GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH [GCTC]
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
JUMAPILI: 04. JUNE, 2017.
Sifa na kuabudu ni maneno yenye maana inayokaribiana. Kusifu
ni kueleza wasifu wa mtu au kitu. Kwa maana nyingine ni Kumuinua Mungu juu, ni Kushukuru
na Kumpazia sauti, kumfanyia shangwe na kujishusha chini ya Bwana Yesu kwa
Unyenyekevu.
Kuabudu maana yake Kusujudia, kuinama kwa kuonesha unyenyekevu, heshima kwa au
kuanguka kifudifudi. Kusifu na kuabudu ni agizo la Bwana kwa wanadamu. Ni
katika sifa Mungu uwatokea wanadamu. Mungu akishuka katikati ya wanadamu siku
zote huleta mabadiliko.
Zamani makanisa ya kiroho yalijulikana kwa
kumsifu Mungu na hata sasa. Kumsifu na
kumwabudu kwa moyo wa kweli kunavuta mtu kwa Mungu. Siku zote Mungu anapenda
kusikia, tukiisifia kazi na uumbaji wake na mambo makubwa aliyotenda maishani
mwetu. Ni kawaida hata wanadamu wanapenda kusifiwa. Mfano kila mwajiri anapenda
kusifiwa na wafanyakazi wake jinsi anavyowatendea au jinsi alivyo bos mzuri.
Mungu ni zaidi ya wanadamu wote maana yeye ndiye aliyewaumba wote na sisi tu
watu wake.
KUSIFU NI AGIZO LA MUNGU
Zaburi 34:1 Imeandikwa, “Nitamhimidi
Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. 2 Katika Bwana nafsi
yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.” Kuabudu na kumsifu Mungu ni jambo
la siku zote na nyakati zote. Unaweza kumsifu na kumwadhimisha Mungu ukiwa
safarini, kazini, shambani au mahali popote. Kumsifu Mungu kunasababisha mtu
ahisi uwepo wa Mungu. Kusifu na
kumwabudu ni mahali pote bila kujali hali uliyo nayo. Kuna wakati mwingine
ambao unapita wakati mgumu hata huwezi kuomba. Lakini jipe moyo na umwimbie
Mungu. Anza kumsifu Mungu kwa kuimba kwa sauti yako, kwa kupiga kinanda, zeze
na zumari. Mwingine anaweza kupiga vigelele na miluzi pia. Katika kumsifu Mungu
hakuna kuangalia nafasi uliyonayo katika jamii.
Platform Ministry wakiongoza sifa na kuabudu. |
Yohana 4: 4-24 Imeandikwa, “ Naye
alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. 5 Basi akafika kunako mji wa
Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu
mwanawe. 6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka
kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. 7
Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. 8 Kwa
maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. 9 Basi yule mwanamke
Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni
mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)10 Yesu
akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye,
Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. 11 Yule
mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi
umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? 12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu,
Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia,
na wanyama wake? 13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu
tena; 14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu
milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji,
yakibubujikia uzima wa milele. 15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji
hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka. 16 Yesu akamwambia, Nenda kamwite
mumeo, uje naye hapa. 17 Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu
akamwambia, Umesema vema, Sina mume; 18 kwa maana umekuwa na waume watano, naye
uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. 19 Yule mwanamke
akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! 20 Baba zetu waliabudu katika mlima
huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. 21
Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika
mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu
tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo
sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa
maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo
yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Hizi ni habari za mwanamke aliyekuwa
anatafutwa na Yesu. Huyu ni mama aliyekuwa na matatizo ya kuolewa na kuachwa.
Ila Yesu akamuuliza maswali mpaka akamfahamu asili yake. Mtafute Yesu na utamfahamu
kwa undani zaidi. Kumwabudu Mungu ni sawa na kuomba, katika kumwabudu Mungu
roho ya mwanadamu inakutana na Roho wa Mungu. Imeandikwa Mungu ni roho, na wale wamwabuduo lazima wamwabudu
katika roho na kweli.
Mathayo 15 : 8- 9 Imeandikwa, “Watu
hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. 9 Nao waniabudu
bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.” Kumbe ili umwabudu Bwana lazima uwe na Bwana
Yesu ndani yako. Moyo uko tayari kuyatenda mapenzi ya Mungu. ndio maana neno
linasema ipo saa ambayo wamwabuduo Mungu watamwabudu katika roho na kweli.
Kumwabudu Mungu katika kweli ni kuishi katika Haki. Neno la Mungu linasema watu
hawa wananiheshimu kwa midomo ila mioyo yao iko mbali nami. Unaona Yesu
anamtafuta mtu mmoja amabaye moyo wake ameuweka tayari kwa ajili ya Bwana Yesu.
Majeshi ya Bwana yakisikiliza somo la kusifu na kuabudu. |
2 Nyakati 5: 13-14 Imeandikwa, “hata
ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja
ya kumsifu na kumshukuru Bwana nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na
vinanda, wakimsifu Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake
ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya Bwana,14 hata
makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu;
kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa Bwana.”
Mungu anamtafuta mtu atakayemwabudu
katika Roho na Kweli. Kusifu na Kumwabudu Mungu kunafanyika katika Roho na
kweli. Anachoangalia Mungu ni kile
kinacho kusukuma kumchezea Bwana Yesu. akitupata wote, tukimwabudu tunakuwa
tumeungana na Roho wa Mungu. Tukishaunganika kwa pamoja tukiimba, na tukiomba Nguvu ya Mungu itaonekana kwa namna ya
tofauti. Zaburi 22: 3 Imeandikwa,” Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za
Israeli.” Tukiungana kwa
pamoja basi Mungu hutokea na kuketi katikati yetu. Mathayo 18: 20 Imeandikwa, “Kwa
kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo
katikati yao.” Tukimwabudu kwa pamoja Mungu ushuka kwa nguvu na uweza
wake wote. Na Mungu akishuka tayari uponyaji unadhihirika. Mtu yeyote katika
maisha anatamani uwepo wa Mungu. Maana uwepo wa Mungu ukiwepo, mtu uwa na amani
kwa kila analolifanya. Kwa sababu uwepo wa Mungu ukiwepo, kazi, biashara,
masomo, huduma inakuwa salama.
SIFA HUFUNGUA VIFUNGO;
Matendo ya Mitume 16:23-28 Imeandikwa, “Na walipokwisha
kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza
awalinde sana. 24 Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha
ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. 25 Lakini panapo usiku wa manane Paulo na
Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa
wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata
misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya
wote vikalegezwa. 27 Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa
milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa
wafungwa wamekimbia. 28 Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema,
Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.”
Mch.Godson Issa akiimba na platform mimistry. |
Katika sifa miujiza hutokea, ni katika
sifa tu hata yale yasiyowezekana kwa macho ya wanadamu, yanawezekana. Hapa
Paulo na Sila walikuwa gerezani. Ni wafungwa waliompiga mkuu wa mji
aliyewapatia mabwana zake mali kwa nguvu za kishetani. Hawa ni wafungwa
waliokuwa wafungwa maaalumu. Kwa kawaida kila mlango wa gereza huwa na kufuli.
Wakaingizwa chumba maalum, wakafungwa kwa mikatale ili wasitoroke. Wakawekewa
walinzi. Lakini cha kushangaza watumishi hawa waliijua siri ya kusifu na
kuabudu. Hawakuangalia hali ya tatizo walilokuwa nalo. Bali katika hali ya vita
ile walianza kumsifu Mungu. Neno la Mungu linasema walimsifu Mungu kwa furaha.
Kuna mambo ambayo umeyaombea mpaka umechoka sana. Usikate tama, bali ndio
wakati wa kuanza kuimba na kumsifu Bwana.
Kwenye kuimba lazima utakutana na Mungu. Kupitia sifa Mungu atakutana na
hitaji la moyo wako nawe utakuwa salama kwa jina la Yesu. Wafungwa wengine
waliwashangaa sana kwa maombi yale. Kumbe kuna tatizo ambalo halijaisha kwa
sababu hujamwabudu Mungu. Mungu aliiangalia Imani yao. Baada ya muda mfupi
misingi ya gereza ilitikisika na milango ya gereza ikafunguka. Kushinda kwao
kulitokana na kumsifu na kumwabudu Bwana.
Yona 2: 1-7 Imeandikwa, “Ndipo
Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki, 2 Akasema,
Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu,
Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. 3 Maana ulinitupa
vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote;
Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. 4 Nami nikasema,
Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini
nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. 5 Maji yalinizunguka, hata
nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka;
Mwani ulikizinga kichwa changu; 6 Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata
milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu
kutoka shimoni, Ee Bwana, Mungu wangu, 7
Roho yangu ilipozimia ndani yangu,
Nalimkumbuka Bwana; Maombi yangu
yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu.”
Yona aliwai kuwa ndani ya tumbo la
Samaki. Katika tumbo Yona hakuwa na maamuzi juu ya maisha yake, hili lilikuwa
gereza. Hiki kilikuwa kifungo cha aina yake. Yona alipokuwa katika tumbo la
Samaki, akamlilia Bwana. Yona alimsifu na kumwabudu Bwana ndipo alipotapikwa
kutoka tumboni mwa Samaki. Siri ya kufunguliwa kwa Yona, ilikuwa ni kumsifu
Bwana. Baada ya kumsifu na kuabudu ndipo Bwana akamwamuru samaki amtapike Yona.
Katika shida yako uelekeze moyo wako kwa Bwana. Mtafute Bwana nyakati zote.
Usiifanye shida yako kuwa ndio sehemu ya maamuzi yako. Mwabudu na kumsifu Mungu
ili ashuke kukusaidia. Yona alipokuwa katika vilindi vya bahari akakumbuka kwa
habari za waliowai kusaidiwa na Mungu. Lazima tujifunze kumwabudu Mungu katika
hali zote. Kuliangalia tatizo na kukata tamaa ni kumtukuza shetani. Hii ni kwa
sababu mabaya utoka kwa shetani. Yakiwepo magumu mbele yako, mwabudu Mungu nawe
katikati ya sifa utapata ufumbuzi wa tatizo lako.
Zaburi 149: 1-6 Imeandikwa, “Haleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa. 2 Israeli na
amfurahie Yeye aliyemfanya, Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao. 3 Na
walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa
matari na kinubi wamwimbie. 4 Kwa kuwa
Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu. 5 Watauwa na
waushangilie utukufu, Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao. 6 Sifa kuu za Mungu
na ziwe vinywani mwao, Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.” Tukiabudu
Mungu hushuka. Uwepo wa Mungu ukiwepo mahali kila kitu utikiswa. Ndio maana
Yesu alipofufuka makaburi yote yalipasuka na wafu wakatoka. Jifunze na tufanye kumsifu na kumwabudu Mungu
kuwe sehemu ya maisha yetu. Kumsifu Mungu kunasababisha miujiza na nguvu ya
Mungu kuonekana katika maisha yako.
Mch. Godson Issa akiombea katika ibada ya leo. |
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)