GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA ---> MOROGORO}
JUMAPILI: 27 AUGUST
2017
MHUBIRI: PASTOR GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Mchungaji Kiongozi akifundisha neno la Mungu katika ibada ya leo. |
Tunaposoma katika YEREMIA 1:8-10 neno la Mungu linasema
hivi “Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema
Bwana. 9 Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana
akaniambia, Tazama, nimetia maneno
yangu kinywani mwako; 10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme,
ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu,
na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”. Kusudi la Mungu kutuweka
hapa duniani ni ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu,
na kuangamiza. Kumbe ipo pia minyororo iliyopo katikati ya
maisha yako ambayo kwa wewe uliyeokoka unapaswa kuing'oa, na kuibomoa,
na kuiharibu, na kuiangamiza. Minyororo hii ni ile ya rohoni. Minyororo ya
rohoni ndiyo inayomfanya mtu kuwa mtumwa, kwamba hana uhuru tena wa kujiamulia
mambo yake mwenyewe. Unafungwa rohoni lakini madhara yanathibitika mwilini. Tunajifunza
kuwa mtu anaweza kufungwa na minyororo ya rohoni na ambayo kwa bahatimbaya huwa
haionekani katika macho ya nyama.
Kwa kawaida
minyororo ni kitu kama kamba ambazo ni za chuma, na siyo rahisi kuvunjwa. Lengo la kutumia minyororo ni ili kumfanya mtu
asiweze kufurukuta, kwa sababu ukitaka kujifungua kwa nguvu itakukuumiza.
Katika ZABURI 105:17-18 imeandikwa
hivi “Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani. 18 Walimwumiza miguu
yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.” Kwa hiyo hata
Yusufu alifanyiwa mambo hayo, akafungwa na pingu na minyororo miguuni mwake. Na
tukumbuke wale waliomfunga Yusufu walikuwa ndugu zake, na wala siyo watu wa
mbali.
Tunasoma pia
katika ZABURI 149:8 “Wawafunge
wafalme wao kwa minyororo, Na wakuu wao kwa pingu za chuma.”. Kwa wewe
uliyeokoka ni mfalme, na kuna uwezekano
kuwa kuna waliofunga maisha yakjo kwa minororo ili usiweze kupiga hatua
za maendeleo maishani mwako. Ingawa minyororo hii haionekani kwa macho ya
mwilini, ukifungwa unakuwa mtu usiyeweza kufanya lolote utakalo maishani mwako
(inacapacitated). Mwishowe unakuwa na maisha ya kusema “mimi ziwezi kuzaa, siwezi tena kula nyama, siruhusiwi kula vyakula
vyenye sukari, siwezi kufanikiwa n.k”. swali la kujiuliiza hapa ni: hivi
kwa nini hao madaktari wa kukuzuia kula
nyama wasikuzuie usile matembele? Shetani kwa kuwa ni roho, huwaingia watu na
kufanya wasababishe hiyo minyororo ya utumwa iwafunge watu wengine. Shetani huyu
huwafunga watu ili wasiondoke kabisa katika utumwa huo kama ilivyoandikwa
katika ISAYA 14:17 “Aliyeufanya
ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?”
Hata hivyo ipo habari njema leo kwako, kwa kuwa imeandikwa katika YEREMIA 40:4 kusema “Na
sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona
ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini
kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote
i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko.”
Mnyororo ukifunguliwa unatakiwa uondoke mara moja, siyo kubaki unashangaa
shangaa tu. Leo Bwana Yesu anataka kuwachilia watu huru ili waende zao kwa Jina
la Yesu.
Platform wakimsifu Mungu katika Ibada ya leo. |
Yesu akisema kitu
na wewe ukikiamini kitakuwa chako. Imeandikwa katika MARKO 11:1-6 “Hata walipokaribia
Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni,
aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, 2 akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji
kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwanapunda
amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. 3 Na mtu akiwaambia,
Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. 4
Wakaenda zao, wakamwona mwanapunda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu,
wakamfungua. 5 Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini
kumfungua mwanapunda? 6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.”.
Tunaona kuwa hawa wanafunzi waliamini kile alichosema Yesu, na walifuata njia
na kumkuta mwana punda akiwa amefungwa. Kuna watu hupenda kufanyiwa muujiza
kwanza ili baadae waweze kuamini. Hiyo siyo sahihi!!!. Ni wangapi leo
wamefungwa na minyororo ya kishetani? Wapo waliofungwa midomo yao ili wasiweze
kufuata wachumba wao na kuwachumbia.
Wapo pia waliofungwa midomo yao ili wasiweze kuongea na wateja ili kufanya
biashara. Vitu vilivyofungwa na minyororo havihitaji ruhusa ya kuvifungua.
Aliyefungwa na akawepo mtu wa kufungua ujue tayari huo ni msaada kwako. Yamkini
kazi au ndoa yako ipo mahali fulani na inahitaji mtu wa kuja kuifungua. Leo
tutafuata mahali hapo ambapo kazi au ndoa
yako imefungiwa na kusababisha ushindwe kupiga hatua kama familia.
Kumbe ni lazima
awepo mtu aliyefunga na wakitokea watu wa kufungua ndipo mashindano huanzia
hapo. Wale wanafunzi walipomfikia yule mwanapunda waliwakuta watu waliomfunga
na ndio waliowaliza maswali ya kwa nini wanamfungua huyo mwanapunda. Hawa
huitwa walinzi wa rohoni. Leo tunafuatilia minyororo iliyofunga maisha yako,
mahali popote ilipo. Tutaiendea minyororo iliyomfunga mtu kwa kansa, minyororo
ya uzinzi, utasa, ububu n.k. na tutavunjilia mbali kwa Jina la Yesu. Leo Bwana
Yesu ametupa neema ya kwenda popote ulipofungiwa na kuwafuata walinzi
wanaosimamia taabu yako na kuwaaambia “BWANA
ANA HAJA NAWE”. Katika LUKA 19:33-34
imeandikwa hivi “Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona
mnamfungua mwanapunda? 34 Wakasema, Bwana ana haja naye.” Wapo adui
zako waliokufunga na endapo wa mtu wa kukufungua atatokea ndiyo hao hao
watajitokeza na kuanza kuuliza maswali ya “kwa nini mnamfugua mtu huyu!!” Wenye
kufunga na walinzi wao ndiyo huuliza maswali kama haya: “Mbona umeanza kufanya kazi? Mbona umeanza kuzaa? Mbona umeolewa? Mbona unafanya
biashara?
Zipo baraka tele ambazo
Mungu alishaziweka mbele yako hata kabla hujazaliwa. Yamkini ulipaswa uwe
mbunge mahali fulani lakini kwa kuwa umefungwa na minyororo umebakia jinsi
ulivyo hadi sasa. Kwa kawaida, mtu aliyefungwa
kwa minyororo akitaka kufurukuta minyororo hiyo humuumiza. Ndiyo maana baadhi
ya watu wanapoombewa makanisani, huanza
kusema “baada ya kuombewa ile shida yangu
nikama vile imeongezeka”. Cha kufanya ni kukaa kanisani na kujifunza zaidi namna
ya kupambana kiroho. Mashetani lazima yaambiwe ukweli, kuwa Bwana ana haja
nawe. Kuna aliyekufunga mnyororo kwamba “Usianze
kazi/ Usisome/ Usiolewe/ Usifanikiwe”. Mbaya zaidi, waliokufunga minyororo hawapo
mbali, ni watu wa karibu. Ndiyo wale wanaokuzuia wewe usiende kanisani, na hasa
wanafanya vita nawe kwamba usikanyage Kanisa la Ufufuo na Uzima. Watakuruhusu
uende makanisa mengine kwa sababu wanajua fika kuwa ukija Ufufuo na Uzima,
ukianza kupiga majeshi ile minyororo waliyokufunga itaachia!!!
Maelfu ya wana wa Ufufuo na Uzima wakijifunza somo la Kuivunja Minyororo ya Utumwa |
UKIRI
Ewe mnyororo
nakuvunja kwa Jina la Yesu. Minyororo
yote iliyosimama mbele zako tunailegeza kwa Jina la Yesu. Aliyesema usianze
kazi akuone ukianza kazi kwa Jina la Yesu. Amen
|
Leo tutafanya vita
vya rohoni na kumshinda shetani na malaika zake, kama vile ilivyoandikwa katika
2WAKORINTHO 10:3-6 (Maana
ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana
silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha
ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya
elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; 6 tena
tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.). Kama
silaha zetu zina uwezo wa kuangusha ngome, ujue kuwa ndani ya ngome kuna ndoa
zimefungiwa humo, kuna biashara zimefungiwa ndani ya ngome, kuna kazi
zimefungiwa ngomeni n.k. Bwana anasema kuwa “sisi ni silaha za Bwana za vita”.
Ili ushinde unapaswa kuvaa SILAHA
ZOTE za Bwana. Kumbuka kuwa tunazitumia Silaha Zote, siyo silaha moja au
mbili tu.
mtu huyu akifunguliwa kutoka Minyororo ya Utumwa |
UKIRI
Imeandikwa
katika YEREMIA 40:4 “Na
sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama
ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana;
lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama,
nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko”.
Kuanzia sasa nataka nifuate yale Yesu aliyosema, kuwa ana haja na mimi. Ingawa nilifungwa minyororo, mimi na familia
yangu, mimi na kazi yangu, kuanzia sasa ewe mnyororo uliokaa kwenye kazi,
miguu, ewe mnyororo uliokaa kwenye akili yangu, leo kwa Jina la Yesu nakataa
kubaki kwenye kifungo hicho kwa Jina la Yesu. Aliyenifunga na anayenilinda
ili nikae kwenye kifungo hicho leo namfyeka kwa Jina la Yesu. Leo nakataa
kubaki kwenye kifungo. Ewe kifungo cha kansa, ewe kifungo cha umaskini leo
fyekwa kwa Jina la Yesu. Naamuru mashetani wote mliokaa kama kifungo achia
maisha yangu kwa Jina la Yesu Kristo.
Amen
|
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro
http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/