GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
[KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO]
JUMAPILI: 19 FEBRUARI
2017
MHUBIRI: Dr. Godson Issa Zacharia (SNP)
Dr. Godson Issa Zacharia (SNP Morogoro) akihubiri Jumapili 19/2/2017 Kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro. |
Tunafahamu kuwa
Mwanadamu anazo sehemu kuu tatu: Roho, Mwili na Nafsi. Katika 1THESALONIKE 5:23 imeandikwa hivi.. (Mungu
wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu
mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu
Kristo.). Mungu mwenyewe alipomuumba mwanadamu hapo mwanzo kutokea kwenye
udongo, alimfanya katika sehemu zote tatu kama tusommavyo katika MWANZO 2:7….(Bwana Mungu akamfanya mtu kwa
mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.).
Kumbe basi MWILI wa Mwanadamu ulitoka
udongoni na kupuliziwa pumzi ambayo ni ROHO
itokayo mbinguni kwa Mungu mwenyewe. Biblia inaposema uraia wetu siyo wa hapa
duniani, ni kwa sababu mwanadamu ni
Roho, na kwa hivyo, Roho hiyo
siku moja itarudi kwenda mbinguni na kukaa huko milele.
Katika YOHANA 6:63 neno linasema…(Roho
ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena
ni uzima.). Kwa maana hiyo basi,
tunajifunza kuwa ‘Mtu ni Roho yenye
nafsi inayokaa ndani ya nyumba na hiyo
nyumba ndiyo inayoitwa Mwili’. Sisi (ambao ni roho) tumepanga kwenye nyumba
ambayo siyo ya milele,na kuna siku
tutaondoka kwenye hizi nyumba tulizopanga na kuelekea kwenye makazi yetu ya kudumu, huko mbinguni.
Kumbe basi mtu aliyepanga katika nyumba iitwayo mwili anaweza
kuwa ndani ya mwili (akiwa hai) na kuna wakati anaweza kuwa nje ya huo mwili
wake (na hapo tunasema mtu huyu amekufa).
Imeandikwa katika 2KORINTHO 12:2-4….(Namjua
mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa
katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo
alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. 3 Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa
katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); 4 ya kuwa
alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu
ayanene.). Kwa kuwa mtu anaweza kutoka nje ya mwili, basi ni hakika
kuwa mtu siyo mwili. Ndiyo kusema, sisi
hapa hatujawahi kuonana uso kwa uso hata mara moja, ila tunachokiona ni miili
yetu ambamo ndani yake roho zetu zimepanga.
Na kwa maana hiyo,
mtu anapokufa, Mwili wake unarejea kwenye udongo ambako ulitwaliwa (MWANZO 3:19….”kwa jasho la uso wako utakula
chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u
mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”). Kwa maana nyingine, KIFO (MAUTI) ni ule ‘utengano kati ya Roho na Mwili’. Kumbe
basi, Kifo ni roho na wala siyo tukio. Tunajuaje kuwa Kifo ni Roho? Tusome kwa pamoja
UFUNUO 6:8… “Nikaona, na tazama, farasi wa
rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu
akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na
kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.”. Kwamba kifo (MAUTI) kinaweza kupanda farasi kama
abiria wake, inamaanisha kuwa kuna uwezekano roho hii ikapanda basi, bodaboda, ndege,
au chombo chochote kile cha usafiri, na msindikizaji wa huyu roho (mauti) anaitwa
KUZIMU. Kwa hiyo Kifo ni roho ya kutengenisha.
Roho huyu akiingia ndani katika
ndoa yako, ndoa hutenganishwa. Roho wa
mauti akiingia katika biashara yako, hata kama biashara ilikuwa nzuri namna
gani, biashara hiyo itakufa vile vile. Kwa lugha nyingine ni kwamba Roho hii ya
Mauti, yaweza kuingia katika masomo, ndani ya kazi, fedha n.k na kusababisha
kifo kwenye vyote hivyo.
Cha kujifunza hapa
ni kwamba, roho ya kifo haiwezi kukuingia hivi hivi bila kuwepo kwa WARAKA WA KIFO. Shetani huja ndani ili
kuleta utengano (yaani ‘mauti’) kwa kuagizwa kupitia waraka maalumu wa uitwao “Waraka wa Kifo”. Waraka wa Kifo ni hati
au karatsi iliyoandikwa maalumu na watu waovu na kupelekwa ili kusababisha
mauti kabla huyo mtu aliyekusudiwa hajafa. Kwa kawaida, hati ya kifo (Death
certificate) huandikwa baaada ya mtu kufa, ila waraka wa kifo (Katika
Ulimwengu wa Roho) huandikwa kabla ya kifo hakijatokea. Unaweza kuwa unaishi na kutembea vizuri na
afya njema, ukidhani kuwa uko salama lakini kumbe wachawi wameshakuandikia
waraka wa kifo bila wewe kujua.
MIFANO YA KIBIBLIA YA NYARAKA ZA VIFO ZA WACHAWI
1.
WARAKA WA KIFO ULIOANDIKWA NA YEZEBELI
Katika Biblia,
kuna waraka wa Kifo wa Yezebeli ulioandikwa maalumu kwa ajili ya kumuua Naboth,
mtumishi wa Bwana. Imeandikwa katika 1WAFALME
21:1-15…(Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu
katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. 2
Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye
shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake
shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na
thamani yake. 3 Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi
wa baba zangu). Kwa kawaida URITHI
ni mali apewazo mtu baada na wazazi wake kufariki dunia. Kwa sisi tuliookoka
URITHI tulioahidiwa ni kupokea mara mia moja ya vile tulivyoviacha, na mwishowe
Uzima wa Milele. Imeandikwa katika MATHAYO
19:29…(Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au
mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na
kuurithi uzima wa milele.). Endapo tumeacha majumba 100 kwa ajilinya
Kristo, maana yake tutapokea hapa duniani majumba 100x100, na mbinguni Uzima wa
milele. Kama ni kutawala, utatawala hapa dniani mara 100. Kama ni kumiliki,
utamiliki mara 100 hapa duniani, na zaidi ya yote, utaurithi UZIMA WA MILELE mbinguni.
Tena imeandikwa
katika MATHAYO 21:33-39…(Sikilizeni
mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la
mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga
mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. 34 Wakati wa matunda ulipokuwa karibu,
akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. 35 Wale
wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu
wakampiga kwa mawe. 36 Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza
wakawatenda vile vile. 37 Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi
mwanangu. 38 Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa
wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. 39 Wakamkamata,
wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua). Kwa hiyo, sisi ni
warithi sawasawa na andiko katika YOHANA 1:12 kwamba “Bali wote waliompokea aliwapa
uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”.
Shetani anajua wewe uliyeokoka ni MRITHI na ndiyo maana mashetani anakuwinda
usiku na mchana ili wautwae urithi wako ulioahidiwa. Na zinaweza kuwepo nyaraka
nyingi sana zinazomlenga mtu mmoja kwa wakati mmoja. Pengine nyaraka za Kifo kwenye
ndoa yako, na kifo cha biashara yako, kifo cha kazi, kifo cha mali ulizo nazo
n.k.
Kuna watu wanaweza
kununa hata kuacha kula chakula kwa sababu unapokuja kanisani wanakuona umekuja
sehemu ya kupokea urithi wako. Imeandikwa katika 1WAFALME 21:4-13…(Basi Ahabu
akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno
lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu.
Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. 5 Lakini Yezebeli mkewe akamwendea,
akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? 6 Akamwambia, Kwa
sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la
mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala
yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. 7 Yezebeli mkewe akamwambia,
Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako
ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. 8 Basi,
akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile
nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa
pamoja na Nabothi. 9 Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya
watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, 10 mkainue watu wawili, watu
wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme.
Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. 11 Wale wazee wa mji wake, na
walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza,
kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. 12 Wakapiga mbiu ya watu
kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. 13 Na hao watu wawili, watu
wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia
Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo
wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa). Kumbe ndiyo
maana wachawi wanapokuona unapiga majeshi, wanakuonea wivu ni kwa sababu
wameshaona urithi wako. Watu wawili wasiofaa waliandaliwa kutoa ushuhuda wa
uongo dhidi ya Nabothi. Na watu wa aina hii, ni wale wa karibu sana kiasi
kwamba watu wengine hawawezi kutilia mashaka juu ya ushuhuda wao. Ikumbukwe
kuwa wakati haya yote yakiendelea, Nabothi hakupewa taarifa ya mipango hii miovu.
Ni hatari sana kwa mtu unapouwa
umebarikiwa ukaanza kubweteka na kumuacha Bwana ukisahau ulipotoka. Nabothi
baada ya kumkatalia mfalme Ahabu aliyelitamani shamba lake, alipaswa mara mmoja
kuingia magotini na kuomba kinyume na tamaa za huyu mfalme. Unapokuwa na shamba
lililoneemeka, biashara iliyoneemeka, kazi nzuri, ndoa nzuri n.k usibweteke
bali ingia magotini na kuwaponda wote wanaokuwinda na kuyatamani hayo uliyo
nayo kwa Jina la Yesu.
Picha ikionesha sehemu ya Umati wa Waumini na Watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro, Jumapili 19/2/2017 |
2.
WARAKA WA KIFO ULIOANDIKWA NA HAMANI BIN HAMEDATHA
Imeanidkwa katika ESTA 3:1-15... (Baada ya hayo mfalme Ahasuero
alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti
chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. 2 Nao watumishi wote wa
mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana
ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala
kumsujudia. 3 Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia
Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? 4 Ikawa, waliposema naye kila
siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai
yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. 5 Hata Hamani
alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. 6
Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila
yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa
wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. 7 Basi
mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme
Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi
kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. 8 Basi Hamani
akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali
mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao
sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme;
kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. 9 Basi, mfalme akiona vema, na
iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi
mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. 10 Ndipo
mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui
ya Wayahudi. 11 Kisha
mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
12 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza;
na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa
mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila
jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la
mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake. 13 Barua zikapelekwa kwa
mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na
kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku
moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa
Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara 14 Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu
katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote wawe tayari siku ile ile. 15
Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko
Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa
Shushani ukafadhaika.). Henu
waza, kuna watu wameandikiwa kifo, Wayahudi wote, wanawake na watoto wao wote
lakini Mfalme na Hamani wanaketi na kunywa divai na kufurahi wakati Wayahudi wanafadhaika.
UKIRI
Ninatangaza kwa
Jina la Yesu, yeyote aliyeandika hati ya kifo, aangamie kwa Jina la Yesu.
|
Kwa kawaida,
Mfalme akeshatia saini kwenye waraka wa kifo, hakuna anayeweza kuutengeua. Ni
kwa wale waliookoka tu ndiyo wanaoweza kuingia magotini kuomba na kubatilisha
hati za kifo za kichawi. Unapoona waraka wa kifo umeandikwa kwako (waraka ambao
siyo wa mwilini bali wa rohoni), cha kukusaidia tu ni kuomba wala siyo kulia.
Tusome katika ESTA 4:1-3 …(Basi
Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika
gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti
kuu ya uchungu. 2 Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna
awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia. 3 Na katika kila
jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa
Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya
gunia na majivu.). Hivi utajjua je kwamba ipo hati ya mauti
iliyoandikwa juu yako? Utajua tu kwa kuyaangalia maisha yako. Endapo upo ugumu
unaoendelea, unapaswa kuingia katika maombi kanisani, hakikisha siku zote
unakuwepo kanisani kwa maombi. Pia
katika ESTA 4:16-17 imeandikwa “Uende
ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu;
msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu
tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami
nikiangamia, na niangamie. 17 Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama
vile Esta alivyomwagiza”. Hapa
tunaona maombi ya kufunga yaliyokuwa rasmi kwa ajili ya kubatilisha Waraka wa
kifo kwa Waahudi wote ulioandaliwa na Hamani.
Pia imeandikwa
katika ESTA 5:9-15 maneno haya…(Basi
Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani
alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka
mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. 10 Walakini Hamani akajizuia,
akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. 11 Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali
zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha
katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. 12
Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote
pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho
pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. 13 Bali haya yote yanifaa nini, pindi
nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? 14 Basi Zereshi mkewe akamwambia, na rafiki zake wote,
Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho asubuhi useme na mfalme
ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na
mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza ule mti.). Unaona jinsi ambavyo moyoni mwa Hamani hakuna amani
pindi anapomuona Mordekai akiwa hai. Usiku
ule Hamani hakuwa na usingizi usiku kucha, huku akipanga jinsi ya kutengeneza
mti wa kumuulia Mordekai.
Ikumbukwe kuwa
imeadikwa kuwa hapa duniani tutapokea mara 100 na mbinguni kuutrithi uzima wa
milele. Mordekai hakuwahi kufanyiziwa heshima yoyote kwa kazi nzuri aliyoifanya
ya kumuepusha Mfalme na kifo kilichopangwa kwake. Imeandikwa katika ESTA 6:1-13…(Usiku ule mfalme hakupata
usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha maandiko ya taarifa, nayo yakasomwa mbele
ya mfalme. 2 Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwachongea
Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango,
waliotaka kumtia mikono mfalme Ahasuero. 3 Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani
au jaha gani Mordekai aliyofanyiziwa kwa ajili ya hayo? Watumwa wa mfalme
waliomhudumu wakamwambia, Hakuna alilofanyiziwa. 4 Mfalme akasema, Yupo nani
behewani? Ikawa Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme,
aseme na mfalme, ili kumtundika Mordekai juu ya mti ule aliomwekea tayari. 5
Basi watumwa wa mfalme wakamwambia, Tazama, Hamani yupo, amesimama behewani.
Mfalme akasema, Na aingie. 6 Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia,
Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni
mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi? 7 Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme
apenda kumheshimu, 8 na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea
kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji ya
kifalme kichwani; 9 na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo
wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme
apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na
kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye
mfalme apenda kumheshimu 10 Basi
mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema,
ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme;
lisipungue neno lo lote katika yote uliyoyasema. 11 Ndipo Hamani alipoyatwaa
mavazi na farasi, akamvika Mordekai yale mavazi, akamrakibisha juu ya farasi
kuipitia njia kuu ya mjini, akapiga mbiu mbele yake, Hivyo ndivyo
atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. 12 Kisha Mordekai akarudi kwenye mlango wa mfalme.
Bali Hamani akaenda mbio nyumbani kwake, mwenye msiba, na kichwa chake
kimefunikwa. 13 Basi
Hamani akawasimulia Zereshi mkewe na rafiki zake wote kila neno lililompata.
Kisha watu wake wenye hekima na Zereshi mkewe wakamwambia, Ikiwa huyu Mordekai,
ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, wewe hutamweza,
bali kuanguka utaanguka mbele yake.).
Tunaona jinsi ambavyo maombi ya siku tatu yalivyoweza kubatilisha mipango miovu
ya Hamani, na mti ule aliouandaa kwa ajili ya Mordekai ukatumika kwa ajili ya
kumtundika yeye mwenyewe. Maombi yana uwezo wa kubatilisha mipango ya maadui
zako. Ndiyo maana Mungu anasema katika ISAYA 43:4 “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami
nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa
ajili ya maisha yako.”.
Waumini na Watendakazi wa Ufufuo na UzimaMorogoro wakimshangilia Bwana baada ya kumchakaza shetani 19/2/2017. |
UKIRI
Ninaamuru yeyote
aliyeshikilia ule mti wa kuangamiza kazi yako wewe, atumike kukuletea barua
ya kukupandisha cheo kazini katika Jina la Yesu. Ninatangaza leo kuwa, yule
aliekuandikia kifo, afe yeye kwa Jina la Yesu .
|
Kama yupo mtu leo hii ambaye hujaokoka, ni nafasi ya
pekee kumkubali na kumpokea Yesu Kristo
maishani mwako ili iwe rahisi
kufuta nyaraka za vifo ziliandikwa dhidi
ya maisha yako.
========== M W I S H O ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
SIMU: 0719 798778 (Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
© Media and Information Ministry
GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +255719612874 / +255713459545
|