Sunday, April 15, 2018

KUFUNGUA KAMBA ZA KUZIMU


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCCT)
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
PASTOR, DR. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI 15 APRILI 2018

Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha somo kuhusu kuzifungua kamba za kuzimu
Utangulizi:
Kamba ni silaha inayotumika kufungia vitu katika ulimwengu wa kawaida. Lakini pia katika ulimwengu wa roho nako kuna kamba kama silaha za kishetani. Kamba ya kuzimu yaweza kuwa jini, pepo, mizimu na majoka. Haya yote yanatumika ili kufunga maisha ya mtu ili asifike kwenye hatima yake. Maandiko yanatuelezea kuhusu kamba za kuzimu na kamba za mauti.“Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.  Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. 7 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake”. 2 Samwel 22:4 – 6

Tunajifunza kwamba kuna kamba za kuzimu, hii ina maanisha kamba hizi zilitoka kuzimu, na chanzo chake ni kuzimu. Kamba hizi sifa yake ya pili zinauwezo wa kuzunguka.

Kuzimu ni wapi? Kuzimu ipo hapa hapa dunia. Shetani alipohasi mbinguni alitupwa hata nchi naye akatengeneza mahali alipoweka ufalme wake ambapo panaitwa kuzimu. Kuzimu ni shimo lenye giza, ni shimo la mashetani, na halionekani katika macho ya mwilini ila lipo katika ulimwengu wa roho.  Kuzimu au shimo la shetani ni mahali mashetani, mapepo, nyoka yanakaa. Pia wachawi na waganga wa kienyeji ni mahali wanapoenda kutafuta mapepo, majoka, majini ili wayatumie kuwaangamiza watu wengi duniani.

Kamba ni nini? Kamba za  kuzimu ni majoka, mashetani, mizimu, zinakuja katika ulimwengu wa roho kama kamba na matokeo yake yanaoneka katika ulimwengu wa mwili. Mashetani, majoka na mizimu wanakuja duniani kufunga kazi, ndoa, biashara, shule na matokeo yake yanaonekana katika ulimwengu wa mwilini.unapoona mwanafunzi anashindwa masomo maana yake kuna kamba za mauti zinatenda kazi.
Mchungaji Kiongozi akitoa mfano wa mtu alifungwa na kamba za kuzimu. Mtu anapokuwa katika hali hii hawezi kutenda kama apendavyo maana amefungwa. kama ni kazi ya mikono hawezi, kama ni kutembea hawezi maana miguu yake imefungwa.
“Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.” Zaburi 18:5 - 6

Daudi alisema maneno hayo si kwa sababu aliona kamba ya kudu/au ya mnazi. Bali aliona kamba katika ulimwengu wa roho. Mambo yake yalikuwa hayasogei. Kamba hizi si za mwili, ni za rohoni hazionekani kwa macho ya mwili.

Kamba za mauti, kuzimu, hapa tunajifunza kamba inafunga kwanza ili uangamizwe na mitego ya mauti inakukabili. Kamba inatumika kama mtego ili ukinaswa uweze kuliwa. Kuzimu zinafanya kazi pamoja na mauti.

“Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi”. Ufunuo 6:8

Yohana aliona maono farasi wakijivujivu na amepandwa na abiria mwenyewe ni mauti na nyuma anafuatana na kuzimu. Mauti na kuzimu ndizo nguzo kubwa mbili za shetani anazotumia ili kuangamiza watu. Kamba hizi si kamba za kibinadamu bali ni za rohoni, mashetani yanaweza kugeuka na kuwa kitu chochote. Wanaweza kugeuka wakawa kifuu cha nazi, paka, mwanaume mzuri au gari na wewe  ukapanda kumbe ni shetani.

Viumbe vya roho wanayo sifa ya kugeuka na kuvaa maumbo.

“Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee RamothGileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo”. 1Wafalme 22:20 – 22

Pepo alikwenda kwenye kikao cha Mungu, Mungu alikuwa anauliza ni nani atakaye enda kumdanganya mfalme Ahabu.  Pepo akasema yeye atakwenda, Mungu akamuuliza jinsi gani atakavyo mdanganya? Pepo akasema ataondoka na kuwa pepo wa uongo kwenye vinywa vya manabii wote. Hivyo pepo wanao uwezo wa kugeuka na kuwa namna wanavyotaka kuwa, wanaweza wakawa uvimbe, au ugonjwa wowote. Pepo anaweza kuwa kamba na kuingia kwako ili wafunge ndoa, shule, kazi n.k.

Makutano ya Bwana wakijifunza namna ya kufungua,kulegeza na kuzikata kamba za kuzimu.
          
Kazi ya kamba ya kuzimu. Kamba hizi asili yake ni kuzimu
Ø  Kumfunga mtu; Kufungwa maana yake ni kuondolewa uhuru wa kutenda. Au kuondolewa uwezo wa kitu ulichokuwa unakifanya hapo awali. Akifungwa mtu anakuwa ameondolewa uhuru. Ukisikia mtu amefungwa magereza maana yake ameondolewa uwezo wake wa kutenda kama atakavyo. Kama alikuwa anaweza kuamua ale au avae nini lakini kamba ikiwepo  hawezi kuamua tena.

Mtu anapofungwa anaondolewa uhuru wa kuomba, ukifungwa akili unakuwa huwezi kufanya maamuzi ya haraka haraka ya maisha yako. Kazi ikifungwa huwezi kuona kazi mbele yako. Zinafunga kazi, fedha, kuoa, kuolewa, biashara. Unakuta kijana amemaliza shahada ya kwanza anakaa kwa mjomba anaangalia Tv lakini hafikirii hata kujishughulisha na kazi ndogo ndogo.

Wengine wameondolewa uwezo wa kutunga mimba, uwezo wa biashara, unaondolewa uwezo wa kutenda yale unayotaka kufanya. Kuzimu inakufahamu inaweza kufungwa uso, macho, akili n.k. Kwa jina la la Yesu ewe kamba ya kuzimu uliyotumwa ukae kwenye uso, mikono, miguu leo nakutangazia na kufungua leo kwa jina la Yesu. Mwovu (ibilisi au abadoni au apolioni) akitaka akuangamize haraka na  vizuri anakufunga kwanza ili usifurukute.

“Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri.” Marko 7:31 – 35

Hapa tunajifunza kamba za  kuzimu zilikuwa zimemfunga ulimi na masikio yake. Hapa tunajifunza kamba zinauwezo wa kufunga sehemu mbalimbali za mwili, macho, miguu, mikono. Anayekufunga ni mwovu. Na kila mtu atafungwa kulingana na sehemu ya umahili wake.

“Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” Isaya 14:17

Ilimpasa kila mmoja kuwa makini maana Mkono wa Bwana ulipita katikati ya makutano ili kuzifungua kamba za kuzimu.
Ukiwa umefungwa unakosa uhuru wa kuchagua kitu cha kufanya. Mfano kila mtu ameamua kuvaa nguo uliyovaa, lakini kuna mwingine amefungwa mapato amevaa nguo aliyovaa ni kwa sababu huna namna bali umevaa. Au mwingine anakula chakula si kwa sababu anakipenda ni kwa sababu hana mapato ya kununua ukipendacho. Unakuta mtu mwingine amesoma na ana shahada mbili anashindwa kuandika hata maandiko ya mradi ni kwa sababu akili imefungwa. Anakubali kuwa mkusanyaji takwimu. Huyu anakuwa amefungwa kamba katika akili. Aliyefunga ndiyo mwenye uwezo wa kukufungua na asipotokea mwenye nguvu kuliko yeye hakuna wa kukufungua.

“Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” Mathayo 18:18

Akipatikana mwenye nguvu kuliko yeye ataweza kukufungua kamba. Shetani akikukufunga kwa muda mrefu, unakuwa na mazoea yaleyale ukifunguliwa unawaza bado umefungwa. Unatakiwa utoke uende kutafutafuta, mfano kuandika barua za kuomba kazi. Mungu alijua watu wamefungwa akamtoa mwanae wa pekee ili aje afungue wafungwa waende zao.

“Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,  Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Luka 4:18-19
wengi walifunguliwa na waliwekwa huru kutoka kamba za mauti.

Katika Biblia Daudi amepitia vifungo vingi vya kamba. Kamba za kuzimu wakati mwingine ni kamba za mauti. Kamba hizi zinaweza kumfunga mtu aliye hai na akaanza kupata matatizo na kuelekea kufa.

“Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni;” Zaburi 116:3

Kamba za mauti zikikupata unaanza kupata na taabu za kuzimu. Kamba ikifungwaa unaishia kupata mimba na kutoka, unapata kazi na kufukuzwa, unaanza biashara inakufa.

“Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.” Zaburi 18:4
Kamba za mauti zinatakiwa zikatwe, na kamba za kuzimu zinatakiwa kufunguliwa. Kamba za kuzimu zinamfanya mtu asiweze kabisa. Unafungwa kwenye ndoa, unafungwa kwenye elimu unafungwa kila mahali. Kamba za mauti zikija una pata mafuriko ya uovu, unapata taabu, maumivu, mafuriko ya uovu. Mafuriko ni kitu kinakuja kwa wingi na hakipimiki. Maovu yakiwa mengi unapata hofu, na hatimaye unakufa. Watu wengi wameharibikiwa ni kwa sababu wanapata hofu ya mambo yaliyopita, yaliyopo na yajayo. Kuna mwingine anapata hofu ya usiku.

“Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.” Warumi 8:15

Hofu haitoki kwa Mungu, bali ni roho inayotoka kwa shetani. Kwa sababu hiyo Mungu alimtoa Yesu Kristo ili aje kufungua kamba za kuzimu.
Watoto nao walikuwa makini ili kuhakikisha kamba zao zinakatika na wanawekwa huru kwa jina la Yesu.
“Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.” Waebrania 2:14 -15

Mungu alimaua kumleta Yesu akaja kwa mwili na nyama kupitia mauti yake Yesu Kristo ili aweze kuharibu zile nguvu za mauti alizokuwa nazo shetani. Unakuta mtu anapewa msaada anakataa ni kwa sababu alipitia shida nyingi sana anakataa anahisi ni mtego anakuwa na hofu. Kamba za uso, kamba za mikono, kamba za mizimu ya ukoo/familia kwa jina la Yesu nazifungua leo kwa jina la Yesu. Japo kamba zimetoka kuzimu ila Bwana ametupa uwezo wa kufungua kamba hizo, ufungue familia yako ufungue watoto wako kwa jina la Yesu.

“Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mathayo 16:18 – 19

Hapa maandiko yanatuambia kuzimu ina milango, kwa hiyo kamba zinaruhusiwa kupita kwenye malango hayo. Bwana amesema atakupa funguo za kufunga malango hayo.
Yesu alitumwa ili kuwafungua walio fungwa na kuwaweka huru. Binti huyu alifunguliwa kutoka kamba za kuzimu na mauti. 
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Yohana 1:12-13

Ukizaliwa na Bwana utapewa ufunguo. Hapa tunaona ukifanyika kuwa mtoto wa Mungu utapewa funguo ya kufungua kamba za mauti, kamba za kuzimu.

Utazaliwaje? Mtu anazaliwa mara ya pili kwa kumpokea Yesu kuwa na BWANA na Mwokozi wa maisha yake.
“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Warumi 10:9-10
Hawa ni baadhi ya Makutano waliokuwa tayari kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao.

Ukimpokea na  ukimkiri  Yesu kwa kinywa chako unapata uwezo wa kufungua kamba za mauti. Yamkini kuna kamba mpya, ambazo hujazijua bado wamezitumia hatimaye umeharibikiwa na kuibiwa. Ukimpokea Yesu anakupa funguo itakayofungua kila kitu, ambapo lolote utakaloliomba utalipokea kwa jina la Yesu. Fungua kamba na vitu vyako vyote ukafanikiwe kila mahali kwa jina la Yesu.


KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro       http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/


Share:
Powered by Blogger.

Pages