GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}
JUMAPILI: 21 MAY 2017
MHUBIRI: PASTOR DR.
GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Mchungaji Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha katika ibada ya leo 21/05/2017 |
Bwana Yesu hapendi
vitu vife katika uchanga wake. Viumbe vyote duniani ni rahisi sana kuviua
katika uchanga wake. Iwe ni ndoa, watoto, binadamu, mnyama, masomo, mimea n.k
huwa rahisi sana kufa au kuharibiwa katika hali ya uchanga wake. Ndivyo ilivyo
hata kwa vitu tuvionavyo vikubwa sana. Mathalani, mbuyu unaanza kama mchicha, na
wakati huo ni rahisi hata kuku kuuharibu. Lakini mbuyu ukeshafikia katika
ukubwa wake, hata ungetumia panga kuukata itakuwia ngumu sana. Leo tutaona aina
tofauti za majoka yanayokula vitu vyetu kabla ya kuvikia mwisho wake na
kuvifaidi.
Platform ministry wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiongoza sifa na kuabudu. |
1.
JOKA (SHETANI) ANAYEKULA VICHANGA
Shetani naye hutumia
mbinu hii kukamata watu au vitu vyao katika hali ya uchanga na kuleta uharibifu.
Shetani humuingia mtu mchanga (katika wokovu wake, biashara changa, ndoa changa
n.k.) ili apate kuleta uharibifu. Leo Bwana Yesu ameleta maneno haya ili kumshinda
shetani anayeharibu vitu vyetu katika uchanga wake kwa Jina la Yesu.
Katika Biblia
tunaona jinsi Joka alipanga kuleta kifo kwa mtoto mchanga, wakati motto huyo
akiwa anazaliwa. Imeandikwa katika UFUNUO
12:1-4 (Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi
ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na
mbili. 2 Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika
kuzaa. 3 Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu,
alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. 4 Na
mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.
Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo,
amle mtoto wake.). Yohana aliona ufunuo wa mwanamke huyu aliyekuwa
akisubiri kuzaa, na pembeni alionekana joka
anayesubiria Yule mtoto ili amle.
Joka huyu mwekundu ni IBILISI.
Hapa tunajifunza si watoto wote wanao kufa wakati wa kujifungua, kwamba wote
ufa kweli hapana, wengine wanaliwa na shetani.
Joka huyu kazi
yake ni kuharibu vitu katika hali ya uchanga. Majina yake ni kama yalivyooneshwa katika UFUNUO 9:11 (Na juu yao wanaye mfalme, naye ni
malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo
jina lake Apolioni.), na jina jingine la huyu joka ni mwizi kama
ilivyoandikwa katika YOHANA 10:10 (Mwivi
haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha
wawe nao tele.). Ni joka anayeharibu vitu vichanga, anayeharibu ndoa
changa, anayeharibu biashara changa, na ndiyo maana joka huyu hakuwa na mpango
kabisa wa kumla yule mwanamke, bali lengo lake ni kumla mtoto aliyekuwa
anasubiriwa kuzaliwa. Hebu waza:- Mama ni
mjamzito amepata wakati mgumu miezi tisa, akisubiria mtoto azaliwe. Pengine mama
wa aina hii alikuwa akitapika, au akikosa usingizi, au mara nyingine akala
udongo n.k. lakini Joka naye yupo pembeni anajiandaa kumla mtoto ambaye mama huyu
amemsubiria muda wote huu!!!!
Joka wa aina hii
ni anayekamata na kuharibu vitu katika uchanga wake. Pengine hata wewe unavyo
vitu vichanga ulivyoanzisha na vikapotea katika hali ya uchanga wake. Pengine Umeanza
mahusiano yakafa ghafla kabla ya kufikia mwisho wa kuitwa ndoa. Ulianza shule
vizuri ukiwa unapata 100% katika mitihani yako ila kwa sasa unapata sifuri. Mwingine
ulianza biashara na sasa hasara imetawala kiasi kwamba umeamua kuacha kuendelea
na biashara. Pengine ulikuwa huna kazi, ukapeleka barua ya maombi ya kazi
mahali fulani, na baada ya usaili ukakubaliwa kuanza kazi, lakini ghafla ndani
ya mwezi mmoja tu ukafutwa kazi. Haya yote ni maroho ya mashetani yapo kazini kwa
ajili tu ya kuharibu vitu vichanga. Mahospitalini
nako hali ni hiyohiyo, ambapo wamama wanapokaribia kujifungua, pamoja na
uchungu wote wa kuzaa, bado wakunga huja na kuwaambia baadhi ya wamama wa aina
hii eti kuwa mtoto aliyezaliwa ni BAHATI
MBAYA (kumaanisha kuwa mtoto amefariki dunia!!). Leo tutawaangamiza wote
waliopanga kuharibu mambo yako katika uchanga wake kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Leo ninakataa roho
ya kupata na kupoteza, kwa Jina la Yesu. Ewe roho la kupata na kupoteza, Achia
biashara, achia masomo, achia vitu vyote vyangu katika Jina la Yesu. Imeandikwa
“mimi
ni rungu la Bwana na silaha za Bwana za vita”, leo nashambulia
mashetani yote yanayosubiria kula vitu katika uchanga wake kwa Jina la Yesu.
Amen
|
Katika UFUNUO 12:5-6 imeandikwa (Naye
akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma.
Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.
6 Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali
palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na
sitini.). Kumbe tunajifunza kuwa Mtu
unapookoka Mungu ukuwekea ulinzi. Ingawa joka atapanga kula vitu vyako, lakini
Mungu hutokezea na kutoa ulinzi. Kumbe kuna namna ya kufichwa na kuwekwa salama
na Mungu kwa wewe uliyeokoka.
2.
JOKA (SHETANI) AITWAE FARAO
Farao Mfalme wa
Misri naye alipanga kuaangamiza watoto wachanga, kwa mtindo huu huu wa majoka. Imeandikwa
katika KUTOKA 1:8-17 (Basi
akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. 9 Akawaambia watu wake,
Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.10
Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao
nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi
hii. 11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao
wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. 12 Lakini kwa
kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao
walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. 13 Wamisri wakawatumikisha wana wa
Israeli kwa ukali; 14 wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya
chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote
walizowatumikisha kwa ukali. 15 Kisha
mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa
Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; 16 akasema, Wakati mwazalishapo
wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume,
basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. 17 Lakini wale wazalisha
walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri,
lakini wakawahifadhi hai wale wanaume.). Huyu mfalme naye ni joka tu, aliyelenga
kuwala watoto. Hapa tunajifunza ya kuwa shetani anaweza kutenda kazi akiwa
ndani ya mwili wa mwanadamu. Neno la Mungu linasema hawa WAZALISHAJI WALIKUWA NI WACHA MUNGU. Swali la kujiuliza hapa: Je, endapo
umeenda hospitalini, lakini mzalishaji
wakosiyomcha Mungu ni kitu gani
kitatokea? Ni dhahiri kuwa wasio wacha Mungu watasababisha VIFO visivyo
na hatia. Mfalme Farao naye ni joka, kama ilivyoandikwa katika EZEKIELI 29:3 (nena, useme, Bwana MUNGU asema
hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye
kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa
ajili ya nafsi yangu.). Tunajifunza kuwa hata baadhi ya wafalme
(viongozi) utendaji wao ni ule ule wa majoka, na ndiyo maana inabidi uwe mtu wa
rohoni sana unapokuwa chini ya uongozi wa watu kama hawa.
Mfalme Farao
anakasirishwa anapowaona watoto wa Kiebrania wakiendelea kuzaliwa na
kuongezeka. Imeandikwa katika KUTOKA 1:18-21
(Basi
mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo
hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? 19 Wazalisha wakamwambia Farao, Ni
kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni
hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. 20 Basi Mungu
akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na
kuzidi kuwa na nguvu nyingi. 21 Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa
wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba. 22
Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume
atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.). Ina maana kuwa wazalisha wasiomcha Mungu ndiyo wanaosababisha vitu vyako kutoongezeka. Wawindaji
wakishashindwa kuua mwanzoni, hutega mitego yao upya hata kwa vile ambavyo Mungu
alikusaidia kuvipata. Ni wajibu wako kuviombea vitu ulivyopata (kazi, mchumba,
ndoa, biashara n.k) na kuvilinda kwa Damu ya Yesu ili shetani
anayetaka kuviwinda asifanikiwe. Hakuna kubweeteka pale unapoona
umefanikiwa. Wapo watu leo hii ambao walikuwa hawana kazi, lakini baada tu ya kuombewa
na kufanikiwa kupata kazi, watu hao hata kanisani hawaji tena.!!! Kumbuka kuwa,
wazalishaji walipoacha hai wale watoto wa Kiebrania, bado Mfalme alikuja na
mpango wa kuangamiza watoto waliokuwa
hai.
Mchungaji Dr. Godson Issa Zacharia akimfungua na kubomoa roho ya kupoteza. |
3.
JOKA (SHETANI) AITWAE HERODE
Herode ni
mwanadamu kama wewe lakini ndani mwake yumo Joka wa kuleta uharibifu. Imeandikwa
katika MATHAYO 2:1-3 (Yesu
alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama,
mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Yuko wapi yeye
aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi
tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na
Yerusalemu pia pamoja naye.) Moyoni mwa Herode, aliona wivu kwa kusikia
eti amezaliwa mfalme wa Wayahudi. Kumbe wapo watu wanaokasirishwa wanapoona
unafanikiwa kama wao au zaidi yao.
Na tena imeandikwa
katika MATHAYO 2:7-8 (Kisha
Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana
ile nyota. 8 Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo
ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.).
Alichoazimia Herode siyo kwenda kweli kumsujudia mtoto aliyezaliwa, bali ni
kumuua mapema ili asije kuusumbua ufalme wake. Mpango muovu wa Herode ni kutaka
kumuangamiza Yesu katika uchanga wake. Ni
kama wewe, ambapo pengine kazi yako inaonekana itawasaidia sana ndugu zako na
familia yako, na matokeo yake wawindaji wanajitokeza ili kutaka kuimeza. Mtu
anaweza kuwa Joka, na ndiyo maana imeandikwa katika MATHAYO 10:36 (na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake).
Kumbe tunajjifunza kuwa joka anaweza kuwa mwanadamu, tena pengine ni ndugu wa
ukoo au mtu wa karibu sana na wewe. Leo tutamkamata joka huyu na kumchinja na
kumuangamiza kabisa kwa Jina la Yesu.
Joka (shetani) ni
adui yetu na leo tutamkanyaga, kwa kuwa tumepewa amri ya kukanyaga nyoka na nge
na nguvu zote za yule muovu na wala hazitatudhuru. Imeandikwa katika MWANZO 3:15 (nami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda
kichwa, na wewe utamponda kisigino.), na pia katika ZABURI 91:13 imeandikwa (Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na
joka utawaseta kwa miguu). Leo tunakamata panga zetu na kumfyeka joka
anayetuzonga zonga, kama ilivyyoandikwa
katika ISAYA 27:1 (Katika
siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu,
atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye
kuzongazonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.). Hata hivyo ni
watu wale tu waliookoka ndiyo wanaoweza kupigana na joka wanaotaka kula vitu
vyao.
Endapo umesoma
somo hili na hajampa Yesu Kristo maisha yako, kwa maana ya kuokoka, Leo Amua
kufanya hivyo ili iwe rahisi kwako kuchinja majoka yaliyojipanga kula vitu vyako.
Kiri maneno haya chini ili upokee Uzima:
UKIRI:
Baba katika jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, nimesoma neno lako na nimejitambua ya kuwa mimi
ni mwenye dhambi, nina tubu leo, nisamehe dhambi zangu zote nilizotenda kwa
kujua au kutokujua, nakusihi ufute jina langu kwenye kitabu cha mauti na
uliandike kwenye kitabu cha UZIMA. Nakupokea Yesu uwe Bwana na mwokozi wa
maisha yetu.
|
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/