Sunday, April 1, 2018

KUHAMISHWA TOKA UTUMWANI KWA NJIA YA PASAKA


KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA
JUMAPILI YA PASAKA: 1 APRIL, 2018

 
Mchungaji kiongozi  Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha somo la kuhamishwa toka utumwani kwa njia ya pasaka
Utangulizi
Pasaka sio kuvaa nguo nzuri, wala kula chakula kizuri, wala sio kujipaka majivu,  bali pasaka ni kuhamishwa kutoka utumwani, kutoka katika utumwa wa gereza la mateso, kukataliwa, kuugua, kuteswa na majini mahaba, kifungo cha kuzaa, mapooza n.k. Ukiwa utumwani unaonewa sana, utumwa ni mateso, biblia inasema katika kitabu cha Isaya 54:14 utathibitika katika haki utakuwa mbali na kuonewa, kumbe kuna watu ambao wanateswa na kuonewa utumwani wanateswa na vifungo mbalimbali na wanaowafunga ni watu kabisa yawezekana ni ndugu kabisa anaweza kuwa kaka, mjomba au mtu yeyote yule lakini leo hii Yesu anaenda kukufungua kutoka utumwani kwa njia ya pasaka. Ukihamishwa kutoka utumwani unahamishwa na vitu vyako vyote vilivyo shikiliwa utumwani, ikiwa ni afya, elimu, kazi, kibali, ndoa n.k.

Sio kwa sababu ya fedha ulizo nazo, au kwa kua wewe unaelimu au una kitu chochote cha thamani bali ni kwa sababu umembeba Yesu. Ukimbeba Yesu akiingia nyumbani mwako nyumba yako inapona, akiingia kazini kwako kazi yako inapona, akiingia kwenye biashara yako biashara inapona hivyo leo hii unatakiwa kumbeba Yesu ili upone utoke katika utumwa wa magonjwa, kukataliwa, kutokuoa au kuolewa n.k. watu walipomuona Yesu akiwa juu ya punda walishangilia sio kwa sababu ya yule punda bali ni kwa sababu yule punda alimbeba Yesu hivyo na wewe leo unatakiwa kumbeba Yesu ndani yako ili uonekane kuwa ni wathamani machoni pa Bwana na mbele za watu wengine pia.

”Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.” (Isaya 43:3-4)
 
Platform team wakiongoza kipindi cha Sifa na kuabudu wakati wa ibada ya leo.
Yesu alichagua punda wa kupanda walikuwepo punda wengi sana Yerusalemu lakini Yesu alichagua punda wa kupanda kwa sababu ya uthamani wa punda yule, hata wewe leo hii Yesu amekupenda na kukuona kuwa wewe ni wathamani sana na ndio maana amekuokoa kwa damu yake ya thamani, Yesu ana haja na wewe, ana haja na kazi yako, anahaja na elimu yako, anahaja na biashara yako, anahaja na ndoa yako, afya yako kwa kuwa amekuona kuwa wewe ni wa thamani machoni pake hivyo unatakiwa kumbeba yeye Yesu ili naye akupende na kukuheshimu na kutoa watu kutoka pande mbalimbali za dunia ili waje kwako kukusaidia, atatoa watu kwa ajili ya kazi yako, elimu yako, biashara yako, afya yako ili waje kukusaidia katika mambo mbalimbali.

 “Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;” (Isaya 43:5)

Mungu anasema usiogope kwa kuwa atakuwa pamoja na wewe ili akusaidie, pengine kuna mambo ambayo unayapitia ambayo kwa akili yako unaona unashindwa Yesu anasema usiogope kwasababu yupo kila mahali, ukiwa bafuni yupo, ukiwa mahali popote yupo kwa ajili ya kukusaidia hivyo usiogope Yesu yupo kila mahali amefufuka yupo tayari kukusaidia mahali popote na muda wowote, usiogope asema Bwana.

 “nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.” (Isaya 43:6)

Kuna kaskazi ambayo inatakiwa ikuletee kazi, mchumba, elimu, au kitu chochote lakini kuna nguvu inayotaka kuzuia leo hii kwa msaada wa jina la Yesu aliye hai natangaza kila anayetaka kuzuia kazi, elimu, ndoa, biashara kutoka kaskazini ninamfyeka kwa jina la Yesu aachie kila kitu chako unachotakiwa kumiliki  na ninaiamuru kusi isizuie kwa jina la Yesu Kristo aliye hai.

Watu mbalimbali wameshindwa kutafsiri vizuri maana ya pasaka wanadhani kuwa siku ya pasaka ni kucheza disko, au kukaa nyumbani na kupika vyakula vizuri na kufanya sherehe, wengine wanadhani kuwa pasaka ni kwenda beach na kustarehe huko lakini kumbe pasaka ni kuhamishwa kutoka utumwani. Kwenye katiba ya ufalme ambayo ni biblia imeeleza juu ya kuhamishwa ambapo Yesu alifanywa kama kondoo aliyewekwa tayari kwa kuchinjwa, akajeruhiwa, akachubuliwa, akafa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu ili mimi na wewe tuwe huru kutoka utumwani, alifanya vyote hivi yaani alikubali kupata mateso haya makali ili wewe na mimi tuhame kutoka mautini na kwa sababu hiyo Mungu akamkirimia jina lipitalo majina yote ili kwa kupitia yeye kila goti lipigwe mbele zake.

 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”( 2 wakorintho 4:4)

Watu wanaweza kuangamia na kupotea kwa sababu mungu wa dunia hii ambaye ni shetani anakuwa amewapofusha fikra zao, amepofusha fikra zao ili wajue kuwa pasaka ni sherehe tu, ni siku ya kula chakula kizuri, kufanya starehe na kusheherekea, utaona hata katika biblia  mama yake Yesu alishawahi kumpoteza Yesu kwenye siku kama hii ya pasaka, walidhani kuwa pasaka ni sherehe wakasherekea sana mpaka Yesu akapotea.
Makutano ya Bwana  wakisikiliza neno la Mungu.

 “Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.  Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu,    na wazee wake walikuwa hawana habari.  Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;  na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.”(Luka 2:41-45)

Hata leo watu wengi wamepotea katika siku hizi za sikukuu wamepotea kimwili na kiroho kwa sababu ya kukosa kutambua kuwa pasaka sio kusheherekea au kuvaa nguo nzuri bali ni kuhama kutoka utumwani.

 “Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?”( Luka 2:49)

Pasaka ni siku ya kukaa kwenye nyumba ya Bwana kama ambavyo Yesu alikaa kwenye nyumba ya Baba yake, unatakiwa uwepo kwenye nyumba ya Bwana kusikiliza neno la Bwana, kutafuta uso wa Mungu kwa kuomba, kufurahi pamoja katika nyumba ya Bwana. Yesu aliona dunia yote imejaa utumwa, watu wanalia kutoka katika vifungo mbalimbali na ndio maana alikuja kuwatoa watu kutoka utumwani, kuna watu wao wanawaza kuwa sio watumwa kwa sababu wana kazi nzuri, ndoa, biashara nzuri lakini wamesahau kuwa mtu anaweza kuwa na kazi nzuri lakini ni mtumwa, anaweza kuwa mbunge, rais, waziri au mtu anayemiliki makampuni makubwa lakini bado akawa ni mtumwa, bila kumpokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako wewe unakuwa bado ni mtumwa kwa maana damu ya Yesu pekee ndio iwezayo kukutoa katika utumwa kwa njia ya wokovu.
Damu ya mwanakondoo ni damu inayonena mema, damu hii inaweza kuja juu ya mtu na kufanyika uzima unaona hata pilato alipokuwa anaambiwa na watu kuwa Yesu asulubiwe alikataa na kunawa mikono ikimaanisha kuwa asiwe na hatia juu ya damu ya Yesu, watu wote wakajibu damu ya Yesu iwe juu yao na watoto wao wenyewe.

Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”( mathayo 27:24-25)

Unaona kuna mambo ambayo unaweza ukapitia kwenye familia kwa sababu ya damu inayonena mabaya juu yenu ambayo ilisababishwa na mtu yeyote kwenye familia, hivyo unahitaji damu ya Yesu inyamazishe kila damu zinazonena mabaya juu yako na familia yako damu hii ya Yesu unaipata kwa njia ya wokovu peke yake yaani kwa kumpokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Pia damu ya Yesu inaweza kunena mema juu yako na kunyamazisha kila damu za makafara ndani ya jina la Yesu imo damu na leo hii naituma damu ya Yesu ije juu ya ndoa yako, damu hii itembee juu ya maisha yako, juu ya kazi yako kwa maana ndani ya damu hii umo uzima, pokea damu ya Yesu kwenye maisha yako kwa jina la Yesu.
 
Kijana huyu anaitwa ISAYA STEPHANO. Kijana huyu aliokotwa kutoka makaburini hapo Kihonda na sasa anaendelea vizuri. nguvu ya kufufua wafu inatenda kazi hata sasa. 
”na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili” (Waebrania 12:24)

Damu hii ya Yesu ina tabia mbalimbali, inatabia ya kusema, inatabia ya kulia, inatabia ya kunyamazisha kila damu za kafara zilizotolewa juu yako. Kuna nguvu katika jina la Yesu kwa maana ndani ya jina la Yesu imo damu inenayo mema, wanaotaka wewe ufe kwa kukuendea kwa mganga wa kienyeji na kutoa damu ya kafara ili iseme, inene usiolewe, usizae, usisome, ufe, ukataliwe n.k. nikweli wamemwaga damu zao ili zinene mabayo juu yako lakini leo tunayo damu ya Yesu pekee iwezayo kunyamazisha damu hizi za kafara na inauwezo wa kukuhamisha kutoka utumwani, tumia damu hiyo kunyamazisha kila damu zote za kafara zinazonena uhalibifu juu yako.

 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;  naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.  Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.  Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.  Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.”( Wakolosai 1:13-18)

Ndani ya jina la Yesu vitu vyote vinashikamana, huyu Yesu ambaye alipigwa akafa na kuzikwa na siku ya tatu akafufufka ukiwa naye vitu vyako vyote hushikamana yaani wewe na mke wako mtashikamana, wewe na elimu yako mtashikamana, wewe na kazi yako mtashikamana n.k. alikuja kutuhamisha kutoka utumwani wewe na vitu vyako, Bwana Yesu alipokuwa msalabani alikuja kutuhamisha kutoka kwenye mateso alipigwa na kuning’inizwa msalabani wajaribu walikuja na kujaribu kama kweli amekufa wakamchoma mkuki ubavuni damu na maji vikatoka roho yake ikatoka na roho ilipotoka ikaenda mpaka kuzimu kumnyang’anya shetani ufunguo wa kuzimu na mauti na kwa kupitia hiyo wewe na mimi tumepewa mamlaka ya kumkanyaga nyoka na ng’e kwa jina la Yesu, kila silaha ya shetani iliyoinuka juu yako, juu ya ndoa yako, n.k. haitafanikiwa kwa kuwa amekwisha kunyang’anywa ufunguo wa kuzimu na mauti mahali popote ambapo shetani amekaa kwenye maisha yako, ndoa yako, elimu yako, mponde kichwa chake kwa jina la Yesu kwa maana hana nguvu kwako tumia jina la Yesu jina lenye nguvu na mamlaka mponde shetani aachie vitu vyako kwa jina la Yesu.

 “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;  watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.” (1 petro 3:18-20)

Yesu hakuja duniani kwa ajili ya watakatifu bali alikuja kwa ajili ya wale wenye dhambi ili wawe huru kutoka katika vifungo vya dhambi. Roho ya Yesu aliteremka mpaka kuzimu kwa sababu alijua kuna kundi la watu ambao walikuwa wapo shimoni akaenda na kuwahubilia ili wapate wokovu.

 “Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani?  Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya.  Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.  Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.   Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;” (Mathayo 27: 45-51)

Yesu aliitoa roho yake yeye mwenyewe na roho yake ikaenda mpaka kuzimu kufanya kazi maalumu, matukio mbalimbali yalitokea mara baada ya Yesu kuitoa roho yake, pazia la hekalu likapasuka, tetemeko kuu la nchi likatokea, pazia lilipasuka ili kisiwepo kizuizi chochote cha wewe kwenda kwa Mungu Yesu alikuja kwa ajili ya wenye dhambi ili wasamehewe na kuwa na haki watu mbalimbali wanaweza wakaleta vizuizi mbalimbali vya watu kwenda kwa Yesu wanaweza kumsema mtu kutokana na tabia yake, mavazi yake, au namna alivyo lakini Yesu alikuja kuondoa mapazia yote yana vizuizi vyote ambavyo mtu anavipata ili asimfikie Yesu au asipate wokovu.

MAOMBI

“Kwa jina lenye nguvu la Bwana wangu Yesu Kristo leo ninapasua kila pazia lililowekwa mbele yangu ili kunitenga mimi na kazi yangu, kunitenga mimi na ndoa yangu, biashara, mume au mke wangu, kunitenga na baraka zangu, wewe pazia nakupasua kwa jina la Yesu.......( endelea kupasua kila pazia lilowekwa kukutenga na baraka zako)”

Tetemeko la nchi lilitokea ili ikiwa kuna mtu yeyote aliyeshikilia kazi yako, ndoa yako, elimu yako, biashara yako, n.k. ukiitumia damu ya Yesu na kusema kuwa unaitumia damu ya Yesu kutetemesha kila walioshikilia vitu vyako wanatetemeshwa kwa jina la Yesu na kuachia vitu vyako kwa jina la Yesu.

MAOMBI
“Baba katika jina lenye nguvu la Bwana wetu Yesu Kristo ninatetemesha kila mashimo yaliyonifungia, yaliyoshikilia kazi yangu, ndoa yangu, elimu yangu, afya yangu, ninaamuru jina la Yesu liwatetemeshe zaidi ya mtu atetemeshwavyo na umeme na kisha waviachie vitu vyangu kwa jina la Yesu. Amina ”

 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;” (Mathayo 27:52)

Aliposhuka kuzimu aliwaendea roho za watu waliopo shimoni, makaburi yakafunguka na watu wakatoka. Kuna watu ambao walikuwa wamechukuliwa msukule na kuwekwa shimoni lakini Yesu aliposhuka kuzimu alizitoa roho za watu waliokufa, alihubiri kwanza na watu waliopo shimoni wakasikia na kisha wakafufuka. Inawezekana na wewe kuna vitu vyako ambavyo vimefichwa makaburini, ndoa yako imefichwa makaburini, nyota imefichwa makaburini, elimu, kibali n.k. vimefichwa makaburini leo ninatangaza mahali popote ambapo vitu vyako vimefichwa makaburini njoooooo toka nje ya kaburi kwa jina la Yesu Kristo.
 
kwa kufufuka kwake lazima mtu atoke utumwani, Mchungaji akimtoa mama huyu kwenye utumwa.
MAOMBI
“Kwa mamlaka ya jina la Yesu Kristo jina lililo hai na lenye nguvu ninatikisa makaburi yote ya kichawi yaliyonishikilia kwa jina la Yesu, makaburi yaliyokamata afya yangu, mikono yangu, moyo wangu, kazi yangu, watoto wangu, mume au mke wangu au kitu changu chochote nakuamuru wewe kaburi upasuke na unitapike na kuachia vitu vyangu vyote kwa jina la Yesu. Amina ”

Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yohana 10:10)

Kuzimu ni wezi, wanawatumia watu mbalimbali kama wachawi, waganga, wasoma nyota ili kuiba vitu vyako na kisha kuvifungia katika jeneza chini kuzimu au mahali popote. Wanaweza kukutengenezea jeneza ili wewe ukataliwe, usifanye vitu vile ambavyo unatakiwa kufanya. Inawezekana hapo mwanzo ulikuwa unapendwa na watu lakini ghafla ukaanza kuchukiwa hata na ndugu zako wa karibu ni kwa sababu ya kufungiwa kwenye jeneza la kuzimu. Wachawi wanaweza kutengeneza janeza kukufungia wewe na kazi yako, na ndoa yako, biashara yako, wanaweza kuiba macho yako, moyo wako yaani hapo mwanzao ulikuwa na moyo mzuri moyo wa kumpenda Mungu na kufanya kazi ya Bwana lakini leo hii moyo umeibiwa na kufungiwa kwenye jeneza mahali Fulani na ndio maana husikii kuomba tena, kufunga tena, ni kwa sababu


MAOMBI
“Leo katika jina la Yesu ninakuamuru wewe shimo mwenye jeneza ambalo limefungia hatima yangu, akili yangu moyo wangu, kibali changu leo ninaamuru wewe jeneza na kaburi pasuka kwa jina la Yesu, wewe joka unayenilinda kwenye jeneza leo ninakufyeka na ninakuamuru achia kila kitu changu, achia mchumba wangu, kazi , ndoa, achia uwezo wangu, ule uwezo wa kufanya kazi, wa kuhubili, kusoma neno la Mungu, kuomba, n.k. nakuamuru achia kwa jina Yesu, ninakuponda leo kwa jina la Yesu na ninavunja nguvu ya kaburi na jeneza na mauti kwa jina lenye nguvu la Yesu Kristo. Amina.”

 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” (Mathayo 27:53-54)

Kuna mambo yamekaa kwa namna ya kufika katika maisha yako lakini leo hii mambo hayo yatatoweka kwa sababu ya kutetemeshwa kwa kufufuka kwake Yesu. Huyu mfalme Yesu anapotoka kwenye mwili wake ardhi inatetemeka lakini pia anaporejea kwenye mwili wake ardhi inatetemeka pia.

 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.” (Mathayo 28:1-2)

 Inawezekana kuna watu wanakulinda kwenye tabu uliyonayo, wanafurahi kukuona upo kwenye utumwa na hata akitokea mtu wa kukutoa wanakasirika na kuzuia mtu yeyote asikutoe katika kifungo, yaani hawa ni walinzi wanaokulinda ili usitoke katika kifungo ulichonacho kama ambavyo walinzi walilinda kaburi la Yesu lakini leo ninaamuru tetemeko kuu la nchi litokee mahali ulipofungwa na walinzi wote watetemeshwe na wawe kama wafu kwa jina la Yesu na kisha wewe utoke mahali ambapo umefungwa kwa jina la Yesu.
 
Showers of Glory Morogoro wakicheza mbele za Bwana Baada ya kutoka utumwani ilikuwa furaha ya ajabu wakati wa Ibada ya leo.
 “Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka.  Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.  Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.” ( Mathayo 28:11-15)

Baada ya Yesu kufufuka wazee wa mji wakakutana kwenye kikao chao wakafanya shauri wakapanga maneno ya uongo ili waseme Yesu hajafufuka bali wezi wamemuiba, wakakusanya hela ili wawalipe walinzi waseme uongo na ndio maana uongo huwa unatenda kazi sana mpaka leo. Mungu leo hii akuhamishe kutoka katika maneno ya uongo kwa jina la Yesu. Kuna mtu mwingine leo hii ukimuhubilia kuwa Yesu anaishi Yesu anaokoa kimsingi mtu huyu huwa haamini kabisa anaona kama ni uongo lakini wewe leo hii unatakiwa kuamshwa kutoka katika usingizi huo wa kudanganywa na umwamini na kumpokea Bwana Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wako. Usipoamini kuwa Bwana Yesu Kristo alifufuka katika wafu imani yako ni bure kabisa.

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro





Share:
Powered by Blogger.

Pages