GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (G.C.T.C)
{KANISA LA UFUFUO
NA UZIMA - MOROGORO}
JUMAPILI: 13 AUGUST
2017
MHUBIRI: PASTOR GODFREY MWAKYUSA (SNP-SHINYANGA)
Kitabu ni kifaa
kinachotumika kwa ajili ya kuweka
kumbukumbu. Kuna aina 4 za vitabu katika
Biblia tutakavyoviangalia siku ya leo.
Kama unavyojua, mtu anapokuwa anaokoka humuomba Mungu alifute jina lake kwenye
kitabu cha Hukumu, na kuliandika upya katika Kitabu cha Uzima.
Katika kitabu cha KUTOKA 32:33 neno la MUNGU linasema “Bwana
akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika
kitabu changu.”. Ni kwamba, Mungu aliwahi kuwaandika watu katika kitabu
cha mafanikio, na kwamba kupitia dhambi MUNGU huyafuta majina ya watenda dhambi
humo kitabuni mwake. Kumbe sababu kubwa ya majina kufutwa ni magazaga ya dhambi.
Kumbe KITABU CHA UZIMA kipo, na mtu
anapotenda dhambi humfanya afutwe kwenye kitabu cha uzima. Jina
la mtu likifutwa kwenye kitabu cha
uzima, huandikwa kwenye KITABU CHA
MAUTI. Maana yake utakuwa na
roho za mauti kwenye kazi, biashara, ndoa,familia,na kila ukifanyacho
kinakuwa katika mfumo wa kuvunwa na mauti.
Leo lazima tukatae
majina yetu kuwepo katika kitabu cha mauti kwa sababu YESU aliyetufia msalabni
alikusudia majina yetu yawepo kwenye kitabu cha uzima ili biashara,ndoa,
familia n.k. ziwe na uzima katika Jina la YESU.
Mauti haina nguvu
kwetu, kwa kuwa imeandikwa katika 1WAKORINTHO
15:26 “Adui wa mwisho atakayebatilishwa
ni mauti.”
Sasa tuangalie aina
nne za vitabu kama ilivyoandikwa katika Biblia na makusudi ya kuandikwa kwa
vitabu hivyo:-
1. KITABU CHA UZIMA
UFUNUO 3:5 Imeandikwa “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe,
wala sitalifuta kamwe jina lake kaika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina
lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”
Tunajifunza kuwa, kabla
ya kuombewa kwa lolote, shindana kwanza. Unashindana kimwili lakini matokeo ya
mashinda haya ushindi unatokea rohoni,
ndiyo maana katika WAEFESO 6:12. imeandikwa “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu
ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”
Ukishindana na Kushinda, Bwana Yesu amekiri
kuwa atalikiri jina lako mbele za Baba yake wa mbinguni. Shetani hawezi kushuka
na kujitaja, “mimi ndiye bwana shetani”.
Atakachofanya shetani ni kuwatumia ndugu
au watu
wa nyumbani kwako kama
ilivyoandikwa katika MATHAYO 10:36. “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.”
Watu hawa ndiyo
watakuwa kikwazo kwako, kukushawishi usiende kanisani au usitoe sadaka na fungu
la kumi. Lengo la ndugu zako hawa wa
karibu ni kukufanya utende dhambi na mwishowe MUNGU alifute Jina lako katika
kitabu cha Uzima.
Ng’ang’ana
ili jina lako lisikosekane katika kitabu
cha Uzima, kama ilivyoandikwa katika UFUNUO
13:8 “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake
halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha MwanaKondoo, aliyechinjwa tangu
kuwekwa misingi ya dunia.”.
2. KITABU CHA
MEMA:
Tusomapo katika
YEREMIA 51:60 “ Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote
yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.”. Endapo Yeremia aliandika ndani ya kitabu cha habari ya mabaya, basi ujue kuwa kitabu cha kuandika habari ya
mambo mema nacho pia kipo.
Na pia katika YEREMIA 45:1 imeandikwa “Neno
hili ndilo ambalo Yeremia, nabii, alimwambia Baruku, mwana wa Neria,
alipoyaandika maneno haya katika kitabu kwa kinywa cha Yeremia, mwaka wa nne wa
Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema..,”.
3. KITABU CHA
TAARIFA AU CHA KUMBUKUMBU.
Imeandikwa katika ESTA 2:23 “Na jambo hilo lilipochunguzwa, na
hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia
yakaandikwa katika kitabu cha taarifa mbele ya mfalme.”.
Lengo la kuyaandika
matukio haya katika kitabu cha taarifa ni ili vizazi vijavyo viwe na kumbukumbu
ya mambo hayo. Leo lazima tufute kumbukumbu za uovu zilizoandikwa dhidi yetu
kwa Jina la YESU.
Uonapo koo za watu fulani zikiwa na matukio ya watu kujinyonga, au vifo vya kufanana ujue kuwa zipo kumbukumbu
za uovu uliofanyika kipindi fulani nyuma
zinafuatilia koo hizo. Zipo koo za watu ambazo watu wa familia hiyo wanakufa
kwa kansa, au ajali za barabaani na wengine wa familia hiyo hiyo kufa kwa
pamoja!!
Leo amua kukataa kumbukumbu za ukoo
kukufuatilia kwa Jina la Yesu.
Kuna watu
walioandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu, na pengine maisha ya ndoa yakaanza
kuyumba na mifarakano kutokea.
Lakini kila wakati mtu wa aina hii akiwa karibu na mume wake, atalalamika kuwa
alikosea kuolewa naye. Cha ajabu mumewe akiwa mbali, mtu wa aina hii atatamani kumuona na kukaa naye. Baadhi
ya koo zenye mitambiko hata kama umeokoka, watakusihi siyo lazima kushiriki ila utume pesa tu na wao
wataendelea.
Kile usichokijua ni kuwa, hizo pesa ulizotuma
zinakuwa zinakuwakilisha katika yote wanayofanya na mashetani yao. Baadhi ya
koo pia ukitokea msiba wao hunyoa nywele. Kitendo hiki huwajumuisha wanaukoo
katika vitabu vya kumbukumbu na mikosi.
Leo kataa kila
maagano uliyofanya kupitia nywele au
vitambaa vya sanda kwa Jina la Yesu.
Kuna watu pengine
waliwahi kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Kwa kawaida, waganga hawa huyaandika majina katika vitabu vyao. Hata kama
utakataa, tayari majina yako yapo kwa waganga leo hii. Wengine waliacha alama za damu zao kwa waganga wa kienyeji baada ya kukubali
kuchanjwa chale.
UKIRI!!!
Leo ninakataa mizimu
yoyote inayonifuatilia, katika Jina la YESU, maana imeandikwa katika YAKOBO
4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”, shetani
uliyekaribishwa na Baba yangu au shangazi yangu, leo nakukataaa kwa Jina la YESU.
|
4. KITABU CHA
UKOO
Katika MWANZO
5:1 imeandikwa “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu,
kwa sura ya Mungu alimfanya;” Kwamba Adamu alikuwa na Kitabu cha Uzazi wake.
Kwamba ukitaka taarifa za ukoo wa Adamu lazima
ukitafute kitabu cha Ukoo wa Adamu. MWANZO
10:1 “Hivi ndivyo vizazi vya wana wa Nuhu, Shemu, na Hamu, na Yafethi. Na
kwao walizaliwa wana wa kiume baada ya gharika.”.
Pia katika MWANZO 9:1-2 imeandikwa “Mungu
akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. 2.
Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa
angani: pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa
baharini; vimetiwa mikononi mwenu.”.
Baba
anapobarikiwa, baraka hizi hufuatana pia na watoto wake, vivyo hivo hata kwa
upande wa laana ikiwepo, ujue kuwa laana hiyo itafuatia watoto pia. Hata Yesu
naye pamoja na kuwa ni MUNGU, alikuwa amendikwa katika Kitabu cha Ukoo .
NEHEMIA 7:5 Imeandikwa, ”Mungu wangu akanitia moyoni
mwangu, kwamba niwakusanye wakuu na mashehe, na watu, ili wahesabiwe kwa
nasaba. Nikakiona kitabu cha vizazi vya
hao waliokwea hapo kwanza, nikaona ya kwamba imeandikwa humo;” Kuna
wengine wamo kwenye vitabu ili wapotezwe. Kuna majina au watu wameandikiwa
kuonewa, kuibiwa au kutaabika, na hayo yamo kwenye vitabu vya vizazi.
KUYAFUTA NILIYOANDIKIWA
NA SHETANI KATIKA KITABU
Je, unaishi yale
ambayo MUNGU alikuandikia uyaishi? Kumbuka kuwa MUNGU hataki kumtesa mwanadamu,
kama ilivyoandikwa MAOMBOLEZO 3:33. “Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu.
Wala kuwahuzunisha.” Ni budi kukataa kuishi masisha yasiyo sawa na kile
alichokuandikia Mungu. Unapaswa kuyafuta maandiko ya mashetani na kuanza kuishi
sawasawa na kile alichokuandikia Mungu.
Kazi alizokuja
kufanya Yesu hapa dunniani pia zilikuwa zimeandikwa, hata kabla ya kuzaliwa
kwake. Katika kitabu cha Nabii ISAYA 61:1
imeandikwa “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta
niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika
moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa
kwao.”. Na pia katika MATHAYO
26:24 imeandikwa “Mwana wa Adamu aenda zake, kama
alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu!
Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.”. Tunajifunza kuwa,
maisha ya watu yanakuwa yameandikwa katika vitabu, na itategemea ni kitabu kipi
jina lako limeandikwa humo.
Simeoni alikuwa
naye ameahidiwa jambo fulani, na baada ya kumbariki Yesu, alienda kulala. Imeandikwa
LUKA
2:34 “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu
amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara
itakayonenewa.”. Tunajifunza kuwa kuna watu ambao Mungu amewaweka kwa
ajili ya kuinuka na kuanguka kwa wengine. Kumbe kuna umuhimu wa
kuziepuka roho za mazoea. Wayahudi hawamuamini YESU, wakidhani ni sawa tu na
kaka yao.
Watu wengine wanamuons
Mchungaji kiongozi wao na kumfanya wa kawaida kawaida tu, na matokeo yake
watu wa aina hii hawabarikiwi. Utii
unaweza kumfanya mtu kufika mbali. Shetani
kilichomfanya afutwe kwenye kile kitabu
cha uzima ni kiburi chake. Biblia inasema watiini wazazi wako katika Bwana. Inamaanisha
kuwa, mchungaji kiongozi wako ni Baba yako wa kiroho, hivyo ukimtii unabarikiwa
na usipomtii kile anachokuagiza unaweza
kuanguka vile vile. Vivyo hivyo, wazazi wako wa kimwili nao vilevile ni
budi kuwatii na kuwapa mahitaji yao, hata kama ni wanga /wachawi ili uweze
kubarikiwa. Usiwalaumu kwa kuwa ni wachawi au wanga, kwa sababu imeandikwa “Kama
shomoro katika kutangatanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake;
Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.” (MITHALI 26:2.).
UKIRI!!!
Ninakataa jina
langu kuandikwa katika kitabu cha laana na mikosi. Damu ya Yesu inifunike kwa Jina la Yesu.
Amen
|
Katika MWANZO 15:13-14 imeandikwa “Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. 14 Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.” Inawezekana hata wewe upo bado utumwani, lakini yupo baba (Mchungaji Kiongozi) aliyepewa silaha za kukuvusha tena kwa Jina la Yesu.
Imeandikwa pia
katika KUTOKA 14:15-19 “Bwana
akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee
mbele. 16 Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na
kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. 17
Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na
kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa
magari yake na kwa wapanda farasi wake. 18 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi
ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na
farasi zake. 19 Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la
Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo
mbele yao, ikasimama nyuma yao”.
Katika KUTOKA 14:24-23 imeandikwa “Ikawa
katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo
ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. 25 Akayaondoa magurudumu
ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele
ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri.”. Kumbe
Mungu huwa anachungulia adui zetu. Kilichowaponza Wamisri ni kuwa nao walidhani
Mungu amewaandika katika Kitabu chake.
Kuna mtu ambaye
hujawahi kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi, binafsi katika maisha yako, hata kama unaenda kanisani lakini
hujamkiri Yesu ujue leo ni siku muhimu
kufanya maamuzi ya kuokoka sasa, kwa kuwa imeandikwa “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa
sana, akiomba kwa bidii.” (YAKOBO
5:16). Ni vyema leo uokoke kwanza
ili kuomba kwako kwa bidii kukubalike
mbele za MUNGU katika Jina la YESU.
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/