Monday, August 28, 2017

PETER MANENO ARUDISHWA TOKA SHIMO LA KUZIMU


USHUHUDA

JUMAPILI 27 AUGUST 2017

YESU ANAWEZA,KUFANYA MAMBO MAKUBWA, HATA MILANGO YA KUZIMU IFUNGUKE HAITALISHINDA KANISA LA MUNGU DUNIANI

Peter - Kulia akishuhudia alivyoteswa huko kuzimu.
Kushoto ni Mch. Dr.Godson Issa Zacharia akimhoji Peter.
Peter Maneno alizaliwa kwa wazazi wake. Anasema  kwa sasa nina miaka 18, na nilikuwa ni Mkristo, lakini nilibadili dini mwaka 2008 na kuitwa Ramadhani. Peter akieleza mbele ya ibada ya jumapili katika kanisa la ufufuo na uzima, linaloongozwa na Mch. Dr.Godson Issa Zacharia, lililoko maeneo ya mkundi minara mitatu, anaeleza na kusema nilipokuwa mdogo shangazi yangu (jina nalihifadhi) alikuja nyumbani  na kuomba wazazi wangu nikakae naye nikiwa bado shule ya chekechea ili kunianzishia Shule ya Msingi huko Chamwino, Morogoro. Wazazi walimkubalia shangazi akanichukua, ndipo siku moja  wakati wa chakula cha usiku akatokea mfanyabiashara mmoja wa asili ya kichaga aliyefika kwa shangazi na kutaka mtu  wa kumsaidia kuita wateja kwenye duka lake la biashara.  Shangazi  akasema nina “kikuku changu kidogo kidogo”(akimaanisha mimi ndio kikuku kadogo),akamuuliza yule mfanyabiashara je atatoa  Shilingi  ngapi!!? Yule mtu akasema nitatoa nyumba na gari. Shangazi  akasema hivyo  vitu havitoshi kwa sababu haka ‘’kakuku’’ kana mizimu. Yule  mfanyabiashara akaondoka na kusema nitarudi nitakupa jibu kesho.

Usiku  huo huo nilipokuwa nimelala lakini macho yangu yakiwa sijayafunga, nikashitukia kuwaona watu wengi wakiwa pale chumba nilichokuwa nimelala wakiwa wanaongea kwa lugha zao,  na kulikuwa na kioo na mshumaa mbele yao. Kwenye  kile  kioo kukatokea mtu, shangazi na watu aliokuwa nao wakawa wanahojiana naye na huyo mtu, yule mtu akasema siyo rahisi haka kakuku(yaani mimi) kuuzwa, kaachwe hadi kakue, na kwa sababu analo agano  alilowekewa tokea miezi mitatu akiwa tumboni mwa mamaye pia aliwekewa muhuri. Wakati hayo yanatokea, mimi  ufahamu wangu ulifungwa, kwani shangazi aliniwekea kitu kama unga kichwani ili kupumbaza akili zangu na hivyo  nilikuwa siwezi  kufanya lolote, na pia ili nisiweze kukumbuka tukio hilo wala sikuweza kumwambia  mtu yeyote.

Kipindi nikiwa darasa la tatu shangazi alinianzishia biashara ya kuuza karanga mitaani huko Chamwino badala ya kunipeleka shule kusoma. Nikawa nazurura mitaani na shule  nikawa nimeacha. Baadae baba yangu akaja kunichukua kukaa nami maeneo ya Kihonda Morogoro. Akiendelea kueleza Peter anasema, siku moja nilianguka mtini na kudondokewa na tunda la mwarobaini kwenye  jicho na pia nilivunjika mkono. Nililazwa hospitalini na baada ya kupona kipindi hicho akaja shangazi mwingine anayekaa Kilosa akaomba nikakae naye ili anipeleke shule darasa la nne. Hata hivyo,akili zangu kwa kuwa zilikuwa zimeshachukuliwa sikuwa nafanya vizuri darasani.


Watu waliokuwa wakisikiliza kwa makini ushuhuda wa Peter katika ibada ya Jumapili.
Nikiwa darasa la sita kuna dawa walinifanyia, mwili wangu ukabaki kilosa kwa shangazi, na roho yangu ikaletwa Morogoro, ikavaa mwili mwingine na ndio ilkuwa ikifanya biashara na shangazi mikoa mbali mbali lakini makao  makuu yakiwa Musoma. Kule Kilosa aliyekuwa anasoma ni mtu tofauti mimi mwenyewe. Nikiwa darasa la saba nilimaliza masomo na kurudi  Morogoro. Hii ilikuwa hila ya shangazi ili wazazi wasijue kinachoendelea, na papo  hapo baba yangu mzazi alirushiwa jini mahaba akawa hatulii nyumbani ili asipate muda wa kutunza watoto wake watano nikiwepo mimi mwenyewe, na kumfanya shangazi kupata fursa ya kunitumikisha.

Peter anaendelea kusema,baada ya hapo nilipangiwa ratiba ya kuwa Siku za Jumanne, Alhamisi  na Jumamosi nilikuwa  nikipewa shilingi moja yenye mwenge ambayo nikiiweka barabarani basi la abiria/daladala, likipita eneo hilo linasimama, kisha abiria wanatolewa na wanashushwa chini wote, na ndani ya basi wanajaza wadudu, wanyama, mijusi,  n.k  na kuwabadilisha kuwa kama wanadamu. Baadae Upepo wa ghafla utatokea na kulipuliza hilo basi la abiria, ambapo litaanguka na baadae watu  wengi wataonekana wamekufa. Wakitambuliwa watazikwa, na wale  walioshushwa chini  wanachukuliwa wakiwa wazima hadi kwenye jumba la huko Musoma (Mkoani Mara) kutolewa kafara.

 Shangazi aliniuza mimi huko  Musoma tokea mwaka 2005, ambapo kuna jumba kubwa sana ambalo sikuweza kulitembelea hadi mwisho maana ni kubwa, niliweza kutembelea vyumba viwili tu kwa muda wote niliokaa huko. Ndani  ya hilo  jumba kubwa wapo watu wa rangi zote, na  makabila yote wengi sana  na hawahesabiki. Na watu walikuwa wanaletwa kila siku katika jumba hilo.

Peter akiwa akisimulia mbele ya maelfu ya watu wa ufufuo na uzima Morogoro anasema, nilikuwa katika kitengo cha  kusababisha ajali, mimi nilikuwa sili pumba kama misukule wengine walivyokuwa wakila. Yupo msimamizi wa jumba, pia niliwaona hata baadhi ya wachungaji (wa makanisa fulani) walikuwa wanaletwa mle ndani  kupewa mafuta ya kuongeza nguvu. Haya ni mafuta ambayo hata waganga wa kienyeji  huyatumia ili kuongeza nguvu. Kitengo cha pili nilichowekwa mimi ni cha kuchukua watoto wachanaga wanaozaliwa mahosipitalini.

Hao watoto wachanga huchemshwa ili kutoa mafuta yanayotumiwa na waganga wa kienyeji, wachawi kwa ajili ya kujipaka katika paji  la uso na kifuani. Kinachofanyika madactari wa zamu wanalazwa usingizi wanapokuwa kazini, kisha madactari wa kuzimu  wanavaa sura za madactari halisi na kutumia nguvu za kugeuza macho ya watu na  kuwaona kama wao ndiyo  madaktari. Huingia mle ndani ya wodi na kumchukua mtoto anayezaliwa.

Peter anasema lile bakuli la  kuzalishia, wanalichukua  pamoja na mtoto aliyezaliwa na kumbadilisha na kuweka mdoli, huyo  mdoli wanampulizia pumzi ya mkataba wa muda Fulani wa kuwa hai, na kumkabidhi mama mzazi wa mtoto. Mtoto huyo(mdoli) aliyepuliziwa pumzi ataishi kwa muda kulingana na mkataba wa pumzi aliyopuliziwa, labda ya mwezi mmoja, au sita au mwaka mmoja, baada ya  muda huo mtoto huyo ataugua na atafariki. (lakini kimsingi  kinachofanyika ni kurudisha mdoli wao  pale walipomtoa ili  aje kutumika tena).  

Anasema watoto hawa wachanga waliochukliwa mahospitalini huchemshwa  wangali hai na kuyakinga mafuta yanayotoka miilini  mwao baada ya kuchemka sana. Waganga wa kienyeji na baadhi ya matajiri na (hata  wachungaji fulani fulani) ndiyo huenda kuchukua  mafuta hayo ambayo huwekwa katika vichupa vidogo vidogo ili kujipatia nguvu  za giza za kufanya mambo yao  yawe yamenyooka. Peter anasema mafuta hayo hayauzwi, ila kwa mtu anaetaka mafuta hayo anatakiwa alete mtu, ili kubadilishana na mafuta hayo. Yaani ni biashara yakutoa mtu, halafu unapewa mafuta.


Peter akisimulia alivyotoka kuzimu na jinsi atakavyo mtumikia Yesu aliyemtoa katika mateso.
JE PETER  ALITOKA JE HUKO MASHIMONI?
Anasema ninachokumbuka ni kwamba siku moja ya Alhamisi nilipewa ofa ya mapumziko katika jumba kubwa la Musoma. Mkubwa wetu alikuja na kusema ole wa mtu  yeyote atakayetoroka siku hii ya leo. Huyo mkubwa huwajia kama mtu lakini anayo mapembe makubwa sana kichwani, siku hiyo kipande cha zege juu ya kichwa chake kikawa kimemeguka,” kipande kidogo” pakaonekana kuna katobo, mwanga mkali  sana uliingia ndani kupitia kile kitobo(tundu). Miongoni mwao watu watano waliokuwepo katika kile chumba waliweza kuangalia ule mwanga, lakini misukule wengine wakageuza nyuso zao wasitazame ule mwanga maana ulikuwa mkali sana.

Peter anaendelea kusame, baadae sauti ilitoka kupitia kile kitobo(kitundu) ikisema “NAWAKABIDHI  PANGA FANYA VURUGU, NJOO, NJOO, NJOO!!!”. Peter anasema wakubwa wao walijua ile sauti ‘’ilikotoka’’, lakini mimi na wenzangu hatukujua chochote. FUJO KUBWA ILIANZA NA KISHA NIKATOROKA. Hata hivyo kule ndani tulijuana kwa namba na siyo kwa majina (Mimi nakumbuka namba yangu ilikuwa ni 105 F) ila sikumbuki kama wenzangu watano ‘’walitorokea wapi’’!!. kwa sasa mimi Peter niliyeitwa Ramadhani zamani  nimeamua kuokoka, yaani nampa YESU maisha yangu na ninaahidi kuwa nitamng’ang’ania Yesu Kristo maishani mwangu,na kamwe sitamuacha kwa sababu  nimetoka kwenye  mateso yasiyovumilika.

Mungu anatenda mambo makubwa katika kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro, lililoko maeneo ya mkundi minara mitatu. Yesu anakupenda na hapendi uteseke, imeandikwa Mungu hapendi kuwatesa wanadamu wala kuwahuzunisha. Huu sio wakati wa kukaa na mateso amua leo njoo kanisani Ufufuo na Uzima, shida yako itatatuliwa. Pia unaweza kwenda kanisa lolote la Ufufuo na Uzima maeneo ya hapo ulipo, na Mungu atakusaidia. Karibu sana.

.......................... information ministry morogoro..............................................




Share:
Powered by Blogger.

Pages