Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya Mungu, Na kuyafahamu matendo yake. 10 Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia,Na wote wenye moyo wa adili watajisifu. Jifunze ya kuwa ukipigwa na Bwana lazima uangamie. Kila atakayewatazama atatikiswa kichwa. Ni kwa mshale huu watu wataokolewa na kuyajua matendo makuu ya Bwana. Mshale wa ushindi huwa unatoka kwenye mikono wa Mungu. Mungu huwa anarusha mshale kwa kutumia mikono ya mwanadamu.

Yeremia 51: 20 Imeandikwa, Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunjavunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;  Mungu anasema ni kwa wewe ataweza kutenda kazi duniani. Ili Yesu atende kazi lazima awepo mwanadamu anayejitambua nafasi yake kwa Bwana. Ukitamka au kuamua jua Mungu ameamua. Mshale huu ni mshale wa ushindi uliotoka mbinguni. Ni kanuni ya Mungu ya kuwa mbingu siku zote uachilia uzima. 2 Wafalme 13: 14-19 Imeandikwa, Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! 15 Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. 16 Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. 17 Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa Bwana wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. 18 Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. 19 Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu. Hizi ni habari za mfalme aliyejua ya kuwa kwa watumishi kuna maneno ya uzima. Elisha alikuwa katika hali ya kufa lakini bado alikuwa bado anayo nguvu ya Bwana. Na akamwelekeza mfalme namna ya kutenda ili kushinda vita. Tunajifunza ya kuwa Mungu akisema rusha mshale wewe rusha mara nyingi wala usinyamaze.  Kumbe ukitaka kuangamiza wachawi, wewe piga mara nyingi. Piga kadri uwezavyo kwa sababu ni mshale wa Bwana wenye kushinda.

 VIFAA VINAVYOTUMIKA:
PODO kazi yake ni kifaa cha kutunzia mishale. Hata mfalme alikitumia. Katika Roho, wewe ni Podo ambaye ndio kifaa cha kutunza mishale. Na huyu ni mtu aliyeokoka. Podo inaweza kuwa na mishale au isiwe na mishale. Isipokuwepo basi utapigwa na mishale ya wachawi. Basi lazima ujaze mishale kwanza kwenye podo lako. Kanuni ya kujaza mishale ni kuyatafari maneno ya MUNGU nyakati zote.  Ni kama ilivyoandikwa katika Yoshua 1: 9 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. ….. lazima kulisoma neno la Mungu, kutafakari na kuangalia namna ya kutanda sawasawa na sheria ya Mungu.

UTA AU UPINDE ni kifaa cha kutuma au kurusha mishale. Kwa Rohoni ni Uta au upinde NI KINYWA cha mtu aliyeokoka. Kutamka au kuamuru ndio kurusha mishale. Kwa maneno mengine kutumia mdomo wako kufanya maombi ndio kukifanya kinywa kuwa upinde.  Kadri unavyoomba zaidi ndivyo unavyoweza kuwa umerusha mishale mingi zaidi. Yeremia 1: 7-9 Imeandikwa, Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi  ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. 8 Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. 9 Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama  nimetia maneno yangu kinywani mwako; Kumbe kuna siri ya kufanikiwa katika kinywa. Maana Mungu alimwambia Yeremia ya kuwa ameweka maneno yake katika kinywa chake. Unaweza kuwa na upinde lakini usijue namna ya kuutumia kurusha mshale. Lakini ukijua jinsi ya kutumia kinywa chako, basi utasababisha mabadiliko makubwa. Lazima usome neno la Bwana ili yaingie moyoni mwako na hatimaye yatumike kupitia kwenye  kinywa chako.


Showers of Glory Morogoro wakiimba katika Ibada ya leo.

Na namna ya kuzitunza silaha ndani yako ni kutafakari neno la Mungu  mchana na usiku. MSHALE ndio silaha ya vita, kwa rohoni mshale NI NENO LA MUNGU. Silaha hii inatunzwa ndani yako, na baadae hiyo silaha lazima iwekwe kwenye kinywa,  ukikitumia vizuri utasababisha matokeo mazuri. Hata wachawi wameunoa ulimi wao, kama ilivyoandikwa katika  Zaburi 64: 3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu.  Hii maana yake mshale ni wa uovu unatoka kwenye vinywa vyao. Na sisi lazima tutumie vinywa vyetu ili kuzipinga kazi za ibilisi. Tumia kinywa chako ukilitaja neno la Bwana, neno hilo moja linageuka na kuwa mshale dhidi ya wachawi. Kwenye vita hii usiende kwa maneno yako. Bali omba kwa kulitumia neno la Bwana kama Yesu. Nenda kwa “Imeandikwa” hata kama hujui wapi neno ilo limeandikwa wapi. Wewe tamka tu na maneno hayo yataenda kama mshale. Kila neno utakalolitumia, amini litaleta mabadiliko kulingana na namna ulivyolituma. Hii ni kwa sababu neno la Mungu ndilo lililobeba uzima. Kwa kadri utakavyotamka zaidi ndivyo utakavyo washinda zaidi.


 Yohana 6:63 Imeandikwa, Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Tena imeandikwa katika Isaya 49:2, Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;.. ili utende kazi Bwana utufanya kuwa mshale uliosuguliwa ili kuleta mabadiliko. Na sisi mshale wetu umesuguliwa, na kwa vinywa vyetu lazima tulete mabadiliko. Ni kutamka neno la Mungu maana hii ndio silaha ya kushinda kwetu katika jina la Yesu.
Share:
Powered by Blogger.

Pages