Monday, March 6, 2017

KUFUNGUA VIFUNGO VYA KISHETANI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

[KANISA LA UFUFUO NA UZIMA]

MOROGORO

JUMAPILI: 05 MARCH 2017

 

MHUBIRI:    PASTOR ISAYA KILYINGA (SNP KILOMBERO)

                  
Pastor Isaya Kilyinga (SNP Kilombero) akihubiri katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro, Jumapili 5/3/2017
  

Mungu ni Mungu afunguaye  waliofungwa.  Katika LUKA 13:10-13 imeandikwa (Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. 11 Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. 12 Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. 13 Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.) na katika mstari wa 16 imeandikwa “Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?” Tunamuona huyu mama kwa muda wa miaka 18 alikuwa hawezi. Pengine kuna ndugu zake waliokuwa wakimtia faraja kama kawaida, kumwambia kuwa hilo tatizo lililompata hata ndugu fulani kwenye ukoo wao, kwa hiyo ni la kawaida avumilie tu.

 

Kwa kawaida kazi kuu ya kifungo ni kufunga, na mwishowe huishia kuwa tatizo la maisha yote kama vile uonavo kifafa, umaskini, kifo n.k. Wanadamu wamefikia mahali pa kuona kuwa haya mambo ya kufungwa ni hali iliyozoleka tu na kwamba ni ya kawaida. Shetani anaweza kumfunga mtu mmoja mmoja au hata ukoo, au biashara, au ndoa yake. Kuna watu wengine tatizo lao siyo kuolewa bali kutodumu katika hiyo ndoa (mtu anaolewa na kuachika, kisha akiolewa tena ndoa inavunjia vilevile). Shetani huwafunga watu ili waendelee kutuseka. Pengine ni mtu ambaye ana wivu tu na hataki wewe ufanikiwe. Aliyefungwa jela anaukosa ule uhuru wa kujiamaulia mambo yake. Hata hivyo vifungo vinafunguliwa kwa Jina la Yesu.


Baba (SNP Dr. Godson Issa Zacharia) na Mama (RPHappiness Godson) wakifuatilia mahubiri Jumapili 5/3/2017


 

Imeandikwa katika KUMBUKUMBU 18:10-11….(Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, 11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.).  Wapo watu wanabutua watoto wao kwa njia ya kafara ili wapate mali za dunia hii. Uchawi wa kupiga mafundo hutokea kwa mtu  anapochukua kitambulishi cha mwili wako (mfano nguo, kucha, nywele n.k) na kuzifunga ili  mtu wa aina hiyo afungwe na asifanikiwe bali awe na matatizo  yasiyoisha. Mtu anapofungwa kwa aina hii dawa yake SIYO KUOMBEWA bali ni KUFUNGULIWA. Mambo ya kuambiwa vumilia siyo ya kukubalika. Wengine wamejikuta wanatafuta msaada kanisa hili hadi jingnine lakini bado tatizo lipo palepale!! Wengine wamedanganywa kuwa watoe sadaka au wapande mbegu lakini yote hayo hayasaidii kwa sababu tatizo litaondoka tu kwa KUFUNGULIWA.

 


 

Katika WAAMUZI 16:21 imeandikwa…(Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.). Kumbe tunajifunza kuwa vifungo vinatofautiana kati ya mtu mmoja na mtu mwingine. Pengine utawakuta watu wako  watatu wenye shida inayofanana,  lakini wawili waao wakafunguliwa na mmoja tu akabaki  na kuanza  kujiuliza maswali “kwa nini tatizo  lake halijafunguliwa?” Cha kujifunza hapa ni kwamba, mashetani nayo yapo ya ngazi tofauti tofauti. Tatizo laweza kuwa moja lakini madhabahu iliyotumika ndiyo tofauti. Wengine walitumia damu ya njiwa wakati wengine wametumia damu ya wanyama wakubwa ng’ombe au hata binadamu. Kwa hiyo kuna watu wenye matatizo ambayo hata ukitamka tu HALELUYA tatizo lake linaondoka.

 

Imeandikwa katika MATHAYO 17:14-18 (Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, 15 Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. 16 Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. 17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. 18 Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile). Tunaona kwamba ngazi ya lile pepo ilikuwa ya juu sana, na ndiyo maana wanafunzi wa Yesu walishindwa kumtoa yule pepo mara moja. Kwa hiyo pepo anapoondoka, mtu anapona saa ile ile. Pepo akeshaondoka kama ni biashara au ndoa vilikuwa haviendi vizuri, vitabadilika saa ile ile. Maana yake ni kwamba, mtu anapofunguliwa, mafanikio yanapaswa yaanze saa ile ile.

 

Tukisoma katika MARKO 5:1-10 maandiko matakatifu yansema  (Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; 4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunjavunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe. 6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. 8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. 9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni,  kwa kuwa tu wengi. 10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.). Kwa sababu ya kifungo, mtu anawekwa mahali ambapo  hakupataka kabisa. Ndiyo maana mtu huyu alikuwa kifungoni akikaa makaburini, mahali ambapo hayupo mtu anayepapenda kukaa. Unapokuwa umefungwa unaweza kuyafanya mambo ambayo wewe mwenyewe huyapendi. Na wapo watu waliofungwa wanalalamika eti hakuna ndugu wa kuwatia moyo. Kumbuka kuwa, Yesu hakuja kuwatia watu moyo, bali kuwafungua waliofungwa.

 

Maombezi yakifanyika kwa mmojawapo ya watu waliokuwa na tatizo la vifungo vya mashetani - Jumapili 5/3/2017




Kuna ulimwengu wa mwili (wa vitu vinavoonekana), na ulimweengu wa roho (wa viumbe na roho zisizoonekana). Hata hivyo, Ulimwengu wa roho ndiyo ulimwengu ulio halisi (original) na ndipo matatizo yote yanapoanzia. Kuna mtu mwingine shida aliyo nayo ilianzia pale tu alipoota ndoto ya kukimbizwa, na hadi  leo shida yake ipo palepale. Ukitaka kuliondoa tatizo shughulikia kwanza CHANZO CHA TATIZO, ambacho ni  mashetani. Katika MATHAYO 9:32-33 imeandikwa (Hata hao walipokuwa wakitoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo. 33 Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote.). Yule bubu baada ya pepo kutolewa, alianza kunena. Hii ni kuonesha kuwa, chanzo kisipoondolewa, matatizo yataendelea kuwepo.  Kuna wengine wamefungwa na ndugu zao wasizae, wawe tasa, au wasiolewe, wawe na matatizo.

 

UKIRI
Nafungua leo kifungo cha familia yetu. Nashambulia mashetani yote, kafara iliyotolewa naiteketeza leo. Ninakata kifungo changu kwa Jina la Yesu. Nikianza jambo, nakataa kuishia njiani kwa Jina la Yesu. Naiangamiza kafara yao kwa Damu  ya Yesu.  Amen
 

 

Zipo madhabahu za kishetani ambazo mashetani yakeshapewa kafara yanaanza kazi papohapo.  Unapofunguliwa shida yako haitorudi tena. Mungu akeshakufungua, utakuwa huru kwelikweli, labda mtu aliyefunguliwa ajichanganye mwenyewe kwenye uzinzi, uwongo na dhambi zinginezo. Mtu wa aina hii mashetani  lazima yamrudie na kumfunga upya. Maombi ya mtu aliyefunguliwa ni ya kushindana siyo kulalamika. Kifungo  humfanya mtu kujidharau  jinsi alivyo: mwingine atalalama kusema kama siyo kuzaliwa akiwa mfupi, pengine angekuwa ameshaolewa!! Hicho nacho ni kifungo kitokacho kwa mashetani. Mwingine huiangalia rangi ya ngozi yake na kusema asingekuwa na rangi hiyo pengine angekuwa tayari keshafanikiwa kimaisha; hicho nacho ni kifungo kitokacho kwa mashetani.!!

 
Umati wa watendakazi na Waumini waliohudhuria Ibada ya Jumapili 5/3/2017, Kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro



Kuna watu ambao hata ukiwaombea kufanikiwa, wao badala ya kupokea kwa imani huanza kujiuliza maswali,”wa kufanikiwa awe mimi??” Uwe umesoma au hujasoma, wakati na bahati huwapata wote kwa Jina la Yesu. Sikuwahi kumuona Yesu akimuuliza mtu “Umesoma hadi kidato cha ngapi? Usiogope kwa sababu hata wewe Mungu anaweza kukuinua kwa Jina la Yesu. Ukizaliwa ukiwa maskini siyo tatizo, tatizo litakuwepo endapo wewe utakubali kufa ukiwa maskini. Ndiyo  maana imeandikwa katika ISAYA 45:3…(nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.). Ni zipi hizi hazina za gizani? Hizi ni mali zote ambazo zinamilikiwa na watenda dhambi na waabudu mashetani. Ni wakati wa kutaka Mungu akupatie hizi hazina za gizani kwa Jina la Yesu. Karama za Mungu hazina majuto.

 

Kama Sara alipata mtoto akiwa na umri wa miaka  90, iweje wewe wa miaka 35 uanze kuwa na wasiwasi??. Upo ushuhuda wa mama mmoja  wa miaka 45 ambaye alikuwa hapati mtoto kwa muda mrefu. Baada ya kumuombea, kwa imani nilimwambia “katika majira kama haya mwakani  utapata mtoto”.  Baada ya maombi yale, Yule mama alikuja kupata ujauzito lakini kipindi cha kukaribia kujifungua madaktari walimpima na kumwambia mtoto amefia tumboni, na hivyo atapaswa kufanyiwa operesheni ili kumuondoa mtoto-mfu. Baadae mama yule alinipigia simu kwa uchungu, nikamshauri kabla ya kwenda huko kwa madaktari subiri kwanza tufanye operesheni ya rohoni!!! Baada ya maombi haya yaliyofanyika kwa simu, yule mama alipiga kelele za furaha kusema mtoto anacheza na kurukaruka tumboni!!! Huyu ndiye Mungu tunayemwamini, Mungu ambaye anafanya mambo makuu na yasiyowezekana kwa akili za wanadamu.

 
Vifungo vikeshafunguliwa, kinachofuata ni Kumshukuru Mungu kwa kutuweka huru.! Ndiyo  maana tupo Ufufuo na Uzima

 

Kwa Wewe ambaye hujaokoka, fanya maamuzi yako leo ya kuokoka. Cha kufanya leo ni kumkubali Yesu maishani mwako kwa maana ya kuokoka ili ukiwa upande wa Yesu ufanyike kiumbe kipya na kufunguliwa vifungo vyako vyote kwa Jina la Yesu.

 

========== AMEN ========

 

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia

Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson

Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson

SIMU: 0719 798778 (Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/

 

   © Media and Information Ministry
GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +255719612874 / +255713459545
Share:
Powered by Blogger.

Pages