Sunday, February 18, 2018

KUKOMBOA MJI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
SNP DKT. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI: 18 FEBRUARI, 2018
MHUBIRI: MCHUNGAJI, DKT. GODSON ISSA ZACHARIA


Mchungaji Kiongozi Dkt Godson Issa Zacharia akifundisha ukombozi wa mji katika ibada ya leo.
Utangulizi: Mji ni sehemu ya makazi ya watu. Ni mahali ambapo wanadamu wanaendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato kila siku kwa ajili ya maisha yao. Mfano hapa Tanzania kuna mji wa Morogoro, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. Neno mji Kibiblia unajumuisha nchi, mkoa, wilaya, kata na hata familia unayoishi. Kufanikiwa kwa watu kunategemea pia mahali wanapoishi, wanachokiamini na wakimtegemea Mungu wanafanikiwa zaidi.

Walikuwako watu wanaoishi kwenye mji fulani ambao ulikuwa mzuri sana lakini maji ya mji huo yalikuwa yakizaa mapooza. maji hayo walipokuwa wakinywesha ng’ombe lazima wafe, ukimwagilia mazao yanakufa, wakinywa wanazulika. Watu hawa wakakutana na Nabii Elisha wakamwomba awasaidie juu ya jambo hilo.

“Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.” 2 Wafalme 2:19-21

Kuzaa mapooza ni sawa na kuharibu mimba. Kila unachotengeneza hakiwezi kufika hatima yake. Ni sawa na mwanamke ambaye kila akitunga mimba lazima iharibike. Hata hivyo jambo hili la kuzaa mapooza halijawai kumpendeza Mungu tunayemtumikia;

“Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.” Malaki 3:11

Kuzaa mapooza ni kupukutisha majani au matunda yake. Mfano unaweza kuwa na shamba lililomea vizuri na likawa linapukutisha matunda. Ni sawa na kuanza mradi ghafla unaharibika, unaanza shule humalizi huko ndiko kuzaa mapooza, lakini Mungu hapendi hata mara moja uharibikiwe yeye ameahidi ahadi ya kubarikiwa katika mambo yako yote.
Mashujaa wa Bwana wakijifunza nanmna ya kukomboa mji katika ibada ya leo.
“Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.” Kutoka 23:25-26

Bwana atatimiza siku zako za kumiliki; kutawala, kutiisha, na ukianza miradi mipya ifanikiwe, ukianza biashara ifanikiwe, ukisoma ufaulu katika masomo yako na yote yanawezekana kwa yeyote aaminiye kwa jina la Yesu.

Watu hawa walimwendea Elisha wakamwambia mji ni mzuri ila maji yake huzaa mapooza. Mambo hayaendi, vitu vinakufa kabla hujafaidi matunda yake. Inawezekana una ndoa nzuri; mke mzuri, lakini ndoa haina watoto, hakuna upendo ndani ya ndoa hiyo, kama ni uchumba ulikuwa mzuri, lakini uchumba unaingia kwenye magonjwa, au ujauzito kabla ya ndoa.

Yawezekana mji wako ni mzuri. Mfano wa mji wa Morogoro ni mzuri ajabu na una vitu vingi vya kuvutia, Wilaya ya Ulanga kuna madini yanaitwa Ulanga, wilaya ya Matombo kuna madini aina ya Red ganet, Reds right na mengine mengi, Morogoro mjini kuna dhahabu safi inapatika hapa. Kuna mbuga za wanyama mfano Mikumi, Seloue na nyingine. 

Morogoro ina udongo mzuri sana ambao unaweza kuotesha kila aina ya mmea au mbegu nyingi sana. Ni sehemu inayofaa kwa ajili ya uwekezaji wa Viwanda. Kuna mradi mkubwa wa Bandari Kavu ambayo itatumika kukusanya na kusafirisha mazao kwenda ndani na nje ya nchi. Kuna mradi wa ‘Treni iendayo Kasi’.

Mji huu ni mzuri sana lakini hatari yake kuna mapooza., mapooza hayo ni kama yafuatayo;
·         HAKUNA AJIRA; Mji huu ulikuwa na viwanda vingi kama Polister, Canvas Moroshoes na vingine. Viwanda hivi vingeajiri watu wengi lakini kuna mapooza. Lazima tuombe kwa ajili ya mji wa Morogoro na viunga vyake. Mji ni mzuri lakini hatuna miundo mbinu. Mchele wa Morogoro ni mzuri lakini utakuta umewekewa jina ‘Mbeya Grade’.
·         WATU WAZEMBE. Hakuna bidii ya kazi; Watu wa mji wa Morogoro ni wazembe kupita kawaida. Ni watu wasioweza kujishughulisha ili kupata kipato. Ni watu wenye nguvu lakini hawawezi kuboresha maisha yao. Maana yake kuna kuna jambo kwenye ulimwengu wa roho linaloitwa Maji yenye kuzaa mapooza. Watu wamefungwa akili hawawezi kuwa na mipango ya kukomboa uchumi wao. Ni wageni waliojenga Morogoro kuliko wenyeji.
·         WATU WANAAMINI UCHAWI SANA; watu wanaamini sana uchawi, Hii ni roho inayotenda kazi sana. Uzembe ni matokeo ya roho ya uchawi. Mtu akianza ujenzi, vita inaanza na inakuwa kali.  Watu wengi wamejaa hofu ya uchawi. Wengine wana mashamba lakini hawawezi kulima kwa sababu ya roho hiyo ya uchawi. Imeandikwa Usimwache mwanamke mchawi kuishi leo tutawashinda wachawi wote kwa jina la Yesu.
·         ROHO YA UMASKINI; utatona morogoro kuna umaskini wa hali ya juu utamkuta mtu mzima kabisa anakaanga karanga anatembeza mji mzima lakini ukimwambia achukue shamba alime kwa mara moja awe tajiri hataki. Watu wengi wameamini uchawi sana kuliko Mungu. Mzunguko wa fedha ni mdogo sana. Watu wana ugumu wa maisha. Shule za Kimataifa (International School) ipo moja tu. Maana yake watu wengi wamelogwa akili hawawezi kuona fursa ya biashara iliyoko mbele yao.
Platform Ministry wakiongoza nyimbo za kuabudu katika ibada ya leo.

  MIGOGORO; migogoro ya wakulima na wafugaji ina pelekea kumwaga damu, hakuna maelewano kati ya wananchi wa kawaida na wafugaji. Wakulima wakilima mazao yao mifugo inapitishwa kwenye mashamba. Wakulima wakiwakamata wanyama wanaua hata kusababisha ugomvi. Hayo yote yana sababishwa na maji yasiyofaa ya rohoni yenye kuleta kuzaa mapooza.
·         MAFURIKO; kila mwaka mafuriko yanapotokea kuna watu wanakufa kwa maji, mali za watu zinaharibika mifugo na mazao yanaharibika kutokana na mafuriko, pia aina nyingine ya mafuriko yanayochukua kazi za watu afya za watu kwa sababu ya ile roho inayoleta kuzaa mapooza.

Maji haya ni ya rohoni, Elisha aliletewa chombo ndani yake kulikuwa na chumvi, akaenda kwenye chanzo cha mapooza akarusha chumvi na akasema Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza”. Bwana anasema leo katika jina la Yesu anatangaza, analituma neno la Bwana liende kwenye kazi, biashara, ndoa kama kuna roho ya kuzaa mapooza inaondolewa kwa jina la Yesu, nuru ikaangaze mbele yako kwa jina la Yesu.

Morogoro hakuna maji; lakini hapo mwanzo maji yalikuwa yanatiririka kwenye milima kuelekea mabondeni, lakini sasa hakuna maji yanayotiririka tena milimani. Morogoro wa imekumbwa na magonjwa ya ajabu ajabu kama vile kipindupindu, lakini watu wa Morogoro si wachafu.

WAKOMBOAJI WA MJI
Watu wanao ukomboa mji, si watu wenye fedha sana, si waliotoka kwenye ukoo mzuri, au wamesoma sana, au wanakaa kwenye nyumba nzuri, bali ni wale wenye utayari, wako tayari kujihatarisha kwa ajili ya kuukomboa mji, ni watu waliochoka kukaa kwenye hali fulani na wakaamua kupiga hatua kuelekea kwenye utatuzi wa matatizo, ni mashujaa wa imani waliojipanga kuvipiga vita kwa ajili ya miji yao.
Mamia ya mashujaa waliompokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao.
“Ikawa baada ya hayo, Benhadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake. Ndipo akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, kikimbakia kichwa Elisha mwana wa Shafati juu yake leo. Lakini Elisha alikuwa akikaa nyumbani mwake, na wazee wakikaa pamoja naye; na mfalme akamtuma mtu wa mbele yake; lakini hata kabla ya kufika kwake yule aliyetumwa, akawaambia wazee, Je! Mwaona jinsi huyu mwana wa mwuaji alivyotuma aniondolee kichwa changu? Angalieni, huyo aliyetumwa akifika, fungeni mlango, mkamzuie mlangoni; je! Sauti ya miguu ya bwana wake haiko nyuma yake? Hata alipokuwa katika kusema nao, tazama, yule aliyetumwa akamshukia; naye akasema, Angalia, mabaya haya yatoka kwa Bwana; kwani mimi kumngojea Bwana tena?” 2 Wafalme 6:29-33

Neno kuhusuru maana yake ni kuzungukwa au kuzingirwa na hakuna mtu kutoka nje wala kuingia ndani, hakuna chochote kupita kutoka nje au kuingia ndani. Shida ya kuzungukwa huwezi kupata hela, wala chakula, ndicho kilichotokea kwa wana wa Israeli. Watu hawa walizungukwa pande zote na adui hawakuwa mpaka wakaishiwa chakula.
Mfalme wa Shamu aliizunguka na kuihusuru Samaria njaa ikawa kubwa sana katika mji, njaa ilipozidi wakakosa chakula hata kufikia kutokosa watoto kwa ajili ya kuwala. Mfalme aliposikia haya alirarua mavazi yake akapaza sauti yawezekanaje kuwepo na nabii katika mji huu na watu wafe kwa kukosa chakula? Akaagiza mtu akilete kichwa cha Elisha kama asipotoa unabii juu ya mji wa samaria. Hapa tunajifunza kuwa kuna baadhi ya majibu yanapatikana kwa mtumishi wa Bwana pekee.

Kuna mambo ambayo wafalme wanaweza kuyafanya na mengine hawawezi, kuna mambo ambayo Raisi anaweza kuyafanya mengine hawezi, kuna mambo ambayo baba yako anaweza kukutendea lakini mengine hawezi. Lakini nakutangazia yupo mfalme Yesu hapa anaweza kukusaidia tena na kukutoa kwenye roho ya kuzaa mapooza kwa jina la Yesu.

Ukiwa mtumishi wa Bwana ni lazima uombe mpaka mtu afunguliwe, kuna watu wanaumwa  na wengine wamechizika wapo milembe ndio maana Mungu anataka watu kama wewe ili  uwasaidie watu wapate  kuwa huru kwa jina la Yesu.

WATU WENYE UKOMA. Ni kawaida sana kwa watu wanyonge kudharauliwa. Usiogope kukataliwa kwako kwa sababu Mungu anakuandaa kuwa shujaa. Ni wewe utakayetumika kuleta ukombozi wa familia, ukoo, kanisa na jamii kwa ujumla. Pamoja na ukoma wao, hawa ndio waliotumika kuleta ukombozi wa mji. Watu hawa wakasema Haya, na tuliendee jeshi. Wakoma hawa wanatufundisha nguvu ya kuthubutu kuanza jambo. Hii ni tabia watu mashujaa. Kumbe ukithubutu kufanya, wale waliokuzuia watakimbia wao wenyewe. Mtu huyu akitembea anakuwa na kishindo kikubwa kwa uwezo wa Bwana. Kuna faida ya kuchukua hatua ili kuzimiliki Baraka zako.

“Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?”  2 WAFALME 7:1-4
Muumini akifunguliwa katika ibada ya leo.
Kumbe ukichukua hatua adui anaanza kutafsiri hatua zako. Maadui wa Israeli walipata tafsiri kutokana na kishindo cha wakoma. Wakoma walipochukua hatua maadui wakajua kwamba wana wa Israeli wamekodi majeshi ya wafalme wengine ili wapigane nao. Chukua hatua leo kuelekea Baraka zako. Piga hatua usikubali kubaki ulipo leo. Hatua yako moja itaungana na kishindo cha malaika na maadui zako watakimbia wenyewe. Kumbe hata kama ukiwa umekataliwa, lakini ukija na habari njema hata waliokukataa watakupokea kwa mikono miwili. Chukua hatua ili uwe chanzo cha Baraka japo ulikuwa mtu wa kukataliwa kwa jina la Yesu. Kinacholeta mabadiliko ni uwepo wa Neno la Mungu. Kwa sababu wakoma hawa walipokea sawasawa na neno la mtumishi wa Mungu Elisha.

Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha. Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme. Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini. Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone. Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie.” 2 WAFALME 7:5 - 12
Children Ministry wakimchezea Bwana Yesu katika ibada ya leo.
Ukombozi hautokani na mtu kubwa, au familia nzuri bali unatokea kwa shujaa wa Bwana. Wakati ukipita kwenye shida watu wanakuona haufai, hauthaminiki watu wanakubeza sana. Bwana akunyanyue leo ukawe msaada kwenye nyumba yako, kwenye ukoo wako, kwenye mji ulioachwa na njaa kwa jina la Yesu. Waliokuzunguka wakazungukwe na wao kwa jina la Yesu, kishindo kianze katika mji wako, Morogoro kwa jina la Yesu.

 “Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme. Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la Bwana.” 2 Wafalme 7:15-16”.


KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr.Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
(WhatsAssp & SMS only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro       http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/



Share:
Powered by Blogger.

Pages