Saturday, February 10, 2018

KUWA HODARI NA MOYO WA SHUJAA

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

PASTOR  DR. GODSON ISSA ZACHARIA

Mchungaji Kiongozi, Dkt Godson Issa Zacharia wakati akifundisha kwa habari ya moyo wa ushujaa.
Shujaa  ni mtu jasiri asiyeogopa chochote na yupo tayari wakati wowote kutetea haki yake ambayo Bwana amempa na anaamini mpaka akipate. Shujaaa ni mtu   mwenye uwezo na uvumilivu wa kushinda hata kama kuna ugumu, dhiki nyingi na matatizomengi  anavumilia mpaka mwisho ili apate haki yake. Shujaa ni mtu mwenye uthubutu, utayari  na ujasiri wa kupambana hadi mwisho na kuhakikisha anarudisha kila kitu kilichopotea kwenye maisha yake, au mali yake iliyotekwa au kuibiwa na adui zake. Shujaa hakubali mpaka apate vitu vyake, shujaa wa ukweli anasimama mpaka mashujaa wa kuzimu wakimbie.

Kuzimu pia wapo mashujaa ambao ni mashujaa wa uharibifu, shujaa anayependa akuibie na kukutesa, kazi yao ni kuharibu maisha ya watu na kushindana ili kuleta uharibifu kwenye maisha ya watu.

Tunamuona Goliathi ni shujaa ambaye ni wa upande wa pili shujaa wa kuzimu, imeandikwa

“Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana”. 1 Samweli 17:23~24

Wana wa Israeli walikuwa wamepakwa mafuta na Bwana, lakini akatokea Goliathi ambaye ni shujaa wa kuzimu ni shujaa aneyepinga kazi ya Bwana, ni shujaa ambaye anapinga maendeleo ya watu,ni shujaa anayepinga kusudi la Mungu kwenye maisha ya watu.

Mungu aliwaita wana wa Israeli na akawatoa kwenye dhiki nyingi na kuwapeleka katika nchi ya ahadi na akawaambia watakwenda na kuimiliki nchi na itakua ya kwao, lakini hapo katikati akatokea shujaa mwingine ambaye ni shujaa muovu anayeitwa Goliathi wa Gathi, huyu Goliathi wa Gathi akawa amesimama anawapinga wana wa Israeli yeye na jeshi lake, na yeye akasimama kama shujaa wa wafilisti akawa anatukana kwa siku arobaini, akawa anasimama anatukana kutwa nzima na akawa anatukana maneno yaleyale mpaka wana wa Israeli walikua wakimuona wanakimbia na kumuogopa. Lakini leo nakutangazia ya kwamba usiogope tena maana Bwana amesema usiogope uwe hodari na moyo wa ushujaa kwa jina la Yesu.

Nabii Isaya akawa anaonesha, Mungu alikua anamuonesha ya kwamba kuna watu ambao yupo nao ambao wanakula pamoja, wanongea pamoja, wanashirikiana pamoja, wale wabunge, wale mabwana shamba,  maafisa, marafiki n.k wale wote Mungu anamwambia ya kwamba hao ni watu walioibiwa na kutekwa,tena Mungu anasema wote sio wawili au watatu ila wote wamewekwa kwenye mashimo na  magereza, 

“Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha”. Isaya 42:22

Kuna magereza yamewekwa ambayo watu wengine hawayaoni tena kuna mashimo fulani ambayo yamewaficha watu, na Mungu alikua anamuonesha Isaya ya kwamba watu wengi  wamefichwa  tena kibaya zaidi wanawindwa, wakitaka kutoka inashindikana, wakitaka kuanza biashara inashindikana, wakitaka kuanza ndoa inaharibika, na bahati mbaya hajawahi kutokea shujaa wa kuwaokoa, yaani hata Isaya Mungu anamwambia hata yeye hajawahi kusema neon japo yupo nao na anakaa nao  lakini wametekwa na hapana shujaa wa kusema rudisha. Ndio maana Mungu anataka wewe uwe shujaa ili uweze kujikomboa kutoka kwenye magereza, magereza ya uchumi, magereza ya familia,magereza ya ndoa, umekua magerezani, ulitakiwa kuwa na fedha hauko nazo, ulitakiwa kuvaa vizuri lakini leo huwezi, ulitakiwa kuwa na maisha mazuri lakini hauko nayo ni kwa sababu uko gerezani,  leo Mungu akugeuze uwe shujaa ili uyakomboe maisha yako kwa jina la Yesu.

 Mungu anashangaa hapana shujaa wa kuokoa, wala hapana asemaye rudisha, Mungu anasema hapana shujaa, kama ilivyokua kwa Goliathi, tunaona Goliathi amesimama upande huu na upande mwingine alikuwepo Sauli ambaye alikuwa mfalme wa wana wa Israeli na alikuwa na Mungu kumbuka, lakini Goliathi hana Mungu kabisa, ana majeshi ana mapanga na visu, ila huyu Sauli ana Mungu lakini alikuwa anaogopa kwa sababu alikosa ushujaa ndani yake, alikosa uhodari, akakaa anaogopa na kulia kwa sababu anaona hana mtu wa kumsaidia. Lakini Goliath ambaye hana Mungu anawatisha na mapanga na visu, alikua anatisha sana.

 Lakini leo nakutangazia wao wanakutisha kwa mapanga yao, wao wanakutisha kwa silaha zao, wao wanakutisha kwa ukubwa wao, wamekutisha kwa fedha zao, wamekutisha kwa ujasiri wao, lakini wewe usimame na jina la Bwana, kwa maana jina la Bwana ni upanga ukatao kuwili, jina la Bwana ni kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande, jina la Bwana linaweza mambo yote, linaweza kufufua, linaweza kuhuisha katika jina la Yesu,  maana imeandikwa

“Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu”. ZABURI 20:7

Tunaona Sauli alikuwa na Mungu lakini alikosa moyo wa ushujaa, hivyo tunajifunza ya kwamba unaweza kuwa na Mungu lakini ukakosa moyo wa ushujaa. Yani unakuwa umeokoka lakini ni Muoga kabisa, unaweza ukawa umempokea Yesu lakini ukakosa moyo wa ushujaa, na anaetia moyo huu ni Bwana Mwenyewe mtu hawezi kukutia moyo.

“Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa”. Joshua 1:6

Tunaona hapa Mungu anamwambia yoshua ambaye anatakiwa kuwavusha  wana wa Israeli kuwapeleka nchi ya ahadi, anamwambia uwe hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewavusha wana wa Israeli. Hata leo Mungu anakwambia wewe kwamba uwe hodari na moyo wa ushujaa mana ni wewe utakaewavusha familia yako, maana ni wewe utakaye ikomboa nchi yako, ni wewe ambae utamilikisha mke wako urithi wa Bwana hakika ni wewe, hapo hawezi kuwa mchungaji wako ila ni wewe mwenyewe. 

Siku zote huwa tunaenda kanisani na mchungaji anatamka kwamba pokea gari, nyumba, mke, n.k, na unasema napokea kwa jina la Yesu, lakini sio rahisi hivyo, inatakiwa upige hatua zaidi ili kukimiliki kile utakachopokea au ulichotamkiwa, maana kwenye kumilikishwa hapo ndipo kwenye shida, ni lazima kuwa hodari na moyo wa ushujaa maana njiani kwenye kwenda kwenye kumiliki kwako kuna mto yordani ambao unatakiwa kuvuka, kuna bahari ya shamu, kuna nyoka wa jangwani, kuna dubu na simba n.k. Unabii ni mzuri lakini kuna namna ya kufanya ili uweze kumiliki kitu hicho ulichotabiriwa kwa sababu hakuna kumiliki bila vita, kwahiyo Mungu akisema jambo kupitia mtumishi wake  kuna mambo ya kufanya ili kuyapokea.

Shujaa huwa anawamilikisha watu, wana wa Israeli waliwahi kwenda kuipeleleza nchi, Mungu alishasema ipo lakini Musa akatuma viongozi kumi na wawili, wakaenda kuipeleleza na kweli kila kitu kipo, maziwa yapo, asali nayo ipo, matunda yapo, lakini viongozi kumi kati ya wale kumi na mbili waliokwenda kuipeleleza nchi wakakosa moyo wa ushujaa wakaingiliwa na roho ya woga ndani yao hivyo wakaleta habari mbaya (Hesabu 13:33), wale kumi waliokuwa na roho ya woga  waliporudi wakasema japo Bwana amesema kwamba tutaimiliki nchi  lakini haiwezekani, kwanza watu wa kule wanakula watu na walituona kama mapanzi nasi ndivyo tulivyo. Lakini hawa wawili wenye moyo wa ushujaa ambao ni Joshua na Kalebu wakachana nguo zao wakatoka mbele wakasema sikilizeni, msilie, nchi ile ni njema mno ya ajabu na yale majitu makubwa uvuli wao au utiisho wao umeondolewa ndani yao, nao watakuwa chakula chetu (Hesabu 14: 6-8). Adui zetu wanaweza kuwa wengi sana na wa kutisha,  na hali unayopitia inaweza kukutisha mpaka ukaingiwa na roho ya woga, haijalishi wingi wa watu wanaosema kwamba haiwezekani au wanaopinga jambo hilo inatupasa kusonga mbele, hivyo wanaoweza kumiliki ni wale tu wenye moyo wa ushujaa, kama tunavyoona walioingia nchi ya ahadi ni wawili tu wale waliokuwa na moyo wa ushujaa, lakini wale wengine wote walifia jangwanii.

 Kuna mali wewe unatakiwa kuwapatia watu, kuna watu wanatakiwa kuanza shule lakini hawajaanza ni kwa sababu wewe hujasema, kuna watu wanatakiwa kuanza biashara lakini hawajaanza ni kwa sababu wewe haujasema,  wanaangalia mbona huyu hasemi, kuna ndugu zako ambao wanakusubiri wewe ambaye ni shujaa kwao  hivyo ni muhimu kuwa shujaa ili uwavushe wengine kuwafikisha kwenye nchi yao ya ahadi

“Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa”. Isaya 42:6~7

Mungu anasema wewe uliyeokoka amekuita katika haki na ukiitwa hauwezi kwenda peke yako, atakuwa pamoja na wewe siku zote na pia atakulinda, hivyo Mungu anaweza kukusimamisha wewe mmoja tu ili kuukomboa ukoo, familia, nyumba, taifa na kanisa kwa ujumla. Kuna watu wamefungwa, hivyo Mungu anataka akutumie wewe ili urudishiwe kile kitu chako, upate ushindi wako, ila sio wewe peke yako bali na watoto wako, mkoa wako, taifa lako, ndoa yako, biashara yako, shule yako n.k, maana vimeibiwa na vimemezwa na adui.

“Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake”.   Ayubu 20:15

Kama shujaa, Bwana akishasema kwamba amememeza mali naye atazitapisha toka tumboni wakwe, Mungu anakuwa ameshasabababisha kichefuchefu cha kiroho, hivyo unapoamini andiko hili hautakiwi kutulia tu, unatakiwa kuchukua hatua ya imani kuendelea kuomba ili kuwatapisha mali zako, biashara yako, kazi yako n.k, kwa maana imeandikwa “Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunjavunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme” ;Jeremiah 51:20
Ni muhimu kujifunza kuwa shujaa  kama tunavyoona kwa Daudi, Ukiwa shujaa kutokea ndani hata mwilini unapotamka kitu kinaonekana ni bora kuliko wengine na unakuwa unaheshimika, na wengine watakuja ili kutaka ushauri kwako. Imeandikwa;

“Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto; nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao. Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka. Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena. Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli. Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika Bwana, Mungu wake. Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko. Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, JE! NIKIWAFUATA JESHI HILI, NITAWAPATA? NAYE AKAMJIBU, FUATA; KWA KUWA HAKIKA UTAWAPATA, NAWE HUKOSI UTAWAPOKONYA WOTE. Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye, nao wakakifikilia kijito Besori, ambapo wale walioachwa nyuma walikaa. Lakini Daudi akakaza kufuata, yeye na watu mia nne; kwa maana watu mia mbili walikaa nyuma, ambao walitaka kuzimia hata hawakuweza kukivuka hicho kijito Besori”. 1 SAMWELI 30:1~10

Utaona Maswali ya shujaa  yaliyoulizwa kwa Bwana sio ya kulalamika wala kunung’unika kwasababu Mungu yeye yupo kila mahali kila wakati (Omnipresent) na kwa wewe uliyeokolewa yupo ndani yako na wewe upo ndani yake hivyo kama shujaa hutakiwi kuomba kwa kulalamika kila wakati mbele za Bwana bali kuuomba kwa ushujaa kama Daudi alivyoomba kwa Bwana na kumuuliza Bwana je awaendee adui zake? Na Bwana akamjibu kwa sababu aliomba kwa ushujaa, lakini unapoomba kwa kulalamika mbele za Bwana au kwa ulegevu hata yeye Mungu anachelewa kukujibu kwa sababu unaomba vibaya. Mfano utamsikia mtu akiomba hivi, Bwana mbona umeniacha, tazama jinsi nilivyo mimi si chochote mbele zako, shuka unipiganie, tazama haujibu maombi yangu, umekuwa mbali sana nami n.k. Haya si maombi ya kishujaa au maswali ya kishujaa. Daudi aliuliza kwa Bwana kishujaa, “Je niwafuate, Nitawapata?”. Ni kweli makazi yake yote yalichomwa na moto, watu wake na jeshi lake likaibiwa pamoja na vitu vyote, lakini alijitia nguvu katika Bwana. Hakuuliza maswali ya kulalamika, oh Bwana, mbona umeruhusu tumeibiwa?, tumetekwa, tumepoteza vyote? Uko wapi Bwana?. Badala yake aliuliza maswali ya kishujaa na Bwana akamjibu wakati huo huo hata akamuongezea maelekezo zaidi ya alichouliza.

Daudi baada ya kujibiwa na Bwana kwamba awafuate, atawapata, ndipo akawakusanya wanajeshi wake mia sita, lakini kati yao hao mia sita kuna wengine ambao hawana moyo wa ushujaa walikua wamekata tamaa , hivyo wale ambao walishindwa kwenda vitani yapata askari mia mbili walibaki hapo mtoni, lakini Daudi na mashujaa wale wengine mia nne wakaenda vitani na wakarudisha vyote wala hakupoteza kitu. Huu ndiyo mfano wa askari waoga (hao mia mbili) na mashujaa mianne waliofuata mpaka mwisho pamoja na Daudi hata wakapokonya vyote.

“Na hapo alipokuwa amewaongoza chini, tazama, hao walikuwa wametawanyika juu ya nchi yote, wakila na kunywa, na kufanya karamu, kwa sababu ya hizo nyara kubwa walizochukua katika nchi ya Wafilisti, na katika nchi ya Yuda. Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia. Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili. Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote”. 1 SAMWELI 30:16~19

Nami nakutangazia leo kila kitu chako kilichoibiwa, mali zako zilizoibiwa, nyota, biashara, kazi, mke watoto, akili, fedha leo virudishwe kwa jina la Yesu, Bwana akutumie wewe kama shujaa ilurudishe vyote vilivyoibiwa kwenye maisha yako kwa jina la Yesu, Ameen.

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr.Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
(WhatsAssp & SMS )
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogorohttp://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
[19:14, 2/9/2018] +255 689 891 661: 
Share:
Powered by Blogger.

Pages