Monday, November 10, 2014

KAFARA YA MADHABAHU-Na: ADRIANO MAKAZI (RP).

JUMAPILI: 09 NOVEMBER 2014 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO


Mtoto Kelvin akiwekwa wakfu tarehe 09/11/2014, na RP
Adriano, mbele ya mama yake Clara Kautipe (kushoto) na MP
wa Watoto Rehema Amos (katikati) Bonde la Maono. Huyu
ni mtoto wa kwanza kuwekwa wakfu katika Bonde la Maono.


Utangulizi: Somo la leo linaitwa Kafara ya Madhabahu”. Kafara ni sadaka ya kuteketezwa waliyoagizwa wana wa Israeli na Bwana kwa ajili  ya kufanya upatanisho, wakichukua kondoo, njiwa au ndama. Jambo hili shetani naye ameliigiza kwa kuwatumia wachawi na waganga wa kienyeji ili kufanya kafara. Zamani watu walikuwa wakitoa sadaka za aina hii aidha kwa Mungu au kwa mashetani. Madhabahu kwa hiyo, ni kiunganishi kati ya ulimwengu wa  mwili na ulimwengu  wa roho.





RP Adriano akihubiri somo "Kafara ya Madhabahu"
Jumapili ya tarehe 09/11/2014 Bonde la Maono - Morogoro.
WALAWI 17:7….[Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.  ]… Jambo hili la majini  kufanya uzinzi na wanadamu lilimuudhi sana Mungu  na ndiyo maana akazuia lisiwepo tena.


KUMBUKUMBU 32:17…[Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa.]….Kumbe wachawi wanapotoa sadaka zao, hawazitoi kwa Jehovah, Mungu tunayemwabudu. Huzitia sadaka hizo kwa majini ili yawatie nguvu ya kufanya uharibifu kwa wanadamu wenzao.


ZABURI 106:37…[Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.]….Jamii hii ilikuwa na kawaida ya  kuwatoa watoto wao kwa mashetani. Kila mtu husimama kwa kutumia nguvu ya madhabahu iliyoko nyuma yake. Mchungaji anatiwa nguvu na madhabahu ya Jehovah, wakati ambapo wachawi nao hutiwa nguvu na madhabahu ya mashetani.


Kuhani wa madhabahu husimama kati  ya wanadmu na Mungu,  kwa kupokea shida na matatizo ya wanadamu na kuyapeleka kwa Bwana. Watu wanapokuja mbele za Bwana, lengo ni kupokea majibu ya shida zao, na siyo kwenda kuombewa na makuhani. Hana alichokozwa sana na Penina kwa habari ya kukosa watoto. Alichokifanya Hana ni kwenda mbele za Bwana huko Shilo na kujimimina mbele za Bwana ili kupokea mtoto, na Bwana akamjibu kwa kumpatia mzaliwa wake wa kwanza aitwae Samweli.


MAOMBI:
Kwa jina la Yesu, asubuhi hii ya leo ni asubuhi ya kuwashughulikia walionichokoza. Kwa Jina la  Yesu, Amen.



Watu wa kale kabla ya  kufanya jambo lolote waliijenga madhabahu kwanza kisha wakazitoa kafara.


MWANZO 12:7…[Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.]… Kumbe madhabahu hujengwa mahali ambapo ni pako, na kwamba ukeshaijenga ni mahali pako kwa ajili ya kutolea sadaka…MWANZO 13:17…[Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo. 18 Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea Bwana madhabahu huko.]… Kumbe hapa tunajifunza kuwa, Mtu yeyote kabla ya kufanya jambo lolote, ni muhimu kuijenga madhabahu.


WAAMUZI 6:22-24 …[Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso. 23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. 24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, YehovaShalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.]… Watu wa kale walipoijenga madhabahu waliipa madhabahu ‘jina’ pia. Wamidiani wa siku za leo ni wale wote wanaoharibu kila kitu kizuri ulichokusudia. Leo hii  lazima tuwachakaze watu wa aina hiyo kwa Jina la Yesu. Wale wote wanaokosesha amani ndoa yako, au wanaokosesha amani kazi yako, n.k tunahitaji amani ipatikane hapo kwa Jina la Yesu. Ulimwengu waweza kutoa amani,  lakini amani ya Bwana Yesu ni tofauti sana na aina zingine zote za amani. Katikati ya matatizo, watu wakuone unayo amani,  na watu wakitaka kuijua siri ya amani yako uwaambie ‘ninaye Bwana wa Amani’


WAAMUZI 6:25-26...[Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.]….Kwenye familia ya akina Gideoni, baba yake alikuwa na madhabahu lakini  haikuwa ya Bwana, bali ya Baali. Madhabahu hii ya familia ya Gideoni, ndiyo ilimfanya Gideoni ajione ‘mnyonge’,  wakati mbinguni wanamjua yeye ni ‘shujaa’. Wapo watu wengine katika familia nyingine hata leo  hii kila wapatapo fedha za mshahara, matatizo ya kuhitaji fedha hujitokeza ili  kwamba pesa yao isifanye jambo lolote la maendeleo. Kwenye ulimwengu wa roho watu wa kusababisha aina hii ya matatizo wapo na ambao hufanya hayo matatizo yakusonge ili usiendelee. Kumbe katika ujenzi wa madhabahu, kuna taratibu zake, ili  iweze kuwa imara na yenye nguvu.


Baada ya Gideoni  kuijenga madhabahu ya ‘Jehovah Shalom’,  Bwana alimwambia sasa ili upate ushindi kamili,  ni  lzima ukaibomoe ile ‘madhabahu ya Baali’. Maana yake ni kuwa,  ‘huwezi kuwa na madhabahu mbili kwa wakati mmoja’. Huwezi kuwa mzinzi,  huku umeokoka.  Huwezi kuwa na Yesu,  huku unamfuata sangoma akutabirie. Huwezi kuwa na boy friend / au girl friend na huku unataka Mungu akubariki ili kuwa na ndoa njema. Kwa Mungu  hakuna michanganyo.


Baada ya Majeshi  ya Bwana kuijua siri ya "Kafara ya Madhabahu" hatimaye waliinua mikono yao  kwa furaha!!!


MAOMBI:
Kwa Jina la Yesu, Kama ipo madhabahu mahali ya kunifanya niwe mtu wa kushindwa; Kama ipo madhabahu mahali kunifanya niwe mgonjwa;  Kama ipo madhabahu mahali kunifanya niwe nisiwe na fedha,  naisambaratisha kwa Jina la Yesu. Na kila kuhani yeyote, makuhani majini, majoka, mapepo, mnaponyunyizia uvumba kunifanya nishindwe, nawateka nyara, makuhani wote, ninawachinja katika Jina la Yesu.  Amen.



Baba yak e Gideoni  alikuwa na madhabahu ya Baali. Inawezekana hata  wewe, ipo madhabahu aliyo nayo baba yako, au mjomba wako, au ndugu yako; na wanatoa sadaka kwa hiyo madhabahu ili kuvuvia matatizo kwako. Ndiyo maana matatizo ya ukoo wako  ni ya kufanafana. Kumbe madhabahu inaweza kujengwa na mtu binafsi. Wakati mwingine, madhabahu inakuwa kwenye begi la boss wako, siyo lazima iwe kubwa sana.  Kama moyo wa mtu haujatahiriwa, mambo ya kujichanganya yatakuwepo tu.


MWANZO 22:1-10…[Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. 3 Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. 4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. 5 Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. 6 Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. 7 Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? 8 Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. 9 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.]… Mungu alikuwa na nia nzuri tu ya kumwambia Ibrahimu maneno haya,  kwamba amtoe kafara mwanae wa pekee Isaka (ni mwana wa pekee kwa Sarai na Ibrahimu, kwa kuwa hakuwepo mwingine tena aliyezaliwa kati ya Sara na Ibrahimu). Kumbuka kuwa ‘Isaka alikuwa mfano wa Yesu Kristo’. Kitendo cha wachawi cha kutoa kafara watoto wao,  kilianzia hapa‼ Pengine mtu mwingine anagekutana na jambo kama hili angemwambia Bwana,  ‘acha mimtoe Ishamaeli’ kwa kuwa umemkataa.


MWANZO 22:11-12…[Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee ]…  hebu jiulize swali, hivi muda wote wa Ibrahimu kuwa na Bwana miaka yote toka aondoke Uru wa Wakaldayo,  je, Mungu hakujua kuwa Ibrahimu amcha Bwana!? Katika maamuzi magumu unapofanya kwa ajili ya Bwana, ndipo  Bwana anajua kuwa wewe ‘wamcha Bwana’. Wakati  wa dhiki, unapoona wapo wanaoendelea kukupenda,  ujue hao ni wa kweli, na wanakupenda kweli  kweli. Mungu hakuachi hata mara moja.


MAOMBI:
Kuanzia leo ninawaangamiaza wote walionizuiakwa Jina la Yesu. Amen



MWANZO 22:13-14 [Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire (Yehova-yire maana yake ni Bwana atapata), kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa Bwana itapatikana.]…. Madhabahu hii aliyoijenga Ibrahimu (Yehova-yire), ni  mfano  wa madhabhu aliyochinjwa Yesu, kama ilivyoandikwa katika YOHANA 3:16…[Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.]…. Yesu Kristo anafananishwa na mwanakondoo wa Mungu.


Mungu alimwambia Musa, kuwa baada ya Farao kukataa kuwaachilia kwa kipindi  chote hiki,  imebakia ishara moja tu ambayo ni wazaliwa wa kwanza wa Misri kuuawa.  Kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajaja duniani kipindi hicho,  wana wa Israeli waliagizwa kuchinja wanakondoo na kuweka damu ya kondoo hawa juuu ya miino ya nyumba zao ili  malaika atakapoakuja kuuwa wazaliwa wa kwanza wa Nchi ya Misri, wasiingie nyumba zozote zenye hii  damu.


Ni kitu gania kinatenda kazi kwenye madhabahu? Kimsingi kinachofanya kazi ni ile damu  ya madhabahu. Kwa nini damu  inafanya kazi? Ni kwa sababu damu ni ‘ishara ya ukombozi’. Yesu alitukomboa kupitia damu yake (Ya miguuni, mikononi, kichwani, mgongoni, ubavuni, Gethsemane) ni ukombozi kamili.


1 SAMWELI 30:7-8…[Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko. 8 Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.]…. Daudi  alikuwa na hakika kuwa akimuuliza Bwana kutokea madhabahuni, atapata kile anachoomba kwa Jina la Yesu.



RP Adriano akimuombea mmoja wa watu tarehe 09/11/2014

MAOMBI:
Leo nipate kwa Jina la Yesu.  leo nipate afya yangu, nipate sehemu inayoniangukia kwa Jina la Yesu. enyi mashetani,  majoka, mizumu mliotumwa ili kunizuia nisiapate,  leo nawapiga kwa Damu ya Yesu. enyi walinzi wa kichawi, mlionizuia, leo nawapiga kwa Jina la Yesu. nimeamriwa na Bwana nipate afya, kazi, kwa Jina la Yesu. Amen



Wapo watu wanaokuzuia usipate.  Ni vizuri ujue kitu gani kinachotenda kazi  katika madhabahu: kitu hicho ni DAMU. Mtu yeyote anapotaka  kuharibu maisha yako, ni kuchinja mnyama (kuku, mbuzi, njiwa,kondoo) katika madhabahu. Mganga wakienyeji hawezi kuagiza kuletewa samaki,  kwa sababu shida ya huyo mganga siyo nyama. Mnyama  huyu akeshachinjwa, damu humwagika. Damu hutolewa katika madhabahu kwa sababu ‘damu ni uhai’….. WALAWI 17:10-12..[Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. 12 Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.]… Kinachofanya mwili  uwe na uhai,ni damu. Damu ya mnyama huyu  ikeshamwagika, maana yake uhai wake unamwagika/unamtoka. Damu alikataza watu kunywa damu kwa sababu damu ndiyo yenye kufanya ‘upatanisho’.


MWANZO 4:10-11… [Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. 11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;]…. Unaona kuwa, damu inaweza kuachilia ‘laana’.  Kaini amelaaniwa kwa sababu ya damu ya ndugu yake Ahbili aliyoimwaga. Damu inweza kuongea,kutoa sauti au kulia. Yamkini upo huku mjini,lakini  kumbe kijijini kuna mtu alimwaga damu, nayo inaendela kulia ili kwamba ‘usifanikiwe,usijenge nyumba,  ufilisike, ufukuzwe kazi’.  Ni  lazima kuinyamazisha damu za ainahii kwa Jina la Yesu.

Showers of Glory wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiimba na kumchezea Bwana Yesu, tarehe 09/11/2014 Bonde la Maono. 

Kulingana na kafara iliyotolewa madhabahuni, tofauti kati ya madhabahu moja na nyingine huwa dhahiri. Katika madhabahu nyingine,  mtu alichinja kuku.  Mashetani  wanaokuja mahali kama hapa ni wa ngazi ndogo. Mwingine analogwa kwa kuwa kilichochinjwa ni mbuzi,  au mbuzi wanachinjwa kila mwezi. Madhabahu ya aina hii ni ya juu zaidi kulinganisha na ile ya kuku. Wengine wanatumia ng’ombe. Hata mashetani yanayokuja katika madhabahu hii, ni wa ngazi ya juu zaidi. Wengine hutumia hata kafara za wanadamu‼!  Pengine ndugu zao, abiria wa basi katika biashara zao n.k. wakeshafanya hivyo, biashara zao huongezeka.


EBRANIA 12:24…[na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.]… Taarifa nzuri nikuwa, hata sisi, tunayo kafara ya damu ya Yesu,  ambaye alifanyika kafara – tena isiyo na mawaa, wala dhambi kwa sababu Yesu hakutenda dhambi.


© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi, Mkundi-Morogoro.
 /or
Contact our Senior Pastor:
 Dr. Godson Issa Zacharia
 (Ufufuo Na Uzima – Morogoro)
Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778

Email: godson.issa@yahoo.co.uk
Share:
Powered by Blogger.

Pages