Friday, November 13, 2015

NYOTA ILIYOIBIWA


JUMAPILI:  08 NOVEMBER 2015 –

UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

 
 

Na:     STEVEN NAMPUNJU (RP)

& DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

 

Utangulizi wa Somo: Nyota nini? Nyota ni kiashiria cha rohoni kinachoonesha mtu atakuwa nini au hatima yake baadae. Hatima na matukio ya baadae au mwisho wa maisha ya mtu ndiyo ambavyo huitwa ‘nyota ya mtu’. Mafanikio ya mtu hayatokani na elimu aliyo nayo, au mali zake bali hutokana na nyota yake. Hata hivyo, hivi viashiria vya mtu kuwa atakuwa nani baadae huweza kuibiwa. Mamajusi pamoja na kwamba watoto waliozaliwa walikuwa wengi kipindi kile, lakini wao walienda moja kwa moja kwa mtoto Yesu, kwa sababu ya nyota aliyokuwa nayo ya kuwa “mfalme”. Mambo yahusuyo nyota yanatufundisha kuwa:

1.      Kila mtu anayo  nyota:  tena nyota hiyo  hutoa tafsiri

2.      Nyota huweza kuonekana: Ndiyo maana mamajusi walisafiri mwendo mrefu kuifuatilia hii nyota. Kumbe nyota ya mtu  yaweza kusababisha safari zitengenezwe. Endapo kwako hayupo mtu anayekuja kutembelea nyumbani kwako ni kwa sababu nyota yako haijaonekana. Siri kubwa watakapoiona nyota basi wasiokuwa wageni kwako watakuja kwako,  tena wakiwa na zawadi mikononi mwao. Nyota yako ikionekana watakaokuja kwako hakuna hata haja ya kuwaambia walete nini, kwani watabeba fedha na zawadi kwa ajili yako. Watatokea mbali, wengine China, Japan n.k watakuja kwako.

3.      Nyota yaweza kufuatwa: Wale Mamjusi walitokea mbali ili kuifuata nyota

4.      Nyota ikionekana huleta zawadi / utajiri: Chanzo kikubwa cha  kufanya hawa mamajusi waje si  tu kuiona nyota, bali kuleta na zawadi. Ukiwa na nyota utapata vyote unavyohitaji.

 

MHUBIRI 9:11…[Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.]….Wakati ukifika na bahati nayo hufika. Ili  upate itategemea na wakati  wako. Upo wakati ukifika mtu fulani anapaswa  kuwa nani‼ Ili ufanikiwe unahitaji wakati. Mamajusi wao waliuona wakati wa Yesu kwamba huyu anayezaliwa ni "Mfalme wa Wayahudi". Mamajusi waliweza kuyaona haya hata kabla ya watu waliopo karibu na ukoo wa Yesu kuyajua. Ni  maombi yetu leo kuwa ‘watu wajifunze kujua wakati’. Baadhi ya wazazi hujisahau na kutabiria watoto wao mabaya: Mfano: wazazi wanaosema “nimezaa huyu binti kahaba” / nimempata huyu kijana wa kiume jambazi

 

Mungu ameviweka vipawa ndani ya maisha ya watu. Wapo watu ambao mafanikio yao huja kwa njia ya kusoma, wengine Mungu amewawekea vipawa vya biashara ili kupitia hivyo wafanikiwe. Lakini pia wapo wanaolazimisha kutumia nyota zisizokuwa zao, na mara nyingi hutumia nguvu za giza. Leo kataa nyota yako kutumiwa na watu wengine kwa Jina la Yesu

 

MIFANO YA WATU NA NYOTA ZAO KATIKA BIBLIA

1.      Musa: Mungu anataka Musa akawatoe Israeli wote kutokaMisri. Hata hivyo Musa akajitetea kuwa siyo msemaji, kama ilivyoandikwa katika KUTOKA 4:10…[Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.]… Musa hivyo  aliteuliwa  kama kiongoozi msikilizaji wa sauti ya Mungu. Musa hata hivyo hakujua kuwa anayo nyota / kipawa cha uongozi.

2.      Haruni: Huyu aliteuliwa na Mungu kama msemaji. KUTOKA 4:11-14…[Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana? 12 Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. 13 Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. 14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake.]…Mungu anamkemea Musa, kumwambia kuwa Haruni ameteuliwa kuwa msemaji  mkuu. Mungu alitaka Musa awe Mungu kwa Haruni. Haruni ni mzuri katika kushawishi. Imeandikwa katika KUTOKA 7:7..[Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao.].. Kwa upande wa umri, Haruni (83) ni mzee zaidi  ya Musa (80), lakini yeye ndiye zaidi mahiri wa kuongea.

 

WALIOPEWA NYOTA NA MUNGU KATIKA BIBLIA

1.      Watu wenye hakima  na uwezo. Imeandikwa katika ZABURI 45:2…[Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.]

2.      Watu wenye roho ya wepesi. Ukiwa na roho  ya uziot Mungu  hakupatii nyota. ZABURI 51:2…[Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.3 Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.]…Mtu aliye tayari kuyakubali makosa yake. Siyo kama Adamu alivyoulizwa na Mungu akasema ‘siyomimi ila yulemwanamke uliyenipa’. Mungu anaweka nyota kwa watu wa aina hii kwa sababu wapotayari. Wapo pia watu  wenye mioyo mizito: MITAHALI 25:20…[Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi;  Ni kama siki juu ya magadi.]….Moyo mzito hautakiwi hata kidogo.

Imeandikwa pia katika KUTOKA 8:15…[Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena.]…Mwenye moyo mzito hutamani shida iishe lakini baada ya nafuu huufanya moyo  wake kurudia kuwa mzito, kama Farao alivyofanya. Kutokana na moyo mzito, Farao na watu wake walipatwa na msiba wa watoto wao na mifugo yao.

 

KUNA HAJA GANI  YA KUIRUDISHA NYOTA ILIYOIBIWA?

1.      Nyota ikionekana huwa na furaha kubwa: Wapo watu leo hii ambao  hawana furaha kwa sababu ya nyota kutoonekana kwapo. MATHAYO 2:10…[ Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.]….Yaani pale nyota ilipopotea wale mamajusi hawakuwa na furaha tena. Mamajusi walikuwa wakijiuliza kwamba zawadi  walizozibeba watazipeleka wapi?

Wapo ambao nyota zao zimepotea na wale  waliobeba zawadi kwa ajili yao hawana furaha. Wapo walioahidiwa kuchumbiwa  aukuolewa lakini mara nyota zao zilipopotea furaha zao zikabakia kuwa majuto. Nyota ikirudi,furaha inarudi. Nyota ikirudi amani inarudi

 

2.      Nyota ya mtu inaweza kubadilisha historia ya mji: Mahali pale ambapo palidharauliwa heshima itatokea. MATHAYO 2:1-6..[ Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4 Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5 Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6 Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.]…Kilichowapeleka mamajusi Yerusalem ni ile nyota ya Yesu,  na kwa kuwa mji huu ulikuwa mkubwa. Hata hivyo mfalme alipoulizia habari za mtoto Yesu kuzaliwa, ilionekana kuwa mfalme alitabiriwa  kuzaliwa humo Bethlehemu. Ingawa Bethlehemu ilionekana kama mji  mdogo, tena wa kudharaulika, maisha duni lakini kwa kupitia nyota ya Yesu, mji  huu ukapata heshima. Nyota ya mji ikionekana, maendeleo  yatatokea. Inahitajika nyota ya mtu mmoja. Nyota ya  mtu  mmoja tu inaweza kubadili historia ya mji wote na kufuta historia za maisha marefu ya kudharauliwa katika Jina la Yesu.

 

3.      Nyota ikionekana hazina huwa zinafunguliwa: Imeandikwa MATHAYO 2:10-11… [Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. 11 Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane.]…Hazina huwa zinafunguliwa pale mwenye nyota akipatikana. Wapo wanaong’ang’ania wafanikiwe, lakini haitokei kwa sababu nyota zao hazijaonekana. Ndoa zitapatikana, watoto watazaliwa pale.

 

4.      Nyota ikionekana utafanikiwa na kuheshimika: Wale wasiokufahamu wataanza kukufahamu. Mamajusi walikuwa hawafahamu Bethlehemu. Lakini kupitia hii nyota, walifanikiwa kupajua. Hata mama yake Yesu aliweza kufahamika kwa sababu ya Yesu kuzaliwa. Mamajusi walisujudu, kwa sababu ya nyota  ya Ufalme wa Yesu. Nyota ikipatikana, watu watakuja wenyewe na kusujudu hata nchi, na heshima yako itakurudia kwa Jina la Yesu. Nyota huwavuta watu watoke walipo ili kukufuata wewe.

 

5.      Nyota huleta mwangaza na kufanikiwa kwa mtu: Imeandikwa katika ISAYA 60:5-6 …[Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia. 6 Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.]….Nyota yako  ikeshaonekana utajiri na mafanikio yatakujia yenyewe kutokea mbali.

 

UKIRI
Kuanzia leo ninahitaji nyota, kwa Jina la Yesu. Ewe nyota ya heshima uliyekwama mahali popote ninakulazimisha kwa Damu ya Yesu njoo, njoo, njoo, kwa Jina la Yesu. Ewe nyota wa kufahamika na kuheshimika uliyezuiliwa na waganga wa kienyeji na wachawi nakuita njoo, kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

DALILIZAMTUALIYEIBIWA NYOTA

1.      Kila  utakachokifanya kitakosa ufanisi: Mtu wa aina hii hukosolewamara zote badala ya kupongezwa kwa kazi anayoifanya.

2.      Mtu hufanya mambo Kwa uzito kwa ugumu: Kama ni biashara hata uitangaze redionina magazetini, utatumianguvu nyingi sana. Mara nyingine mtu huyo huzunguka hapa na pale akitafuta mafanikio yake lakini haimsaidii. Mtu wa aina hii hujikuta akikiri ‘maisha ni magumu’

3.      Kila anachokifanya hakifiki kwenye mafanikio yake: Mathalani endapo ni  biashara,  huishia kuwa hasara na kuacha.mwingine huacha kazi.

 

TAHADHARI YA NYOTA:

Nyota ikishaonekana kuna watakainuka na wengine kuanguka: Kuna wengi utakaowainua na wengine utakuja kuwapoteza. Simeoni  baada ya kumpokea Yesu  mikononi mwake alisema maneno haya, katika LUKA 2:34...[Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.]… Wapo ambao ni  rafiki zako wanaweza kukuacha nyota yakoikionekana.

 

UKIRI
Kuanzia leo,na kuanzia sasa, Nitaishi sawasawa na nyota yangu kwa Jina la Yesu. Mtu yeyote unayezuia nyota yangu, leo nashambulia kazi yako, niachie kwa Kwa Jina la Yesu.Wewe unayetumia nyota yangu, niachie kwa Jina la Yesu.Naweka uhuru kuanzia leo.ninaamuru kuanzia leo, na kuanzia sasa wale wanaotumia umahiri wako, wayaachie maisha yako kwa Jina la Yesu. Ewe nyota yamafanikio uliyefichwa  mahali popote nakuamuru njoo kwa Jina la Yesu. Amen.

 

Endapo mtu hujaokoka, leo ni siku muhimu kwako kufanya uamuzi huo. Hii itakusaidia kwamba asiwepo mtu yeyote atakayeiiba nyota ya maisha yako.

 

=== © Information & Media Ministry ===

(Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

/or

Contact our Church Leadreship:

Bishop Dr. Godson Issa Zacharia

(Glory of Christ (Tanzania) Church in Morogoro).

Cellphone: (+255) 765979866 /or +255 713459545.
Share:

Related Posts:

Powered by Blogger.

Pages